Tuliendelea mpaka akamaliza Chuo, akiwa katika harakati za kutafuta Kazi mie nikawa nimeshika Ujauzito. Nilimueleza akakubali akasafiri.
Baada ya muda nikagundua alipata Kazi na alipangiwa huko Mkoani alikoenda na anaishi na mwanamke.
Kabla sijagundua hayo yeye alinambia yupo kwa Wazazi na anasimamia Miradi ya kwao, nilipomuuliza akakana lakini baada ya kumpa ushahidi akakubali na kusema ndio anaishi na mwanamke na ndio Mkewe mtarajiwa. Mimi na yeye basi ila tulee tu mtoto kwani mapenzi hakuna tena!
Niliumia sana nilifikiria alivonidanganya kwamba yupo kwao na anasimia miradi na anaendelea tafuta kazi na akipata nitaenda ili tukaishi wote.
Mpaka sasa maelewano hakuna ni ugomvi tu maana mie nimekuwa namlalamikia sana na yeye hapendi.
Naomba nishauri nifanyaje ili nimpotezee maana nampenda sana, yaani nimepungua mno Uzito kwa mawazo.
Tangu mtoto kazaliwa hajawahi kumuona, hivi sasa anamwaka mmoja, anatoa matunzo ya mtoto anatoa kiasi na kasema lazima atakuja kumchukua Mtoto ili nisimsumbue.
Nifanyaje pia ili asimchukue mtoto maana sitaki alelewe na mama mwingine, mie uwezo wa kumhudumia ninao nataka nikae na mwanangu.
Nisaidie kwa ushauri.
************
Dinah anasema: Habari ni njema tu Mrembo, ahsante kwa ushirikiano.
Kuachwa/Kuacha/Kuachana na mtu unaempenda kote kunauma sawa....sababu za Kuachwa/Kuacha/Kuachana hutofautiana lakini bado maumivu yake hufanana. Ili kusonga mbele siku zote unapaswa kukumbuka na kukubali kuwa Penzi halilazimishwi!
Najua unavyojisikia (najaribu kujiweka kwenye situation yako). Unadhani alikupenda kama ulivyompenda, kwa vile ulikuwa mdogo (at 19), huenda alikuwa ndio wa kwanza kwako na hiyo ikakupa Matumaini kuwa yeye ndiye atakaye kuwa mume wako....baada ya ujauzito ukadhani hakuna kitakachomfanya akuache kwa sababu mtakuwa na mtoto pamoja!
Unaumia, pengine unajutia muda wako, unajutia kwanini hukua Makini na kumjua mapema, Unajuta kwanini hukutumia Kinga na mengineyo....Unahisi kutaka au unataka kujua sababu hasa iliyomfanya akuterekeze na kuendelea na Maisha yake bila wewe na mtoto wenu ili uweze kusonga Mbele!
Kwavile hakuambii na hatokuambia basi mie nitakuambia....alikuwa anakutumia kwa Ngono akiwa Masomoni lakini hakuwa akikupenda wala hakuwa na mpango wa kuishi na wewe kama Mkewe.
Alitegemea wewe ujikinge kwa namna yeyote ili kuzuia Mimba na akikushawishi au kataa kutumia Condom na wewe kupata Mimba basi Kosa ni lako na sio lake.
Vijana wengi tu huwatumia mabinti wa watu kwa ajili ya kumaliza mahitaji yao ya Mwili, tatizo la wasichana hasa wale wadogo ni kuamini kuwa kwa vile "kanikuta Bikira basi atanioa".....unajisahau au unashawishika kirahisi kutojikinga dhidi ya Mimba ukiamini ukiishika basi ndio Tiketi ya Ndoa.
Bikira sio guarantee ya Kuolewa au mwanaume kuwa Muaminifu kwako, pia Mimba/Mtoto sio sababu ya kufunga ndoa au Uhusiano kudumu na kamwe usiitumie Mtoto ili kumkomoa/sumbua Mwanaume aliekuacha na Mimba.
Mwanaume aliekuacha baada ya Mimba hajali kwani hakai na Mtoto(Mimba) kwa miezi tisa, hana connection/bond na mtoto kama wewe Mama yake....Mwanaume habadiliki Kimwili, Kihomono wala Kiakili!
***Ufanye nini ili umpotezee:
Sio rahisi na itachukua muda lakini inawezekana. Nitakupa "therapy" yangu binafsi (sio rasmi) ya kufuata hatua za kuomboleza kama vile umefiwa na mpendwa wako ila tofauti ni kuwa hutomuombea au kumkumbuka Ex wako....ambayo naamini inaweza kukusaidia pia.
