Friday, 26 March 2010

Naogopa uhusiano mpya, nikizidiwa najichezea je kunamadhara?

"Habari zenu wakubwa kwa wadogo,
Mimi ni mwanamke umri wangu ni miaka 25 tatizo langu ni mimi nilikuwa na mume wangu ambaye tuliishi pamoja kwa miaka 4 na nilikuwa nikimpenda sana mume wangu lakini kutokana na kutokuwa mwaminifu kwangu na mateso aliyokuwa ananipa kwa sababu alijua wazi nampenda nilishindwa kuendelea kuvumilia na mwaka jana mwezi wa 4 tukaachana.


Mimi nikaanza maisha ya peke yangu basi sikuhitaji tena mwanaume kwani nilimpenda sana mume wangu na sikupenda kuachana naye ila tabia zilinichosha.Kama unavyojua binadamu huwezi ishi mwenyewe mwezi wa 7 nikapata mkaka mmoja ambaye mwanzo sikumpenda kabisa lakini baadae nikajikuta nimeingia kwenye mapenzi yake.

Tumedumu na huyu kaka kwa muda wa miezi 3 kumbe naye hakuwa mwaminifu, sasa tatizo langu kubwa ni hili; tangu niachane na huyu bwana'ngu nimekuwa muoga kuanzisha uhusiano mpya wa kimapenzi kwahiyo nipatapo hamu ya kufanya mapenzi huwa najilaza kitandani kajichezea kinena hadi najiasikia raha kama vile nakojoa.

Nimekuwa nikijifanyia hivyo kwa muda mrefu, je inamadhara gani? na je huku ni kujichua? maana najua kujichua kuna madhara nifanyaje jamani na kuanzisha mahusiano na mtu mwingine naogopa isije kuwa yale yale.

ASANTENI NASUBIRI MAWAZO YENU
TINA-MOROGORO"

Dinah anasema: Siku zote sio vema kukimbilia uhusiano mpya baada ya ndoa kuvunjika au hata kutoka kwenye uhusiado uliodumu kwa muda mrefu. Kihisia na kimapenzi unakuwa hauko tayari kujua kama unampenda mtu au unakubali kuwa na mtu kwa ajili ya comfort. Hii inajieleza wazi pale uliposema kuwa hukumpenda bwana'ko mwanzo lakini ukaendelea nae kwa muda wa miezi 3.

Kuchezea kinena huwezi kusikia raha yeyote (kinena ni eneo linaloota nywele/mavuzi) na dhani unamaanisha kisimi a.k.a kiharage hicho ndio pekee kitakachokufanya usikie raha. Kuna njia nyingi za kujichua/chezea.....tafuta topic ya kujichua kwa mwanamke.

Kujichua kwa mwanamke kiasili hakuna madhara yeyote, lakini kama unatumia au unajingizia vitu au vifaa Ukeni (Sanamu) zinaweza kukusababishia maaambukizo, "kutifua" misuli ya uke na kusababisha uke wako kulegea, nyama kujitokeza kwa nje.

Ukizoea kutumia Sanamu kujichua utashindwa kusikia utamu kila utakapofanya ngono na mwanaume kwa vile sanamu ni ngumu japokuwa watu watakudanganya kuwa ziko na texture kama uume asilia lakini sio kweli, Mungu aliumba uume kwa ajili ya kuingia ukeni na sio sanamu.

Mazoea hayo yatakufanya kihisia udhani kuwa mwanaume hana uwezo wa kukuridhisha kingono na hivyo kumuomba akufanye kwa kutumia sanamu badala ya uume wake kitu ambacho nitakiita "madhara ya kujichua kwa kutumia sanamu".

Kujichua kiasilia kunakusaidia wewe kama mwanamke kuujua mwili wako, kuongeza nguvu kingono na hali ya kupenda tendo (utakapokuwa tayari kwa ajili ya uhusiano mpya), kukaza misuli ya tumbo na kufanya kuwa na shape nzuri ya makalio......inategemea na mtindo wa kujichua unaotumia, sio lazima iwe kidole.

Kila la kheri!

Thursday, 25 March 2010

hivi kusamehe ni ugonjwa? kila akicheat mie nasamehe tu-Ushauri


"Pole na kazi dada dinah,
mimi ni mwanamke wa umri wa kati nina boyfriend wangu ambaye hadi sasa tuna kama miaka 2 na nusu. Nilikutana nae wakati yupo mwaka wa mwisho Chuoni. Wakati huo mimi nilikuwa nimeshaanza kazi.

Nilimvumilia hadi akamaliza Chuo na kufanikiwa kupata kazi Benki akapangiwa kituo cha kazi Wilayani hapa hapa kwenye Mkoa huu tunaoishi. Wakati nakutana na huyu bwana alikuwa ndio ametoka kuachana na demu wake wa chuo, ila kipindi hicho pia niligundua kuwa ana demu mwingine ambaye alikuwa anasoma Chuo mkoani Arusha.

Nilipomuuliza inakuwaje akaniambia huyo mtu ni kama wameachana kwani kwa umbali waliokuwa nao asingeweza kuwa nae tena na ndio maana alikuwa na mahusiano na yule demu wa chuo, Basi nikaamua tu kuendelea nae nikijua atakuja kubadilika kwani tangu mwanzo nilihisi jamaa yangu ana utulivu.

Matatizo yalianza wakati alipoitwa kwenye interview ya kazi, kumbe kule alipoenda alikutana na msichana aliewahi kuwa nae kipindi wanasoma. Kwa maelezo yake ya awali aliwahi kuniambia kuwa yule dada ndie msichana ambae alimpenda sana kuliko wasichana wote aliowahi kuwa nao ila walipotezana.

Sasa aliporudi tu nikagundua mabadiliko kwa mtu wangu, kwanza kwenye simu yake alikuwa ameweka jina langu lakini nikakuta kaweka jina la kwanza la huyo dada, pili nikakuta msg za mapenzi akimwambia huyo dada kuwa yeye ndio mkewe aliepangiwa na mambo mengine yanayoumiza sana moyo.

Mbaya zaidi mimi mwenyewe hajawahi kuniambia maneno kama hayo tangu nimfahamu, basi nikamuuliza kwasababu jina nililolikuta ni kama la mtu yule ambaye alishaniambia je ni yeye ndie amekutana nae huko kwenye interview?

Akaniambia hapana ila huyo ni mtu mwingine ambaye amemkuta hiyo sehemu anafanya kazi Benki na akaomba msamaha kuwa ni bahati mbaya na hatarudia tena. Siku ya mwaka mpya wa kuingia mwaka 2009 tulibadilishana line kwa bahati mbaya. Ya kwake aliiweka kwenye handset yangu basi wakati tupo kwenye mkesha mida kama ya saa 5 nusu hivi.

Nikapigiwa simu na mdada sasa kwa kuwa nilisahau kama line iliyokuwepo haikuwa ya kwangu, nikapokea huyo dada akaniambia anaomba kuongea na mwenye simu, nikmjibu anti simu ni yangu akan'gan'gania nimpe mwenye simu.

Nikakumbuka nikampa simu huyo boyfriend wangu, akaangalia tu no akakata simu alafu akaitoa line na kuitupa simu yangu kwenye moto. Ukweli kile kitu mmii kiliniboa sana nikaamua kuondoka kurudi nyumbani.

Kesho yake akaniomba msamaha na kuahidi kuninunulia smu nyingine, pia ndio akaniambia ukweli kuwa yule dada aliepiga simu ni yule mwanamke wake wa zamani na ndiye aliekutana nae kwenye intrview. Nikamuuliza sasa itakuwaje?akaniambia kuwa yale yalishapita na hawezi kuniacha kwani ananipenda sana.

Nikamuuliza tena nitaamini vipi asemayo? akampigia simu yule dada mbele yangu na kumwambia kuwa hawezi kuwa nae tena ana mtu mwingine hivyo huyo dada aendelee tu na maisha yake.

Nikasahau kabisa dada dinah kuhusu huyo dada na kufungua ukurasa mpya na mpenzi wangu, Ikaja kipindi cha valentine mwaka huo huo, tulikuwa Dar basi huyo dada akapiga simu usiku wa saa kumi wakati bado tulikuwa tumelala, nikaamka na nikapokea mimi akanijibu kwa jeuri kubwa kuwa kwa nini napokea simu zisizonihusu?

