Siko Comfortable kuwa karibu na Ma'mkwe-Ushauri

"Hongera sana dada Dinah kwa jinsi unavyotusaidia kwenye mambo mbalimbali, nimeshapost maswali yangu mawili lakini umeyatia kapuni dada yangu kulikoni?? chonde chonde usilitie na hili kapuni.

Dinah anasema: Mama M, sijapokea swali lolote kutoka kwako, hili ni la kwanza. Kwa kawaida kila swali linanolifikia ni muhimu na huwa nali-publish kwa kufuata lini nimepokea.

****************************************************************************

Mimi ni mwanamke niliyeolewa na nina watoto wawili, mume wangu alishawahi kunicheat hapo awali na nikagundua lakini bado aliendelea. Mpaka sasa bado sijatulia kutokana na kutendwa na mume wangu.


Mimi na mama mke hatupatani kutokana na yeye mama kumtetea mume wangu alivyonicheat. Mama huyu alinifokea sana na kuniambia nimuache mume wangu, Yaani alinijia juu mpaka wake wa mashemeji zangu wakawa wanamsema kwa kumwambia anavyofanya sio vizuri.


Nimejifungua hivi karibuni na mtoto sasa anamiezi saba, sijawahi kuwasiliana na mama mkwe wangu tangu mwezi wa kumi na mbili mwaka jana alipokuja kwangu hapa Dar ambapo aliondoka vibaya na hata kusema kuwa kamwe hata kanyaga kwangu.


Mama mkwe yeye anaishi Mkoani, na kiukweli mimi nilikuwa nikimuonyesha heshima zote wala sijawahi kumchukia wala kujibishana nae sembuse kubadilishana maneno makali. Nakumbuka kuna wakati nilimpelekea nguo za Christmass, lakini aliziponda sana akasema atazitupa "nguo gani mbaya hivyo"? japokuwa ilikuwa ni suti nzuri tu jamani! mpaka wifi yangu (mtoto wake) akajisikia vibaya akaja kuniambia mbele ya mama yake ambaye aliona aibu na kuanza kukana.


Tatizo kubwa naona kama huyu mama mkwe anachuki binafsi na mimi japokuwa ndio mchezo
wake kwani keshawakorofisha sana hata hao wake wengine wa mashemeji zangu ila naona kwangu kazidi.

Sasa hivi niko kwenye uhusiano mzuri kiasi na mume wangu japo bado machungu hayajaisha ila anajitahidi, aliniita akaniomba nimsamehe mama yake akidai kuwa "nyie wanawake mnajuana wenyewe sijui kwa nini anakuchukia hivyo" akaniomba nimsamehe na niwe nampigia simu na niwe karibu nae. Siku mjibu kitu mume wangu na wala sikumpigia huyo mama mkwe kwani mimi nimejifungua hata yeye angeweza kuja au kunipigia simu naa kuulizia mtoto lakini anaongea na mwanae tu.

Swali: Mume wangu anataka tukambatize mtoto wetu mkoani (kwa mama mkwe) Xmass hii na mimi sijisikii huru kwani sitamani hata kumuona yule mama kwa alivyonipa stress kwenye maisha yangu, yani hapa sijaandika yote, hata watu baki na ndugu zangu wanajua matatizo niliyoyapata kutokana na chuki ya mama mkwe.

Naomba ushauri kwanza, nikubali nikambatizie mtoto huko kwa mama mkwe au la, na kama nikikubali kwenda huko je nimnunulie huyu mama zawadi kama nguo?? kwani mume wangu huwa hana utaratibu wa kununua nguo za mama yake kabisa!! tafadhali nisaidieni nideal vip na huyu mama??
Wenu mama M"

Dinah anasema: Pole sana kwa kukabiliana na chuki ya mama mkwe wako, hili ni tatizo kubwa linalowakabili wanawake wengi sana hapa Duniani. Hata mimi sijui ni kwanini hasa mtu umchukie mkweo kiasi hicho. Tena mbaya zaidi ni pale Mumeo akiwa ndio mtoto wa Kiume kwa kwanza/mwisho/mtoto wa kiume pekee kwenye familia yao.....hapa mama wakwe/wifiz huwa hawataki mchezo!

Tatizo letu wanadamu huwa tunategemea kupendwa mara tu baada ya kuungana na familia nyingine (kufunga ndoa), Jamani! Mtu mmoja kukupenda haina maana Ukoo mzima ukupende. Kama ikitokea kwa bahati nzuri mkapendana poa, ikitokea hawakupendi safii tu au kama wewe huwapendi ni kawaida vilevile (kwani mlizaliwa pamoja bwanaaa!).....kitu muhimu ni kuheshimiana na kila mmoja wenu kujua mipaka yake kati ya yule aliye waunganisha in ur case mumeo.


Unachotakiwa kuzingatia ni Kumpa heshima lakini kamwe usijipendekeze kwa mama mkwe huyo, usijilazimishe kumpenda (huwezi kulazimisha hisia kama hazipo kubali kuwa hazipo), kutokumchukia (mchukulie kama alivyo na dharau uchokozi na chuki zake kwako), hata siku moja usimzungumzie vibaya kwa watu wengine (kwa kufanya hivyo itakufanya ujenge chuki dhidi yake) kumbuka kuwa huyo ni bibi wa watoto wako hivyo kubali kuwa hakupendi na muache kama alivyo aili mradi tu hamkai nyumba moja.

Ni kama kuwa Kazini/Shuleni, kutakuwa na watu wanakupenda na wengine hawakupendi(ni nature ya mwanadamu)....... lakini huwezi kuacha kazi au masomo kwa vile tu watu fulani wanakuchukia. Unawadharau na kufanya kazi/masomo yako kwa bidii.

Ukiangalia kwa undani asilimia kubwa ya wanawake huwa na tabia ya kuchukiana kweli kweli bila sababu, inawezekana kabisa mtu humjui lakini unajenga chuki. Sasa mimi nadhani hii asili ya baadhi ya wanawake kuwa na chuki za ovyo-ovyo ndio husababisha baadhi ya wakwe zetu kuwa hiyo kwani uanamke hauwatoki hata kama ni watu wazima sana.


Wataalam wa Saikolojia wanadai kuwa mama na mtoto wa kiume huwa na bond maalum, ukaribu huo kati ya mama na kijana wake kuendelea kwa muda mrefu sana. Mama huyu huendelea kudhani kuwa Kijana anahitaji kumsikiliza na kufanya maamuzi ambayo yeye mama anakubaliana nayo kama akipinga basi Kijana hapaswi kuendelea na maamuzi hayo na kiendelea basi atakumbwa na mabaya (si umewhai kusikia kuwa Radhi ya mama ni Kali kwa mtoto wa kiume kuliko wa kike? Jiulize kwanini iwe kwa mtoto wa kiume tu?).


Sasa Kijana anapokuwa na kuanza kujitegemea mama hupata hisia za kupoteza sehemu kubwa maisha yake na hivyo ataendelea kujiweka karibu na kutaka kujua kila kitu ambacho Kijana wake anakifanya. Ikitokea Kijana kaamua kuchumbia Binti ampendae mama huyu anaweza kukubali au kupinga (huwezi kuambiwa hili ni suala la familia yao).


Mama akikubali basi ataanza kujiweka sana kwenye uhusiano wenu na kuhoji vitu kama vile mtafunga ndoa lini? nani asimamie, aina ya nguo zitakazo valiwa, sherehe iwe wapi na iwe vipi? n.k. Baada ya kufanikiwa kufunga ndoa mama huyu ataanza "nataka mjukuu" wakati tayari wapo wengine waliozaliwa na dada/kaka wa mumeo....

Hii yote ni katika kutafuta ushindi na kukuonyesha wewe Mkwe (anakuona kama mwanamke mwingine unaechukua nafasi yake kwa mwanae) kuwa yeye ndio mwenye sauti na mamlaka kwani huyo Mumeo ni mtoto wake hivyo anatakiwa kufanya akisemacho yeye na sio wewe.

