Mume hana uzazi, naombwa kumimbisha-Ushauri

"Mimi ni bosi nimeanzisha Kampuni yangu hivi karibuni. Kwenye Kampuni yangu nimeajiri wanawake wengi kuliko wanaume. Sifa ya kampuni yangu ni nidhamu na kweli wafanyakazi wote wanajiheshimu, kosa likitokea linaamuliwa kihekima.


Mimi ni mume wa mtu na ninaiheshimu sana ndoa yangu na hakuna kitu kinachoniuma kama kutoka nje ya ndoa, haya nayasikia mitaani na kwenye vyombo vya Habari. Watu wanasema tembea uone, Ishi na watu ujifunze na lisemwalo lipo kama halipo hujaliona tu bali linakuja.


Siku moja nikiwa Ofisini nikichambua CVs za wafanyakazi wangu na utendaji wao, hodi ilisikika mlangoni. Sio kawaida mida kama hiyo ya jioni kwa wafanyakazi kuja ofisini kwangu wengi wanakuwa wakifunga mahesabu yao tayari kuondoka.


"Bosi samahani sana, kama huna muda nitakuja siku nyingine, lakini hili tatizo nililo nalo halihitaji muda, kwani nimehangaika nikaona mtu pekee ninayeweza kumuamini ni wewe" alisema huyo mbisha hodi na alikuwa bado anaogopa huku akiwa kainama chini. "Ok, kaa hapo kwenye kiti nasema shida yako" Nilimwambia, huku nikijiuliza kichwani ni shida gani? kwani katika wafanyakazi ninaowaheshimu ni pamoja na huyu dada, umri wake ni miaka 34.


"Bosi naomba chonde chonde, hiki ninachokuambia kiwe mimi na wewe na naomba saana unikubalie, kwani usiponikubalia sidhani kama nitaweza kufanya kazi hapa tena, je nitakuangaliaje machoni, je nitaiwaka wapi sura yangu. Naomba usinielewe vibaya, mimi tangu nizaliwe sijawahi kutenda dhambi, sijawahi…" Alinyamaza nakuanza kulia.


Hali hii kidogo ilinishangaza, nakunifanya niache kazi yote niliyokuwa nikiifanya, nilimwangalia kwa makini huyu dada na kujaribu kufikiria tatizo analoweza kudiriki kuja kuniambia nikashindwa kuelewa.


"Naomba ujisikie amani, kwani nakuheshimu na moja ya kazi zangu ingawaje mimi ni bosi wenu, lakini pia ni kama mzazi, kaka, hata ukisema mume au vyovyote ilimradi haivunji hadhi, heshima ya kila mmoja wetu au sio? sasa ongea kama unaongea na mtu unayejisikia huru kuongea nae".


"Sikuhakikishii moja kwa moja kuwa ninaweza kulitatua tatizo lako, lakini nikilisikia kama lipo ndani ya uwezo wangu nitalitatua. lakini kama nikishidwa nitakuambia na halitatoka nje ya mimi na wewe kama unataka iwe hivyo, sasa uwe huru’’ nilitulia na kumwangalia.

"Bosi naogopa sana, na tangu tulizungumze mimi na mume wangu, nimekuwa sina raha, sio kwasababu limetusibu bali ni hizo njia za kulitatua ni nzito na sizipendi kama asivyozipenda mume wangu, lakini yeye sasa ameng’angania kuwa tufanye"


Akaanza kuelezea tatizo hilo, kuwa wao wameoana siku nyingi karibu ya miaka 16 sasa, katika mihangaiko yao wamechuma na wana hali nzuri kimaisha, kwani wana nyumba zaidi ya nne walizopangisha , wana magari ya biashara nk. Yeye alikuja kufanya kazi kwangu kwasababu alihitaji kupata ujuzi wa kuweza kufungua kampuni yao baadaye, alishanieleza hili kabla. Tatizo linalowakabili, tangu waoane hawajawahi kupata mtoto.


Awali walidhani mke ndiye mwenye matatizo, na jamii ilijaribu kuingilia kati ikashindwa kutokana na mapenzi waliyokuwa nayo. Baada ya miaka kwenda, waliamua kwenda kuwaona Wataalamu ili wajue tatizo ni nini.

Kila hospitali waliyokwenda waliambiwa kuwa "mume" ndiye mwenye matatizo. Na kweli katika kukumbuka, wakati wapo kwenye fungate walipata ajali, na mume wake aliumia maeneo ya mgongo, na kiunoni. Alitibiwa akapona na majombozi yalikuwa kama kawaida, lakini kumbe ile ajali iliharibu na mengine.


