Tuesday, 26 May 2009

Yaani hata sielewi nimjibu nini huyu EX-Ushauri

"Shikamoo dada Dinah, natumai wewe ni mzima wa afya na unaendelea kutusaidia sisi wenye matatizo mbalimbali ya kimapenzi. Hii ni mara yangu ya kwanza kuomba msaada kwako japo nimekuwa nikisoma article zako mbalimbali kupitia blog yako na kuona jinsi unavyosaidia watu mbalimbali.

Mimi ni msichana mwenye miaka 22, nipo masomoni nje ya nchi. Kabla sijaondoka hapo nyumbani nilikuwa boyfriend ambaye tulikutana kwenye pilikapilika za kimasomo (tuition). Sikuwa na uhakika kama kweli ananipenda lakini nikajikuta nimeanza nae urafiki na hatimaye kukutana kimwili.


Kwa nilivyouona uhusiano wetu nilihisi kama alitaka kuwa na mimi sababu ya uwezo wa kifamilia tulionao na si mapenzi sababu alikuwa na maisha ya kawaida sana (samahani kwa kutumia neno kapuku) na mara baada ya kufanya mapenzi nae alianza kunitreat tofauti na mwanzo. Hata nilipomwambia naenda kusoma nje hakurespond kama nilivyotarajia kwani hakuonyesha dalili ya kujali. Kwakifupi ilikuwa kama tumeachana japo hakuna alietamka.


Mara baada ya kufika huku nikamtumia namba yangu ya simu na tukawa tunawasiliana hadi niliporudi likizo yangu tukaendelea kama kawaida japo hali ya yeye kupenda kufanya mapenzi kila tukutanapo haikuisha. Alitaka tukutane kila wiki (ilifika kipindi hata nikiwa kwenye siku zangu alitaka tufanye na nikimgomea inakuwa ishu).


Niliporudi huku tuliendelea kuwasiliana tena kwa muda baadae akakata mawasiliano, nami nikaamua kukaa kimya nimuone atafanya nini lakini ndio akawa kimya moja kwa moja. Nikajua ndio tumemalizana.

Baada ya kuona kimya hicho nikaamua kuanzisha uhusianio mwingine na mtu mpya ambaye hakuwa mTanzania. Nilikuwa nae kwa mwaka na tulikuwa tunaendelea vizuri hadi alipo graduate na kwenda kwao na sitegemei kukutana nae tena.

Nilikaa kwa mwezi mmoja nikaanza kuwa na uhusiano na mvulana mwengine ambaye ni Mbongo mwenzangu. Najua dada unaweza kuniona somehow kicheche lakini naomba unisaidie maana nimechoka kubadili wavulana na tatizo langu kubwa siwezi kujizuia hasa mvulana akiwa mzuri.

Huyu mbongo nilienae sasa nilisoma nae O-level huko nyumbani. Kiukweli ni mzuri na historia yake ya nyuma alikuwa kigongo hasa kwa wasichana japo nilikuwa sijui wakati tunasomanae. Yeye mwenyewe ameniambia kweli alikuwa kicheche na akanipa album yake nimeona picha za hao wasichana wake wa zamani lakini kaniambia ameamua kutulia.

Nikaamua kujaribu bahati yangu kwa mara nyingine, nampenda sana huyu nilienae sasa na najaribu kumridhisha kwa kum-treat anavyotaka. (yeye ni out-going sana japo mimi si mtu wa viwanja kabisa). Yaani naona kama nimepata nilichokuwa natafuta kwa muda mrefu maana ana kila kitu nilichotaka mwandani wangu mtarajiwa awenacho ikiwemo elimu, uzuri, kujali na mambo mengine ndio maana najitahidi nim-keep ili tufike mbali na Mungu akipenda tufunge ndoa japo sina uhakika.


Dada kiufupi nimeshakuwa na wavulana 6 kabla ya huyu wa kwanza(1) alitaka tu awe wa kwanza kutembea na mimi na baadae alinidump. Wapili(2) alinipenda lakini alikuwa na elimu ndogo and tulikuwa tunaishi mtaa mmoja so nikam-dump. Watatu(3) nilikutana nae thru marafiki wa kalamu na tulisex siku moja baadae tukaachana sababu alitaka ndoa nami umri haukuruhusu naye alinizidi miaka7. Wanne(4) nilikutana nae kupitia rafiki yangu na tulishindana tabia tukaachana. Watano(5) ndo huyo tuliekutana nae tuition na tumeachana kimya kimya. Wasita (6)niliekutana nae huku kutoka Taifa lingine ambaye ame-graduate na kuondoka na wasaba(7) ndio huyu nilienae sasa katika wote hao niliekaa nae sana ni namba 5 & 6 wengine nilikaa nao si zaidi ya miezi3.


Tangu nilipojua nia ya huyo wa kwanza nikawa na hasira na wanaume so nikawa nawabadili kama nguo kulipiza kisasi lakini baadae nikaona ni ujinga na kuamua kutulia na huyo namba 5 nikajua nimepata.

Mwisho kabisa dada Dinah. Hivi karibuni huyo namba 5 ameanza kunitumia msg kuonyesha kuwa bado anajali baada ya kuwa kimya mwaka mzima ambao sikurudi huko, anasema ananipenda na alikuwa busy sababu ya maisha. Mimi sitaki kumrudia na hajui kama nilisha move on na kuwa na watu wengine.

Ninachotaka sasa ni kuwa na huyu nilienae lakini sijui jinsi gani nimwambie huyo wa huko Tanzania. Pia nimesikia mkilingana umri ni shida kuelewana, naomba imaana huyu wa sasa tuko nae sawa lakini naamini tutafika mbali japo sasa tuna miezi minne.

Natumai utanisaidia dada yangu.
Ni mimi Ney de great."

Dinah anasema:Marhaba Ney, mie ni mzima wa afya namshukuru Mungu. Asante sana kwa mail yako na kwa kueleza kwa uwazi historia ya maisha yako ya kimapenzi. Hakika umeanza kujihusisha na masuala ya Ngono na mahusiano ya kimapenzi mapema na kwa kasi kubwa sana.

Kutokana na maelezo yako inawezekana ktk ukuaji wako ulikosa sehemu fulani ya mapenzi kutoka kwa wazazi wako, kama ulivyodai kuwa kwenu mnauwezo wa kifedha. Mara zote familia zenye kujiweza huwa "busy" na shughuli za kuhakikisha pesa zinaingia na miradi inakwenda vema ili watoto na familia kwa ujumla kuendelea kuishi comfortably.....


Hii hufanya wazazi kujisahau na kutowapa mapenzi ya kutosha watoto wao na hivyo watoto ku-miss hayo mapenzi na matokeo yake baadhi huwa na tabia kama yako. Kwamba wanakuwa na msululu wa wapenzi wa muda mfupi ktk umri mdogo na kwa muda mfupi.


