Kiburi na dharau ya Mke...

Habari dada Dinah, hongera kwa majukumu. Mimi ni kijana wa miaka 36 nimeoa na nina watoto wawili.

Wakati naoa dada Dinah nilifurahia sana maisha yangu ya ndoa lakini sasa dunia
imenigeuka, sifurahii hata chemba ndoa yangu.

Tatizo lilianza hivi; mwanzo mke wangu hakuwa Mtumishi wa Serikali hivyo niliamua kumsomesha Sekondari. Baada tu ya kupata kazi alibadilika na kusahau majukumu yake kama Mke.


Kwani inafikia mahali anadai hivi sasa
simbabaishi kwani anamshahara na kazi yake. Sasa Dinah najiuliza je ndoa
zote za Watumishi ndivyo zilivyo au ni hii ya kwangu tu?

Nifanye nini kunusuru ndoa yangu maana nahurumia watoto wangu kwani first born wangu ana miaka 9 tu.Sitaki kushutumu upande mmoja tu pengine hata mimi nina mapungufu lakini nimejaribu kushauriana nae lakini amejawa jeuri na
dharau.


Naomba ushauri wako dada.


********************


Dinah anasema: Hakika nahitaji Hongera ya majukumu maana sio lelemama. Ahsante sana kwa ushirikiano.

Hapana! Sio wanawake wote wanaofanya kazi nje ya nyumbani huwa wajeuri na wenye dharau.

Nadhani uoga wa mwanaume kuwa na mke anaejitegemea kiuchumi na mwenye sauti kwenye maamuzi muhimu kwenye uhusiano humfanya adhani kuwa mkewe ni mjeuri au hamheshimu tena.

Ila mwenzangu maelezo yako yamekaa kibinafsi mno utadhani Mkeo hausiki kwenye Ndoa hiyo, "ndoa yangu"....."Watoto wangu", "first born wangu"....umajaa Umimi ambao unaweza kuwa tatizo kutoka upande wako, jaribu "Ndoa yetu", "Watoto wetu" "firstborn wetu".

Kwaharaka haraka ningesema kuwa tatizo la mkeo ni...ULIMBUKENI. Lakini kutokana na maelezo yako umesema kuwa "anadai sasa hivi humbabaishi kwani anakazi na mshahara wake"......

Hiyo inaonyesha kuwa umewahi kumbabaisha au hata kumnyanyasa kwa vile hakuwa na kipato. Hebu rejea huko nyuma na uangalie matendo yako dhidi yake yalivyokuwa.

Wakati mwingine binadamu tunafanya mambo bila kujua au kutilia maanani kwavile ni madogo (not big deal kwetu) na wenza wetu wakikaa kimya basi ndio limepita hilo(hujui kama ulikosea).

Ukweli ni kuwa huwa yanabaki kwa muda mrefu mpaka mwenza wako atakapo pata namna ya kuliweka mezani ili lizungumzwe na hapo umuhimu wa mawasiliano hujitokeza kwenye uhusiano.

Nirudi kwake sasa; Wanawake wengi wameaminishwa vibaya kuhusu suala la "Usawa" na "kujitegemea" kiuchumi na mkeo ni mmoja kati ya hao wakimama.


Wanawake wengi wanachukulia Mwanaume ni "chombo" kiuchumi na watafanya lolote ili wanaumr waendelee kukidhi mahitaji yao kiuchumi.


Sasa wanawake wa aina hiyo wakifanikiwa kiuchumi inakuwa ni "kulipiza kisasi" kwa wanaume. Badala ya kutumia kipato chao kama sehemu ya umoja kwenye muungano husika(ndoa).

Hali huwa mbaya kama wanaume wamewahi kuwanyanyasa kiuchumi na kuwasimanga kuwa wao ni mama wa nyumbani tu (actually umama wa nyumbani ni kazi, tena ngumu kuliko kwenda ofisini kila siku).

Kaa na mkeo chini na mzungumze sio umwambie au kusema bali kuzungumza.....unaweka hofu zako na kero unazohisi na yeye anaweka zake kisha kwa pamoja mnakubaliana ni hatua gani mzifanye ili kubadilika na kuokoa ndoa yenu.


Umegusia kuwa hafanyi majukumu yake kama Mke.....unamaana Usafi, kupika, kuangalia watoto wakati wewe upo kazini?


Hayo ni majukumu ya "mke" ikiwa tu mkeo ni Mama wa nyumbani (haendi ofisini, anafanya kazi nyumbani).....lakini kwa vile wote mnafanya kazi 'majukumu ya Mke" yanakuwa yenu....mnashirikiana/saidiana.


Ikiwa wewe unachoka na yeye pia akifika nyumbani anakuwa kachoka, huoni ni sahihi kusaidiana au kukubaliana na kuweka Msaidizi.


Kumbuka kuomba radhi kwa makosa ambayo pengine hujawahi kuyafanya (unadhani haikuwa makosa) na hakikisha unasisitiza suala la hisia, usalama na furaha ya Watoto wenu mtakapokuwa mkizungumza.

Kila la kheri.
Mapendo tele kwako...

Comments