Nilishawahi kuomba ushauri zaidi mara mbili na nilishauriwa vizuri nakutatua matatizo
yangu. Leo nimekuja tena kuomba ushauri katika haya yanayo nisumbua . Ninaishi na mchumba wangu ambaye ndio baba wa mtoto wangu huu ni mwaka wa pili sasa.
Nilikuwa nampenda sana ila sasa mapenzi yameisha kwani nina wasiwasi kuwa yeye hanipendi kutokana na vitendo vyake na pia hana samahani, hana pole, wala nakupenda tena wakati mwingine akikosa yeye atanigeuzia kibao mimi ndio niombe samahani.
Kwa mfano siku moja alilala nje ya nyumbani kwetu, aliporudi asubuhi sikumuuliza kitu nikakaa kimya, yeye alikwenda moja kwa moja kitandani kulala kwani ilikua 11 asubuhi na mimi kwakua usiku sikulala nikiwaza kapatwa na balaa gani nikarudi kulala, baada ya nusu saa hivi akaniambia oh kazini kulitokea wizi kwa hiyo haikuwezekana kuondoka.
Nikamuuliza mbona hujanitumia hata sms kua kuna tatizo limetokea unanipenda kweli?
akajibu "sikupendi! kwani nimekuletea mwanamke hapa ndani?akaniambia tena ndugu yako amewekwa ndani na kwakuwa ilikua Jumamosi hamna dhamana nika mwambia basi naenda kumuona huko nitaujua ukweli. Cha ajabu alikuja juu na kunikataza nisitoke nyumbani siku ile hata kwenda dukani hakutaka niende.
Dinah anasema: Kosa kubwa ulilofanya ni kukaa kimya, hii inaonyesha kuwa unamuogopa jamaa na yeye anajua kuwa unamuogopa na hivyo kuwa huru kufanya atakalo akiwa na uhakika hutosema kitu.
Tunapokuwa kwenye uhusiano na mnaishai pamoja technically mnakuwa mnaendesha maisha kama wanandoa hivyo kila mmoja wenu anakuwa na haki ya kuhoji mabadiliko yeyote yanayojitokeza Mf: uchelewaji, unajua muda wake ambao huwa narudi nyumbani sasa siku akichelewa kurudi katika hali halisi unapaswa kuhoji kwanini amechelewa au yuko wapi kwani muda umepita.
Aliporudi asubuhi yake, ulitakiwa kuhoji kilichomfanya alale nje na ungemwambia kabisa unataka maelezo ya kutosha na kuridhisha kwani kitendo chake kimekufanya ushindwe kulala kwa hofu, wasiwasi wa hali ya juu....sio kusema "kama kunatatizo ungeni sms".....alafu unaishia kuuliza "unanipenda kweli?".
Maelezo aliyokupa hakika hayaridhishi au niseme sio sababu ya kutosha ya kumfanya mwanaume mwenye familia na mwenye kujali kushindwa kuwasiliana na mpenzi wake na kumpa taarifa, kwa kifupi huyo mwanaume hana heshima juu yako na wala hajali hisia zako.
*********************************************************************
Siku nyingine tena nilituniwa sms na mwanamke akaniambia "hivi unajijua kua wewe ni bi mdogo tupo tulio anza?" nikamuuliza wewe nani? akajibu "siongei na mbwa naongea na mwenye kufuga mbwa", nikamwambia samahani maana inaonekana mimi ndio kikwazo cha wao kuwa pamoja akajibu "tuko pamoja wewe tu ndio ulikuwa hujui ila sasa umejua naona utapata presha".
Kwakuwa ile namba nilikua naijua toka mwanzo ni mdada ambaye tulikua tunakaa naye jirani ila alishahama nikaacha na naye, mume wangu aliporudi nilimuuliza na kumpa zile sms lakini cha ajabu aligeuka na kuniambia "hamuwezi kuniita mbwa kesho utaniambia vizuri la sivyo nitajiua au nitakuua nikafie jela" niliumia sana haijawahii kutokea.
Tangu siku ile sina tena wivu naye hata kidogo yaani hata akiamua kualala na mwanamke mbele ya macho yangu roho haini umi tena, niko hapa kwa sababu ya mwanangu kwani nampenda sana na sitaki ajeteswa na mama wa kambo.
