Thursday, 26 April 2012

"Mambo Dinah, mimi ni mpenzi mkubwa wa hii blog yako, kwa mara ya kwanza nimeamua kukuandikia ili na mie nipate ushauri.


Mimi ni mwanamke wa miaka 27 nina mpenzi wangu ambae tumekua pamoja kwa muda miezi 3 sasa. Bado tunazidi kujuana na mungu akisaidia tutafunga ndoa hapo baadae kwani wote tupo tayari kwa hilo.


Kuna mambo yafuatayo anayafanya na mimi nakuwa simuelewi,

1-Anapenda sana kushinda kwa marafiki zake kwa ajili ya story kiasi kwamba anaweza asikujulie hali  siku nzima.

Dinah anasema: Kutokana na umri (nachukulia nae ni late 20s kama wewe) rafiki zake ni sehemu ya maisha yake, amekuwa nao kabla hajakutana na wewe.

Sasa kwavile ndio mmeanza kutoka kimapenzi na labda hajakutambulisha bado(anasubiri muda muafaka) inamuia vigumu kuchomoka na kukujulia hali.

Siku mkiwa pamoja mjulishe tu kuwa unafurahi sana ukipata ujumbe au simu kutoka kwake kabla siku haijaisha.

Taratibu atazoea tu.

2-Lazima mimi ndio nianze kumtafuta kwenye simu na akianza yeye ujue anataka kuomba umsaidie kitu.

Dinah anasema:
Hapa kuna mawili! Moja hajui umuhimu wa mawasiliano kwako(mjulishe), pili huenda nakosa uhuru wa kufanya hivyo kuepuka maswali kutoka kwa rafiki zake, kama nilivyosema hapo juu.


3-Ameanza tabia ya kuzima simu usiku kitu ambacho mwanzoni hakuwa akikifanya.

Dinah anasema: hili linaweza kusababishwa na Tanesco! Huenda anazima simu ili ku-save battery, ili kujua ukweli jaribu kumuuliza kwanini anazima simu usiku wakati wee unapenda kuongea nae kabla haujalala...kwa Mfano!


Dada na mengine mengi sana lakini nikiwa nae huwa anadai ananipenda sana na anataka mwakani tufunge ndoa, ila dada swali langu ni kweli ananipenda au ananipotezea muda tu?
Ni mimi Sab"

*****************************

Dinah anasema:
Asante kwa mail na salamu.
Miezi 3 ni hatua ya mwanzo kabisa na pengine sio vema kuita uhusiano mpaka angalau mtakapofikisha miezi 6.

Maelezo yako yanaonyesha kuwa unaharaka sana na pia hakuna mawasiliano ya kutosha, nikisema mawasiliano nina maanisha ninyi wawili kuzungumza kama wapenzi.

Inaelekea wewe tayari umejikita ama unaharaka ya kuwa kwenye uhusiano wakati mwenzako bado yupo kwenye hatua ya "anatoka na wewe" hachukulii kuwa ni uhusiano kamili.

Katika hali halisi kuwa na mtu ndani ya Miezi 3 ni mapema sana kuita "uhusiano" tunaanza kuita uhusiano baada ya miezi 3.

Huenda kweli anakupenda japokuwa wewe huamini kwa vile "kupendwa" kuna maana tofauti kwako.

Mf: kama mambo 3 uliyoweka wazi hapa yakitimizwa ndio unahisi kupendwa basi ni vema ukaliweka wazi hilo kwa mpenzi wako.

Ila kumbuka kuna baadhi ya wanaume hawajui kuelezea hisia zao, wanakupenda lakini hawajui wakuonyeshe vipi kimatendo.

Sasa ni muhimu sana kuwa wazi kwa mpenzi wako na kumueleza ni vitu gani akifanya kwa ajili yako unahisi kupenda au spesho.

Nenda taratibu usije ukamtisha na haraka zako, uhusiano haulazimishwi hutokea wenyewe tu jinsi siku zinavyokwenda...

Hebu tusikilize wengine wanasemaje....

Kila la kheri!!

------------------

Thursday, 12 April 2012

Safari ya Ughaibuni imebadili Mume wangu!

Habari za kazi dada Dinah, mimi nina matatizo na ndoa yangu niliyofunga mwaka 2009 mwezi 4 Kanisa la Romani Katoliki.


