Tuesday, 24 June 2014

Umekuja kunipenda au Kunitawala?

Dada dinah shikamoo
Mimi ni mfuatiliaji mzuri wa blog yako, nakupongeza kwa kazi nzuri na umekua msaada kwa wengi, Ubarikiwe.

Mimi ni binti/mama mwenye umri wa miaka 24 mhitimu wa chuo kikuu shahada ya kwanza na nina mtoto mzuri wa kiume mwenye mwaka 1 na nusu.

Dada nimeishi na baba wa mtoto wangu (hatuna ndoa ya Kidini wala ya Kanisani) kuanzia nikiwa Mjamzito mpaka sasa lakini ndani ya hicho kipindi sijawahi kuwa na furaha ya kweli kwa sababu nimegundua ni mwanaume Mgomvi, Mkatili (ameshanipiga na kuniumiza vibaya mara mbili na kutishia kuniua zaida ya mara 1) ana dharau (ananijibu ovyo hata mbele ya kadamnasi), hajali hisia zangu kila usiku anataka haki yake ya kufanya mapenzi hata kama anajua naumwa/nimechoka).

Ananipa conditions kwamba nitafute kazi Mkoa tunaoishi tu nikipata kazi nje ya Mkoa nichague mahusiano au kazi na isitoshe ndani ya Mkoa ananipangia sehemu za kuomba kazi.


Dada, ananikagua simu yangu kila akirudi kazini, ikiingia sms anataka kujua nani kaituma na nimemjibu vipi hata kama ni wazazi wangu au ndugu (nimekata mawasiliano na classmate wangu na hata marafiki zangu wa kike na wakiume lakini wapi kunikagua hakuishi). Kununa/kuzira kula nyumbani ni kawaida kwake!!

Dada nimechoka! mapenzi yangu kwake yanafifia na kufa kila kukicha. Ushauri please.

NB; Anamjali mtoto kwa kila kitu, lakini mimi nikiomba kitu (naomba sababu sina kazi kwa sasa) naishia kuahidiwa tu bila utekelezaji.


Shukrani kwa ushauri na naahidi nitaufanyia kazi.

************

Dinah anasema: Marhabaa Mrembo, shukurani kwa Ushirikiano wako.

Kwanza pole sana!! Katika umri mdogo unakabiliana na unyanywasaji wa Kijinsia, Kimwili, Kihisia, Kisaikolojia na Kiuchumi.

Kama ilivyo kwa wanawake wengi, pengine hata hujui kama Unanyanyaswa, wewe unadhani tu kuwa Jamaa anatabia mbaya.


Lakini kuja hapa na kuliweka wazi ni mwanzo mzuri na Hongera sana kwa ujasiri wako.

Kisheria (kama hawajabadilisha) ukikaa na mwanaume nyumba Moja kama Mume na kuzaa nae kwa jumla ya Miaka miwili au zaidi mnatambulika Kiserikali kama Mke na mume kwamba kukitokea mfarakano na Uhusiano kufa basi watoto/mtoto na Mama yao hupata Haki sawa kama mke na Watoto waliokuwa kwenye Ndoa.

Isingekuwa kukupiga na kukutishia kukutoa Uhai, ningekushauri uchukue mapumziko kutoka hapo ulipo na uende kwenu au kwa Ndugu yako wa karibu(tumbo Moja) unaemuamini ukapumzike.

Mapumziko hayo yangemfanya atafute sababu za kwanini umeondoka nyumbani na hapo ndio ungehusisha Wazazi wake na Wazazi wako na kuweka wazi sababu zako zote kama ulivyonieleza mimi, wao wangemonya na kumsihi abadilishe tabia.

Kwavile anakupiga, anakutishia uhai na anakuwekea vikwazo kwenye kutafuta Kazi ni wazi kabisa nitakushauri UKIMBIE, yaani achana nae (Naamini katika Wivu wa kuonyesha mapenzi lakini sio kutawalana) huyu Mwenza wako ANAKUTAWALA, huo sio Wivu, pia ni abuser....lazima ana issues kichwani.

Nenda kwenu bila kumuaga, alafu ukifika ndio umwambie via wazazi wako. Kama unahofu na fujo au ukatili wake kwa familia yako basi usimwambie ulipo.

Kapumzike na wakati upo huko anza kutafuta kazi....pia jaribu kutafuta Wanasheria Wanawake ambao huwa wanasaidia akina mama(wanawake) Kisheria wenye issue kama yako ya kunyanyaswa wenza wao.

Ukiwakosa hao basi nenda moja kwa moja Ustawi wa jamii ili wakushauri kuhusu nini cha kufanya Kisheria ili kulinda "mafao" ya mtoto wenu (ili aweze kuhudumiwa na Baba yake).


Waelezee unyanywasaji wote kama ulivyoweka kwenya mail yako, na wao watakusaidia.


Elimu inahitajika kwa wanawake ili tutambue tofauti ya Wivu wenye kivuli cha Unyanyaswaji (kupo kwa aina nyingi nitaweka topic nikipata wasaa) na Wivu wa Mapenzi.


Kila la kheri.
Mapendo tele kwako...

No comments: