Tuesday, 12 August 2014

Mume kapitiliza kwa Kudeka!

Natumaini wewe ni mzima wa afya na family yako pia. Nakushukuru kwa kazi nzuri unayoifanya ya kutuelimisha kwani tunapata vitu vingi sana vya kutujenga kutoka kwako. Ubarikiwe sana.
      


Mimi ni mwanamke wa miaka 25 sasa, Ni mara yangu ya pili kuomba ushauri kwako mara ya kwanza ulinipa ushauri mzuri sana na umenijenga vilivyo na ndio maana nimeamua nirudi tena kwa jambo jingine.


Nimeolewa na mwisho wa mwaka nitatimiza mwaka mmoja wa Ndoa. Mume wangu amenizidi sana kiumri kwani ana miaka 44.

Kutokana na umri wake kunipita watu wanaona nimeolewa na mwanaume aliyenizidi sana wananisema kichinichini nami nazipata habari zao.

Mume wangu mzuri ana mapenzi kwangu na ananiheshimu sana mimi pamoja na familia yangu. Ananipa matunzo vizuri  kwani sijafanikiwa kupata kazi bado na hiyo ni kutokana na kuishi mbali mimi na yeye kwa sababu nitakozokueleza.

Mume wangu na familia yake wanakaa nje ya nchi(Marekani)  ila ni Watanzania waliondoka kitambo kidogo baada ya baba yake kupata uamisho wa kikazi. Aliondoka akiwa mdogo hivyo ana miaka zaidi ya thelathini anaishi huko hivyo ana tabia za kizungu na mambo yake kama wazungu.

Alikuja Tanzania tukakutana tukapendana tukafikia uamuzi wa kuoana. Wazazi wake walikuja ikawa harusi nzuri kweli. Ila mimi bado nipo Tanzania kaniacha huku tukishughulikia mambo ya Visa, ikitick niende.


Anajitahidi kuja mara tatu kwa mwaka  akipata likizo tu anakuja kwani anafanya kazi huko. Mume wangu bado anakaa na wazazi wake huko.

Nawapenda sana wakwe zangu ni watu wazuri, ila kuna tabia siipendi kutoka kwa mume wangu ni mtu flani anapenda kuwataja taja Baba na Mama yake muda mwingi yaani anawataja mno kama mtoto mdogo.

Haiwezi kupita siku bila kuwataja baba yake na mama yake hadi kwenye chakula anacompare akimaanisha cha mama yake kitamu kuliko tunachopika sisi.
      

Muda mwingine tupo na watu tunapiga story yaani lazima atafute sehemu achomekee kitu kuhusu baba na mama yake kama mtoto mdogo na huku kiumri ni mkubwa. Sasa sijui ni sababu ya kukaa na wazazi wake mpaka umri huu.

Nawapenda sana wazazi wake lakini kwa hili sipendi, naona anazidi mpaka sometimes naona kama angeendelea tu kukaa na wazazi wake maana kukaa na mke hakumfai.


Yaani hata akija Tanzania akiongea na wazazi wake kwa simu akimaliza atasema nimewamiss sana wazazi wangu mpaka namuhesabiaga siku ziishe aondoke aende kwa wazazi wake mie nibaki zangu peke yangu.


Unakuta roho hainiumi yeye akiondoka maana naona anapapenda huko zaidi. Kuna muda natamani nisipate Visa mapema maana nikienda huko nitajisikia vibaya zaidi.


Naomba ushauri wako dada yangu kama ni kawaida na nifanyaje ili nizoee hii hali maana naona kama naanza kumchukia na kumuona kama anadeka yaani upendo unaisha kabisa.


Na kumwambia siwezi maana sitaki kuingilia chochote na familia yake. Ahsante sana.
    


**********


Dinah anasema: Mie na familia yangu afya tele, mbio-mbio tu. Ahasnte kwa kujali na shukurani kwa ushirikiano.


Unajua kila Binadamu anamapungufu yake (kasoro), kuna mapungufu ya kimwili (nje au ndani), kitabia, n.k.....Baadhi ya mapungufu huonekana na mengine hayaonekani(utayaona ukianza kuishi na mhusika).

Unapompenda mtu kwa penzi la kweli, mapungufu hayo huwa hayaonekani.....yapo lakini penzi linayaziba hivyo unamchukulia Mpenzi wako kama alivyo.

Unapoyaona mapungufu hayo na ukahisi hayakupendezi na ukahisi unaweza kumsaidia mwenza wako kuacha au "kupona" basi unajitahidi na kujitolea kumsaidia.

Inawezekana Mumeo alidekezwa sana na wazazi wake na hivyo kumfanya ashindwe kujiamini kufanya mambo peke yake kama Mwanaume na hivyo wazazi wakawa tegemezi kuu kwake.

Pia inategemea na alivyokua kimazingira, ujue mtoto kuhamia na kuishi Nchi za Magharibi unakumbana na mengi Hasi ambayo kwa kawaida watu waishio huko huwa hawayasemi na badala yake wanasema yale Chanya tu.

Sasa huwezijua Mumeo alipitia nini Miaka yote 30na alipokuwa huko hali iliyomfanya ahisi kuwa Baba na Mama yake ndio kila kitu kwake(zaidi ya Wazazi).

Kingine ni kuwa Maisha ya Kimagharibi wakati mwingine yanaweza kuwa ni ya Upweke sana.....hasa kama umetoka kuishi "kiafrika" halafu ukaenda mahali ambapo kila mtu anajifungia kwake (unaita kizungu, mie naita Kimagharibi), utajikuta Mnyonge na watu pekee ni wazazi wako na ndugu zako.

Nadhani hata wazazi wake wanatamani sana Mtoto wao aanze "kujitegemea" wakihofia siku wakifa basi Kijana wao anaweza kuwa Mwehu au hata kujiua na yeye.

Ni mumeo na mnapendana, sasa penye hasi weka Chanya na ujichukulie kuwa wewe ndio muongozo wake, chukulia wewe ndio utamsaidia aanze kujitegemea "kiakili" na "kisosho" (baadhi ya wanaume huchelewa ku-mature).

Anza kumuandaa taratibu kuwa ungependa kuishi mbali na wazazi ila tafuta namna ya kufikisha ujumbe wako ili asijisikie vibaya(usiumize hisia zake).

Unapozungumza nae kuhusu maisha yenu pamoja huko US, jaribu kumuuliza mtakaa wapi kama mke na Mume....akisema kwetu as in kwa Baba na Mama, uliza mtakaa hapo kwa muda gani kabla hamjatafuta kwenu?.

Kumbuka utafika US hautokuwa na Kazi hivyo itakubidi utafute kazi (kama una ujuzi tayari) ama urudi Shule kuongeza/kupata Ujuzi ili uweze kuajiriwa kirahisi huko US.....vinginevyo itakuwa rahisi kwenu kama Pea kujibanza kwao mpaka mtakapojiweka sawa kiuchumi.

Kukutumia senti za matumizi Tz inaweza kukufanya udhani jamaa anamahela....Tsh haina thamani hivyo Dola inalipa (ukibadilisha) lakini utakapokuwa huko US hali inaweza kubadilika kiasi, kwamba matumizi yatakuwa ghali....usilishau hili!


Akiuliza kwanini unahofia kuishi na wazazi wake nyumba Moja....Weka wazi kuwa haupo comfortable kuishi na Wakwe nyumba moja....weka sababu zako za ki-romantic zaidi na kwamba hautokuwa huru ku-romantic-a na yeye (Mumeo).


Wanaume wote wanapenda kufananisha/linganisha Wake zao na Mama zao kwenye Mapishi!

Ni wanawake waliowalea na kuwapikia maisha yao yote ya mwanzo hivyo huwachukua Muda mpaka waje kuzoea mapishi ya watu wengine.

Muhimu ni wewe kuongeza mautundu kwenye kupika na ataanza kusahau ya Mama yake na kusifia ya mkewe kwa Wifi zako (watanuna hao) na marafiki.

Nadhani maelezo haya yatasaidia kukupa mwanga na kutuliza hofu yako.


Kila la kheri.
Mapendo tele kwako...

1 comment:

Anonymous said...

Dina, Umemshauri vizuri sana huyu bibie. Nimekupendaje kwa ushauri mzuri sana!!!

Bibie,mimi niko US ba alichokueleza dada Dina ndivyo hivyooo kabisa.Kuwatjhataja wazazi ni kitu cha kawaida mno na huku unaoambatana nao masaa 24 kama hauko kazini ni wazazi tu. Hivyo usimwelewe vibaya huyo mumeo. Tena ushukuru anawataja wazazi, je angewataja wapenzi aliokuwa nao ingekuwaje?

Jiandae maisha ya huku utayaona vema,na pia hiyo nyumba ya wazazi wake inategemea imejengwaje, kuna nyumba ambazo ziivyojengwa ni kama mnagawana sehemu kiasi kwamba unaweza usionane na wakwe zako hata mwezi kama hutazunguka kuwasabahi.Muhimu ni kujua kuwa maisha ni kupanga, na kupanga ni kuchagua. Ukifika huku shati litakubana tu na utaona vema mbanane hapohapo hadi kitakapoeleweka. Na itachukuwa muda mrefu hata ukipata kazi bado utaona mambo ni mzegemzege tu.Fuata ushgauri wa Dina.Hata akitaja wazazi usiku kuchwa hakuna siku atahamishia penzi kwao hahahahahaa bado utabaki wewe kuwa mke na mpenzi wake mkuu.Muhimu ni jinsi wewe utakavyomuondoa na hayo mazoea ili mdomo wake uanze kukusemasema wewe. Karibu sana US.Yuko state gani bibie labda tunaweza kukusaidia zaidi.