Wednesday, 30 June 2010

Mume kanitelekeza kisa Ndugu zake, Je nina ndoa au sina Ndoa?-Ushauri

"Pole na kazi Dada Dinah,
Mimi ni Mama wa watoto wawili, nilifunga ndoa 2004. Kwenye ndoa yetu ikatokea upande wa mume wangu hawajanikubali sana. Siku zilivyosonga mbele kukawa hakuna maelewano kabisa nyumbani kati yangu na mume wangu.

Mwaka 2008 December, Mume wangu akahama nyumbani na aliniachia mtoto ambae kwa wakati huo alikuwa bado ananyonya, nilijaribu sana kumbembeleza arudi nyumbani lakini sikufanikiwa, kwa sasa anaishi Arusha.

Mwaka 2009 July mtoto wetu mdogo aliumwa sana kiasi kwamba nilichanganyikiwa, nilimueleza baba yake ambae ni mume wangu alienikimbia lakini hakuja kabisa kumuona mtoto. Toka 2008 alivyoondoka mpaka leo amesha kuja kututembelea kama mara mbili tu kwa madai kuwa Dar na Arusha ni mbali sana, hivyo hawezi kuja mara kwa mara kwani huwa anachoka.

Mara chache anatuma zawadi kidogo za watoto. Na toka aondoke ameshatuma kama laki tatu hivi na watoto wote wanasoma sasa, hajui naishije na watoto wanakula nini, yaani kwa kifupi hana habari na watoto wake.

Sasa dada naomba ushauri wako, unaona hapo kuna ndoa tena?
Mimi ninafikiria nitafute makazi yangu nihamae na watoto wangu kwani ninapokaa ni kwake yaani ni nyumba yake.

Kama watoto wakimkumbuka sana baba yao huwa nawadanganya, ila huyu mkubwa (5yrs) naona ameanza kuelewa kwani akiniuliza huwa namwabia hali halisi namuona kama ananza kuelewa na anapata uchungu sana.

In short naona kuliko niendelee kuumia moyo wangu ni better ni give up, nianze maisha mapya, nifanye juu chini nisomeshe hawa watoto na nijihesabu kuwa ni single parent.
Unanishaurije?"

Dinah anasema:Pole sana kwa yote unayokabiliana nayo, inasikitisha kuwa mumeo amefuata matakwa ya wazazi wake na hivyo kukuoa na kisha kukuacha "solemba". Kwasababu tayari mmekwisha funga ndoa na bado of course mko kwenye ndoa kwa vile hakuna Talaka iliyotolewa na kwa mujibu wa Imani za Dini, wewe kama mkewe na mama wa watoto wake unahaki zote za kubaki kwenye nyumba hiyo. Hiyo nyumba ni yenu na sio yake.

Kutokana na maelezo yako nadhani kinachomshinda kuja kuwaona watoto mara kwa mara ni mwanamke/mke mwingine anaeishi nae huko, Arusha na Dar sio mbali kiasi kwamba mtu ukatembee mara moja kila baada ya miaka miwili! Lazima kuna kitu kinamzuia kuja huko mara kwa mara bila "sababu ya msingi" hasa kama mwanamke alienae hajui kama jamaa alioa/anawatoto.

Kibinaadamu Dada mpaka sasa huna ndoa, ni kama vile jamaa amekuweka spea tairi kwamba yakimshindwa huko Arusha basi wewe upo hapo kwa ajili yake (wapo wanaume wengi tu wa Kitanzania wanafanya hivi).Huyo mwanaume kama anajali maisha mema ya watoto wake hakika hawezi kukufukuza kwenye nyumba hiyo, lakini kwa vile sio muaminifu (amekukimbia) hivyo kumuamini kwenye masuala mengine sio kitu rahisi. Inawezekana kabisa siku moja akaamua kuiuza nyumba yenu alafu wewe na watoto kuhamishwa bila kupenda.

Sasa ili kujiondolea hofu na kuwa na uhakika wa mahali pa kuishi na watoto wako ni vema ukawahi kumtaliki mumeo (mpe Talaka), kisheria ndani ya Tanzania una haki hiyo. Ni vema ukienda Ustawi wa Jamii lakini tatizo la hawa jamaa wanakalia kesi za watu kwa muda mrefu sana. Pia TAMWA inawanasheria wazuri ila wanazile za "njoo kesho" nyingi na hivyo kucheleweza mambo.

Mimi kama Dinah nakutokana na uzoefu wangu na "Mahakama" ningekushauri uende moja kwa moja Mahakama ya Wilaya ya hapo unapoishi na kuomba kumuona Hakimu anaeshughulikia masuala ya Familia na ndoa. Ukipata nafasi ya kumuona (inategemea how busy she/he is) then muelezee matatizo yako ya kindo tangu mwanzo, maisha yalivyo hivi sasa na nia yako ya kutaka kumtaliki mumeo.

Mumeo anaandikiwa barua ya kuitwa Mahakamani ili Hakimu aweze kusikiliza upande wa pili na kupata ushahidi au sababu zilizomfanya jamaa akukimbie, baada ya hapo unaweza ukapewa nafasi ya kueleza nia yako ya kumtaliki mumeo au Hakimu anaweza kuisema moja kwa moja (kwa vile tayari umekwisha mueleza nia yako).

Kesi itaendeshwa kwa muda wa kati ya wiki 2 mpaka mwezi mmoja, inategemea kama mumeo atakuja Mahakamani na kuwa mbishi kuchukua/kubali Talaka kwa sababu zake azijuazo yeye au atataka kurudiana na wewe n.k.

Kutokana na urefu/umri wa ndoa kisheria mali zinagawanywa kwa manufaa yenu wote wawili na watoto mliozaa, lakini wewe utapendelewa zaidi kwa vile umekuwa ukilea watoto peke yako kwa muda wa miaka miwili hivyo ni wazi nyumba itakuwa yako pamoja na mali nyingine zinazowahusu ninyi kama wanandoa tangu 2004-2010.

Vilevile mumeo atalazimika kisheria (Mahakama itaamua) kuwa anatoa kiasi fulani cha pesa kila mwezi kwa ajili ya matunzo na elimu ya watoto, hata kama wewe unuwezo huo bado kisheria atalazimika kuchagia unless otherwise wewe mwenyewe ukatae.


Ikitokea umefanikiwa kuachana na mumeo kisheria, hakikisha hujengi chuki na mpe nafasi ya kuwaona watoto wake au watoto kumuona baba yako kila anapopata nafasi ya kufanya hivyo. Hakikisha watoto wanakuwa na uhusiano mzuri na baba yako.

Kumbuka tofauti zenu na chuki ya wakwe zako haziwahusu watoto waliozaliwa. Ikitokea watoto wanataka kujua kwanini baba hakai hapo nyumbani unaweza kuwaambia tu kuwa anafanya kazi mbali na siku akipata likizo atakuja kuwaona. Kamwe usiwaambie watoto kuwa baba yenu hawaenzi ndio maana hayupo hapa.....hakikisha unajenga uhusiano mzuri kati ya baba na watoto hata kama baba huyo anakuja kuwaona mara moja kila baada ya mwaka.

Talaka sio suluhisho na siku zote wanaoteseka ni watoto, lakini kutokana na unayokabiliana nayo Talaka itasaidia wewe kuwa huru kiakili na kuendelea na maisha yako kama mwanamke na vilevile kuwa na mahali penye uhakika ili kukuza watoto wenu.

Hongera kwa kuonyesha msimamo wako kama mwanamke, hongera kwa kusimama imara kwa watoto wako kama mama.

Nakutakia kila la kheri katika maisha yako na watoto wako.

Saturday, 26 June 2010

Wakwe hawataki niolewe na Kijana wao, nahisi nina ujauzito-Nifanyeje?

"Za kazi dada, pole kwa kazi ya kuelemisha jamii.
Mimi ni mwanamke mwenye miaka 23 sasa, lakini bado sijabatika kuolewa japokuwa nina boyfriend ambaye nampenda sana ila tatizo limejitokeza hivi juzi alipoenda kuwataarifu wazazi wake kuwa anataka tufunge ndoa.

Wazazi wake wamekataa na kumwambia mke wa kwanza wa mtoto wao ni lazima wamkabidhi wao kama wazazi, baada ya mpenzi wangu kunipa habari hizo sikujua nifanye nini wala niseme nini kwake.

Yeye anadai kwamba ananipenda hawezi kuniacha, lakini nimvumilie kwa muda na ndani ya miezi miwili ili atimize mashariti ya wazazi wake kwanza kwanza ndio ajue nini cha kufanya, leo hii (Email imenifikia Dinahicius wiki iliyopita) ndio kaenda kuoa nami najihisi mjamzito ila yeye bado sijamwambia,

Naomba ushauri please, nifanye nini?"

Dinah anasema: Namshukuru mungu kwa sasa niko salama baada ya kukamatwa na Hay Fever na ndio maana nilishindwa kujibu swali lako mapema, samahani kwa hilo.

Pole sana kwa Mkasa unaokabiliana nao. Kwa kweli nashindwa kuamini kama kuna Makabila ambayo bado yanasisitiza/lazimisha watoto wao kuolewa na watu walioawachagua wao kama wazazi. Hili la mke wa kwanza atafutwe na wazazi alafu baada ya hapo ndio kijana aoe anaemtaka yeye ndio nimeliesikia hapa! Inasikitisha sana.

Nadhani kuna mawili hapa Moja, ni kuwa wazazi wanamlazimisha kufunga ndoa na binti waliomtafutia wao (Inanikumbusha wimbo wa Binti Kimanzi) kama kijana anaeheshimu wazazi wake na kuwaridhisha kwa kila hali ni wazi itakuwa ngumu kwake kutaaa matakwa yao (inategemea na Mila, Utamaduni wao na Uoga wake yeye kama mwanaume).

Baadhi ya wanaume hufunga ndoa za kulazimishwa na kuishi na wake zao ambao hawana hisia nao kwa muda bila kushirikiana nao kimwili na kuwapa vituko mpaka wake hao kuomba Talaka na baada ya Talaka jamaa huenda kufunga ndoa na yule ampendae ambae ni chaguo lake ambae aliendelea na uhusiano nae wakati yuko kwenye ndoa batili.

Kama hii ndio nia ya mpenzi wako then hakuna haja ya kuwa na wasiwasi as long as unajua nini kinaendelea na siku zote anakuwa kwako.....hii haikufanyi wewe kuwa the other woman bali unamsaidia kuridhisha wazazi wake. Kumbuka mke "mtafutwa" ndio the other woman....ukimsadia kufanya vituko ni wazi mwanamke yule ataomba Talaka mapema.

Pili, inawezekana kabisa kuwa huyu jamaa anashindwa kukuambia ukweli tu kuwa hataki kufunga ndoa na wewe kwavile sio "wife type", anakupenda sawa lakini haoni kama unafaa kuwa mke wake. Kuna wanaume wengi sana hasa Afrika wanatekereza zoezi hili, utakuna Girlfriend wake mzuri kwa kila hali na wamekua pamoja kwa miaka mingi lakini anaishia kuoa "kitu cha ajabu" (mwanamke ambae wala hawaendani) na baada ya ndoa jamaa ataendelea na Girlfriend wa zamani au kuwa na Girlfriend mwingine ambae wanaendana nje ya ndoa yake.

Hii ni kwa vile baadhi ya wanaume wa Kiafrika wanaamini kuwa mke ana viwango vyake tofauti na mpenzi mzuri alienae mwenye kujipenda, kupenda maisha, kujali na kujituma/jitegemea kiuchumi. Nadhani umewahi kusikia wengi wakisema Uzuri wa mwanamke sio sura bali ni tabia.....imani hii ndio inapelekea wanaume kuoa bila mapenzi au attraction na hivyo ku-cheat on their wives kwa kutokana wanawake ambao wanawavutia na pengine kuwapenda nje ya ndoa zao. Inasikitisha lakini ni ukweli.

Sasa, kwavile unahisi kuwa unamimba nadhani ni vema kama utamjulisha jamaa kuwa umeshika mimba, kama kweli anakupenda na anania yakufunga ndoa na wewe baada ya "kuridhisha wazazi" na anajali maisha ya mtoto wake atakaezaliwa mwakani hatoendelea na ndoa au hata kama ataendelea nayo na kufanya kama "Binti Kimanzi" kwamba mume hatoi ngono, hali chakula chake, halali nyumbani n.k basi itakuwa vema.

Lakini kama mjamaa yuko serious na mke "mtafutwa" na anataka ku-share kitanda na kum-treat kama mke then sahau kama alikuwa mpenzi wako, hakikisha anajua umebeba mimba ya mtoto wenu ili asaidie kwa matunzo na malezi ya mtoto hapo baadae.

Mtoto atakapozaliwa (Mungu akijaalia mwakani) utakuwa na miaka 24, bado ni binti mdogo na una nafasi kubwa sana ya kuweka sawa maisha yako na kumlea mtoto wako kwa mapenzi yako yote. Mungu atakujaalia na utakutana na kijana mwenye kujali ambae atakuwa mume mwema hapo baadae.

Ni vema ukajifunza kudadisi asili, mila na desturi za mpenzi wako mpya ili kujua taratibu za kwako. Hupaswi kumuuliza yeye mwenyewe bali zungumza/uliza watu wenye asili kama yake ili usirudie makosa.

Usijipe hofu kipindi hiki ambacho unakuza kiumbe tumboni, jaribu kutuliza akili na kumfiria zaidi mtoto wako huyo atakae zaliwa. Ingekuwa nchi zilizoendelea hakika jamaa wa huduma ya Afya wangekupa Ushauri Nasaha na kukupa nafasi kama unataka kuendelea kutunza mimba au kuisitisha ikiwa changa (mimba ya mwezi mmoja ambayo ni kijibulungutu cha damu kinakumbwa wa mbengu ya Apple na Kisheria nchi za Magharibi unaruhusiwa kutoa) kwa njia za kisasa na salama zaidi.

Kwa bahati mbaya Tanzania hatuna utaratibu huo japo kuwa watu wanatoa mimba kienyeji na kwa njia za kizamani ambazo ni hatari kwa maisha yako, hivyo nisingekushauri ufanye hivyo japo baadhi ya wachangiaji wamegusia hilo.

Nakushauri utunze hiyo mimba kama kweli ipo na lea mtoto wako kwa kusaidiana na baba yake.

Kila la kheri!

Tuesday, 22 June 2010

Alinichumbia lakini akaoa mwingine, sasa ananisumbua, nimkomeshe vipi?

"Nawasalimu wote,
Mimi ni mdada mwenye umri wa miaka 33 hivi na nina mtoto mmoja wa miaka miwili na nusu. Nilitokea kupendana na kijana mmoja hivi wa kichaga ila kweli alichonitendea sitasahau. Ukweli mimi nilimpenda kutoka rohoni na sikuangalia ana nini ila nilisikiliza roho yangu na nikampenda, na kwa wakati ule niliamini pia na yeye alikuwa amenipenda kwa dhati.

Tulikaa muda wa kutosha na wote kwa pamoja tuliamua kuanza process za kuoana na kwa wakati huo nilikuwa na miaka 28, basi tulikubaliana kuona na mipango mbalimbali ilianza ikiwa ni pamoja na kunivalisha engagement ring.

Mimi nilishauriana na wazazi wangu na ikaamuliwa shughuli ya engagement ifanyike nyumbani kwetu, na ndivyo ilivyokuwa. Baada ya engagement nilisafiri kikazi nikaenda Nje na nilikaa huko kama wiki nne hivi, wakati wote huo nilikuwa nalazimika kumpigia mchumba wangu simu mara kwa mara kumjulisha hali.

Baadaye nilirudi Tz baada ya kazi iliyonipeleka huko kuisha. Kama mwezi hivi tangu nirudi nikagundua kuwa nilikuwa mjamzito, sikushtuka nilijua kisingeharibika kitu kwa sababu nilikuwa nimeshaweka mambo wazi.

Wakati huo nikaanza kupata tetesi kuwa huyo kaka ambae sasa ni mchumba wangu alikuwa ana uhusianao na mama mmoja aliyekuwa ameachika kwa mume wake akiwa na watoto watatu, hivyo huyo kaka alikuwa akiishi kwa huyo mwanamke, mimi sikuwahi hata kumshtukia kwa sababu pia mimi kazi zangu nyingi zilikuwa za kusafiri mara kwa mara.

Nilipofuatilia nilikuta ni kweli na ushahidi ni kuwa siku moja nilikamata wallet yake ikiwa na vyeti viwili vya angaza kimoja kikiwa na jina la huyo aliyekuwa mchumba wangu na kimoja kikiwa na jina la huyo mwanamke.

Kumbe walishakubaliana kuona, hata hivyo kulikuwa na picha ndogo ya huyo mwanamke kwenye wallet hiyo ya mchumba wangu. Nilipomuuliza alikana akasema sio wallet yake eti ni ya rafiki yake.

Niliendelea kukuza mimba yangu bila hata kupata msaada wowote kutoka kwake, na wakati huo ndio alikuwa akila maisha na huyo mwanamke aliyekuwa akiishi kwake na wakati huo huyo mwanamke alikuwa amemkabidhi Rav 4 ya Bluu, taratibu za kufunga ndoa na mimi zikawa zinapigwa chenga tu.

Kila nikimuuliza alikuwa hana jibu kamili, sasa na mimi nikaacha kumuuliza maana yake mtu mzima niliona kufunga ndoa sasa ni ndoto, siku moja kipindi cha Xmas huyo aliyekuwa mchumba wangu aliondoka na huyo mwanamke hadi nyumbani kwao Moshi kwenda kumtambulisha kwa wazazi wake hao hao waliomsindikiza kuja kwetu kunivalisha engagement ring ndio hao hao walimpokea huyo mwanamke na kukaa naye kwa muda wa wiki mbili.

Wakati akimpeleka huyo mwanamke kwao, nilikuwa nimebakiza wiki mbili tu kujifungua, Mungu akasaidia nikajifungu salama, na alikuja Hospitali, lakini hakutoa hata Shilingi moja na bili iliyokuwa inatakiwa ni 148,000.

Siku niliyokuwa natoka Hospitali alisingizia kuwa alikuwa anaenda Airport kumpokea rafiki yake lakini ukweli ni kwamba alikuwa ameenda kwa yule mwanamke. Hiyo haikuwa tatizo kwangu, kama niliendelea kujitunza mwenyewe kwa kipindi kile cha Ujauzito bila yeye kujishughulisha sitoshindwa sasa.

Huyo mwanaume alikuwa akija nyumbani kwangu na kutoa maneno ya kashfa na alikuwa akikuta mtoto amelala anamuamsha, haikuishia hapo, maternity ilipoisha, nilirudi kazini kwangu, na ndipo aliponifuata na kuniomba msamaha huku akalia.

Mimi nikamsamehe kwa sababu niliona labda hatarudia tena, basi nikampa sharti la kuhama ule mji tuliokuwa tukiishi mwanzo tukahamia mji mwingine na akafungua bisahara zake huko ambazo kweli ilibidi nimuongezee mtaji, niliamini angetulia.

Lakini kumbe haikuwa hivyo, baada ya kuona bisahara imekolea akaanza ufuska tena, na kwa kuwa mimi nilikuwa nafanya kazi field zaidi, basi kila nikisafiri alikuwa anaoa, wanawake wa kila aina, pete ya engenement aliyonivalisha akaichukua akamvalisha mwanamke mwingine tena, ikawa ni vurugu tu.

Nikirudi nyumbani nakuta Condom zimetumika zimetupwa chini ya uvungu, na siku moja nilikuta condom saba zilizotumika zimetupwa bafuni. Kweli ni story ndefu na siwezi kuandika yote. Niligundua huyu mwanaume alikuwa akipenda hela zangu sana kwani kila mshahara ukitoka anautaka wote hata senti habakizi, usipompa ndani hakukaliki.

Basi nilioona hali inakuwa mbaya nikaamua kuachana naye nikatafuta kazi sehemu nyingine nikapata, nashangaa alikuja katika huu mji ninaoishi akaulizia watu hadi akapajua ninaposihi sasa ameanza kunitishia, mara ataniua, mara atanifanya hiki na kile.

Shida yake anataka arudiane na mimi na baada ya mimi kuachana naye biashsra zake zimeyumba, manake hana msimamo ni kuhonga wanawake tu hana kai nyingine, na mpaka sasa mtoto ana miaka miwili na miezi 4 hajui anakula nini, anavaa nini wala anaishi vipi.

Sasa naomba mnishauri nimfanyeje manake nimeshatamani hata angetoweka duniani tu, maana hana anachofanya cha maana zaidi ya kunikosesha amani, mpaka sasa nimeamua kuishi na mwanangu tu. Naombeni msaada, ni nini naweza kufanya ili nimkomeshe.
Asante".

Friday, 4 June 2010

Ex analazimisha nirudieane nae, nimekataa anatishia maisha yangu-Ushauri

"Habari dada Dinah! pole sana kwa kazi nzito uliyonayo ya kutusaidia kwa mawazo na kutuelimisha. Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 32 ni mwajiriwa wa Shirika moja hapa Dar.Nilipo kuwa Kidato cha 2, nilikuwa na mahusiano ya kimapenzi na dada mmoja, kwa ukweli nilimpenda sana.

Tulivyohitimu Kidato cha 4 kwa bahati mbaya mwenzangu hakuchaguliwa na mimi kuchaguliwa kwenda Kidato cha Tano, Wazazi wake waliamua arudie Kidato cha 3 Shule 1 ya Sekondari ambayo ilikuwa Wilayani na wakati huohuo mimi nilitakiwa kwenda kuendelea na masomo shule 1 huko Dar!

Kifupi ilikuwa siku ya majonzi kwetu kutengana kwani ndio ilikuwa mara yetu ya kwanza kuwa mbalimbali. Nashukuru Mungu nifanikiwa kumaliza Kidato cha 6 na mpenzi wangu alifanikiwa kumaliza Kidato cha 4! Mimi nilijiunga na Chuo Kikuu nae akaamua kwenda kujiunga na Chuo cha Ualimu.

Matatizo ya uhusiano wetu yalianza pale ambapo mwenzi wangu alimaliza na kupangiwa kituo cha kazi huko mkoa wa Tabora! kwani kwa kipindi chote ambacho tulikuwa mbalimbali tulizoea kupigiana simu angalau mara 3 kwa siku na hamna siku kupita hatujapigiana simu!

Baada ya yeye kupata hiyo ajira akawa hapigi simu hadi mimi nimpigie, nilikuwa naumia sana natabia ile mpya, siku 1 nikamwambia ukweli kwanini mimi ndio nimpigie simu na nisipopiga ndio siku hiyo hatuwasiliani? Akanijibu tena kwa ukali kuwa yeye kapelekwa huko(Tabora) kufanya kazi na wala sio kunipigia simu mimi.

Kwa kifupi yupo busy! Niliumia mno na jibu lile lakini kwa kuwa nilimpenda nilimuomba radhi kama swali lile limemuudhi, tukaongea mambo mengine tu. Baada ya miezi michache kupita, ghafla simu yake ikawa haipatikani.

Niliteseka sana ikabidi nimtafute dada yake ambaye yeye hakunificha aliniambia wazi kuwa mdogo wake(yaani mpenzi wangu) amefunga ndoa na anadai kaniacha mimi kwa kuwa sina future!

Nilihisi kuchananyikiwa nikawa kama siamini nachokisikia! Nilikubaliana na hali halisi japo iliniathiri kimasomo na ilinichukua zaidi ya miezi 6 kumsahau! Nashukuru nilimaliza Chuo na baada ya muda mfupi nilipata kazi nje ya nchi. Kitendo cha kuondoka Tz kilinisaidia kwa 90% kumsahau kabisa mwanamke yule na nimekaa huko miaka 4 nikachoka nikaamua kurudi Tz.

Niliporudi Tz nilianza kufanya kazi hapa nilipo(ilikuwa mwaka jana mwezi wa 8)!Mwezi February mwaka huu, asubuhi moja nikiwa kazini nilipokea simu kutoka kwa yule dada(Ex~girlfriend wangu) akadai kwa muda ule yuko Dar kaja kwangu kwani anamazumgumzo ya kina nami(kumbuka ni zaidi ya miaka 5 hatujaonana wala kuwasiliana).

Tukakubaliana, tukaongea mengi mojawapo ndio lililonileta kwenu ndugu zangu mnishauri, nalo ni:-Anadai kuwa kuolewa kule alilazimishwa na alikuwa hampendi yule mwanaume hata kidogo. Kwa kuwa alikuwa ananipenda mimi ndio maana ameamua kumwacha yule mumewe na kunifuata mimi!