Kutokana na maelezo yako inaonyesha kuwa Mama mkwe wako hakupewa nafasi sana kwenye uhusiano wenu na ndio maana anakuwa bitter kila kukicha, na kilichonifanya nigundue hilo ni kutokana na maelezo yako kuwa alimtetea mwanae alipotoka nje ya ndoa.....alimtetea mwanae ili aweze kum-win back Kijana wake na wewe ubaki mwenyewe na maumivu yako moyoni.....alitaka Ushindi kwani wewe ndio unaemjali kwa kumnunulia zawadi na si mwanae......kwa mama mkwe huyu hili ni pigo kubwa kwani anadhani kuwa wewe as "mwanamke tu" ndio una-control kila kitu kwenye maisha ya mwanae.


Nini cha kufanya: Mimi binafsi sioni sababu yakwenda kumbatiza mtoto huko Mkoani unless otherwise kuna sababu za msingi kama vile Kabila la Wachaga (Xmas kuliwa Nyumbani Moshi kind muhimu), mnamtegemea yeye Mama mkwe kiuchumi, labda ndugu wengi wako huko Mkoani na wanataka kushuhudia Ubatizo na ili ku-save ni bora ninyi muende huko kuliko wao kuja Dar, Mama mkwe huyo mgonjwa na hawezi kusafiri lakini anataka kumuona mtoto n.k.

Ili kuondoa vurugu, wewe kubali kwenda kubatiza mtoto huko aliko mama mkwe lakini hakikisha unaelewana na mumeo kuwa hamkai sana ili kuepuka "chokochoko" za huyo mwanamama. Utakapo kwenda huna haja ya kumnunulia chochote huyo mwanamama asie na shukrani.....ili apate ujumbe kuwa kuponda zawadi =hakuna zawadi.

Baada ya shughuli ya Ubatizo kuisha ni vema wewe na mumeo kuwasiliana kwa mara nyingine tena kuhusiana na unavyojisikia kwa mama mkwe wako. Usipozungumza na mumeo na kuliweka hili wazi na kumfanya akuelewe ili asaidie kumaliza chuki za mama yake kwako.

Mumeo mpenzi ataendelea kudhani (mwanaume akisema "sijui kwanini mnachukiana, ni mambo yenu wanawake...naomba umsamehe mama") yaya tachukulia kuwa yameisha, kuwa umemsamehe mama yake na hivyo kuendelea kufanya mambo ya kumhusisha mama yake na wewe mara kwa mara hali itakayosababisha maumivu makali ya hisia kwa vile utadhani kuw amumeo hakujali pia hautokuwa comfortable na mkweo.


Liweke wazi suala la wewe kujisikia huna thamani kwa mama mkwe huyo kutokana na dharau zake, kutetea usaliti wa ndoa...tena sisitiza hapa kuwa ukimuona mama mkwe huyo unakumbuka uchafu aliokufanyia mumeo (umesema kuwa bado unamachungu/hujasahau japokuwa unajitahidi kusamehe....itachukua muda mpaka kurudia hali yako ya kawaida). Mwambie yote yalioujaza moyo wako bila hasira wala chuki.

Muombe mumeo amwambie na ikiwezekana amsaidie mama yake abadilishe tabia yake mbaya, na mara baada ya kubadilisha tabia yake basi anza kumnunulia/tumia zawadi lakini sio ktk kujipendekeza bali kumjali.

**Nani alisema maisha ya ndoa ni rahisi eei? Ni magumu ila ukijua namna ya kukabiliana na wanawake (mama mkwe/wifi) kila kitu kina kinaenda vema na kila mmoja wenu anafurahia maisha yake kivyake na familia yake.

Natumaini kuwa maelezo ya wachangiaji na haya yangu yatakuwa yamekusaidia kufanya uamuzi wa busara.

Kila la kheri!