Mwaka 2010 nikapata post ya kwenda nje ya nchi kwa mkataba wa miaka 2 , baada ya kuondoka nilikuwa napata likizo ya siku 21 au wiki moja. Chakusikitisha tangu mwaka jana mume wangu alianza kubadilika.


Nikirudi likizo mara ananiambia nenda kwenu ukawatembelee. Naweza kukaa wiki nzima lakini anafanya sex na mimi mara 1 tu mpaka naondoka.


Mwaka jana mwezi wa kumi na mbili nilipata taarifa kuwa amezaa na mwanamke wa pale mtaani kwetu na mtoto anamiezi 3.


Mwezi wa kwanza tarehe 12 alikwenda kumtabulisha kwao kijijini pamoja na mtoto na pia hapo hapo ana mwanamke mwingine anamimba anakaribia kujifungua na hao wanawake wote huwa anawaleta pale kwenye nyumba kwetu wanalala kitandani kwangu!


Mimi nategemea kumaliza huu mkataba mwezi wa sita mwaka huu, nimejaribu kuongea na mume wangu na amenitamkia kuwa hanitaki tena.


Nimeongea na wazazi wake mpaka sasa sijapata jibu lolote, roho inaniuma sana kwani nilipokuja huku tulikubaliana vizuri.

Sasa hivi nikienda likizo anafunga chumba hataki nionane naye, nikipiga simu ananikatia,nikituma sms hajibu, naomba ushauri wako dada maji yamenifika shingoni dada.

****************************

Dinah anasema: Pole sana kwa matatizo unayokabiliana nayo. Sina hakika ni kitugani hasa kilipelekea ninyi wawili kufunga ndoa...kwani si ndoa zote zinafungwa chini ya misingi ya mapenzi...wapo wanafunga kwa ajili ya kuanzisha familia? Kurahisisha maisha(pesa), Umri, Mkumbo, kuondoa mkosi n.k


Kutokana na maelezo yako inaonyesha kuwa hamkuwa na muda wa kuzungumza au kuwasiliana kama pea na pengine hamkuweka au hamkuwa na nia/mipango inayofanana ya kimaisha hapo baadae.


Inaonyesha mumeo alitaka sana kuanza familia na wewe ulitaka career vyote ni vizuri na ni muhimu ila vimekutana wakati mbaya na labda kwavile hamkujadili haya mwanzoni kabisa mwa uhusiano wenu kabla ya ndoa.


Hongera kwa jitihada zako za kutaka kurudisha ndoa yako, hakika inauma lakini suala zito kama hili huwezi kulizungumza wakati wewe mwenyewe uko mbali.


Ni vema kuzungumza na mumeo na wakati huohuo kujaribu kuwasiliana na aliewafungisha ndoa Kanisani au wale waliowapa Semina kabla hamjafunga ndoa.


Natambua Ndoa za Kikatoliki zina hatua zake, basi ni vema ukijaribu kuzifuata mara utakaporejea nyumbani.


Umejaribu kuzungumza na wazazi wake ambao kwao kidogo inaweza kuwa ngumu kufanya chochote kwani hujui mtoto wao(mumeo) amekuzungumziaje kabla ya kutambulisha mwanamke mwingine na mtoto.

Muombe Mungu akutie nguvu kipindi hiki uko mbali kikazi lakini pia shukuru kuwa mumeo anakukwepa kwenye kufanya mapenzi...:uwezi jua anakuepusha mangapi.


Maneno yangu sio sheria, lakini nashindwa kujizuia kusema haya:-

Mwanaume aliekosa uaminifu kwa mkewe na kungonoka na wanawake ovyo na hata kuwapa ujauzito hafai kuwa Mume.


Unaweza kushawishika kupigania penzi lako na hata kushika mimba ili umpe mumeo mtoto so that ndoa iokolewe lakini baadae ikakuongezea matatizo zaidi.


Hatua mliyofikia sidhani kama kuna umuhimu wa "kupigania penzi" ni vema kuanza maisha yako upya.


Kisheria unaweza kumtaliki mumeo lakini Kikristo huwezi kufanya hivyo. Sasa kwasababu imani yako ya Dini inakataza Talaka haina maana uendelee kuishi mpweke ndani ya ndoa.

Tusikilize wengine watasemaje...
Pole na kila la kheri!!
------------------