Nakuelewa uliposema kuwa uliamua kutoka au kubadili wanaume mara kwa mara (hope u were and still using Condoms) kwa vile ulikuwa unadhani unawakomoa, kitendo cha wewe kufanya hivyo au kuamini hivyo ni wazi ulikuwa umeathirika Kisaikolojia kutokana na uzoefu wako mbaya uliosababishwa na Mpenzi wako......baadhi ya wanawake huathirika vibaya kiasi kwamba wanapoteza hisia juu ya wanaume na kuibua hisia juu ya wanawake wenzao!


Lakini wewe ni mwanamke, na kwa kawaida mwanamke anachagua nani wa kumpa mwili wake na lini hivyo basi suala la wewe kushindwa kujizuia ikiwa mwanaume ni "mzuri" sio sababu ya kutosha kukufanya wewe kujipelekesha kwa wanaume hao ambao kwa namna moja au nyingine hawana mapenzi juu yako.....anyway, hatuwezi kubadili yaliyokwisha tokea tusonge mbele sasa.


Pongezi za dhati kwa uamuzi wako wa busara wa kuacha "katabia kale kachafu ka kulipiza kisasi", kutokana na maumbile ya mwanamke kitendo cha kufanya ngono na wanaume wengi hasa ktk umri mdogo unaweza kusababisha mabadiliko makubwa sana ya mwili wako hasa sehemu nyeti licha ya hivyo pia unaweza kupata maambukizo ya Zinaa.


Kutokana na umri wako mdogo na bahati uliyonayo ya kuendelea na masomo ni vema basi ukazingatia zaidi masomo na kufikiria maisha yako ya baadae kama ambavyo baadhi ya wachangia walivyokushauri.


Pamoja na kusema hivyo sina maana kuwa uachane na huyo mpenzi wako, la hasha! Endelea na uhusiano wenu lakini usiweke effort yote kwenye mapenzi na kum-treat kwa kila anachokitaka na badala yake jifunze kuwa na mipaka ili usije umia baadae ikiwa uhusiano hautokuwa vile unavyotaka hapo baadae.

Huyo Namba tano achana nae, Block namba yake au wewe badilisha namba yako, huitaji kumuambia chochote wala kumhabarisha kuhusu maisha yako na mpenzi wako wa sasa kwani hausiki in what so ever!

Kama kweli mnapendana na mmetulia (wewe na Mpenzi No.7) endeleeni hivyo na furahieni maisha yenu ya ujana. Kumbuka kuchukulia uhusiano wenu kawaida na kama Mungu anataka ninyi wawili siku moja kuwa mume na mke basi itakuwa hivyo, usilazimishe.

Kuwa muangalifu, na kumbuka mwanamke ana haki zote juu ya mwili wake, hakikisha men dont abuse it kwa kujiheshimu nakuheshimu utu wako, pia maisha yako ya baadae yapo mikononi mwako usiruhusu mtu baki akupokonye!

Kila la kheri!

Thursday, 21 May 2009

It's Two!!


Leo ni Siku na Mwezi ambapo D'hicious inasheherekea Miaka miwili tangu ianzishwe. Siku hii ni maalumu (Special) sana kwangu, sio kwavile ni muanzilishi wa Dinahicious Blog/Live na labda mwanamke wa kwanza kuzungumzia "Unyago" kwa uwazi na kwa faida ya kila mtu (wake kwa waume) bali pia tarehe kama hii kuna tukio muhimu sana lililo badilisha maisha yangu lilitokea hivyo basi ninafuraha sana.....miaka 2! Huh!
Kabla sijasema mengi napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukurani zangu za dhati kwako wewe Msomaji, Mchangiaji, Msikilizaji wa Bongo Radio na Muuliza maswali, wote kwa pamoja ndio mnaifanya D'hicious Blog/live kuendelea kuwepo. Pia shukrani kwako wewe uliyoiweka D'hicious kwenye blogs/tovuti yako.

D'hicious imefanikiwa kwa kiasi kikubwa tangu ianzishwe miaka miwili iliyopita. Dinahicious imerudisha mahusiano mengi ambayo yalivunjika au yalikuwa yakielekea kuvunjika. Dinahicious imefanikisha baadhi ya wasomaji wake kufanikiwa kushika Mimba na kuzaa kwa kutumia njia asilia kabisa.

Dinahicious imerudisha ndoa na kuboresha ndoa nyingi, Dinahicious "imesababisha" watu kupata wapenzi na hatimae kufunga ndoa kwa kutumia mbinu zilizoelezwa mahali hapa, vilevile D'hicious imefanikisha wake kwa waume kubadili mienendo yao na kufurahia maisha na mafanikio makubwa kupita yote ni kwa Jamii ya Kibongo taratibu sasa inakubali kuzungumzia Ngono, Mahusiano na Mapenzi kwa uwazi bila uoga wala aibu.

Dinahicious ilivyoanza hakukuwa na blog au tovuti ya Kiswahili yenye kuzungumzia Ngono kwa uwazi katika mtindo wa kufundisha na kukumbusha. Lakini hivi sasa hali ni tofauti kwani wengi wameibuka na kujisikia huru kuizungumzia ngono bila aibu.....ni mafanikio makubwa kwa upande wangu na ninahisi faraja sana kuona kuwa, kwa kufanya kitu kidogo tu nimeweza kusababisha mabadiliko kwenye sehemu fulani ya Jamii yangu ya Kibongo.

Kama ambavyo mmeshuhudia tangu kuanza kwa mwaka huu kumekuwa na mabadiliko kwa maana kuwa, nimekuwa nikijibu maswali zaidi kuliko kutoa mafunzo kama ilivyokuwa hapo awali. Hii yote sio tu kutokana na uwingi wa maswali ninayopokea bali pia ni kwasababu matumizi mabaya ya kazi zangu.

Baadhi ya Magazeti ya Udaku na Blogs wamekuwa wakitumia kazi zangu bila kuweka vielelezo kuwa wametoa kwangu au kuweka anuani ya D'hicious, sasa ili kupunguza matumizi mabaya ya kazi zangu nimeamua kufanya mafunzo kwa njia ya sauti (radio) na sio maandishi (blog).

Kwa maana hiyo basi D'hicous itaendela ku-publish maswali yote ninayopokea na nitakuwa nayajibu kwa uwazi kabisa kama kawaida yangu na mafunzo yataendela kupatikana Radioni.

Juma Pili hii kutakuwa na kipindi maalum radioni kwa ajili ya kuadhimisha Miaka miwili ya blog na kipindi chenyewe, unakaribishwa sana ili kutoa mchango wako kwa njia ya simu.

Mungu aendelee kukupa uzima na endelea kujikumbusha/kujifunza mambo muhimu ili kuboresha uhusiano wako wa kimapenzi kupitia D'hicious blog/live.

**GQ, Dj Dennis, Mpenzi Mume wangu na SamChom bila ninyi heri nitoweke Duniani.

Mwisho mzuri wa wiki,
Asante sana.

Tuesday, 19 May 2009

Mume hana uzazi, naombwa kumimbisha-Ushauri

"Mimi ni bosi nimeanzisha Kampuni yangu hivi karibuni. Kwenye Kampuni yangu nimeajiri wanawake wengi kuliko wanaume. Sifa ya kampuni yangu ni nidhamu na kweli wafanyakazi wote wanajiheshimu, kosa likitokea linaamuliwa kihekima.


Mimi ni mume wa mtu na ninaiheshimu sana ndoa yangu na hakuna kitu kinachoniuma kama kutoka nje ya ndoa, haya nayasikia mitaani na kwenye vyombo vya Habari. Watu wanasema tembea uone, Ishi na watu ujifunze na lisemwalo lipo kama halipo hujaliona tu bali linakuja.


Siku moja nikiwa Ofisini nikichambua CVs za wafanyakazi wangu na utendaji wao, hodi ilisikika mlangoni. Sio kawaida mida kama hiyo ya jioni kwa wafanyakazi kuja ofisini kwangu wengi wanakuwa wakifunga mahesabu yao tayari kuondoka.


"Bosi samahani sana, kama huna muda nitakuja siku nyingine, lakini hili tatizo nililo nalo halihitaji muda, kwani nimehangaika nikaona mtu pekee ninayeweza kumuamini ni wewe" alisema huyo mbisha hodi na alikuwa bado anaogopa huku akiwa kainama chini. "Ok, kaa hapo kwenye kiti nasema shida yako" Nilimwambia, huku nikijiuliza kichwani ni shida gani? kwani katika wafanyakazi ninaowaheshimu ni pamoja na huyu dada, umri wake ni miaka 34.


"Bosi naomba chonde chonde, hiki ninachokuambia kiwe mimi na wewe na naomba saana unikubalie, kwani usiponikubalia sidhani kama nitaweza kufanya kazi hapa tena, je nitakuangaliaje machoni, je nitaiwaka wapi sura yangu. Naomba usinielewe vibaya, mimi tangu nizaliwe sijawahi kutenda dhambi, sijawahi…" Alinyamaza nakuanza kulia.


Hali hii kidogo ilinishangaza, nakunifanya niache kazi yote niliyokuwa nikiifanya, nilimwangalia kwa makini huyu dada na kujaribu kufikiria tatizo analoweza kudiriki kuja kuniambia nikashindwa kuelewa.


"Naomba ujisikie amani, kwani nakuheshimu na moja ya kazi zangu ingawaje mimi ni bosi wenu, lakini pia ni kama mzazi, kaka, hata ukisema mume au vyovyote ilimradi haivunji hadhi, heshima ya kila mmoja wetu au sio? sasa ongea kama unaongea na mtu unayejisikia huru kuongea nae".


"Sikuhakikishii moja kwa moja kuwa ninaweza kulitatua tatizo lako, lakini nikilisikia kama lipo ndani ya uwezo wangu nitalitatua. lakini kama nikishidwa nitakuambia na halitatoka nje ya mimi na wewe kama unataka iwe hivyo, sasa uwe huru’’ nilitulia na kumwangalia.

"Bosi naogopa sana, na tangu tulizungumze mimi na mume wangu, nimekuwa sina raha, sio kwasababu limetusibu bali ni hizo njia za kulitatua ni nzito na sizipendi kama asivyozipenda mume wangu, lakini yeye sasa ameng’angania kuwa tufanye"


Akaanza kuelezea tatizo hilo, kuwa wao wameoana siku nyingi karibu ya miaka 16 sasa, katika mihangaiko yao wamechuma na wana hali nzuri kimaisha, kwani wana nyumba zaidi ya nne walizopangisha , wana magari ya biashara nk. Yeye alikuja kufanya kazi kwangu kwasababu alihitaji kupata ujuzi wa kuweza kufungua kampuni yao baadaye, alishanieleza hili kabla. Tatizo linalowakabili, tangu waoane hawajawahi kupata mtoto.


Awali walidhani mke ndiye mwenye matatizo, na jamii ilijaribu kuingilia kati ikashindwa kutokana na mapenzi waliyokuwa nayo. Baada ya miaka kwenda, waliamua kwenda kuwaona Wataalamu ili wajue tatizo ni nini.

Kila hospitali waliyokwenda waliambiwa kuwa "mume" ndiye mwenye matatizo. Na kweli katika kukumbuka, wakati wapo kwenye fungate walipata ajali, na mume wake aliumia maeneo ya mgongo, na kiunoni. Alitibiwa akapona na majombozi yalikuwa kama kawaida, lakini kumbe ile ajali iliharibu na mengine.


Binti yule aliendelea "hivi karibuni mume wangu amesema anahitaji mtoto, lakini hataki wa kurithi anataka azaliwe na mimi na anataka isijulikane kuwa anatatizo. Kwahiyo wazo lake ni mimi nimtafute mume anayefanana nae, mwenye heshima na anayejua kutunza siri na ambaye hataweza kwa vyovyote kuleta fujo hatiamaye" alimiliza kwa uchungu.


"Masharti yake mengine ni kuwa, yeye hataki kumjua huyo mume nitakayetembea naye na asijue nini kinachoendelea. Pili huyo mume akubali na ajue kuwa yeye ameridhia, kwa masharti kuwa iwe siri, pia mke wa huyo mume asijue", alimaliza binti yule.


Jasho lilinitoka, nikatamani kumfukuza huyu dada, lakini niliheshimu wadhifa wangu na kweli nilibadilika kwani yule dada aliponiona nilivyobadilika alianza kutetemeka kwa woga. Nilichoweza kumwambia ni kuwa anipe muda nifikirie kwanza mimi sio Mungu kuwa natoa watoto. Pili nitahakikishaje aliyoyasema ni kweli? tatu, hilo linavunja miiko ya ndoa yangu.


Alivyoondoka pale nilimuonea huruma, kwani nahisi alijuta kuniambia. licha ya kumpa matumaini ya kuwa asijali azidi kuja kazini, na nitajitahidi kusaidiana naye kulitafutia ufumbuzi.

Je dada Dinah na wengine mwasemaje, naomba busara zenu!
emu-three"

Sunday, 17 May 2009

Mume ni "control freak" nifanyaje aache?-Ushauri

"Hi dada dinah, pole na mizunguko kazi na maswali mengine magumu hata kuyatatua mwenyewe. Mimi ni mama mwenye mtoto mmja nimeolewa nina miaka minne katika ndoa yangu nilizaliwa miaka kadhaa iliyopita but not below 23.


Mimi na mume wangu tulikua tuna pendana sana na mpaka sasa mimi bado nampenda tena sana. Dada Dinah tatizo langu kubwa kwa mume wangu ni kwamba simuelewi kwani tangu tumeanza kuishi pamoja hataki mimi niende nyumbani kwetu wala niwasiliane na ndugu zangu ila kwao na kuwasiliana na ndugu zake hanizuii.


Nimejaribu kumtumia mama yangu amuombe niende lakini bado anatoa sababu, kwa mfano mama alimuomba niende kuwaona mume wangu akasema muda bado. Muda ulipo fika akatafuta safari akaniaacha mimi nikashidwa kuondoka.

Dinah anasema; Nadhani hii tabia yake ya kukukataza wewe kwenda kwenu ni uoga unaoweza kusababishwa na uzoefu mbaya kutoka kwa watu wengine wanaomhusu, huenda ikawa ex's au hata ndugu jamaa na marafiki ambao wapenzi/wake zao walikuwa wakitumia kisingizo cha kwenda "kuwaona nyumbani" na huko walikuwa wakifanya mambo machafu.


Natambua kwenda nyumbani ni muhimu na wazazi wako wangependa kukuona sio tu wewe bali hata wajukuu zao lakini kama inashindikana kutokana na kutojiamini kwa mume wako basi jaribu kumshawishi muende wote kuwaona nyumbani, ikishindikana basi waombe ndugu zake waje kukutembelea nyumbani kwako.

Umesema kuwa unampenda mumeo, kama kweli unampenda basi jaribu kumuelewa. Yeye kama mwanaume wa Kibongo hata siku moja hawezi kukueleza yaliyomkuta huko nyuma hasa kama yalihusu mpenzi wake wa zamani au yanahusisha yeye kuonekana muoga wa "kuchezewa denge" na wajanja.

********************************************************************************

Pili siku hizi kabadilika sana kiasi najuta hata kuolewa yaani kidogo kanitukana mara mshenzi mara mjinga mara ananitisha kunipiga kwa kusema mimi simjui vizuri ndio maana nashindwa kufanya atakavyo, ukweli ninachanganyikiwa mume wangu anakuwa kigeugeu anaweza akakwambia mimi sipendi uvaenguo ndefu ukivaa fupi kwa muda huo aliosema anafurahi sasa itokee siku nyingine akuambie tutoke ukivaa hiyo nguo fupi anaanza unaenda kumuonyesha nani? unatakautongozwe kwani mimi sikutoshi? ukivaa ndefu au suruali ananyamaza.

Dinah anasema; Mumeo anaamini ktk umilikishi, pamoja na kusema hivyo uhusiano wenu unakosa mawasiliano kitu ambacho ni muhimu sana ili yeye akuelewe wewe na wewe kumuelewa yeye na hiyo itaepusha hali ya kuchanganyikiwa kwako.

Mumeo anadhani kitendo cha kukuoa wewe basi anakumiliki na anataka ufanye yale atakayo yeye bila kujali hisia zako. Mumeo hajui kuwa wanawake huwa tunavaa kutoakana na tunavyojisikiwa au "mood", mavazi hutufanya tujisikie wazuri, warembo na tunavutia, mavazi hutufanya tufurahie siku, mavazi hutufanya tuwe na huzuni, mavazi hutufanya tutake kufanya mapenzi n.k.

Sasa, ili mumeo aelewe hilo ni kazi wajibu wako wewe kama mwanamke kumuelewesha kwa kutumia moja ya nguzo muhimu ya kuboresha uhusiano nayo ni Mawasiliano. Wakati unawakilisha hoja yako hakikisha unaiwakalisha kwa upendo, upole ili akuelewe vema pia kumbukakutumia uanamke wako ili kupata utakacho.

Wanaume wanajua nini hasa huwavutia kutoka kwa wanawake, wapo wanaovutiwa na vifua, wengine wanavutiwa na sura na baadhi ni makalio na wengi huvutiwa na sehemu ya mapaja. sasa kama mumeo anavutiwa zaidi na mapaja yako niwazi kuwa hatopenda ku-share sehemu hiyo na wanaume wengine hata kama ni kwa kuyaangalia tu.

Anashindwa kukuambia moja kwa moja kuhusiana na kutojiamini kwake na badala yake anatumia lugha ya ukali ili kufikisha ujumbe kuwa "sipendi wanaume wengine waone mali zangu"....sijui unanielewa dada mdogo?

Kumbuka kuwa huyo ni mumeo hivyo anatsahili kuheshimiwa na kama akikataa kata kata wewe kuvaa nguo fupi nje ya nyumba yenu basi jaribu kumuelewa na wewe tafuta mavazi mengine ambayo yataendelea kukufanya uvutie, ujisikie mrembo na mwenye furaha...sio lazima yawe mafupi sana (juu ya magoti) yanaweza kuwa chini kidogo ya magoti nakuachia sehemu kuwa ya miguu yako kuonekana na hiyo itakufanya ujisikie swaaaaaafi kabisa.

*****************************************************************************

Nimefikisha mara mbili nakuta msg zisizoeleweka kwenye simu yake ukimuuliza anakwambia hivi mara vile ilimladi tu usiendelee kumuuliza. Lakini hivi yeye akipiga simu ikatokea nimechelewa kupokea akirudi kutoka kazini nyumba inakosa amani kabisa.

Dinah anasema; Unatakiwa kupangilia maswali yako ili kupata majibu ya kuridhisha kama ujumbe wa simu ulioukuta unahashiria yeye kutokuwa muaminifu, kamwe hata siku moja usikubali maelezo yake ambayo unahisi kutoyaamini.

Hakikisha unafikiri huku unaongea/uliza pia sikiliza majibu yake huku unayatafakari ili akimaliza kujibu unamtundika swali lingine hii inakusaidia kupata ukweli na kama ukihisi unadanganywa basi ni wakati wa kuweka rules kwenye uhusiano wenu.

Huyo ni mume wako, mmeoana na sio amekuoa hivyo basi unahaki ya kusikilizwa, kuthaminiwa, kujua marafiki zake, wafanya kazi wenzake, ndugu na jamaa zake, kujua anawasiliana na akina nani na uhusiano wao gani, wapi hufanya matembezi na nyingine zote uzijuazo wewe ndani ya ndoa yanu. Kama unahisi unakosa haki zako kwenye ndoa yako ni wakati wa kuzidai na kuhakikisha zinaheshimiwa.

**************************************************************************

Juzi simu yangu ilijizima nikiwa salon iliyo nje ya uzio wa nyumba tanayo ishi akampigia rafiki yake akaja mpaka saloon nikaongea naye kupitia simu ya rafiki yake jamani hakukaa mpaka muda wa kazi uishe karudi hakuna salam ananiambia utanieleza uliko kuwa huku anatafuta mkanda aanze shunghuli mimi nikamwambia labda anasababu zake tu nyingine lakini mimi sijatoka hata gengeni sikwenda.


Siku hiyo ndipo alipo muita mtoto wake mwenye miaka minne nilimkuta naye akamuuliza, ndipo mtoto akamwambia "mama leo hajaenda mahali zaidi ya saloon anako sema" mume wangu akaona aibu akaondoka dada hata sasa nikimuuliza kwa nini ananifanyia hivyo ananiambia nisimkumbushe anakasirika mpaka nashindwa hata kuendelea kumuuliza dada ni mengi lakini naomba niasidae kwanza kama haya mama na nikisema nimalize yote leo nita kesha naandika. Ni mimi Mama T"


Dinah anasema: Samahani nilipitiwa na kudhani nimekwisha kujibu, pole sana kwa usumbufu niliokusababishia. naja kumalizia....Mama T, mume wako hajiamini hali inayomfanya ashindwe kukuamini wewe. Ukijiamini kuwa ni mpenzi mwema, unajua wajibu wako kwa mkeo huwezi kuhofia vitu vidogo kama kutopokea simu......wanaume wengi ambao sio waaminifu ndio huwa na tabia hiyo aliyonayo mumeo.


Huenda hajawahi kutoka nje ya ndoa yenu ila yuko njiani kufanya hivyo ndio maana anaonyesha wivu kupita kiasi, kutokana na ego zao (wanaume) huwa hawapendi au niseme hawawezi ku-hadle the idea ya "kutiliwa/tombewa" mkewe achilia mbali mpenzi wake, sasa kama yeye anafanya hivyo au anataka kufanya hivyo anataka kuhakikisha hakuna wa kulipiza kisasi kwa mkewe kwa kudhani kuwa atakaefanikiwa kukufanya wewe atafaidi kama yeye anavyo/atakavyofaidi mwanamke mwingine.


Suala muhimu ni kuzungumzia matatizo yenu kwa wazi na bila kuhusisha hasira. Unapozungumza na mumeo kamwe usianze kwa kuuliza maswali kama "kwanini unanifanyia hivi au vile" na badala yake unamuweka katka mazingira mazuri na tulivu kiakili na kimwili (usihusishe ngono, kwani atakupa majibu ili kupata mambo na sio kumaanisha) kisha unazungumza nae sio kutaka majibu kwa kuuliza bali akusikilize na kukuelewa.


Unaweza kuanza..MF-"Ayoub nakupenda sana mume wangu, najua kuna vitu vingi sana nafanya ambavyo huwa havikufurahishi lakini kati ya hivyo hakuna hata kimoja kinahusisha mimi mkeo kusaliti ndoa yetu. Naomba mpenzi wangu ujenge uaminifu kwangu kamavile ninavyokuamini".....wakati unasema hayo na mengine unayodhani ni muhimu ili kusaidia kubadilisha tabia yake mbaya basi unapaswa kutumia uanamke wako kumfanya aendelee kuwa interested kukusikiliza.

Wanaume wakati mwingine wanahitaji muongozo kutoka kwa wake zao as if ni mama zao, sio ktk kuwa-control,lisha, ogesha,beba n.k bali kuwaelekeza namna ya kuishi kama pea/wapenzi/wenza......sisi wanawake tunabahati kuwa tunafundishwa kabla hatujaishi na wanaume au hata kuolewa. Wanaume wengi wanajifunza wenyewe tu hapa Duniani hivyo basi kuna mengi hawayajui hasa namna ya kuishi na mwanamke lakini wewe kama mwanamke unatakiwa kuongoza (sio kwa kumuambia hujui kitu la hasha! tumia busara na mapenzi).


Sasa, ikiwa hamtoelewana ninyi kama wapenzi basi ni vema kupeleka matatizo yenu juu zaidi. Kwa kawaida wanandoa huwa tunakimbilia kwa wazazi, lakini kumbuka wazazi wanatupenda sisi watoto wao hivyo kwa vyovyote vile kutakuwa na "kaupendeleo" upande mmoja tofauti kabisa kama mkikutana na mtu baki lakini anauzoefu au niseme mtaalam wa mambo ya ndoa na mahusiano itakuwa vema zaidi.


Labda nikuulize au unaweza kujiuliza mwenyewe....je unampenda mumeo? Uko tayari kujaribu kuifanya ndoa yenu iwe bora au unahisi kuchoka na mapenzi yanapungua kutokana na visa vingi, ila unakaa ndoani ili "usidhalilishe" wazazi wako na jamii kw aujumla?

Kumbuka kwamba, tunafunga ndoa kwa vile tunapendana na tunataka kuishi pamoja kila siku za maisha yetu kwa furaha, amani na upendo mpaka kifo kitutenganishe. Lakini kama ndoa inakosa au haina vile vigezo muhimu kwanini hasa ilifunga ndoa kwanini uendelee kuwepo ndani ya ndoa hiyo?

Majibu utakayopata kuhusua hisia zako juu ya ndoa yako, uhusiano wako na mumeo na hisia zako za kimapenzi kwa mumeo zitakusaidia kufanya moja ya maamuzi makuu mawili yafuatayo:-

1-Kwa kushirikiana nyote wawili mjitahidi na kufanya ndoa yenu iwe bora.
Au
2-Kuvunja ndoa hiyo na kila mmoja wenu kuendelea na maisha kivyake.

Kila lakheri.

Wednesday, 13 May 2009

Ndoa imenishinda, Mume anitaka tena-Ushauri!

"Dada dinah! Baada ya kusoma blogu yako na kuona unawasaidia wengi nami leo nimeamua kuandika mkasa wangu. Mimi nina umri wa miaka 28 nimeolewa miaka minne iliyopita na kwenye ndoa yetu tumebahatika kupata mtoto mmoja wa kike.


Dada dinah kabla ya kuoana na mume wangu tulikuwa wachumba kwa takriban miaka minne, kwenye kipindi cha uchumba ni mwaka mmoja tu ndo tuliishi kwa mapenzi ya kweli na raha za kila aina mwaka uliofuata akaanza visa, mara namfuma na msg za wanawake nikimuuliza anakuwa mkali, nikienda kwake nakutavipodozi au nguo za ndani nilizoacha zimefichwa.


Dada dinah mapenzi yakawa hayapo tena, naweza nikakaa wiki mbili sijaenda kwake na siku nikienda yeye amechoka na hataki tufanye chochote. Kuna siku nilienda akanikatalia tusifanye kitu, kesho yake asubuhi nikawa nafanya usafi wa nafagia nje nikakuta mfuko ndani kuna condom 3 zilizotumika.


Nilisikia kufa nikaziweka kitandani nikaacha kufanya usafi nikaondoka kwa hasira. Aliporudi alipozikuta akaanza kupiga simu na kuomba msamaha, kwa kuwa bado nilikuwa nampenda yakaisha. Lakini tabia hiyo iliendelea na nilipozidi kumbana akatamka kwamba hatujaoana kwahiyo bado anachagua yupi atakayemfaa kuwa mke kwa kweli niliumia sana na mapenzi yakaanza kupungua.


Ikafikia mahali nikawa nasikia tetesi kwa majirani anavyobadili wanawake kama haitoshi akatembea na rafiki yangu nilipojua hilo kwa kweli nikaamua kuachana nae. Alikiri na kuomba msamaha lakini ilikuwa nimeshachoshwa nae, akawa anaomba msamaha sana na kunibembeleza kwa bahati mbaya nikaja kushika ujauzito wake. Alipojua akaanza kuharakisha kufunga ndoa na kunisihi nisitoe.

Kama binadamu nikamuua kusamehe na tukafunga ndoa 2005, nikajua atabadilika ktk ndoa lakini wapi mambo yakawa yaleyale kufuma msg, akisafiri nakuta condom kwenye begi kasahau, mbaya zaidi akaanza manyanyaso na kashfa ndani ya nyumba na vipigo bila sababu za msingi.


Nikaamua kuvumilia nilee mtoto, Mungu amenisaidia mwanangu ana miaka mitatu sasa na nimebahatika kupata kazi kwenye Shirika moja nje ya Dar nikaamua kuondoka na nimeanza maisha mapya. Kwa kweli mapenzi naye yameisha kabisa hata yale ya kujilazimisha.

Sasa anaomba msamaha nirudi atajirekebisha na kwa mwezi anakuja mara 3. Jamani mie nimechoka kurudi siwezi na ninamuogopa saana kukutana nae kimwili kwa tabia zake tusijepeana maradhi huwa namsihi tutumie condom hataki.

Mie nimeamua kuachana nae kabisa na yeye nimemwambia lakini anazidi kuomba msamaha na kukiri makosa yake na anahidi kujirekebisha, kaahidi mpaka kuninunulia gari nimsamehe. Jamani hebu mnishauri mie nimechoka nae na sitaki kurudiana nae maisha nayoishi sasa ni ya amani sana."

Jawabu: Hongera sana kwa hatua uliyoichukua na msimamo unaoendelea nao. Inasikitisha kuona kwamba kile kipindi ambacho watu ndio hufurahia zaidi wewe ulikutana na vituko vingi kuliko umri uliokuwa nao kipindi hicho.

Nashindwa kujizuia kufikiria kuwa ulikubali kufunga ndoa kwa vile tu ulikuwa na Mimba, kama isingekuwa mimba labda usingeolewa nae.....kwa bahati mbaya hatuwezi kubadili yaliyokwisha tokea.

Kwa kawaida wanandoa huwa wanashauriwa kuto kuachana au kuvunja ndoa, hata mimi sipendi kabisa kuharibu ndoa au uhusiano lakini ikiwa mhusika anahatarisha maisha yako basi inabidi ndoa ivunjike tu ili kuokoa maisha yako.

Kuachana nae kienyeji tu haitomfanya aache kukusumbua. Suala muhimu ni kutafuta Wanasheria wanajihusiaha na masuala ya Ndoa na Talaka kwa msaada zaidi ili umtaliki mumeo kisheria kitu kitakachomuondolea "mamlaka" anayodhani anayo juu yako kwa vile tu mlifunga ndoa.

Kama unapata taabu kuwapata Wanasheria (najua Wakibongo wanamaringo sana, watakuzunguusha weee), unaweza kutembelea Mahakama yeyote iliyokaribu na wewe na kuomba kuonana na Jaji na kumueleza nia yako ya kumtaliki mumeo na sababu ya kutaka kufanya hivyo.


Yeye atakuuliza maswali machache kama vile, mara ya mwisho kufanya mapenzi ilikuwa lini? Sasa anaishi wapi? na wewe unaishi wapi? Mmetengena kwa muda gani? pia unaweza kuulizwa kama unaweza kumudu mahitaji ya mtoto n.k. kisha utapatiwa barua ya kumulika mumeo hapo Mahakamani ili wasikilize upande wake wa "hadithi".....haijalishi hata kama atatoa machozi ya damu na kuomba misamaha yote hakikisha unabaki na msimamo wako, kuwa ndoa imekushinda kutokana na tabia yake chafu.


Pamoja na kuwa wewe na soon Ex mume wako mnatofauti na hutaki kubaki kwenye ndoa, hakikisha mtoto anakuwa na uhusiano mzuri na baba yake. Kamwe usim-feed mtoto wako na uchafu aliokuwa anaufanya baba'ke, kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha Binti yako kujenga chuki na baba yake kitu ambacho nisingeshauri.

Kila la kheri!

Friday, 8 May 2009

Mchumba anipenda mie Moyo mzito-Ushauri!

"Dear dinah, Natumaini hujambo na mwenyezi Mungu anazidi kukuongezea nguvu katika kazi yako ya kudumisha mahusiano ya watanzania wenzako. Dinah mpenzi mimi ni binti mwenye umri wa miaka 24.

Tatizo langu linalo nileta hapa leo ni ukosefu wa mapenzi kutoka kwangu mimi kwenda kwa mwenzangu. Labda nikuelezee scenario ya mapenzi yangu. Mimi na kijana mmoja tulikuwa majirani enzi za utoto wetu na tukaenda shule moja ya msingi, ila tulivokuwa wakubwa wakati tunaingia sekondari wazazi wa mwenzangu walihama mkoa tuliokuwepo na kuhamia mkoa mwingine.


Tukaja kukutana high school moja tena tukawa marafiki wa kawaida tu kwa sababu tulikuwa tukijuana kabla. Baada ya hapo kwa sababu mwenzangu kwao walikuwa na uwezo akaenda kusoma chuo kikuu nje ya nchi mimi nikabaki chuo kikuu hapa Tz.


Akiwa huko hatukuwahi kuwa na mawasiliano hata siku moja. Ikatokea siku nikapokea simu kutoka kwake akisema alinikumbuka na anataka kunisalimia tu hii ilikuwa mwaka mmoja kabla hajarudi nchini. Tangu hapo akawa anakawaida ya kunipigia simu kila siku.


Kikafikia kipindi akaniuliza kama nina mpenzi nikasema sina naye akasema hana tukaanza kuwa wapenzi kwa simu tu kama ilivyo kawaida ya wapenzi wa mbali. Tukaanza kuahidiana tutaoana akawa amejenga mawazo anamchumba Tz na mimi nikajua yeye ndiye mchumba wangu.


Lakini hapa katikati takribani miezi sita imebaki ili yeye mwenzangu arudi toka shule nikapata mtu (intruder) ambaye tulipendana ile ya mhemko kwa kuonana kwa mara ya kwanza.Wakati naanza mahusiano ya mapenzi na huyo intruder nilijitahidi kumfuta huyo rafiki yangu wa mbali katika mawazo yangu na nikafanikiwa.


Nilikuwa naona mapenzi ya simu ni kudanganyana tu hamna lolote. Ikafikia kwamba nikawa sina uhakika tena kama nampenda huyo rafiki wa nje(Ambaye tunapigiana simu) ama la. Mara nayo mahusiano yangu na intruder yakawa ya muda mfupi sana na wao walihama nchi kabisaa, kwani baba yake alikuwa Balozi nchini Tz kutoka nchi fulani ya nje.


Ilimbidi aondoke awafate wazazi wake na akawa amepata na shule ya masters huko huko kwa hiyo asingeweza kubaki Tz hata kama angependa, akanishawishi twende wote na wazazi wake watanitafutia shule nikakataa kwenda. Baadae nikashtuka na kuona kwamba huyu mtu atanipotezea wakati kwani sioni future kati yangu na yeye japokuwa mawasiliano yetu yalikuwa mazuri tu.


Sikuwa na la kufanya ikanibidi nimuache mwezi mmoja tu baada ya yeye kuondoka chini. Japokuwa kilikuwa kitu kigumu sana kufanya kwa wakati huo ukizingatia nimeshaharibu mahusiano na mchumba wangu wa nje.


Miezi miwili baada ya intruder kuondoka mwenzangu naye akarudi Tz. Na aliporudi alikuwa na higher expectations kuhusu mimi akataka sana kuniona nikawa namkimbia. Kijana wa watu haku give up na alikuwa akinifuatilia kila pahala, Sikuweza kumkimbia tena ikabidi sasa nimpe nafasi aweze kuonana na mimi.


Tukaanza kuzoeana kidogo kidogo. Ikafika siku tukaelezana story za maisha na nini kilipita hapo kati na kwanini nilikuwa sitaki kumuona, sikumficha nikamwambia ukweli kwani alikuwa na haki ya kuamua lolote na isingekuwa vizuri kuwa na siri kati yetu kama nimeamua kujitosa kuwa naye.


Mungu akasaidia hakuniacha na akanisamehe kwa sababu alikuwa akinipenda kwa dhati. Miezi mitatu baadae mpenzi huyu akapropose nami nikakubali. Lakini kusema ukweli ndani ya nafsi yangu nilikuwa nimeshamfuta wakati tunakutana ikawa najilazimisha kuwa naye na sikujua hata kwanini nilikubali hiyo proposal yake.


Siku zilivozidi kwenda ikawa nazidi kuona simpendi ikafikia hatua kila kitu akikifanya mie nakiona kibaya. Sasa nashindwa kuelewa what is happening to me. Mwenzangu ananipenda sana na anajionesha dhahiri kama ananipenda lakini mimi nimeshidwa kurudisha mapenzi, harusi bado miezi mitatu na bwana harusi simpendi nifanye?


Labda nimuelezee kidogo jinsi yeye alivo kitabia.. Ni mtaratibu anaongea kwa adabu, nimsikivu na anamapenzi kwa ndugu zake na ndugu zangu pia. Mapenzi anayajua vilivyo. Zaidi ya yote kusema ukweli kaka wa watu ni mzuri anamvuto wa haja, anapesa za kutosha hatuwezi kulala njaa.


Ukweli ni kwamba kumuacha sitaki nataka kupewa ushauri vipi nifanye nipate mapenzi nimpende yeye kama yeye. Maana yake sijawahi kupata mtu mwenye mapenzi ya dhati kama aliyo nayo yeye? Lakini moyo wangu umekuwa mzito kwake.

Please Help kuyajenga haya mapenzi na si kuyabomoa. Kwani niliambiwa we can learn to fall in love!
yours Tumaini"

Dinah anasema: Tumaini hadithi yako ni nzuri mpaka raha kuisoma, ulichonifurahisha ni kuwa wazi kw ampenzi wako na kumueleza ukweli ulivyokuwa ni wanawake wachache sana wenye uwezo wa kufanya hivyo, wako radhi kudanganya wapate "kumchuna" mtu kuliko kumpa mtu ukweli na nafasi ya kufanya uamuzi wa busara.


Kutokana na maelezo yako hakika mpenzi wako anakupenda na hata wewe unampenda kwa maana ya "love" lakini humpendi kwa maana ya "dislike", kwasababu kama ungekuwa humpendi kwa maana ya "love" basi usingefikiria kutaka kujenga nae mapenzi wala usingetaka ushauri wa namna ya kumpenda au hata kuhisi mapenzi na badala yake ungeachana nae siku nyingi.


Nadhani umeingia kwenye uhusiano "serious" mapema kabla hujamfuta yule mtoto wa Balozi a.k.a Intruder, sasa kwa vile bado hujaondokana na zile hisia za kimapenzi na yule mtoto wa Balozi itakuwia vigumu kuachiamoyo wako kwa huyu mchumba wako.


Unajua, Enzi zile za Bibi zetu pengine hata Mama zetu, wengi walikuwa wanajifunza kupenda ikiwa wanafungishwa ndoa na wanaume wasiowapenda. Hali kadhalika wanawake hao walikuwa wakitumia mbinu fulani-fulani (sio madawa/uchawi) ili kuwafanya waume zao kuwapenda ikiwa itatokea wameozwa kwa wanaume waliowapenda lakini wao mwanaume hawawapendi na wanaishi nao tu kwa vile wazazi walitaka iwe hivyo.


Kumdondokea mwenzio kimapenzi ni kitu nadra sana (haikupati kama vile hamu ya kula)hivyo basi kudondokewa na mwanaume ambae anakila kitu unachokitaka kwa mwanaume a.k.a "the one" ni sawa na miujiza na unapaswa kushukuru Mungu, kufurahi na kulienzi penzi la huyo mtu aliyekudondokea ambae anavyote utakavyo mwanaume kuwa navyo.


Nini cha kufanya; Msifunge ndoa wakati moyo wako ni mzito juu ya huyo Kijana na badala yake tafuta uwezekano wa kuisogeza mbele tarehe ya kufunga ndoa kwa kushirikiana na Mchumba wako ili upate muda wa kutosha wa kuufungua moyo wako ili kupokea penzi lake kama sio kujifunza namna ya kumpenda mumeo wa baadae.


Kumfanya mtu akupende ni rahisi zaidi kuliko wewe kumpenda yeye hasa kama huna kabisa hisia, lakini kwavile tayari mmekuwa pamoja kwa muda na sasa ni wachumba inamaana kuwa kuna hisia fulani kati yenu, pia kuna vitu umegudua ambavyo vinakufurahisha kuhusu yeye mchumba wako na vingine labda vinakuudhi lakini kubwa zaidi ni kuwa kuna mengi mnafanya kwa kukubaliana, shirikiana na mnafurahia "interest" za aina moja.


Kinachopungua au kukosekana hapo ni wewe kuufungua moyo wako zaidi ya ulivyo ufungua hivi sasa na ili kufanikisha hilo basi fanyia kazi yote haya nitakayokueleza hapa chini, bila kujali mtiririko wake.

1-Kuwa mkweli na nafsi yako ilikujua unataka nini kutoka kwake in terms of mapenzi sio alichonacho.