Dinah anasema: Huna wivu kwa vile hakuna hisia za mapenzi juu ya mwanaume huyo, unajua wivu hujitokeza ikiwa kuna hisia kali za kimapenzi, sasa kama hakuna hisia za kimapenzi wivu utatoka wapi?
**************************************************************************
Imefikia mahali sasa kutoamini mwanaume hata siku moja, labda ashuke toka mbinguni lakini aliye zaliwa na mwanamke hapa Duniani sito thubutu kutoa moyo wangu tena. Huyu ndio aliye niingiza katika ulimwengu wa mapenzi nikamwamini sana lakini kwa sasa
nimemchukia zaidi ya upendo niliokua nao mwanzo.
Naomba mnisaidie ushauri je! niendelee kuishi na huyu mwanaume au ni toke nduki? Maana ninao uwezo mkubwa tu wa kumlea mwanangu bila baba yeke na kumove on with life all alone na sitopenda tena. Lakini nikiondoka mwanangu itakuaje maana sitaki kumuacha kwa kwa baba yake.
Dinah anasema: Huyu mwanaume aliekutambulisha kwenye Ulimwengu wa mapenzi ameumiza hisia zako vibaya mno na ndio maana umepoteza imani kwa wanaume kwa kunadhani kuwa wanaume wote wako hivyo, ukweli ni kuwa sio wote wanatabia za kishamba n akibinafsi. Wapo wanaume wametulia sana kiakili na wanajua kuthamini na kuheshimu wanawake.
Hamjafunga ndoa na huna hisia za kimapenzi juu ya huyu jamaa kutokanana vitendo vyake viovu hakika hakuna cha kupigania hapo ili ndoa isimame Imara! Nakubaliana na wewe kwenye kutoka nduki, tena wala usiangalie nyuma.
Kumbuka kuwa kuzaa sio uzee, wewe ni binti mdogo sana (nadhani unaona kina mama wa miaka 45-60 wanavyolazimisha ujana) sasa imagine wangekuwa na umri wako wa miaka 25? Tunza mtoto wako lakini kumbuka kuwa huyo ni baba wa mtoto wako na hivyo anatakiwa kuchangia matunzo ya mtoto wake na ana haki ya kumuona mtoto au mtoto kumuona baba yake. Hakikisha tofauti zenu zisisababishe mtoto kutomjua baba yake.
*****************************************************************************
Angalizo tu ni kwamba sina ndoa na huyu mtu, ilikua tufunge ndoa lakini mwezi ule ambao tulipaswa tufunge ndoa mama yake alifariki dunia na ndoa ikaahirisha na mpaka sasa hakuna kilichoendelea .
Nilimpenda sana na anauhakika siwezi muacha kwani nilimpa moyo wangu wote nilimfanyia kila kitu alichotaka, nilimtreat kama mtoto akiumwa naomba ruhusa kazini namhandle kama katoto kachanga na mlisha namuogesha namuimbia nyimbo hadi analala.
Inauma jamani ukimpenda mtu alafu akaku dissapoint kiasi hiki, yaani kweli sito penda tena! mwanzo na mwisho kupenda mtu anaye vaaa suruali. Naona niishie hapo maana machozi yanani tiririka kwa uchungu nilio nao kazi njema dada yangu.
Nitafurahi kama niyapata msaada wenu wa mawazo.
Dinah nasema: Pole dada mdogo kwa machungu unayokabiliana nayo, wala usilie kwani huyo mwanaume hastahili machozi kutoka kwa binti mrembo, mwenye kujali, ujuae kupenda na kijana kama wewe. Nimetoa maelezo yangu kutokana na maelezo yako hapo juu.
Ngoja nikupe kisa changu kilichotokea years ago ambacho natumaini kitakusaidia kuelewa situation yako. Mimi nilipokuwa nakua na hata kufikia umri wako nilikuwa mpinzani mkuu wa suala la ndoa, lakini hayo yote yalibadilika baada ya kushawishiwa na kimapenzi.
Wiki mbili kabla ya kufunga ndoa kuna kisa cha kifamilia kikajitokeza, nilikasirika sana na nikaomba ndoa ife, kwamba sikutaka kuolewa tena. Mdogo wangu wakati huo alokuwa na umri kama wako akaniambia " Da' Dinah mshukuru Mungu kuwa Mkasa huu umejitokeza kabla hamjafunga ndoa, huenda ni onyo juu ya huyo mchumba wako".
Nikaendelea kuishi na yule Mjamaa (mchumba) niliekataa kuolewa nae kutokana na issues za kifamilia....then from nowhere jamaa akaanza kuwa abusive(Emotinally as in masimango, lawama zisizokuwa na mwanzo n.k).....ikabidi nitoke nduki bila kuangalia nyuma...Lol! Nikaanza maisha yangu upya kama Mimi kwa kuhama mjini, kubadili kazi namtindo wa maisha yangu na baada ya mwaka na nusu hivi nikakutana na huyu ambae ndio Mume wangu wa sasa ambae ni mwema.
Ninachojaribu kusema hapa ni kuwa kuna mambo Mungu huruhusu yajitokeze ili kutufumbua macho, sasa mama yake alipofariki ndio pazia lilifunguliwa ili wewe uone ukweli wa tabia ya mchumba wako. Imagine mngefungandoa then alafu akaamua kuendelea na tabia zake chafu? Ingekuwa ngumu na ingekuuma zaidi ya inavyokuuma hivi sasa......Mshukuru Mungu amekuonyesha tabia halisi ya Mpenzi wako ambae soon atakuwa Ex.
Natambua kuwa bado unahasira sana, lakini ukijitoa kwenye maisha ya kunyanyasaji kutoka kwa baba mtoto wako utakuwa huru na utapenda tena.
Ni matumaini yangu kuwa maelezo ya wachangiaji wengine na nyongeza ya kisa changu halisi yatasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya uamuzi wa busara na kuendelea na maisha yako.
Kila la kheri!
Comments
Unajua huyu jamaa yako kiukweli hana heshima wala adabu kwako. Hana moyo wa shukurani wala mapenzi ya kweli. Inauma sana na ni ngumu sana kuishi na kumpenda mtu wa namna hiyo.
Mimi nakushauri dada mapenzi ni kila kitu katika dunia hii, yanachukua sehemu kubwa sana ya maisha yetu, kama unakosa mapenzi ya dhati hata uwezo wako wa kufikiri, kutenda na hata kujiamini unapungua sana.
Mimi nakushauri, kaa na huyo mpenzi wako kwa upole bila jazba, uongee naye umweleze A-Z jinsi unavyofeel moyoni mwako na jinsi ulivyochoshwa na tabia yake, na kuwa unahisi huna mapenzi naye tena kwa kuwa yeye haonyeshi kukuheshimu wala kuthamini penzi adimu unalompa. Jitahidi tu bila jazba wala hasira zozote umwambie ukweli wako wote bila kubakisha hata chembe, then umwambia tu kuwa unatamani kung'atuka ktk huo ushusiano ili uendelee na maisha yako kwani dunia hii imeharibika, ukijifanya kuendelea kumwendekeza huyo mjinga mwishowe atakuja kukuua kabisa na ukimwi.
Mtoto siyo sababu kabisa ya wewe kuishi maisha ya utumwa ktk mapenzi, mwishowe utapata ukimwi na mtoto utamwacha. Achana naye huyo mjinga songa mbele na maisha yako. Hivi ni kwa nini wanawake mnashindwa kujiamini hivyoo? Iweje mtu tu asiyejua thamani ya mapenzi wala kupendwa akunyanyashe kiasi hicho nawe unasifa zote?
Wewe anza zako mama, ila ondoa wazo wa kuwachukia wanaume wote, kwani wapo wengi waaminifu na wanaojua kupenda na kujua pia thamani ya mwanamke. Utampata mwingine atakayekupa penzi la kweli na kukusahaulisha machungu yote. Kuumizwa ni sehemu ya maisha mama, kila binadamu anapitia sema tu wengi hawapendi kuanika mambo yao hadharani la sivyo wewe ungejiona unanafuu sana.
Uwe na moyo mkuu na ujasiri, pigania maisha yako na ujiokoe kwenye domo la mambo, angalia ustaarabu mwingine, usikubali kuwa mtumwa wa mapenzi, utampa mwingine bora mara kumi zaidi yake.
Nakutakia kila la heri mama.
Kwanza dada nikupe pole, Pili amua moja kusuka au kunyoa,mapito uliyonayo sasa hayatofautiani sana na niliyopitia mie, Uamuzi wangu niliochukua kipindi hicho (miaka sita iliyopita) ni kunyoa na tena ni baada ya kupata ushauri kupitia kipindi kimoja hivi sikikumbuki lakini ni Clouds fm.