Hatua ya kwanza: Omboleza...ruhusu Akili na Moyo kwa mara ya MWISHO kukumbuka yote mazuri mliyofanya, ahadi mlizopeana, maeneo mliotembelea na kila jema ulilomfanyia na yeye kukufanyia.
Hiyo inakufanya ulie sana na kujiuliza kwanini? Umekosa nini wewe....lia huku unajiangalia kwenye kioo, lia wee na kujisemea mpaka upate hisia za kujiona Mjinga.
Hatua ya Pili: Unapohisi au kujiona Mjinga ni kwamba unakubali kuwa hata ukilia hawezi kurudi kwako, sasa kwanini Ukufuru wakati una afya njema, Mshukuru Mungu kwa hilo (au kwenye Msiba unakubali kuwa Kaenda na hawezi kurudi, jina la Bwana litukuzwe).
Hatua ya Tatu: Kabla hali ya kujiona "mjinga" haijakutoka kusanya(bila kusoama au kuangalia) kila kinachomhusu (sio mtoto) bali Picha, zawadi alizokupa (kama ni Vito vya Thamani, viuze), Kadi, Nguo n.k kisha piga Moto (teketeza) huku unamlaani kwa lana zote uzijuazo.
Hatua ya Nne:Kama ilivyo kwenye Msiba, baada ya Mazishi huwa unapata "unafuu" na hali ya kutokukumbuka alieenda exactly....unamkumbuka lakini hupati taswira yake halisi (Mungu wa ajabu bana)....basi utahisi unafuu huo ila tofauti ni kuwa hujamzika bali "umemteketeza kwa moto".
Hatua ya Tano: Ifunze akili yako kupoteza kumbukumbu nzuri kuhusu Ex, kwamba zikianza kuja tu unaziziba kwa ku-focus kwenye Kasoro zake....Mf: Mdomo ulikuwa unanuka, alikuwa hajui kubusu....Miguu yake sijui ilikuaje, kwanza alikuwa serial muongo n.k.
Trust me kila mwanadamu anakasoro zake sema Penzi hufunika....ila mkiachana lazima utaziona Kasoro za kutosha tu!
Hatua ya Sita: Kama hapo unapoishi sasa ndipo alipokuachia (mlikuwa mmepanga) basi angalia uwezekano wa kuhama ili uanze maisha Upya.
***Ufanye nini ili Ex asimchukue Mtoto:
Hawezi kumchukua, anakutishia tu ili uache kumtumia mtoto unapomsumbua na malalamiko yako ya Uhusiano mliokuwa nao, hasira za kudanganywa n.k.
Sasa pima umuhimu kati ya hisia zako za zamani juu ya Ex ambae keshasema wazi kuwa hakutaki au Maisha na uhai wa Mwanao kisha chagua moja.
Kama Maisha ya Mtoto ni muhimu zaidi kuliko hisia zako kwa Ex, basi kuanzia leo poteza mawasiliano yake na mengine yote yanayomuhusu yeye (sipokuwa mtoto ambae asilimia kubwa ya DNA yake ni yako na sio ya Baba yake anyway) na ndio iwe mwisho wa kuwasiliana nae.
Kisheria (Tz) hawezi kumchukua akaishi nae kwani umri wake ni chini ya Miaka Saba, akija kumchukua "kwalazima" au kwa nguvu atakuwa kafanya Kosa la kuiba Mtoto na unaweza kumfungulia mashitaka.
Na hata kama Mtoto akifikisha Miaka Saba sio lazima aende kwa Baba yake hasa kama wewe huna matatizo (ugonjwa) na unauwezo wa kumtunza mwenyewe.
Kubali kosa ulilolifanya na kusababisha Mimba na sasa ni Mtoto.....hakikisha hurudii tena kosa hilo.
Ni muhimu kutumia Kinga kwa kila tendo ili kuepuka Mimba na Mgonjwa ya Zinaa kwa faida yako na Mwanao pale utakapokuwa tayari kuanza Mahusiano ya Kimapenzi tena.
Jipe muda wa kutosha kupona na kukuza mwanao kabla hujaanza tena kutoka na Mwanaume mwingine.
Mtoto akikua na akitaka basi atamtafuta baba yake. Usimjaze mtoto maneno mabaya kuhusu baba yake. Akifikia umri wa kuelewa na kuanza kuhoji "kwanini baba hakai nasisi?", "Kwanini fulani ana baba mimi sina?" mueleze ukweli.
Uamuzi ni wake kumchukia Baba yake kwa kitendo chake(naturally kwa kuanzia atamchukia) au kumpenda na kumheshimu kwa kuwa sehemu yake.....Usilazimishe au kuhamishia Chuki yako juu ya Ex kwa mtoto.
Kila la kheri.
Mapendo tele kwako...
Comments