Mimi nilimwambia ukweli kuwa; KWANZA ndoa ya Kikristo haina Talaka, PILI siwezi kuwa nae kutokana na ukatili alionifanyia! Wadau naomba ushauri wenu kwani sasa hivi imekuwa kero kwangu. Yaani mwanamke amekuwa akipiga simu na kutoa vitisho kuwa kama sitomkubalia basi atakunywa sumu nakuandika Waraka kuwa mimi ndio nimesababisha hivyo. Ili mimi nishikwe na Polisi na kutumikia kifungo kwa rest of my life.

Kwa ukweli mimi siwezi kurudiana nae hivyo naomba mnielekeze njia gani nizitumie ili niondokane na kero hizo! Kingine ni kuwa toka niachane na mwanamke huyu nimetokea kuwa chukia sana wanawake, sina hamu tena ya kuwa na mwanamke na ni mwaka 5 sasa sijawa na mahusiano ya kimapenzi na mwanamke!

Je hali hii ikiendelea ndio kusema sitooa tena na ukizingatia umri unaenda? Naombena msaada wenu ndugu zangu na akhsanten sana.
Collns H.M
Dar "

Dinah anasema:Kabla hatujapoteza muda, hebu chepuka kwenye kituo Cha polisi na ripoti vitisho kutoka kwa huyo Ex na waeleze sababu ya Mwanamke huyo kukupa vitisho hivyo, kisheria Polisi wanatakiwa kukulinda wewe kutokana na vitisho vya mwanamke huyo.

Kama anakufuata-fuata Ofisini au nyumbani kwako yeye atapewa barua kwa mujimu wa Mahakama kuwa haruhusiwi kukatiza karibu na wewe na akionekana eneo hilo (unapofanya kazi/ishi) polisi wanahaki ya kumuondoa kwa nguvu.


Sasa ikitokea kajiua atakuwa kajiua kwa matatizo yake mwenyewe na wewe utakuwa salama kwani Polisi watakuwa na maelezo yako yote. Hakikisha unapata copy (nakala) ya maelezo yako, jina na cheo cha Polisi aliechukua maelezo yako, muda (siku, tarehe na mwaka), na jina la kituo just incase polisi huyo atahamishwa au kupoteza ushahidi.

**********************************************************

Baada ya kutendwa na kuumizwa na mtu uliemuamini na kumpenda imekuwa ngumu kwako kuamini wanawake, sidhani kama unatuchukia wanawake wote bali hutuamini. Kuna hali fulani ya uoga wa mwanamke mwingine kurudia kilichofanywa na Binti uliempenda.

Kwa kawaida huwa nashauri mtu ajipe muda (kaa mbali na uhusiano wa kimapenzi) mpaka utakapo pona kabisa kihisia, kupona huko kunaweza kuchukua muda mrefu kuanzia miezi sita mpaka miaka saba. Urefu wa uponaji kihisia unategemea zaidi na muda wa uhusiano wenu.

Kama uhusiano...kwa Mfano: ulikuwa wa miaka miwili na zaidi kupona kwake huchukua muda mrefu pia. Kutokana na maelezo yako inaonyesha ulikuwa umepona lakini baada ya huyu mwanamama kuanza kukufuata fuata katonesha kidonda hivyo kukurudisha nyuma.

Hali hiyo ya "kuchukia" wanawake ikiendelea hakika hutoweza kuoa au tuseme kuishi na mwanamke unless other wise uamue kufunga ndoa na mwanamke ili kutimiza wajibu kitu ambacho ni hatari sana.

Ili kuepuka hilo wewe mwenyewe unatakiwa kuchukua hatua madhubuti za kukaa mbali na huyo binti "machafuzi" ili uweze kuendelea na maisha yako mapya, hilo moja.

Pili, unatakiwa kurudisha imani juu ya wanawake, kwani si wanawake wote tunatabia chafu. Kuthibitisha hilo angalia wanawake wote kwenye familia yako je wanatabia kama ya Ex wako? Hapana! sasa hiyo inamaana kuwa kosa la mwanamke mmoja halibebwi na wanawake wote Duniani. Kurudisha kwako imani juu ya wanawake ndio njia pekee ya wewe kuwa karibu na viumbe hao na hivyo kudondokea mmoja kimapenzi.

Ni matumaini yangu maelezo ya wachangiaji yamesaidia kwa kiasi kikubwa kufanya uamuzi wa busara ili uendelee kuishi kwa amani na hatimae kupenda tena.

Kila la kheri!

Thursday, 3 June 2010

Niko nae kwa ajili ya mtoto wangu tu, sina hisia nae-Nitoke vipi?

"Hi dada dinah pole na kazi za kuisaidia jamii katika masuala muhimu ya maisha , mimi ni dada mwenye umri wa 25 nina mtoto mmoja wa miezi tisa sasa. Nimsomaji mzuri sana wa safu hii na nimefaidika sana katika suala zima la mapenzi.