Nilihangaika na Mwanangu na sasa yupo STD 1 na Maisha yanaendelea kwani ni mwajiriwa. Alirudi kuomba msamaha tuyamalize lakini no siwezi, tena kachoka ile mbaya..
Kuhusu kuchukia wanaume hapo si dhani labda ni kwa sababu ya situation uliyonayo. Mie niliapa sitapenda,Mmmh ndugu usiusemee moyo, kupenda kupo tu.
Dada tuliza akili angalia uthamani wa maisha yako pili huyo mtoto. Mama wa kambo hawafai hata kidogo, kama ni mwenza utampata tu umri bado unaruhusu saaana tu,25yrs?!!!. Dada jipange tu kimaisha kwa ajili ya future ya mtoto.
Mdau Mwanza.
KWA SABABU YUPO ANAYEMUONA MBORA ZAIDI YAKO TOKA HAPO KAKAE MWENYEWE HUENDA ATAJIRUDI.
NA IKATOKEA AKARUDI KWAKO HAKIKISHA MNAKWENDA KUPIMA VINGINEVYO ANAWEZA KUKUPA GONJWA AMBALO HUKULISTAHILI
Asante na kila la heri!
Anonymous
aya kwa maradhi hasa UKIMWI,Kwa kif
upi mi nakushauri ufanye haraka san
a bila hata kuangalia nyuma na kuli
anzisha fasta kivyako tena hata kum
uaga maana ni NY*K* sana huyo mtu.
Mimi ni mwanaume, nimekasirika sana na vitendo vya huyo mchumba wako.Watu wanatafuta wanawake wenye moyo kama wako hawawapati,lakini huyu anachezea shillingi chooni.Zungumza naye akueleze kitu kulikoni!!
Nimechukia sana usemi wako wa kumchukia mwanaume anayevaa suruali.Wewe umetendwa na mwanaume mmoja tu hadi umefikia kuwalaumu wanaume wote?? Hujaona wenzio wanaoishi na wapenzi/waume zao kwa raha?Upumbavu wa huyo mcumba wako usiuingize kwa wanaume wote.Huyo si kipimo cha wanaume walioko duniani.Huo ni upuuzi wake tu kama walivyo wapuuzi wanawake wengine wanaowaletea shida waume/wapenzi wao.
Cha muhimu kupenda hakuna formula.Leo utasema hutapenda tena mwanaume lakini kesho utaingizwa mitini.Hapa nina maana kwamba hata wewe hukutumia akili na busara kukubali kubeba mimba ya mtu ambaye si mume wako.Kwa mantiki hiyo hata wewe nina wasiwasi nawe ni kwa jinsi gani umekosa uaminifu.Uliyavamia mapenzi kwa pupa mno na hadi leo unaonekana bado hujajifunza kitu.
Ni muhimu uwe na akili timamu na malengo unapoingia katika mahusiano na mwanaume.Ujue ni nini unataka katika mahusiano hayo usiingie tu kama kipofu na hatimaye unaanza kulaumu wanaume.
Kuhusu suala la mtoto sidhani kama ukiwa na huyo mwanaume ndio utamlea vema na hasa kama unapata hizo kashiokashi hata malezi yatakuwa hoi bin hoi.Ni afadhali uwe peke yako mtulivu bila bughudha kuliko una mtu anayekukondesha.Kimbia haraka.
wanaume wapo kwa ajili ya wanawake, na wanawake wapo kwa ajili ya wanaume.
huyo mtu usitake kukaa nae muongee mmesha fanya hivyo tayari huyo ni jeuri na jeuri yake ndo inamtia kiburi dada kimbia.
dada mimi tatizo langu ni moja tu dada'ngu.. UKIMWI. UKIMWI jamani tusiusahau jamani upo.. atakuleta magonjwa huyo alafu mkafa wote ndo na mtoto wako akapata tabu za milele tena.. bora umpe mwanao nafasi ya kuwa na mzazi mmoja ambae ni wewe kuliko mkafa wote akabaki bila hata mzazi.. tabia ya mumeo mwisho wake huwa ni mauti ya magonjwa na siyo ugonjwa mwingine bali UKIMWI..
sikutishi dada'ngu ila nakuambia ukweli kwa lugha kali ili uelewe kuwa swala lako ni zito mno zaidi ya hapo unapofikiria..
tafakari mapema chukua hatua.. KIMBIA HARAKA
Hakuna kitu kibaya kama kumpenda mtu asiyejua nini kitu mapenzi, mapenzi siku zote ni kipaji ambacho mtu anakuwa amezaliwa nayo na amelelewa nayo kwenye familia yao, kuna wale ambao kwenye familia aliyotokea hakuwahi kuona mapenzi kati ya wazazi wake kwa hiyo basi ninachotaka kukueleza ni kwamba jamaa inaonekana ni mmoja wao kwenye kundi la wasiojua nini kitu mapenzi na nini thamani yake.
