Wednesday, 28 July 2010

Mume wangu aninyanyasa nakudai "mimba ikitoka utapata nyingine"...

"Mimi ni mama wa kitanzania ninaeishi na familia yangu UK, nimeolewa miaka 12 iliyopita na ndoa yetu imejaaliwa watoto wa wiwili na mwingine wa tatu yuko njiani. Mimi nilikuja UK kwa ajili ya masomo na kumuacha mpenzi wangu ambae sasa ndio mume wangu nyumbani Bongo.

Wakati naondoka tulikubaliana kuwa nikikaa kwa muda nimfanyie mpango ili na yeye aje huku kusoma, lakini kutokana na ugumu wa maisha kwangu kama mwanafunzi niliekuwa chini ya wazazi sikuweza kufanikisha hilo na yeye hakuwa na pesa za kutoshana kumleta huku. Basi tukaamua kusitisha suala la kusoma na kwavile tulikuwa tunapendana tukaamua kuwa yeye aje huku kama mwenza wangu na hivyo mimi nitaendelea na shule wakati yeye akifanya kazi ili kumudu maisha yetu.

Baada ya mimi kumaliza na kufanikiwa kupata kazi kwenye Bank na tukafunga ndoa mwaka uliofuata, maisha yakawa mazuri, mapenzi motomoto kama mke na mume na baada ya mwaka mmoja tangu tufunge ndoa nikajifungua mtoto wetu wa kwanza.

Baada ya kumaliza likizo ya uzazi mume wangu akaamua kuacha kazi bila sababu ya msingi, mimi haikunisumbua kwa vile kazi yangu ilitosha kutufanya tuishi maisha ya kawaida. Mtoto wa pili akaja, nikaamua kukaa chini na mume wangu ili tujadili maisha yetu ya mbeleni kwani familia inakua, mume wangu akaahidi kurudi kazini. Lakini hakufanya hivyo na sasa mtoto wa tatu yuko njiani.

Mume wangu amekuwa mvivu, hajali, hana umpendo na asie na ubinaadamu kabisa, natoka nyumbani asubuhi na mapema kwenda kazini, narudi jioni nikiwa nimechoka si unajua tena ujauzioto! nikifika nyumbani kitu pekee nahitaji ni kupumzika, lakini wakati napumzika utasikia mume wangu anauliza "leo hatuli humu ndani?" wakati yeye anatazama TV. Kwavile nakuwa nimechoka na sitaki ukorofi mwanamke nainuka naenda jikoni na kuanza kuandaa chochote cha haraka haraka ili nipate muda wa kupumzika.

Siku moja nikaamua kuzungumza na mume wangu na kumwambia jinsi ninavyojisikia kuhusiana na suala zima la ujauzito, masaa mengi kazini na kumuomba tusaidiane shughuli za ndani ili kuepusha matatizo kwangu na kwa mtoto alie tumboni.

Sikuamini masikio yangu pale mume wangu aliposema kuwa " wewe ni mwanamke wa kiafrika ni lazima uhakikishe nyumba safi, chakula kinapikwa na kuangalia watoto. Kwani kuwa na mimba ni ugonjwa? wangapi wanakuwa na mimba zinatoka na wanapona alafu wanashika nyingine na wanazaa? ikitoka hiyo utapata nyingine".

Dinah ghafla nikajisikia sina nguvu, nikanyanyuka taratibu bila kusema kitu nikaenda zangu kupumzika. Tangu siku hiyo nikaamua kuwa kila Juma Pili nitakuwa napika chakula/kuandaa chakula kingi kwa ajili ya wiki nzima ili watoto wangu na baba yao wasishinde njaa.

Sasa ndugu zangu nauliza hivi, kama hali imefikia hivi na watoto wetu hawajafikia umri mkubwa kuishi na mzazi mmoja nitakuwa nakosea kama nikimvumilia mpaka watoto wakuekue kidogo ndio nitafute ustaarabu wangu au nitengane nae sasa ili nisimpatie matatizo mtoto alie tumboni?.

Mimi binafsi hisia za mapenzi kwa mume wangu hazipo tangu aliponiambia kuwa mimba sio ugonjwa na mameno mengine yote, yaani namuona kama mtu tu pale asie na umuhimu wowote kwangu. Sina uhakika kama hali hii nikutokana na ujauzito, hasira au mapenzi yameisha?

naombeni msaada wenu wa kimawazo.

Mdau wa UK"

Tuesday, 13 July 2010

Ni mdada mwenye Elimu zaidi ya Mchumba, je haiwezi kuwa tatizo tukifunga ndoa?

"Dinah mdogo wangu, hujambo?
Mimi ni mama wa miaka 41, niliolewa na kukaa na ndoa kama miaka 10 hivi na kupata mtoto mmoja. Mwamaume yule akaanza vituko na hata akanza kulala nje yando ayetu. Nilivyoona karaha zimezidi nilimueleza kua nitahama nyumbani kwake lakini hakuonyesha kujali na wala hakunibembeleza ili nisihame.

Siku ya siku nikatafuta nyumba, nilipofanikiwa nikamueleza kuwa nimepata nyumba na nategemea kuhama, lakini hakuniomba nibaki. Nikajua hakua ananihitaji tena basi nikahama. Baada ya mda mfupi nikatafuta shule nikaenda nje ya nchi kusoma.

Huku nyuma yeye akafunga ndoa na yule hawara yake (sisi ni Waislam). Nikadai Talaka akaitoa bila ubishi. Nikaendelea na masomo na Mungu akanisaidia nikamaliza salama na sasa nimepata PHD yangu tayari.