Binti yule aliendelea "hivi karibuni mume wangu amesema anahitaji mtoto, lakini hataki wa kurithi anataka azaliwe na mimi na anataka isijulikane kuwa anatatizo. Kwahiyo wazo lake ni mimi nimtafute mume anayefanana nae, mwenye heshima na anayejua kutunza siri na ambaye hataweza kwa vyovyote kuleta fujo hatiamaye" alimiliza kwa uchungu.


"Masharti yake mengine ni kuwa, yeye hataki kumjua huyo mume nitakayetembea naye na asijue nini kinachoendelea. Pili huyo mume akubali na ajue kuwa yeye ameridhia, kwa masharti kuwa iwe siri, pia mke wa huyo mume asijue", alimaliza binti yule.


Jasho lilinitoka, nikatamani kumfukuza huyu dada, lakini niliheshimu wadhifa wangu na kweli nilibadilika kwani yule dada aliponiona nilivyobadilika alianza kutetemeka kwa woga. Nilichoweza kumwambia ni kuwa anipe muda nifikirie kwanza mimi sio Mungu kuwa natoa watoto. Pili nitahakikishaje aliyoyasema ni kweli? tatu, hilo linavunja miiko ya ndoa yangu.


Alivyoondoka pale nilimuonea huruma, kwani nahisi alijuta kuniambia. licha ya kumpa matumaini ya kuwa asijali azidi kuja kazini, na nitajitahidi kusaidiana naye kulitafutia ufumbuzi.

Je dada Dinah na wengine mwasemaje, naomba busara zenu!
emu-three"

Comments

Anonymous said…
Sasa jamani bwana kaka mbona ushatoa siri, hao wausika kama wakisoma hapa si wanweza wakaunganisha matukio jamani.
Anonymous said…
Hakuna kitu kama hicho humu duniani eti mume hapati mtoto kisha aagize utafute mwanaume anayefanana nae. Jamani hii ni hatari ipo siku tu tatizo litatokea tena kubwa la kuweza hata kutoana roho hilo jambo siyo rahisi kama ambavyo unavyolifikiria. Tafadhali chunga ndoa yako achana na mambo ya hadithi za vitabuni au ya kwenye filamu. Na mama nae achunge ndoa yake. Akitaka kuzaa atoke kwenye hiyo ndoa kwanza ndipo aamue kuzaa.
Anonymous said…
kwanza kabisa huyu dada pole zake ila mungu atamsadia pili huyu boss kwa maoni yangu na kwa mujibu wa dinizote hiyo ni zambi kumbwa kwa muumba kamwe asifanye hivyo na pili huyu dada maelezo yake ni mazuri ila aspende kuweka wazi kila kitu ipo siku yatamrudi mimi yeye dada hata kama angekuwa na nia na jambo la mtoto angefanya vishawishi vyake kwa akili na upeo wake ila lengo libaki kuwa siri yake ili afanikinishe lakini sisi waume hatuna siri kihivyo.pole dada japo kwetu uswazi mambo ya kawaida kitanda hakizai haramu na ua ni siri bila mama kumwambia muhusika nini alikitaji kwake.dada Dinah salam sana ubalikiwe
Anonymous said…
Jamani hakuna mwanaume au mwanamke yeyote awaye katika dunia hii ambaye anaweza kufanya kitendo kama hicho. Bwana kaa na ndoa yako na we mama kaa na ndoa yako. Hii ni kwamba ipo siku utakuja kudai tu mtoto wako hata iweje!!!! Naomba tuache mambo ya hadithi za vitabuni na magazetini kama siyo filamu. Ni kitu hakiwezekani kabisa. We bosi heshimu ndoa yako na usithubutu kufanya kitu kama hicho utauwawa siku si zako!!!
Anonymous said…
Kama wanauwezo wa kifedha sio lazima mwanamke alale na mwanaume wa pembeni. Kuna njia mbadala huku kwenye nchi zilizoendela.In vitro fertilisation (IVF) is a process by which egg cells are fertilized by sperm outside the womb. Hii ni njia common sana hapa US, lakini naamini kuna nchi nyingi tuu ambazo zinafanya hii process.

Kuna njia nyingi tuu siku hizi ambazo sio lazima ulale na mtu.
ed
Simon Kitururu said…
Duh!Kazi kwelikweli!
Anonymous said…
Mimi sidhani kuwa pendekezo lake juu yako ndiyo suluhu ya shida yake na ya mumewe. Kama shida yao ni mtoto, basi ni vyema kwa wote wawili kufuata mtindo wa kupandikiza mbegu za uzazi za mtu mwengine, wasiyemjua wala asiyewajua, ambao mbegu zao za uume ziko kwenye baadhi ya hospitali mbali mbali. Wako watu ambao wamejitolea kutoa mbegu zao za uzazi, na kutoa maelezo kamili ya kihistoria na kibaologia juu yao, pasi na kutaja majina yao, ili mbegu hizo ziweze kutumiwa kupandikiza kwa mwanamke anayehitaji huduma hiyo kwa ridhaa yake na ya mume.

Utaratibu huo siyo tu utalinda na kuhifadhi imani yako ya kutotemea nje ya ndoa, bali pia utakulinda kwenda kinyume na mkeo; au kufanya tendo la ngono nje ya ndoa. Utawezaje kukaa na uwongo wa kumficha mkeo? Utaweza kumficha mkeo, sawa. Je, pia utamdanganya Mungu wako? Utadanganya hata moyo wako?

Zaidi kuna hatari ya tendo kama hilo. Huyo dada anaweza sana akaja kudai, siku za usoni, kwamba huyo mtoto ni wako na ulitembea naye na kwamba anaweza kuthibitisha kupitia DNA! Dunia hii ya leo, jiamini mwenyewe tu, hasa katika kujihusisha na jambo ambalo halina maadili au lina udanganyifu.

Huo ndio ushauri wangu.

Ebby
Anonymous said…
Kwa kuwa huyo dada anataka kuzaa ili kumpatia mume mtoto, hilo jambo ni la hatari sana kwa huyo bosi kwa sababu 1.Yeye bosi atajua kuwa huyo ni mtoto wake 2.kuna uwezekano baada ya kukutana kimwili uhusiano wao ukaendelea na kuleta shida kwenye kazi na familia zao 3.Huyo mwanaume anaweza kupatwa na wivu baadaye na kuanza kumsumbua huyo mtoto na hata mkewe (nadhani wakristo wanafahamu habari za Ibrahimu na Sara, Sara alimwambia Ibrahimu azae na mjakazi wake lakini baada ya mtoto kupatikana kukatokea chuki kubwa kwa Sara dhidi ya Mjakazi na Mtoto)5.Huyo bosi ana mke wake, si vema kuvunja ndoa yake kwa kutoa misaada nje ya ndoa, hili ni jambo baya sana 6.Pamoja na kuwa anasema mume wake anasema hataki kumjua atakayezaa naye, lakini inawezekana baada ya mtoto kuzaliwa akapatwa na uchungu akatafuta kumjua huyo mwanaume ni nani. 7.Ndugu wa pande zote mbili, mume na mke watajua tu kuwa huyo mtoto si wa ndani ya ndoa, hili litaleta kero nyingine kwenye ndoa. Baadhi ya ndugu wanaweza kufanya utafiti mpaka wakajua kuwa huyo mama amezaa na bosi wake, itakuwa kashfa kubwa kwa huyo bosi kuwa anatabia ya kutembea na wafanyakazi wake na ndiyo maana ameajiri wanawake wengi hapo ofisini kwake. Asidhani haitajulikana, itajulikana tu, hakuna siri na Mungu hawezi kudanganywa, huyo mtoto atafanana naye kama kamtapika vile, na itakuwa siyo siri tena. Hata heshimika tena kamwe!!!

Ushauri wangu ni kuwa huyo Bosi amkatalie katakata huyo mwanamke na wala asimuonee huruma, kwani huruma inapaswa isizidi uwezo. Kwanza hakuna ushahidi kuwa mume wake ndiye kamtuma, inawezekana kayaanzisha mwenyewe tu akimsingizia mumewe.

Ninavyojua mimi wanaume wana wivu sana, hawawezi kuvumilia kuona mume mwingine akivinjari na mkewe. Sasa linapokuja suala la kuzaa mtoto, yaani akae akilea huku akijua kuwa kuna jamaa anamlelea, mimi najua si rahisi kwa wanaume kulikubali hili. Kama hivyo ndivyo, basi huyo mume ndiye angeenda kumtafuta mume wa kuzaa na mkewe na si mke kujitafutia, kuna walakini sana hapa.

Tena inapaswa amuondoe kazini kwasababu kubaki kwake pale kazini kutaendelea kuleta matatizo. Kwa kuwa hana shida ya maisha, halitakuwa jambo baya sana, lakini hata kama lingekuwa baya, basi ni kwa usalama wa watu wengine na kazi zao. Matatizo yake yasiharibu ndoa za watu wengie, huyo analeta kifo kwenye ndoa ya bosi wake.

Kwa kuwa wana uwezo wa kifedha, mimi nadhani kama kweli wanahitaji mtoto, basi watafute njia za kisasa ambazo hazitahusisha kukutana kimwili na mwanaume mwingine wala hata kumjua, wanaweza kwenda hospitali wakajinunulia mbegu za kiume wakazaa mtoto ambaye wala hawatakuwa wakimjua baba yake.