Wewe ni mama na naelewa kuwa unampenda sana mtoto wako hivyo basi utafanya kile kilicho sahihi wewe una uwezo wa kumtunza mtoto wako basi hakuna haja ya kutaka kukaa na huyo mshkaji kisa mtoto wake sikutanii amka sasa kuliko kuja kuamka baadae ambapo utakuwa umechelewa achana na huyo mtu atakupa homa bure tafuta mtu mwenye uwezo wa kukupenda wewe na kukuthamini usitafute sababu kusema eti kisa mtoto wewe fanya kile ambacho kiko sahihi
Chakufanya
Mweke chini mshkaji mwambie wewe umeamua ni uendelee na maisha yako kabla hajakuua kwani nyie hamna ndoa rasmi sawa mdada? halafu hayupo mtu mwenye mapenzi ya dhati na mchumba wake alafu akatishia kukuua dah hapo hakuna mapenzi sasa ni heri umuache aendelee na huyo aliyenaye na wewe ujilelee mtoto wako mpaka akue na ikibidi baadaye uje umuonyeshe baba yake.
Kuna wanaume wengi sana duniani huwezi jua wewe tulia then utakuja kuona kama Mungu kakuwekea mumeo atakuja tu.
ni hayo 2
strawberry
kama unavyosema utoshindwa kumlea mtoto wako mwenyewe basi muda umefika... tafuta nyumba yako na uanze maisha yako na mwanao. yale mapenzi uliyokuwa unampa bwana ss mpe mtoto yote na wakati ukifiaka utapenda tena wanadamu tumeumwa kusamehe na kusahau yaliyopita.
Kila la heri mwanzo utakuwa mgumu lkn utafanikiwa ktk maisha yako na mwanao. ww sio mama wa kwanza kulea mtoto bila baba na wala utokuwa wa mwisho
Mi nakushauri tafuta namna nzuri ya kuachana nae kwani amesha kukutamkia kwamba anaweza akuue afie jela au mfe wote, watu wa namna hii ni kweli wanawena kuua anaroho ya kinyama,hatakama umemzoea achana nae,
Dadangu fanya mazungumzo nae ya kuachana na uchukue taadhari zinazofaa, ikiwezekana asiwe na taarifa zako zozote baada ya kuachan nae, kwani akijua una mume mwenye kukujali na unaependana nae atajisikia wivu kwa vile anayajua malovedavi yako. NASEMA KWA MSISITIZO ACHANA NAE ACHANA NAE TENA KWA RB YA POLISI
Mungu atakupa mume mwema wewe sali na kufunga kwa kumaanisha utaona atakvyokujibu kwa kishindo
TENA KAMA ULIKUWA HUJUI HIYO NDOA KUSITISHWA KUFUNGWA KWA SABABU YA MSIBA NI MPANGO WA MUNGU KWANI ANAKUPENDA NA ALIONA UKIOLEWA UTANYANYASIKA KWANI NDOA YA KIKISTO INGEKUWA NGUMU SANA KUVUNJIKA SASA BORA HIVI SASA HAMJAFUNGA NDOA HUNA SABABU YA KUENDELEA KUKALIA MOTO NARUDIA ONDOKA SANA KIMBIA ATAKUUA
Pole rafiki, kama ulivyoamua ondoka chukua mwwanao anza mbele, watoto wa mjini wanakwambia...chapa lapa fasta.
mwenzio nilifunga na ndoa na mtoto mmoja juu lakini nilichapa lapa fasta na sijaangalia nyuma na ukweli ni kwamba nilitia nguvu, juhudi na nia kwenye masomo na kwasasa namshukuru Mungu nina kazi nzuri mwanangu kakua na sina majeraha tena.
wanaume nawacheck kwa mbaaali, nacheka nao lakini moyoni nawaambia hamniumizi tena.