Nilishawahi kuomba ushauri zaidi mara mbili na nilishauriwa vizuri nakutatua matatizo
yangu. Leo nimekuja tena kuomba ushauri katika haya yanayo nisumbua . Ninaishi na mchumba wangu ambaye ndio baba wa mtoto wangu huu ni mwaka wa pili sasa.

Nilikuwa nampenda sana ila sasa mapenzi yameisha kwani nina wasiwasi kuwa yeye hanipendi kutokana na vitendo vyake na pia hana samahani, hana pole, wala nakupenda tena wakati mwingine akikosa yeye atanigeuzia kibao mimi ndio niombe samahani.


Kwa mfano siku moja alilala nje ya nyumbani kwetu, aliporudi asubuhi sikumuuliza kitu nikakaa kimya, yeye alikwenda moja kwa moja kitandani kulala kwani ilikua 11 asubuhi na mimi kwakua usiku sikulala nikiwaza kapatwa na balaa gani nikarudi kulala, baada ya nusu saa hivi akaniambia oh kazini kulitokea wizi kwa hiyo haikuwezekana kuondoka.

Nikamuuliza mbona hujanitumia hata sms kua kuna tatizo limetokea unanipenda kweli?
akajibu "sikupendi! kwani nimekuletea mwanamke hapa ndani?akaniambia tena ndugu yako amewekwa ndani na kwakuwa ilikua Jumamosi hamna dhamana nika mwambia basi naenda kumuona huko nitaujua ukweli. Cha ajabu alikuja juu na kunikataza nisitoke nyumbani siku ile hata kwenda dukani hakutaka niende.

Dinah anasema: Kosa kubwa ulilofanya ni kukaa kimya, hii inaonyesha kuwa unamuogopa jamaa na yeye anajua kuwa unamuogopa na hivyo kuwa huru kufanya atakalo akiwa na uhakika hutosema kitu.

Tunapokuwa kwenye uhusiano na mnaishai pamoja technically mnakuwa mnaendesha maisha kama wanandoa hivyo kila mmoja wenu anakuwa na haki ya kuhoji mabadiliko yeyote yanayojitokeza Mf: uchelewaji, unajua muda wake ambao huwa narudi nyumbani sasa siku akichelewa kurudi katika hali halisi unapaswa kuhoji kwanini amechelewa au yuko wapi kwani muda umepita.

Aliporudi asubuhi yake, ulitakiwa kuhoji kilichomfanya alale nje na ungemwambia kabisa unataka maelezo ya kutosha na kuridhisha kwani kitendo chake kimekufanya ushindwe kulala kwa hofu, wasiwasi wa hali ya juu....sio kusema "kama kunatatizo ungeni sms".....alafu unaishia kuuliza "unanipenda kweli?".

Maelezo aliyokupa hakika hayaridhishi au niseme sio sababu ya kutosha ya kumfanya mwanaume mwenye familia na mwenye kujali kushindwa kuwasiliana na mpenzi wake na kumpa taarifa, kwa kifupi huyo mwanaume hana heshima juu yako na wala hajali hisia zako.

*********************************************************************

Siku nyingine tena nilituniwa sms na mwanamke akaniambia "hivi unajijua kua wewe ni bi mdogo tupo tulio anza?" nikamuuliza wewe nani? akajibu "siongei na mbwa naongea na mwenye kufuga mbwa", nikamwambia samahani maana inaonekana mimi ndio kikwazo cha wao kuwa pamoja akajibu "tuko pamoja wewe tu ndio ulikuwa hujui ila sasa umejua naona utapata presha".

Kwakuwa ile namba nilikua naijua toka mwanzo ni mdada ambaye tulikua tunakaa naye jirani ila alishahama nikaacha na naye, mume wangu aliporudi nilimuuliza na kumpa zile sms lakini cha ajabu aligeuka na kuniambia "hamuwezi kuniita mbwa kesho utaniambia vizuri la sivyo nitajiua au nitakuua nikafie jela" niliumia sana haijawahii kutokea.

Tangu siku ile sina tena wivu naye hata kidogo yaani hata akiamua kualala na mwanamke mbele ya macho yangu roho haini umi tena, niko hapa kwa sababu ya mwanangu kwani nampenda sana na sitaki ajeteswa na mama wa kambo.

Dinah anasema: Huna wivu kwa vile hakuna hisia za mapenzi juu ya mwanaume huyo, unajua wivu hujitokeza ikiwa kuna hisia kali za kimapenzi, sasa kama hakuna hisia za kimapenzi wivu utatoka wapi?

**************************************************************************
Imefikia mahali sasa kutoamini mwanaume hata siku moja, labda ashuke toka mbinguni lakini aliye zaliwa na mwanamke hapa Duniani sito thubutu kutoa moyo wangu tena. Huyu ndio aliye niingiza katika ulimwengu wa mapenzi nikamwamini sana lakini kwa sasa
nimemchukia zaidi ya upendo niliokua nao mwanzo.

Naomba mnisaidie ushauri je! niendelee kuishi na huyu mwanaume au ni toke nduki? Maana ninao uwezo mkubwa tu wa kumlea mwanangu bila baba yeke na kumove on with life all alone na sitopenda tena. Lakini nikiondoka mwanangu itakuaje maana sitaki kumuacha kwa kwa baba yake.