Najua tatizo wanaogopa asije akawa mzungu, lakini ni afadhari awe mzungu kuliko kuhamishia matatizo yao kwa watu wengine. Njia rahisi zaidi ni kuafuta mtoto wa kumlea na kumfanya wao, kwanza si ajabu kuwa wao hawana mtoto, kwani ni wanandoa wangapi hawana watoto?

Narudia tena, huyo bosi asithubutu hata siku moja kutembea na huyo mwanamke iwe kwa msaada au huruma, aache kabisa, anaweza akashangaa anaambukizwa UKIMWI huku akitoa msaada.

Jambo lingine ni kuwa amshirikishe mkewe, amweleze juu ya tukio hilo ili mke naye ajue asaidie kumchunga, MKE SI NDIYE MWENYE MALI? Zaidi ya yote, anatakiwa kuogopa dhambi, kutembea nje ya ndoa ni dhambi na kutembea na mke wa mtu ni dhambi pia. Ndoa inapaswa kuheshimiwa na wati wote.
Anonymous said…
Akumbuke kuwa wanawake ni wajanja sana wakimtaka mwanaume, inawezekana huyo mama alishaanza kuonyesha dalili za kumpenda lakini yeye hakugundua ndipo akaona amtokee tu huku akilia, kulia si tatizo kwa mwanamke, anaweza akalia wakati wowote ule.

Vile vile inawezekana ni mpango umesukwa na wafanyakazi wake kutokana na kuwa na wafanyakazi wengi wanawake (si vibaya kuwa na wafanyakazi wengi wanawake) na kutokana na msimamo wake wa kuheshimu kazi na kutojihusisha na mapenzi. Atashangaa akishatembea na huyo atakuaj mwingine akimtaka na kusema mbona umetembea na fulani, na kama hutaki kutembea na mimi basi nitamwambia mkeo, itakuwa vita sana kwake awe mwangalifu, asiwaamini wanawake amwamini mke wake tu.

Namshauri aangalie sana asije akaenda na maji. WEMA NA HURUMA VISIZIDI UWEZO na HILI SASA LIKO JUU YA UWEZO WAKE. Amwambie huyo mwanamke akaombe ruhusa kwa mkewe (mke wa bosi) maana ndiye mwenye mali, na hata kama ruhusa itatolewa, bado hilo jambo asilifanye, huo ndio utakuwa mwisho wake.

Siku njema
Anonymous said…
hii ngumu
Anonymous said…
huyu dada kama kweli anahitaji mtoto akawekewe mbegu hospital,lkn kutembea na bosi, bosi atajishushia heshima.Huyo dada amejaribu sababu ni tabia ya mabosi kutembea na wafanyakazi wao. ushauri bosi akatae liko nje ya uwezo wake.
Anaweza akaonja asali halafu ashindwe kutoka
Anonymous said…
Kwani jamani bongo kuna utaratibu wa kudonate mbegu za kiume? Na kama upo ni hospitali gani wanafanya hivyo?
Anonymous said…
pole sana Boss wala usithubutu kutenda kitendo kama hicho...na ww dada nendeni kamapala au nairobi kuna hospital huko ukawekewe mbegu za usiyemjua..usilete hadithi Boss wako unataka kumharibia ndoa yake.ukishindwa kabisa kwa akili za kibinadamu na kitabibu yupo YESU MWANAMUME ASIYESHINDWA, HUYO2 MUMEO ATAOMBEWA NA MAMBO YATAKUWA SWAFI ATAKUMIMBISHA TENA UTAJIFUNGUA MAPACHA MARA MBILI.NENDENI KWENYE MAKISA YA KIROHO MAHALI PA ISHARA NA MAAJABU WINNERS CHAPEL
Anonymous said…
we mwanamke gani ambaye umekosa maarifa! mwanamke mjanja kama kweli anatafuta mtoto wala asingemwambia huyo bosi wake, angeweza kumpata huyo bosi na kumtegeshea mimba iingie bila bosi kujua. Hakuna siri ya watu wawili sembuse watu watatu!! kuna siku bosi atataka mtoto wake tu!
Anonymous said…
wewe bosi upewe nini tena? ama kweli kwenye miti hakuna wajenzi
Anonymous said…
Du pole sana, manake nilikuwa nasoma marejeo, ili namimi niwe mwanachama, hii hapa imenivutia, kwasababu nahisi hili tukio nalijua, mmmh, ngoja nisiropoke, manake, siku hizi hakuna siri