Nikamwamsha boyfried wangu kama mara ya kwanza akakata simu, tukagombana sana siku hiyo akasema anamshangaa huyo dada kwa nini bado anamfuata wakati yeye hampendi! basi akanidanganya nikajikuta nimemsamehe dada dinha.

Sasa kilichonifanya niombe ushauri kwa wadau ni hiki,ulipofika mwezi wa 7 nikapata ujauzito nikamwambia mwenzangu inakuwaje mimi naona wakati wa kufunga ndoa umeshafika kwani sitaki kuzaa nje ya ndoa.

Huwezi kuamini alikataa eti yeye hayuko tayari kwa ndoa hivyo mimi nizae tu na yeye atalea mtoto ndoa bado sana, nikamwambia naona sitaweza kuendelea kufanya mapenzi na yeye tena kwani hayupo tayari na mimba nitatoa siwezi kuzaa nje ya ndoa tena hasa ukizingatia siku za nyuma nilishazaa nyumbani wazazi wangu watanielewaje?

Basi tukawa na ugomvi mkubwa kwa kweli na sikwenda kumtembelea tena kama kwa miezi 2 hivi na hata mawasiliano yakawa hafifu sana. Sasa nahisi kipindi hicho ndio alikitumia kufufua tena mahusiano na yule dada.

Siku moja nikatumiwa msg na rafiki yangu kuwa anamuona mtu wangu na mwanamke nyumbani kwake je nimeachana nae?kama naweza niende nikahakikishe mwenyewe! Kweli nikapanda gari nikaenda nikamkuta huyo dada nyumbani kwake, sikumuliza kitu huyo dada nikamfuata huyo bwana ofisini kwake nikamuuliza akanijibu kuwa yule ndio yule dada niliekuwa namsikia mwanzo.

Nikamwambia vipi kuhusu mimi? akanijibu kuwa yeye hajui na majibu mengine ya kifedhuli tu, siku hiyo nililala guest da dinah,baada ya hapo alikuja nyubani kuniomba msamaha nikaamua kumsamehe, ila tatizo ni kwamba amekuwa sio mwaminifu kwani siku ya valentine nilimkuta tena na mtu mwingine akimlalamikia kuwa hamuelewi bora aachane nae kwani haoni faida ya kuwa nae.

Nikamuuliza ila majibu yake bado hayaeleweki na hataki kabisa tuachane, naomba ushauri kwa wadu nifanyeje?

Dinah anasema: Pole sana kwa usumbufu unaoupata Mdada, maelezo yako yanafanana sana na ya Binti mmoja wa Kikoloni nilikuwa na-share nae nyumba nilipokuwa Chuoni. Binti alikuwa na Bf ambae alikuwa anamtreat kama unavyofanyiwa wewe. Wakati mwingine wanawake aliolala nao jana yake wanampigia simu yule Binti (my housemate) nakuwambia kuwa walichokifanya na jamaa, binti anakuja kwangu na kulia.

Lakini kila nikimpa ushauri wa kuweka miguu yake chini na kumpa ukweli jamaa, binti anaomba kuonana na jamaa, ile njemba imefika tu inaanza kumfokea, wanagombana wee kisha wanaishia kufanya ngono as unasikia kukurukakara zao huko chumbani.....akitoka hapo naenda kuchovya kwingine....kesho yake binti anasamehe.

Nikachoka kuliliwa nikaamua kumwambia ukweli kuwa, jamaa yako anajua kuwa wewe unampenda kwa dhati na anauhakika wa kusamehewa kwa makosa na uchafu wake wowote atakaoufanya, kitu ambacho mwanamke mwingine yeyote hawezi kufanya. Ili kumuonyesha kuwa unathamani kubwa kuliko anavyodhania mtose bila kumwambia.

Nikamwambia kuanzia sasa mchunie, badili mawasiliano, badili kitasa cha mlango, anza kujichanganya na watu wengine, ndugu,jamaa na marafiki yaani keep busy na maisha yako......... Hivi ndivyo nitakavyo kuambia na wewe Binti mrembo.

Mwanaume akikutenda kwa kuwa na wanawake wengine kabla hamajafunga ndoa na ukamsamehe ni wazi ataendelea kufanya hivyo akijua atasamehewa tena na tena, sasa unachotakiwa kufanya hapa ni kutoka Nduki (achana nae) kabla hujapewa HIV.

Huyu mwanaume hakuthamini, hakupendi, hakuheshimu na hana mpango wowote wa kuishi na wewe maishani mwake, Mshukuru Mungu kuwa aliweka wazi hilo mapema pale uliposhika mimba, katika hali halisi siku hiyo ndio ilitakiwa kuwa mwisho wa uhusiano wenu.

Hataki muachane sio kwa kuwa anakupenda.....ni kwasababu anajua wazi hakuna mwanamke yeyote hapa Duniani ambae anaweza kusamehe unayomsamehe wewe, uko hapo ili kutumiwa kama back up! na si vinginevyo. Mpe buti la meno huyo hakufai kabisa.

Wachangiaji wamesema mengi mazuri na haya yangu kwa namna moja au nyingine yatasaidia kum-buti huyo looser!
Kila la kheri.

Wednesday, 24 March 2010

Nahisi Mtumwa ndani ya ndoa yangu!-Ushauri

"MAMBO DADA DINAH,
POLE NA MAJUKUMU YA HAPA NA PALE PALE. NAOMBA SANA MY DIA UNISHAURI MAANA NIKO NJIA PANDA. JAMANI MWENZENU MIE NIMECHOKA SANA NA MAISHA YA KUKWARUZANA NA KUPIGIANA KELELE KILA WAKATI NA MUME WANGU.

MUME WANGU NI MTU ANAEPENDA KULAUMU SANA NA KITU KIDOGO KIKITOKEA KINAKUZWA KINAKUA KIKUBWA HASA, HATA UKIOMBA MSAMAHA HAELEWI. IMAGINE MIMI NAFANYA KAZI ARUSHA NA NINAISHI MOSHI KILA SIKU ANATAKA NIWE NAENDA NA KURUDI KWAVILE NAMPENDA NIKAKUBALI INGAWA NACHOKA SANA.


MARA NYINGI NAFIKA USIKU KWENYE SAA MOJA AU MBILI USIKU NA NINAKUA NIMECHOKA KWELI, WAKATI MWINGINE HATA MUDA WA KUANGALIA MAZINGIRA YA NYUMBANI SINA.

BASI AKIKUTA HATA GLASS ALIOACHA ASUBUHI CHUMBANI ATAONGEA MANENO MENGI SANA MARA OOH "WEE MWANAMKE HUJUI WAJIBU WAKO" UKIMWOMBA MSAMAHA BADO ATANUNUA.

KWA KWELI MIMI SIMUELI, KWA KIFUPI YEYE ALISHAISHI NAWANAWAKE WAWILI TOFAUTI MMOJA KWA MIAKA 4NA MWINGINE KWA MIAKA 10 ANAWATOTO 4 LAKINI WALISHINDANA NA HAWAKUFUNGA NDOA MIMI NDIO NILIEFUNGA NAE NDOA NA TUNAISHI NA MTOTO MMOJA WA KWAKWE.

YAANI HATAKI MTOTO AULIZWE KITU AGOMBESHWE ANAONA KAMA VILE ANAONEWA YAANI MIMI SIJABAHATIKA KUPATA MTOTO NA MUME WANGU HUYU INGAWA NINA MTOTO MMOJA KUTOKA UHUSIANO WANGU WA AWALI.

MATUMIZI NDANI YA NYUMBA KUTOA NI KWA SHIDA SHIDA UKIMWAMBIA AACHE HELA YA CHAKULA MARA ASEME AMESAHAU UKIMPA LIST YA VITU VYA KUNUNUA BADO ATADAI KASAHAU.

ANANICHOSHA KWAKWELI, WAKATI MWINGINE NAAUMUA KUFANYA MWENYEWE TU KUEPUKA KERO HANIHUDUMII CHOCHOTE KAMA MKEWE, NIFANYAJE JAMANI NA HUYU BABA?