Hivi sasa kuna wanaume wawili mamekuja wanataka kunioa, mmoja kaishia form two na mwengine form four, shida yangu ni kua viwango vyao vya elimu ni vidogo mno na ndio kitu pekee kinanipa hofu kuingia kwenye hayo makubaliano ya ndoa na mmoja wao, ingawa nahisi bado nahitaji kuwa na mume.

Naomba mnishauri wanablog, Jee mwanaume ukimzidi elimu sana na hata kipato haiwezi kuwa tatizo ndani ya familia? ili kuwe na amani ndani ya ndoa ya hivyo mtu ufanye nini? Nahitaji kufanya maamuzi kati ya mmoja wao. Nahitaji sana kuolewa kama Mungu akinibariki. asanteni wote".

Friday, 2 July 2010

Ex ananirudisha nyuma kihisia, nami nataka ndoa-Ushauri

"Dada Dinah na wasomaji wote, Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 22, nina mchumba wangu tunapendana sana na hivi karibuni tunatarajia kuoana.

Tatizo langu kubwa ni hivi, kabla ya huyu mchumba wangu nilikuwa na boyfriend ambaye nae mwanzo tulipendana sana ikaja kutokea hitilafu katika mapenzi yetu kwani alikuwa na mahusiano na mwanafunzi nje ya uhusiano wetu. Kabla ya kuchukua uamuzi nilijaribu kukaa nae nikamweleza ni jinsi gani naumia juu ya tabia yake aliyoianza.

Ilionyesha kuwa alinielewa na tukaendelea na mapenzi yetu kama kawaida, baada ya muda tena nikaja kuona sms ya yule yule mwanafunzi aliekuwa akitembea nae akimtaka aende kwake, kwakweli nilishindwa kuvumilia.

Nikaongea na Dada zake kwani yeye hana baba wala mama hao dada zake na kaka zake ndio walezi wake, japo kua mama yake mzazi amefariki hivi karibuni akiwa ananitambua kama mkwe wake mtarajiwa.

Dada zake walikaa Ex wangu na kuongea nae kwa kirefu zaidi, akawa kama ameelewa lakini baada ya mda mfupi mambo yakawa yale yale, basi dada zake wakaniambia kua wamejaribu kumuonya lakini hawaoni msimamo wake ni upi! Basi nikajitahidi kwenda nae hivyo hivyo, baadae nikachoka nikaamua kumwacha aendelee na mambo yake.

Sasa huyu Mchumba wangu ambaye nimeamini kuwa ananipenda labda aje abadilike hapo baadae nami nampenda pia lakini kila nikikutana nae njiani yule Ex ananiambia kua anaomba turudiane kwani amejifunza na amejua umuhimu wangu.

Anadai kila mwanamke atakae mpata anakuwa nae siku chache tu baada ya kugundua kua anamwanaume mwingine, na mimi nashindwa kumsahau kabisa na kila nimwonapo huyu Ex mwili wangu wote unasisimka.

Sijajua nifanye nini ili niweze kumsahau kabisa japokuwa alinitenda lakini nahisi kama kuna hisia zimebaki, naombeni ushauri wenu wadau japo kua najua wengine wataniponda hilo sinto jali zaidi nahitaji ushauri ili nijue njia ya kumsahau huyo Ex ili niweze kufunga ndoa kwa amani na Mchumba wangu wa sasa.

Asanteni
Mwanablog"

Dinah anasema: Hey asante sana kwa mail yako. Kutokana na maelezo yako inaelekea kuwa wewe umeingia kwenye uhusiano mpya muda mfupi tu baada ya kuachana na Ex wako hali inayosababishwa wewe kushindwa kuelewa hisia zako.

Ikiwa tayari umechumbiwa na mwanaume unaempenda na yeye anakupenda kwanini upoteze muda na huyo mwanaume ambae anakuja kwako kwa vile tu kila mwanamke anaekua nae anakuwa sijui na nini? Mwanaume anakuja kwako na kutaka mrudiane kwa vile anakupenda sio kwa vile wanawake wengine anaokua nao wanakuwa na tatizo fulani!!! hii ni sababu tosha ya wewe kuhama mtaa kabisa achilia mbali kubadili njia ili usikutane nae.

Nini cha kufanya ili umsahau Ex: Kama inawezekana basi hamisha makazi, ikiwa haiwezekani basi tafuta namna ya kumkwepa kama ulivyofanya mara tu baada ya kuachana. Hilo Mosi.

Pili, hakikisha unapotoka unakuwa na mchumba wako au mtu yeyote anaejua uchumba wenu kwa sababu za "kiusalama" kwamba jamaa likikuona na mtu mwingine halitopata nafasi ya kuongea nawe kuhusiana na hisia za kale.

Tatu, epuka kukaa mwenyewe kwani kunaweza kukufanya uanze kukumbuka yaliyopita, hakikisha akili yako inafanya kazi kila wakati kwa kufikiria mambo mengine muhimu kama vile kazi/masomo, maisha yako ya baadae na nini ungependa kufanya baada ya kuolewa, mipango ya ndoa yenu, aina gani ya gauni, rangi, ukumbi, wageni n.k.

Nne, jitahidi kuzungumza na mpenzi wako kwa njia ya simu kila siku kabla hujalala hii itasaidia kutokuwaza Ex, ukizungumza nampenzi wak kuhusu hisia zenu za kimapenzi na jinsi mnavyopendana ndio yatakayotawala akili yako mpaka utakapo pitiwa na usingizi.

Nakutakia kila la kheri kwenye kumsahau Ex na hatimae kufunga ndoa namchumba wako.