Dinah anasema: Huyu mwanaume aliekutambulisha kwenye Ulimwengu wa mapenzi ameumiza hisia zako vibaya mno na ndio maana umepoteza imani kwa wanaume kwa kunadhani kuwa wanaume wote wako hivyo, ukweli ni kuwa sio wote wanatabia za kishamba n akibinafsi. Wapo wanaume wametulia sana kiakili na wanajua kuthamini na kuheshimu wanawake.

Hamjafunga ndoa na huna hisia za kimapenzi juu ya huyu jamaa kutokanana vitendo vyake viovu hakika hakuna cha kupigania hapo ili ndoa isimame Imara! Nakubaliana na wewe kwenye kutoka nduki, tena wala usiangalie nyuma.

Kumbuka kuwa kuzaa sio uzee, wewe ni binti mdogo sana (nadhani unaona kina mama wa miaka 45-60 wanavyolazimisha ujana) sasa imagine wangekuwa na umri wako wa miaka 25? Tunza mtoto wako lakini kumbuka kuwa huyo ni baba wa mtoto wako na hivyo anatakiwa kuchangia matunzo ya mtoto wake na ana haki ya kumuona mtoto au mtoto kumuona baba yake. Hakikisha tofauti zenu zisisababishe mtoto kutomjua baba yake.

*****************************************************************************

Angalizo tu ni kwamba sina ndoa na huyu mtu, ilikua tufunge ndoa lakini mwezi ule ambao tulipaswa tufunge ndoa mama yake alifariki dunia na ndoa ikaahirisha na mpaka sasa hakuna kilichoendelea .

Nilimpenda sana na anauhakika siwezi muacha kwani nilimpa moyo wangu wote nilimfanyia kila kitu alichotaka, nilimtreat kama mtoto akiumwa naomba ruhusa kazini namhandle kama katoto kachanga na mlisha namuogesha namuimbia nyimbo hadi analala.

Inauma jamani ukimpenda mtu alafu akaku dissapoint kiasi hiki, yaani kweli sito penda tena! mwanzo na mwisho kupenda mtu anaye vaaa suruali. Naona niishie hapo maana machozi yanani tiririka kwa uchungu nilio nao kazi njema dada yangu.

Nitafurahi kama niyapata msaada wenu wa mawazo.


Dinah nasema: Pole dada mdogo kwa machungu unayokabiliana nayo, wala usilie kwani huyo mwanaume hastahili machozi kutoka kwa binti mrembo, mwenye kujali, ujuae kupenda na kijana kama wewe. Nimetoa maelezo yangu kutokana na maelezo yako hapo juu.

Ngoja nikupe kisa changu kilichotokea years ago ambacho natumaini kitakusaidia kuelewa situation yako. Mimi nilipokuwa nakua na hata kufikia umri wako nilikuwa mpinzani mkuu wa suala la ndoa, lakini hayo yote yalibadilika baada ya kushawishiwa na kimapenzi.

Wiki mbili kabla ya kufunga ndoa kuna kisa cha kifamilia kikajitokeza, nilikasirika sana na nikaomba ndoa ife, kwamba sikutaka kuolewa tena. Mdogo wangu wakati huo alokuwa na umri kama wako akaniambia " Da' Dinah mshukuru Mungu kuwa Mkasa huu umejitokeza kabla hamjafunga ndoa, huenda ni onyo juu ya huyo mchumba wako".

Nikaendelea kuishi na yule Mjamaa (mchumba) niliekataa kuolewa nae kutokana na issues za kifamilia....then from nowhere jamaa akaanza kuwa abusive(Emotinally as in masimango, lawama zisizokuwa na mwanzo n.k).....ikabidi nitoke nduki bila kuangalia nyuma...Lol! Nikaanza maisha yangu upya kama Mimi kwa kuhama mjini, kubadili kazi namtindo wa maisha yangu na baada ya mwaka na nusu hivi nikakutana na huyu ambae ndio Mume wangu wa sasa ambae ni mwema.

Ninachojaribu kusema hapa ni kuwa kuna mambo Mungu huruhusu yajitokeze ili kutufumbua macho, sasa mama yake alipofariki ndio pazia lilifunguliwa ili wewe uone ukweli wa tabia ya mchumba wako. Imagine mngefungandoa then alafu akaamua kuendelea na tabia zake chafu? Ingekuwa ngumu na ingekuuma zaidi ya inavyokuuma hivi sasa......Mshukuru Mungu amekuonyesha tabia halisi ya Mpenzi wako ambae soon atakuwa Ex.

Natambua kuwa bado unahasira sana, lakini ukijitoa kwenye maisha ya kunyanyasaji kutoka kwa baba mtoto wako utakuwa huru na utapenda tena.

Ni matumaini yangu kuwa maelezo ya wachangiaji wengine na nyongeza ya kisa changu halisi yatasaidia kwa kiasi kikubwa kufanya uamuzi wa busara na kuendelea na maisha yako.

Kila la kheri!