2-Focus kwenye nini hasa uta-offer kwenye uhusiano wenu.

3-Jifunze kufurahia/kupenda na ku-appriciate kila effort anayoifanya juu ya uhusiano wenu.

4-Mfundishe/mwambie afanye vitu vile unavyopenda/furahia.

5-Jjitahidi ku-share moyo wako wote kwa mwenzio, kamwe usiachie nafasi kwa jaili ya mtu mwingine aliyepita (mtoto wa Barozi) au mabaya aliyokufanyia huyu Mchumba hapo mwanzo.

6-Weka wazi ndoto zako za kimaisha kwa mpenzi wako.

7-Weka wazi uoga wako au vitu unavyohofia kuhusu uhusiano wenu au maisha yenu ya baadae.

8-Tumia muda wako mwingi kuwa na mchumba wako, jinsi utakavyokuwa unamzoea kiukaribu zaidi ndivyo hisia zitakapoibuka.

9-Fanya shughuli pamoja, Mfano; kutoka kwa ajili ya matembezi, chakula, kuona ndugu, jamaa na marafiki, kujichanganya kwenye sehemu ambazo mara nyingi pea/couple huwa pamoja (hii pia itakusaidia kuzalisha hisia zaidi juu yake).

10-Ukipata nafasi ya kuwa pekeyako jaribu kum-fantacise anakufanyia mambo fulani matamu ambayo hajawahi kukufanyia.

Baada ya muda usiozidi miezi miwili utaona au kuhisi tofauti juu ya hisia zako....hilo likitokea au kutotokea basi nitafute tena.

Kila la kheri!

Wednesday, 6 May 2009

Kanitambulisha kwao, anamtu yaani sielewi-Ushauri

"Jamani me dada Dinah nina jambo ila sifahamu tu wapi ni kutumie kwa mail gani lakini hii issue imekaa hivi: Mimi nina mpenzi ambae tunapenda sana sana na siku ya kwanza alivyoniona tu akawaambia ndugu zake kuwa ameshapata mke yule ambae anamuhitaji na kumuelezea mama yake mzazi. Mimi nimekuja kuambiwa na Binamu yake kuwa najulikana kabisa home cha kushangaza hajaniambia chochote hiyo moja.

Pili huyu anamtu amezaa nae na uzuri ameshaniambia kama anamtoto kinachoniuma mpaka leo wanaendelea kula bata mimi roho inaniuma sana sana sio siri, mtihani ulionipata ni kwamba nilimpigia simu kama mara 4 hivi hajapokea imepita masaa kadhaa anipigia na kunifokea "we si unajua kama niko na huyu mwanamke kinachokufanya upige non stop nini? sipendi mgambane ndio mana nimeamua kutopokea simu yako"


Kwa kweli imeniuma sana huwa hasemi lakini siku hiyo alinidhihirishia kabisa kwamba asipo pokea simu yangu nielewa tu yuko na huyo mwanamke. Niligomba sana pasipo kujibu neno lolote haikutosha nilituma msg za kumkashifu mwanamke pamoja na yeye yote ni hasira tu, nikawa kimya na yeye kimya.


Nikajirudi kwa kuona kimya kimezidi, na chat nae tuna story kama kawaida lakini hana mapenzi tena na mimi yaani inaniuma sana sana kumkosa. Alikua akinipa gudtime sana sikua nikipiga simu kwake yeye ndio alikua akipiga lakini sasa mimi ndio napiga na nisipopiga yeye hapigi. Nikituma msg za malalamiko kwanini anafanya hivyo? yeye hanijibu.

Sasa hapa sielewi kanimwaga au vipi ni bora anitamkie tu kama hataki kuendelea na mimi lakini si kukaa kimyaa jamani inauma sio siri kukaa kimyaa ina maanisha nini jamani mbona mwenzenu niko njia panda?

Naombeni ushauri nifanye nini?"

Dinah anasema;Pale ulipolitumia ndio mwake kabisa, shukrani kwa ushirikiano wako.
Kutokana na maelezo yako inaelekea sehemu ya familia ya jamaa yako hasa Mama yake kama ulivyogusia hawampendi huyo mwanamke aliyezaa nae sasa ktk kuwazuga ikabidi atafute mwanamke mwingine ambae ndio wewe na kumtambulisha kwa Mama yake huenda ni kwa jina, picha, au kwa mbali yaani unakatiza kwa mbali mtu anaonyeshwa "yule dada ndio mpenzi wangu nataka kuoa".

Kuna uwezekano mkubwa kabisa kafanya hivyo ili asipate "radhi" ya mama'ke au anataka tu kumfanya mama yake apunguze kidomodomo ili yeye na mama watoto wake waendelee kuishi vema. Kinachosikitisha ni kuwa wewe umezama kwenye mapenzi na mwanaume wa mwanamke mwenzio kwa maana nyingine inakuwa kama vile umeingilia mapenzi yao (well hii ndio itawajia kichwani wanawake wengi) lakini ktk hali halisi haikuwa hivyo, wewe ulipendwa na kijana huyo kisha ukampenda alafu ndio ukajatambulishwa kuwa kuna mwenzio ambae amezaa nae.


Ulichokosea hapo ni kuendelea na uhusiano na huyo Njemba huku ukijua kabisa kuwa unachangia na mwenye mali (aliyezaa nae) na mara kwa mara anakuwa huko na anathubutu kukufokea kabisa kuwa "unajua niko na yule mwanamke, kinakufanya unipigie non stop nini ?"hapo ni wazi kuwa hajali hisia zako na hakuthamini wewe kama mpenzi wake. Siku hiyo ungenawa mikono kutoka kwenye uhusiano huo.


Sio lazima mtu akutamkie kuwa hakutaki au hataki kuwa na wewe, wakati mwingine unasaoma vitendo vyake (Mf, kutokupokea au kukupigia simu), namna anavyoku-treat(Mf,anakufokea) na kadhalika. Huyu Jamaa hakuhitaji tena, kwani alichokitaka tayari kimepatikana nacho ni kufunika ukweli kwa Mama yake kuwa yeye bado anaendeleza uhusiano na mzazi mwenzie.


Natambua unavyojisikia, nafahamu maumivu ya kimapenzi unayokabiliana nayo lakini ni vema kuumia sasa na kujitahidi kumsahau huyo jamaa, kuyasahau yote mliyokuwa mkiyafanya pamoja kama wapenzi.

Njia nzuri ya kumsahau ni kumchukulia kuwa ni "kicheche", kumbuka kuna UKIMWI, fikiria.....kama ingekuwa wewe ndio umezaa na huyo jamaa alafu kijimwanamke kingine kinamsumbua bwana wako kwa simu ungejisikiaje?

Mungu atakusaidia na utasahau kila kitu na utakutana na Kijana mwingine asiye na mtu.
Kila la kheri.