MIMI NA MIAKA 29 YEYE ANAMIAKA 42 LAKINI VITUKO NAVYOFANYIWA NAHISI KAMA MTUMWA, MARA AJITENGE NA MWANAE YAANI KILA NALOFANYA ALIONI YEYE NI KULALAMIKA TU.

JAMANI EMBU NIAMBIENI KOSA LANGU NINI NA NIFANYAJE? SAMAHANINI KWA KUWACHOSHA ILA NILITAKA MPATE PICHA HALISI."

Dinah anasema: Mambo ni mazuri tu mdada, namshukuru Mungu. Shukrani kwa ushirikiano wako. Mumeo ni Mbahili/mchoyo, mlalamishi, mkorofi, hana huruma, hakuthamini, mvivu, sio mwelevu, hajali na mbinafsi hizi ni baadhi tu ya tabia ambazo mtu yeyote alie na akili timamu hawezi kuzivumilia.

Yaani unasafiri kutoka Mji mmoja kwenda mwingine kila siku na bado anakusimanga kuwa hujui wajibu wako? Wala sikulaumu kwa kuchoka mdogo wangu.

Huyu mwanaume anasumbuliwa na "mfumo" dume uliochanganyika na hali ya kutokujiamini kwa vile wewe ni mdada unaejitegemea kiuchumi, pia inawezekana ameathirika kisaikolojia kutokana na uhusiano wake na wanawake Mf mama yake, mama wa kambo, bibi, wapenzi wa awali n.k. Hali hiyo ndio iliyomsukuma kukulazimisha wewe kusafiri kila siku kutoka Arusha kwenda Moshi kwa kufanya hivyo anahisi kuwa ana-control juu yako wewe kama mwanamke.


Nijuavyo mimi maisha ya ndoa ya siku hizi ni kusaidiana sio kwa vile tu mwanamke unauwezo wa kiuchumi sawa au zaidi ya mumeo basi ndio iwe sababu ya kuchukua majukumu yote kuanzia ujenzi wa nyumba/kodi mpaka shughuli za nyumbani....ni sawa na kuwa single mama mwenye watoto na mume.

Hakika unampenda mumeo lakini vilevile unamuogopa, kwa sababu hata kama unampenda mtu huwezi kukubali kufanya kitu ambacho unajua wazi kitahatarisha afya na maisha yako, pamoja na kuwa unampenda unatakiwa kujiamini pia kuwa na msimamo na kumpa challenges mumeo sio kila akisema wewe ni "ndio bwana"......"nisamehe mume wangu" hata kama kosa ni lake!


Tabia za mumeo zinaweza kubadilika ikiwa wewe mwenyewe utasimama imara na kutaka mabadiliko, akijua wazi kuwa anayofanya ni makosa na ukampa nafasi ya kujirekebisha atafanya hivyo hasa kama anakupenda na anataka ndoa yenu iendelee. Lakini kabla ya kumtaka abadilike unatakakiwa kujua historia ya maisha yake.


MF; Kama mumeo aliwahi kuishi na mama wa kambo na mama huyo wa kambo kwa namna moja au nyingine alikuwa akimnyanyasa yeye kama mtoto pia mama huyo wa kambo alikuwa akimtawala baba yake (baba mkwe wako) then itakuwa imejiweka wazi kuwa Mumeo anakuwa na tabia hiyo kama sehemu ya kujilinda dhidi ya "mwanamke" kwa kifupi atakuwa ameathirika kisaikolojia.

Na suala la kujitenga na mtoto wake pia linaashiria "maumivu yake ya kisaikolojia" kwa vile wewe sio mama wa mtoto huyo anadhani kuwa utamfanyia vile alivyofanyiwa yeye na mama wa kambo, hivyo chochote utakachokifanya kwa vile tu wewe sio mama mzazi basi inaonekana ni uonevu hata kama unafanya hivyo kumsaidia au kumkanya mtoto.


Nini cha kufanya: Chukua likizo ya uhusiano, nenda kwa wazazi/ndugu ukatulize akili kwa siku mbili-tatu au hata wiki mbili. Utakaporudi utakuwa tayari kujaribu na kuweka mambo sawa ili ndoa yenu iendelee au kuimaliza.

Sasa, kwa vile wewe ni mdogo kwa mumeo (kibongo bongo huna nguvu) itakuwa ngumu kusikilizwa, hivyo jaribu kutumia watu wazima (wazee) unaowafahamu nakuwaamini, itakuwa vema kama watakuwa wale waliowafungisha ndoa.

Hawa watawapa ushauri na kuwapatanisha ninyi kama pea ili muishi kwa amani na upendo kiimani zaidi na sio kivitendo kwa maana kuwa maelezo yao hayatomfanya mumeo kubadilika kwa vitendo lakini itatoa nafasi kwako wewe kama mwanamke mdogo (kwa mumeo) kuweza kuwakilisha hoja zako za kutaka mabadiliko kirahisi.

Zungumza na mumeo kwa uwazi, weka hisia zako zote ili ajue kuwa anayokufanyia yanakuumiza na yanakusukuma nje ya ndoa yenu kitu ambacho wewe usingependa kitokee. Mwambie ni jinsi gani unampenda, unamheshimu na kumthamini.

Weka wazi hisia zako kwa mtoto wake, kwamba huna nia mbaya na unamjali kama unavyomjali mtoto wako.....kama historia yake inahusisha mateso ya mama wa kambo, itakubidi umhakikishie kuwa wewe sio kama wanawake wengine wenye roho mbaya.

Sema, kamwe hutomtesa wala kumnyanyasa mtoto wake, utamsaidia kila atakapohitaji msaada wako, utamfunza ili awe mtoto mwema na mwenye adabu kama unavyofanya kwa mtoto uliemzaa. Hutombagua wala kumnyanyapaa.

Mueleze ni kiasi gani unachoka kusafiri kutoka mkoa hadi mkoa kila siku, na kwa pamoja mtafute njia ya kuodoa kero hiyo (sio kuacha kazi tafadhali), ni mmoja wenu kuomba uhamisho ili kumfuata mwenzie.

Zamani kisheria ilikuwa mwanamke anamfuata mume siku hizi hata mume anaweza kumfuata mke, angalieni nani kazi yake inalipa zaidi na hivyo mmoja wenu kutafuta kazi nyingine huko ambako mwenzie analipwa vizuri zaidi (kamwe usikubali kuacha kazi) hata akikupa choice kazi au yeye, mama chagua kazi kwani wee bado mdogo na kumbuka unajukumu lingine hapo ambalo ni mtoto wako kutoka uhusiano wa awali.

Acha uzembe wa kukubali kila anachokisema mumeo, mpe challenges, pia sahau suala la kuomba misahama isiokuwa na sababu, omba masamaha pale tu unapojua kuwa umemkosea.

Ukifanikiwa hapa, njoo tena ili nikupe mbinu za kumfanya ajifuze kukusaidia shughuli za ndani unapokuwa kazini......ukimjulia mwanaume vijishughuli vya ndani sio deal sana kwake, sema tu sisi wanawake huwa tunawazoesha vibaya hawa wanaume ktk harakati za kuwakosa ili watangaze ndoa.

Mara wanapofunga ndoa nasi tunagundua kuwa hatuwezi kufanya yote, kazi Ofisini, kazi za nyumbani, kupika, kuwa mbunifu ili kumridhisha kingono, kuweka vionjo ili mapenzi yasifubae, kuangalia, watoto n.k Jamani eeh maisha ya sasa ni Tofauti, mwanamke huwezi kufanya yote hayo peke yako!

Natumaini wachangiaji na maelezo yangu yatasaidia kwa kiasi fulani ktk kufanya uamuzi,
Kila la kheri!

Wednesday, 17 March 2010

Bado nampenda Mume wangu lakini Dini imetutenganisha-Ushauri!

"Dinah mdogo wangu hujambo? Nawasalimia wanaGlob wote, nami naleta shida yangu ili nisikie wanajamii wa Dinahicious itanishaurije. Mimi ni mmama mkubwa tu, ni Muislamu na niliolewa na Bwana ambae alikuwa Mkristo nikiwa na umri wa miaka 23. Alikuwa ni mwanaume wangu wa kwanza tukiwa wanafunzi wa Chuo.

Uhusiano wetu uliendelea vizuri na baadae tukapata mtoto mmoja, Mpenzi wangu alikubali kufunga ndoa ya udanganyifu ya Kiislamu ili wazazi wangu wamkubali hivyo alislimishwa na tukafunga ndoa, baada ya siku tatu akaungama na kurudi Kundini.

Tuliendelea kuwa pamoja kwa miaka kadhaa kama mume na mke na tulipofikisha miaka mitano alidai tuende tukabariki ndoa yetu Kanisani lakini mimi sikuwa tayari kwa hilo hivyo akatafuta mwanamke mwingine kama nyumba ndogo na akasema kuwa anaoa.

Mimi sikumkatalia lakini nilimuambia kuwa nitaondoka nyumbani kwake, hapo tayari alikuwa ameanza ratiba ya kulala huko mara tatu kwa wiki, iliniuma sana Dinah. Lakini nilivumilia hali hiyo kama mwaka na kila nikimuambia kuwa naondoka kwake wala hakuwa akionyesha kujali yaani hata kusema usiondoke hasemi.

Ilipofika siku maudhi yamezidi, nikatafuta nyumba nikapanga, kabla sijahamia nikamueleza kuw animepta nyumba na nitaondoka nyumbani kwake kama kawaida hakupinga wala kuonyesha kujali basi mimi nikaondoka na kuanza maisha mapya huko nilikopanga. Baada ya muda mfupi nikaenda masomoni na niliporudi nilikuta tayari amefunga ndoa ya Kanisani na yule Mdada.

Mimi na yeye hatuna maswasiliano ya mara kwa mara lakini tunapowasiliana huwa anadai kuwa hana amani na inamuuma sana na itaendelea kumuuma mpaka anaingia kaburini. Kuna wakati maneno yake hunigusa sana hasa ukizingatia bado nina hisia nae.

Kwa sasa sijaolewa lakini akanibariki kwani kuna watu wawili-watatu wamejitokeza kutaka kunioa lakini mimi bado sijaamua kuolewa tena. Moyoni nahisi ingekuwa inawezekana kumrudisha Mume wangu ili tumkuze kijana wetu basi ningefanya hivyo, Ila nitakuwa tayari kama atakubali kurudi kuwa Muislam.

Da Dinah nimeileta hii ili nisikie ushauri wako pamoja na wachangiaji wengine. Je nimshauri aingie Uislam ili turudiane kwani nahisi bado nampenda au nikaze tu Moyo ili niolewe na mmoja kati ya hao wengine wanaotaka kunioa?

Naomba ushauri wenu tafadhali, natanguliza shukrani."

Dinah anasema: Mimi sijambo kabisa mdada, vipi wewe. Asante sana kwa ushirikiano wako. Dini ni Imani au mfumo wa maisha hapa Duniani ambao tunaufuata baada ya kukuta wazazi wetu wanauabudu lakini ukweli unabaki palepale kuwa wewe unapozaliwa na wazazi wenye kuamini Imani fulani haina maana na wewe ukiwa mtu mzima mwenye uwezo wa kufanya maamuzi juu ya maisha yako bila kutegemea wazazi uendelee kuiamini Imani hiyo.

Mfumo huu wa maisha unatusaidia sisi kuwa karibu zaidi na Mungu ambae wote tunaamini kuwa anatulinda, kutusaidia na kutuepusha na mabaya yote hapa chini ya Jua (Duniani), lakini linapokuja suala la mapenzi Dini huwa haina nafasi kwa sababu hujui ni mtu gani utamdondokea kimapenzi na yeye akakupenda jinsi umpendavyo!

Itakuwa ni mara chache sana kukutana na mwanaume mwenye Imani kama yako na mkapendana kwa dhati unless mnajumuika pamoja kwenye shughuli za kiDini au wazazi wake na wake wawaunganishe AGAIN itakuwa bahati sana kwako wewe kumpenda huyo uliyetafutiwa ili kufunga ndoa.

Sina uhakika na jinsi ndoa za Kiislamu zinavyofuatiliwa ili kuidhinisha "Talaka" ukiachilia ile ya "kisheria za kijadi" ambayo wenza hujulikana wameachana ikiwa hawajakutana kimili kwa muda fulani.

Nina uhakika na ndoa ya Kikristo kuwa haina Talaka, japokuwa siku hizi kuna sheria inayomruhusu mtu yeyote kumtakili mwenza wake Kisheria ili kuepuka usumbufu na unyanyasaji ambao unatokana na umilikishi (mume wangu, mke wangu) vinginevyo ndoa hiyo itaendelea kujulikana kuwa ni wanadoa waliotangana na kila mmoja hatoruhusiwa kufunga ndoa tena mpaka mweza wake afariki Dunia huko aliko.

Ndoa ya Kiislam uliyofunga haikuwa halali kwani wote mlikuwa mnajua kuwa mnafanya hivyo ili wazazi wako wamkubali, lakini kama kuna uthibitisho kuwa mlifunga ndoa basi hata ndoa yake aliyofunga Kanisani ni batili kitu ambacho kinaweza kurahisisha mambo kama wote wawili mtakubaliana kuhusiana na Imani zenu za Dini.

Kutokana na maelezo yako inaonyesha kuwa Imani zenu za Dini ni muhimu zaidi kuliko uhusiano wenu wa kimapenzi na kama ukweli ndio huo basi itakuwa ngumu sana kwa ninyi wawili kuishi pamoja kwani wote hamtaki kubadilisha Mfumo wa maisha yenu kiimani.

Natambua unampenda mzazi mwenzio na ofcoz anakuwa wazi sana kwako na comfortable kuongea na wewe mambo mengi kwa vile mmekuwa pamoja kwa muda mrefu na anatambua kabisa kuwa wewe ni mwanamke unaemuelewa vizuri kuliko Mkewe wa kanisani. Pia inawezekana anataka kuwa na uhusiano mzuri na wewe kwa faida ya mtoto wenu.

Kama kweli unampenda na unataka kurudiana nae basi utafanya lolote ili kurudiana na "mumeo", tunapozungumzia kufanya lolote ni pamoja na kubadili Dini na kufuata Imani anayoiamini yeye.

Wapenzi huwa radhi kubadili Dini, wengine hata Kukana wazazi wao kwa ajili ya wapenzi wao, sasa kama kweli wewe unampenda Jamaa na una uhakika anakupenda kwanini usifanye atakacho ili kuwa nae?

Ndoa yake ya Kanisani sio batili kama unauthibitisho wa aina yeyote kama vile cheti cha ndoa n.k...hivyo isikutishe kabisa. Huyo mwanamke aliefunga nae ndoa ameingilia ndoa yako na hakika huyo ni mume wako wa kudumu kama utaamua kuafiki na kubariki ndoa hiyo Kanisani.

Lakini kama Dini yako ni muhimu zaidi na labda hutaki kuwaudhi wazazi wako ambao mimi naamini kabisa kuwa hawahusiki na maisha yako ya kimapenzi basi kubali kuolewa na hao wanaume wengine waliojitokeza.

Natumaini sehemu ya maelezo yangu na michango ya watu wengine yamesaidia ktk kufanya uamuzi wa busara.

Kila la kheri!

Monday, 15 March 2010

Nifanyeje? Tuna VVU Binti wa kazi adai Mimba ni ya Mume wangu?

"Hodi wenyewe, mama nanihii upo?’ ilikuwa sauti ya mama mmoja alikuja kuchota maji. Mimi nilikauka kimya, siunajua tena siku ya Jumatatu unatakiwa uwe kazini lakini kwa vile bado nipo kijiweni, sikupenda majirani wajue hili.

Mama watoto alikimbilia nje na kumkaribisha huyu mgeni ambaye hakutaka kuingia ndani zaidi ya kuchota maji na kuondoka. Yule mama alimuuliza mama watoto wangu kama anataka mfanyakazi, niliguna moyoni, nikijua nini jibu atakalopata.‘Kwa hivi sasa sihitaji, inagwaje kweli ni muhimu ningekuwa naye, kwasababu nashindwa kufanya shughuli nyingine au kutoka kwa vile sina mtu wa kumkabidhi majukumu’ mama watoto alimijibu.

‘Sawa, lakini huyo ni mtoto mzuri kitabia, ingawaje hawa watoto wa nyumbani unaweza ukawaamini sana lakini wakafanya jambo ambalo hutazamii. Yaani mimi hapa nilipo natamani duniani inimeze kwa tukio lililotokea kwangu, kisa cha mfanyakazi wa nyumbani’ Huyo mama akaamua kukaa kwenye ngazi za nyumba yangu ili aweze kumhadithia mke wangu.

Nilikuwa dirishani kwahiyo maongezi yao nilikuwa nikiyasikia vizuri, na kwa vile Yule mama hakujua kuwa nipo aliongea kiundani mambo yake, kama unavyowajua akina mama wakiamua kuongelea swala Fulani kwa mtu anayemuamini.‘Ndiye unayetaka kuniletea mama?’ mke wangu aling’aka.

"Hapana sio huyo, huyo wangu namuandaa aende kwao kalikoroga mwenyewe’ Yule mama alisema , na kabla mke wangu hajamuuliza vizuri alianza kuhadithia kisa ambacho kilinifanya nishituke na kuamua kukiweka hapa ili wale wenye nia njema wachangie na huenda iwe fundisho kwa wenye wafanyakazi wa nyumbani.

Binti huyu niliye naye nilimchukua akiwa mdogo, alipomaliza darasa la saba. Tuliishi nae kama binti yetu, na kwa vile alikuwa na adabu , mchapakazi mzuri niliamua kumsomesha Sekondari hadi kidato cha nne. Hakufaulu, lakini tulikuwa na malengo ya kumsomesha zaidi.

Lengo hilo lilikwama kwasababu mume wangu kibarua chake kiliota majani, ikawa mimi ndiye mhudumiaji wa familia. Kama unavyojua kipato changu ni kidogo nisingeweza kumsomesha na kuilisha familia, kwahiyo tukakubaliana kuwa asubiri hadi mume wangu atakapopata kazi.

Siunajua maeneo ya huku kwetu kama unafanyakazi ili uwahi kazini inabidi uondoke saa kumi na moja alifajiri na kurudi nyumbani ni kuanzia saa mbili za usiku. Hili halikuwa tatizo kwasababu mume wangu alikuwa katika mkumbo huo kabla hawajampunguza kazini kwao.

Na pia yupo huyo binti ambaye tulimchukua kama mfanyakazi wa nyumbani na bado tunaendelea kumlipa licha ya kujitolea kumsomesha na kumpa huduma zote kama mtoto wetu. Lakini kama walivyosema wahenga, kuku wa kienyeji hafugiki, na kweli kwa hili sidhani kama nitahitaji mfanyakazi wa nyumbani tena.

Wakati mwingine nawashangaa sana hawa waume zetu, sijui akili zao zikoje. Unajua ninakuhadithia hili sio kwasababu nimjinga wa kutoa siri za mume wangu nje. Hapana, lakini lilotokea inabidi nimhadithie mtu ninayemuamini ili anipe ushauri.

Naujua ushauri nasaha nimeshaupitia, lakini huu sasa ni mkali zaidi. Wiki kama mbili zilizopita nimepata kalikizo kadogo nikaona nishirikiane na familia kujifanyia miradi midogo midogo na hapo ndipo nilipogundua kubwa kuliko.

Mfanyakazi wangu huyu wa nyumbani ni mjamzito nilipomuombana aniambie ni nani aliyempa hiyo Mimba, alikataa katakata, hadi nilipomwambia na mrejesha kwao kijijini ndio akanitajia. (Nitamrejesha kwao ingawaje hataki lakini kwa hali ilivyo sitaweza kusihi naye tena).

Nilishindwa kuamini kuwa Mume wangu ndio mwenye mzigo huo yaani hadi sasa siamini mbaya zaidi nilipomuuliza Mume wangu nae alikataa kakataa kabisa sasa sijui nimuamini nani? hili linawezekana kweli?.

Isingekuwa mimi na mume wangu tumeathirika na VVU ningefungasha virago vyangu ili kumuachia nafasi, manaake kaona simfai mpaka anatembea na Msichana wa kazi, lakini kutokana na tatizo letu tunahitajiana hasa kwenye kumlea mwanetu ambae pia aligunduliwa kuwa ameambukizwa.

Tuliamua kupima baada ya mtoto wetu kuwa anaumwa mara kwa mara, alipopimwa akaonekana ana Virusi vya UKIMWI hivyo na sisi tukalizimika kupima na majibu yakawa hayo kwamba wote tunavyo.

Sio siri kuwa mimi na mume wangu na mtoto tumeathirika, sasa sikutegemea kuwa mwenzangu anaweza kukosa imani na kudiriki kutembea na mfanyakazi wetu ilihali anajua kuwa anamtataizo haya ya kiafya.

Mume mume wangu kakataa katakata na kusema huyu binti kaumua kumpakazia ili asiondoke hapa nyumbani. Je nifanyeje ili kuupata ukweli? Japokuwa namuamini sana mume wangu na tangu tuoane naye hajawahi kunisaliti au kunidanganya. Sasa mimi nachanganyikiwa sijui nishike wapi? Nisaidie ushauri, nifanyeje?" Akamaliza huyo Mgeni mchota maji.


Kwa haraka haraka Mke wangu akamuambia Mgeni wake kuwa afuate Sheria, kwamba amshitaki na huko kwenye vyombo vya Sheria atapata ukweli na ushauri huo ulimfanya Yule mama ainuke na kwa hasira akaaga huku akisema‘Nini?, nimshitaki mume wangu?kwaheri" aliaga mama huyo!

Je ingetokea kuwa huyu mama kaja kwakokutaka ushauri ungemsaidiaje? Ungemshauri vipi?
Asanteni.
M3.

Wednesday, 10 March 2010

Alinitenda na rafiki yangu, sasa niko Ughaibuni anitaka tena-Ushauri

"Habari za kazi dada dinah, Mungu akubariki sana kwa kuanzisha uwanja huu wa ushauri kwa watu wenye matatizo, kwa kweli kupitia Blog hii watu mbalimbali tumeweza kuelimika. Nami kama walivyo tangulia wenzangu kuomba ushauri nami naomba ushauri wako na wachangiaji wengine wote kutoka na tatizo hili linalonisumbua.

Mimi ni mwanamke nilikuwa na mwanaume naishi nae kwa bahati nzuri tukabahatika kupata mtoto mmoja, mapenzi yetu yalivunjika baada ya mpenzi wangu huyo kutembea na rafiki yangu mpenzi. Mwanzo wa mapenzi yao nilikuwa naletewa taarifa na watu wa karibu yangu lakini kutokana na kumuamini sana huyo jamaa na rafiki yangu nikawa napuuza nikijua ni maneno ya watu tu.

Lakini siku moja ndipo nilipokuja kupata ukweli baada ya kuzikuta msg za mapenzi kwenye simu yake. Mimi katika kupata ushahidi nikatumia zile msg dada yangu, baadae mpenzi wangu alipokuja kujua kuwa nimegundua hakuonyesha hata dalili ya kuomba msamahaa na siku moja tukagombana sana mbele ya mama yake mzazi kuhusiana na suala hilo na katika kunionyesha ujeuri akazungumza mbele ya mama yake kuwa hawezi kumwacha huyo rafiki yangu.

Mimi sikuona sababu ya kuendelea kuwa nae ikabidi niondoke. Baada ya hapo akaamua kuhamia kwa huyo rafiki yangu na kuishi nae kama mke na mume, Mungu si athuman nilikaa kwa muda wa mwaka mmoja na nusu bila mpenzi wala rafiki wa kike kutokana na jinsi nilivyotendwa.

Baada ya hapo nikapata rafiki wa kiume ambaye alionesha kunipenda na kutaka kunioa lakini kwa vile nilishatendwa nikawa makini, huyo rafiki wa kiume nimefahamiana nae kwa muda wa miezi mitatu tu nikapata safari ya nje ya nchi na kipindi chote cha miezi mitatu sikuwahi kufanya nae mapenzi.

Rafiki huyu wa kiume aliniambia kuwa anataka kunivisha pete ya uchumba kabla sijaondoka, lakini hadi naondoka hajatimiza ahadi yake nami sikutaka kumkumbusha. Sasa baada ya kuwa huku nje yule mwanaume wa kwanza ameanza kunibembeleza eti turudiane na kwamba yeye alifanya vile kwa bahati mbaya.

Huyu rafiki yangu mpya nae ambaye tulipanga kufunga ndoa nitakaporudi nae amepata safari ya kwenda nje kulinda amani kwani yeye ni Mwanajeshi na tangu alipopata taarifa hizo za safari hajagusia tena nia yake ya kunivisha pete ya uchumba, hadi sasa nashindwa kujua la kufanya, sina uhakika kama huyu mpya anania ya kweli nami au nirudiane na yule wa zamani ambaye kwa watu wa karibu wananiambia kuwa bado wanaendelea na yule rafiki yangu.

Naombeni ushauri wenu ndugu yangu na wachangiaji wengine kwani nimechanganyikiwa. Watinga"

Dinah anasema:Tubarikiwe wote Watinga, asante sana kwa ushirikiano wako. Huyo baba mtoto wako hafai kabisa na futa wazo la kurudiana nae kwani hakukuheshimu na wala hakukuthamini sio tu kama mpenzi wake bali mama wa mtoto wake na akakutenda na rafiki yako.


Kama ulivyosema mwenyewe alipogundua kuwa umejua uchafuzi wake bado hakuonyesha kujutia makosa yake, hakuomba msamaha na badala yake alionyesha kiburi. Mimi binafsi naamini kuwa kama mtu anakupenda kwa dhati kamwe hawezi kukuumiza na ikitokea mnashindwa kuelewana kwa sababu zozote zile na mmoja wenu kutaka kuondoka.


Lazima mtu huyo (mkosaji) atapigania penzi lake kwa kuomba msamaha, kujutia makosa na kuahidi na kuhakikisha anabadilisha mwenendo wake na ikibidi kuwekeana "sheria" hasa kama wewe ulietendwa unataka kuendelea na uhusiano. Uamuzi uliochukua ni wa busara hasa ukizingatia hamkuwa kwenye ndoa hivyo hakukuwa na suala la kupoteza muda kujiuliza shold i stay...should I go?


Siku hizi nasikia wanaume wa wetu wa Kibongo wanapenda sana kutumia wanawake kiuchumi, akijua tu umefanikiwa kimtindo au uko nje (as wanaamini kuwa Ulaya = kupata senti kiurahisi) basi Exes wengi hujaribu sana kujipendekeza kwa kujidai kuwa wanataka kuoa au kurudiana na wewe kwa vile wanauhakika ulikuwa unawapenda hivyo utakubali haraka kurudiana nao. Lakini ukweli ni kuwa hawana nia na wewe bali wanataka kukutumia nahuko waliko wanaendeleza mahusiano na wanawake wengine.


Muda uliochukua kupumzika (kuwa nje ya uhusiano) unatosha kabisa kwa wewe kuwa tayari kujaribu tena uhusiano wa kimapenzi japokuwa, lakini miezi mitatu ya kuwa kwenye uhusiano mpya ni mapema sana kwa wewe na yeye kupeleka uhusiano huo kwenye level ya juu ambayo ni uchumba kuelekea Ndoa.

Huyu Mpiganaji huenda anania njema sana tu na wewe lakini baada ya kutumwa kwenda kulinda amani huenda imeingilia mipango yake hasa ukizingatia kuwa wewe uko Ughaibuni. Kuna mawili-matatu huenda yalikuwa yanasumbua akili yake Moja ni kukuchumbua na yeye kupoteza maisha by doing that atakuwa amekuumiza sana kuliko akijifia bila kujicommit kwako kama mume wako wa baadae.

Pili huenda amepoteza ile hali ya kujiamini baada ya wewe kwenda Ughaibuni, amekuwa na wewe kwa muda mfupi sana hivyo ni rahisi kwako wewe kama mwanamke kubadilisha mawazo mara baada ya kukutana na wanaume wengine Makini huko Ulaya.


Kama unampenda kiukweli huyu Mwanajeshi basi mimi nakushauri uendeleze urafiki ambao ni a bit special kwa vile mnapendana kimapenzi hii itawasaidia sana wote wawili kujua nini mnataka out of uhusiano/urafiki wenu na Mungu akijaalia kila mtu akamaliza shughuli zake huko aliko na kurudi Nyumbani basi mtaungana na kuwa full time wapenzi na hata ndoa kama mtapenda iwe hivyo.

Hapo hakuna cha kuchanganyikiwa wala nini, ni uamuzi tu. Kama unataka keep urafiki na Mpiganaji au achana nae uanze upya pale utakapo kutana na mtu mwingine aliekua na kutulia kiakili.

Natumaini ushauri wa wachangiaji na nyiongeza ya maelezo yangu yatakuwa yamekusaidia kufanya uamuzi wa busara.

Kila lililo jema!

Tuesday, 9 March 2010

Kwanini wanaume mnapenda kuterekeza Familia zenu?

"Habari yako Dinah, pole na majukumu. Mimi ni mama wa miaka 40 sasa nina watoto 2 lakini nimetengana na mume wangu kwa miaka mitano sasa. Uniwie radhi kwa hii habari ni ndefu sana ila nataka kushare na wamama na wababa kwa ajili ya kile kinachotokea ktk maisha ya ndoa unapobainika udanganyifu kwa mmoja wapo.


Tumekuwa kwenye ndoa kwa miaka 11 mpaka nilipoamua kumuacha mume wangu January 2006, kwa muda wote tulioishi pamoja tulipitia maisha magumu na ya wastani na tulikuwa tunasaidiana sana. Nilikuwa nampenda mume wangu kwa dhati, akiwa hana kitu nilifanya kwa niaba yake na sikuona tatizo.

Mwaka 2002 mume alipunguzwa kazini na kwa maelezo yake hakulipwa hela ya maana, mimi nikaona sio tatizo nilikuwa na kipato cha kutuwezesha kuyamudu maisha ya familia yetu kwa furaha, hapo tayari nilikuwa nimenunua kiwanja maeneo ya Tegeta.


Mume alikuwa hayapendi maeneo hayo ya Tegeta hivyo hakujishughulisha hata kukiona hicho kiwanja. Muda mwingi mume wangu alikuwa anabaki nyumbani mimi nikiwa kazini. Hapo nyumbani tulikuwa na msaidiza wa kazi na watoto 2.

Wakati huo mtoto wetu mkubwa alikuwa anasoma darasa la 2 na mdogo alikuwa chekechea, nilikuwa na akiba niliokuwa naitunza kwa ajili ya kujenga lakini tukajadiliana tukaona bora tununue gari ili mume wangu awe na shughuli kwa kutumia hivyo gari. Mume wangu alitafuta gari nikalinunua na yeye akawa analitumua kama tax. Tatizo likaanzia hapo.

Naomba niwaambie hivi mimi ni mama mwaminifu ninamwamini Mungu katika kweli yote sikuwahi kumfikiria mume wangu vibaya au kama angaliweza kuwa na mwanamke mwingine au kutembea na house girl nilikuwa namwamini sana na nilikuwa bize sana nikidhani namsaidia mwenzangu kumbe wapi.


Gari lilianza kunionyesha mambo, mume akawa hataki kufanyia kazi akawa anazunguka nalo tu, asubuhi naulizwa hela ya mafuta, matengenezo mpaka nikajuta kununua hilo gari. Nikaamua kuwaambia ndugu zake waongee nae.


Walipoongea nae yeye akasema hawezi kuendesha taxi kama nataka ninunue fuso ndio atafanya kazi hiyo, hilo likaniwia gumu nikachukua gari nikampa dereva mwingine. Jamani! wakati mimi ninahangaika kutafuta pesa za matumizi na kusomesha watoto kumbe mwenzangu kaanzisha uhusiano na dada wa nyumbani ndio maana hata kazi hataki kufanya ila mimi nilikuwa sijui kinachoendelea.


Mwaka 2003 tulianza kujenga na yeye ndio alikuwa anasimamia ujenzi ila cha moto nilikiona, tunapanga bajeti ya site vizuri namkabidhi pesa akirudi jioni ana shoti laki 2 au laki inategemea na wingi wa pesa utakayompatia lazima apunguze materials bila sababu mpaka nikaanza kumchunguza.

Hapo tulikuwa tunaishi Kinondoni kumbe bila mimi kujua alikuwa kampangishia mwanamke chumba huko Gongo la Mboto. Tukaanza kukorofishana maana ukiweka hela ndani yeye kazichukua hata simu anabeba.

Alivyojua kuwa najua habari za huyo mwanamke akaanza kusema mimi nataka kumwacha kwasababu hana kazi, oh sababu unajenga na mambo mengi mabaya kwa kweli. Tulisuluhishwa lakini hakuwa tayari kuacha tabia ya wanawake wa nje na mimi nilimchukia sana kwa tabia zake ndicho kilichotutenganisha mimi na huyo mume wangu.

Tulipoamua kutengana aliniambia niondoke na watoto niliondoka nao na wanasoma vizuri tu kwani niliamua kuwapeleka Boarding School ili wasiadhirike na kutengana kwetu japokuwa wakirudi likizo Mume wangu anakuja kuwaona lakini hawasaidii kwa chochote hata chupi hawanunulii.

Kwa sasa anafanya kazi nzuri tu lakini hataki kuwasaidia watoto. Mwaka huu kabla watoto hawajarudi Shuleni waliniomba sana nimsamehe baba yao na nilifikiri sana nikawaita wazee na nikawaambia kuwa nimemsamehe kilichotushangaza ni kwamba yeye hajakubali kusamehewa anachotaka ni nyumba niandikwe kwa jina lake kwanza na gari ninalotumia nimpe au niliuze ndio atarudi.

Kwa masharti hayo mie nimesema basi na kila mtu aishi peke yake maana naona mwenzangu anawivu na nilichonacho ambacho kimsingi ni cha familia yetu, nimeogopa masharti yake maana anaweza kutufanya tuanze kupanga tena.

Kinamama ninachotaka kujua ni hiki; Kwa kina mama hivi waume zenu nao wakijua kuwa umejua anachokukosea na kutengana huwa wanawasusia familia?

..... na kina baba naomba kuwauliza mpaka lini mtawatesa wake zenu kwa kuwasusia familia zenu?

Samahani sana Dinah usilitoe jina langu.
Nina hasira sana na wanaume na ninawachukia kwa kweli."

Dinah anasema: Asante sana kwa maelezo yako uliyoyapangilia vema kabisa. Maelezo ambayo hakika yanatia Moyo wote waliopatwa na matatizo ya kindoa, Inaonyesha kuwa hata sisi wanawake tunaweza kusimama Imara na kuhakikisha watoto wanapata maisha bora hata kama baba yao hataki kusaidia.


Hongera sana kwa kutumia muda wako mwingi kuhakikisha kuwa familia inaendelea kula na kuishi mahali bila usumbufu wowote, lakini kujituma kwako kumezaa tatizo lingine ambao ni hali ya kutokujiamini kwa mumeo.

Mwanaume yeyote hapendi kulishwa na mwanamke, kwa maana ya kuwa na mwanamke mwenye nguvu kiuchumi. Huyu mwanaume atahisi kuwa unamdharau hata kamahufanyi hivyo bado atadhani kuwa unamdharau kwa vile tu hana kazi au hata kitu.

Mwanaume huyu atatafuta namna nyingine ili ku-gain ile hali ya yeye " kuheshimika" nakuwa in control na ndipo sasa anakwenda kuanzisha uhusiano na mwanamke mwingine na ili kurudisha hali ya kujiamini na nguvu as a man akatumia pesa za kujengea nyumba kuhonga, akatumia gari kufanyia shughuli zake nyingine na sio kazi ya kubeba abiria.....hii yote ilikuwa inamfanya ahisi kuwa bado ni MWANAUME out there!


Lakini kitu ambacho wanaume sio tu mumeo ni wote, huwa wanakisahau au hawajali ni kuwa unapoamua kufanya uchafu nje na kuharibu ndoa yako atakae umia sio Mkeo bali ni watoto ambao hakika hawana hatia na hawakuomba kuzaliwa na nanyi bali uamuzi wenu ndio umesababisha uwepo wao hapa Duniani.


Ndoto ya Mtoto yeyote Duniani ni kuwaona baba na mama yake wako pamoja, na mtoto huyo hatopenda kuona mtu mwingine anaingilia uhusiano wa baba na mama yake. Inasikitisha unaposhuhudia watoto wanatamani ndoto hiyo itimie lakini mzazi mmoja anaendelea kuwa mbinafsi na kutokujali matakwa, hisia na haki ya watoto hao.


Mumeo hapendezwi na maendeleo yako kiuchumu na anahisi kuwa humueshimu tena kwa vile alikuwa hana kitu napengine hata aliwahi kudhani kuwa kuna mwanaume mwingine anakupa hizo pesa za kujenga nakufanya mambo mengine ya kifamilia na kimaendeleo.....wanaume wengine ni wanadhana potofu sana, wanadhani mwanamke huwezi kufanikiwa kimaendeleo unless kuna mtu unamtumia.

Yeye kutaka Gari iuzwe na Nyumba iandikwe jina lake ni wazi anataka ku-gain power au control kama mwanaume. Hakuna dalili za yeye kutaka kuendeleza penzi ili kuwa na maisha bora kama familia.

Kama unahisia za kimapenzi juu yake, kwamba bado unampenda na yeye anakupenda na ungependa ndoa yenu ifufuliwe then ni vema wote wawili kushirikiana na kupata ushauri wa kitaalamu zaidi na baada ya hapo mali zote ziandikwe majina ya watoto kama alivyogusia mmoja wa Wachangiaji nami nitaongeza maelezo yangu kwenye hili kama utakuwa tayari.


Lakini kama unataka kurudiana na Mumeo kwa vile tu watoto wanataka kuwa na baba yao karibu then nakushauri utafute Mwanasheria wa masuala ya ndoa (unaweza tu kwenda Mahakamani ukaeleza nia yako na wao watakupa ushauri wa nini cha kufanya) ili kumtaliki mumeo Kisheria ili asije kukupa matatizo baadae, pia Talaka itakusaia wewe kuwa huru na kuendeleza maisha yako.

Nikijibu swali lako kama mwanamke: Inategemea na asili ya Mwanaume, mazingira aliyokulia, uzoefu wake, maisha ya wazazi wake n.k., ila wanaume wa Kibongo kuterekeza familia zo ni kawaida sijui wamerogwa?

Hata kama baba yako alikuwa mchafuzi au alimterekeza mama yako haina maana kuwa na wewe "urithi" hayo, jitahidi na uwe tofauti, kuwa baba bora kuliko alivyokuwa baba yako. Muonyeshe baba yako kuwa alichokifanya sio Uanaume ni upumbavu na wewe ni mwanaume na unafanya kinyume kabisa na lichokifana.

Wanaume wa kibongo wenye t abia ya kuterekeza Familia zetu kwa sababu ya Vimada mnatakiwa ku-MAM UP!

Ninyi wanawake (Vimada) kama unajua kabisa jamaa anafamilia yake kwanini ukubali aiterekeze? Kwanini unakubali mwanamke mwenzio ateseke? Hebu fikiria ingekuwa ndio wewe umeterekezwa ungejisikiaje?

Wanawake wote mnaopenda kunyatia/kubali waume za watu mnatakuwa ku-WOMAN UP nakujifunza kusema "SITAKI kuharibu maisha ya watoto wako"....utakuwa umesaidia watoto hao kuendelea kuwa na wazazi wao wote wawili. Jifunzeni kujitegemea na kuendesha maisha yenu bila kutegemea kubebwa na wanaume wa watu.

Dada tafadhali kama utaamua kuendelea na ndoa kwa vile bado mnapendana basi hakikisha afya yake ni safi na unasimamia hapo kwenye mali kuwa ni za watoto, vinginevyo atakumsikinisha (kukufanya uwe masikini) huyo mwanaume.


Kila la kheri mwanamke wa Shoka!

Tuesday, 2 March 2010

Mke asikiliza wambea na sasa tunaishi ki Juma na Roza

"Habari za kazi Dada Dinah na heri ya mwaka mpya.
Mimi Naitwa Emmi nipo Iringa nimekuwa mpenzi sana wa blog yako hasa kwa ushauri na maoni mbalimbali yatolewayo humu.

Mimi nina mke nimeoa miaka mitatu iliyopita na tumejaaliwa mtoto mmoja wa miaka miwili sasa. Shida yangu sister ni kwamba mke wangu anapenda sana kusikiliza maneno ya mitaani. Mimi ni mnywaji wa pombe kiasi lakini yeye hanywi na aliniruhusu kunywa isipokuwa nisizidishe kiwango na hilo nalizingati sana.


Sasa yeye akiambiwa tu umbea kuwa mmeo ana wanawake wengine basi akirudi kutoka huko atokako hunijia kama Mbogo na hataki kusikia cha mtu, yaani ananitukana sana lakini mimi kwa sababu nampenda na pia kujali sana uwepo wa mwanangu huwa simlipizi kwa kutusi zaidi ya kukaa kimya.


Ila kuna wakati nilimwambia aachane na hao wambea kwani watambomolea nyumba yake lakini anabisha. Kwa sasa imefikia hatua hataki kukaa na mimi na anatafuta kila sababu ili nimfukuze ila mimi ni kimya nasubiri uamuzi wake.


Jamani nipeni ushauri juu ya huyu mwanamke, je nimuache au niendelee kukaa kimya huku yeye akiendelea na matusi yake ndani ya nyumba? Kwani kwa sasa tunaishi kama kaka na dada yaani kila mtu ana chumba chake, nafikiri umenielewa.
Nitashukuru sana kwa ushauri wenu Wadau.
ahasante!!! Manuel"

Dinah anasema: Manuel asante sana na heri ya Mwaka mpya! Unajua ndoa inajengwa na watu wawili ambao ni mume na mke. Huyo Mke asingesikiliza maneno ya watu na angekuamini kama ungekuwa unakunywa pombe na yeye akiwa pembeni.


Lakini kwa vile huwa hayupo unapokwenda kulewa anahaki zote za kuwa mkali nakukubali anachoambiwa na Mashoga zake ambao baadhi huenda ni walevi nahuenda huwa unafanya nao utani au wao wanakutania wewe kupita kiasi na pengine umewahi kuwtaongoza bila wewe kujua kutokana na pombe na hivyo kuhisi kuwa unaweza ukawa na mwanamke wa nje na hivyo kupeleka habazi ambazo hazina uhakika kwa mkeo.

Unajua tena Mji wa Iringa ni mdogo na usikute watu wanajuana na wanajua unanywea bar gani na huko bar huwa unakaa na kina nani......kama marafiki zako hawajaoa au wameoa lakini sio waaminifu kwa wake zao ni wazi baadhi ya watu wanaweza kuhisi kuwa hata wewe unafanya kama wanavyofanya watu wote unaokunywa nao Pombe hapo kilabuni/baa.

Ni kweli marafiki zake (Wambea) wanaweza kutunga na kum-feed maneno mkeo ili kuharibu ndoa yenu nahivyo wao kuwa huru kutoka na wewe....yote yanawezekana.

Tatizo hapo sio mameno ya wambea, tatizo hapo ni kuwa Mkeo anahisi upweke ndani ya ndoa yenu, ni wazi kuwa humpi muda wa kutosha kwa vile muda mwingi unautumia ukiwa kazini na kilabuni. Unaporudi nyumbani unakuwa na kilevi kichwani hivyo sio wewe kwa asilimia zote....sijui unanielewa hapa?!!

Sasa kutokana na upweke huo ambao unaweza kumfanya afikirie mengi mabaya na hata kuzaa wivu mkali ndio unaomfanya asikilize na kuamini kila anachoambiwa na marafiki zake kwa vile wako pale kwa ajili yake na wanaonyesha kumjali, kumsikiliza na kumpa ushauri.....hata kama ushauri ni wa kubomboa bado atawaamini kwa vile Saikoloji yake inaamini kuwa "wanamjali, wanamsikiliza na kumthamini" zaidi kuliko wewe.

Ninachokiona hapa sio "umbea" bali ukosefu wa mawasiliano na wewe kushindwa kuzingatia nguzo muhimu iitwayo "Maelewano" Mf: wewe ni mnywaji ili asikunyime kile unachokipenda kutokana na pombe amekubali kuwa endelea kunywa lakini sio sana.....mkeo ame-complimise hapo!

Je! wewe umekubali kitu gani ambacho labda wewe hukipendi lakini kwa vile ni mkeo mpenzi na hutaki kumnyima raha ya kufanya jambo alitakalo ukakubali aendelee kufanya jambo hilo....SIDHANI!


Unatakiwa kumshukuru Mkeo kwa kukuamini na kukuruhusu uendelee kunywa pombe lakini usizidishe. Mkeo sio tu anakupenda bali pia anajali afya yako kwani sote tunajua Pombe sio nzuri kwa afya zetu.

Sasa kwa vile ameruhusu uendelee kunywa haina maana uende kilabuni kila siku na badala yake unaweza kunywa ukiwa nyumbani na hivyo yeye kupata muda wa kuwa na wewe. Unaweza kabisa kufurahia Bia ukiwa na familia yako sio washikaji kila siku.....wewe ni mume na baba hivyo jaribu kuzingatia majukumu yako kama Mwanaume wa kisasa.

Ukimya wako ndio unamfanya mwanamke huyo kuzidiwa na hasira na ndio maana hatakaki hata kuwa karibu na wewe, sio hivyo tu inawezekana anaamini kuwa umetoka nje ya ndoa na hataki kupata maamubukizo ya HIV (kitu ambacho hata mimi nampongeza) incase ulitereza nje kiukweli.

Nini cha kufanya: Watu wengi hukimbilia Talaka, lakini tukumbuke kuwa Talaka sio suluhisho la matatizo na mkikimbilia Talaka ni wazi hutomkomoa yeye mkeo au rafiki zake bali mtoto mliemleta hapa Duniani. Mtoto wenu ndio ataumia japokuwa ni ngumu sana kwa ninyi wazazi wake kuona maumivu yake Kiakili, Kimwili, Kisaikolojia na Kihisia.

Tafuta muda mzuri, ukiwa umetulia kiakili na zungumza na mkeo, Omba msamaha kwa kutokuonyesha kuwa unajali (hii itamlainisha na kumfanya akusikilize vema), mhakikishie ni kiasi gani unampenda na ni muhimu kiasi gani kwenye maisha yako.

Mwambie kuwa yote anayosikia kutoka kwa rafiki zake sio kweli na ili kumthibitishia hilo basi uko tayari kwenda kuangalia afya yako (vipimoo vya HIV)...majibu yakitoka safi ni wazi itampa amani moyoni na hivyo kuanza kulala kitanda kimoja na mume wake (wewe Manuel).

Weka wazi yote yalioujaza moyo wako kutokana na tabia ya mkeo ambayo ni wazi imesababishwa na unywaji wako wa Pombe.

Kumbuka Ndoa inajengwa na Nguzo 3, (1) Zote ambazo ni kwa mujibu wa Imani za Dini zenu, alafu kuna zile mbili za kidunia/kabila (inategemea unatoka wapi) ambazo ni (2) Uhusiano wa kimapenzi (3) Uhusiano wa kingono.

Uhusiano wa kimapenzi nao una Nguzo tano muhimu ambazo ni Heshimiana, Thaminiana, Shirikiana, Sikilizana/Elewana/kubaliana na mwasiliano (kuna topic inazungumzia kwa kirefu )sasa wote wawili mnatakiwa kuzingatia hayo ili kuimarisha uhusiano wenu wa kimapenzi.

Pia ongeza muda unaotumia kuwa na mkeo, badala ya kuzungumzia masuala kuhusu maisha na mtoto hakikisha mnazungumza kuhusu ninyi wawili kama wapenzi kitu ambacho kitawasaidia kuw akaribu zaidi na hata kuboresha uhusiano wenu wa kingono.

Punguza unywaji wa pombe kwa maelewano kuwa nae apunguze marafiki wasiokuwa na mpango, badili utaratibu wako wa kwenda kunywa pombe kilabuni na badala yake nunua chupa/kopo za pombe na kunywa huku mkeoyuko pembeni.

Kila la kheri!