Comments

Anonymous said…
pole sana mama M
mimi nakushauri nenda ukambatize mtoto kwani huyo mama ni bibi yake tu huwezi kulibadili hilo na ujitahidi kutumia wakati huo kumaliza tofauti zenu kwani sio vizuri kukaa bila maelewano na mkwe wako, jitahidi yaishe my dear then usiwe karibu nae sana sababu tayari unajua udhaifu uko wapi.
pili zawadi ya nguo mnunulie hilo litamuonyesha yeye kuwa pamoja na tofauti zake bado unamthamini.hivyo ni kwa mtazamo wangu mimi.

Mama D
Anonymous said…
Ningekuwa ni mimi wala nisingeenda kumbatizia mtoto kwake. Muulize huyo mumeoangekuwa ni wewe angeenda? Pia kutokukupigia simu kwa muda wote huo inaonyesha hakupendi na hakutaki.
Batiza mwanao nyumbani kwako. Kama vipi mwambie mumeo muende mkabatizie kwenu ndio utakuwa huru zaidi. Ya nini uende kufuata matatizo mengine? Na usimnunulie tena nguo. Mpe mumeo hela akamnunulie apendacho.
Wa mama wakwe wana matatizo sana.
Anonymous said…
Pole sana dada,yaani machozi yamenitoka,kwnai naelewa nini machungu ya mume kucheat,na haikutosha hiyo na visa vya mama mkwe,kwa kweli pole sana.
Mimi ninaeandika hapa ni mama wa mtoto mmoja pia, ushauri wangu ni kuwa ningekuomba ukae chini na baba watoto wako,uhakikishe kwanza hii chuki ya mama mkwe inaisha kwa machoni tu,maana kwa rohoni mtu hawezi jua.Aende yeye kwa mama mzazi wake,amueleze yote,na ikiwezekana amuombe samahani kw ayote.
Ikiwa hicho hakikufanyika dadaangu kwa kweli hakutofaa kwenda huko kwa mama mkwe buree,lazima na sisi wanawake tuwe wajasiri,zama za kuingiliwa kimaisha zimeshakwisha sasa,ikiwa mama mwenyewe ndio hivyo hana ubinaadamu.
Umemuheshimu ameshindwa kuiilinda heshma uliyompatia,sasa basi kaa na mume wako mpange na ikiwa hatokubali,basi muache aende nae mtoto wake akabatizwe then watarudi.Wewe baki kwako,na pia ushauri wangu naomba uzungumze na wazazi wako pia hususan mamaako mzazi,na yeye ndie mtatuzi au mshauri wako wa mwisho kwa hili.

Nachukia wazazi wanaopenda kuingilia ndoa za watoto zao.
Hamisi M. said…
Dawa ya kuelewana na mkwe wako ni hii, kwanza ukubari na uwe mvumilivu sana, inaweza kuchukua miezi kadhaa au hata mwaka lakini utafanikiwa.

Mara nyingi hii inatokana na kutojiamini kwa mmoja wenu au wote, yaani wewe na mkwe wako.

Labda wewe unataka/unamuonyesha mkwe wako kwamba wewe ndiyo mke na una maamuzi fulani fulani ndani ya nyumba kama mke (kitu ambacho si kibaya)lakini inategemea na uelewa wa huyo mkwe/wifi/ndugu/rafiki/shemeji.

Akiwa muelewa hakuna shida, tatizo ni pale uelewa unapotofautiana.

Na yeye anaweza kuwa anajihisi kunyang'anywa nafasi yake kama mkwe/ndugu/wifi/shemeji/rafiki na kwa kuwa uelewa wa wote au mmoja wenu ni mdogo ndiyo mwanzo wa kuhisi kuonewa/kunyang'anywa haki na ndiyo mwanzo wa ugomvi.

Sasa basi kwa kuwa mume/ndoa ni muhimu na Mkwe(mama wa mumeo) ana uzito/umuhimu sana kwa mumeo inabidi wewe uwe na akili ya ziada kuweka mambo sawa.

Fanya hivi, kubali kwenda hiyo safari na zawadi wewe beba tu nyingi kadri ya uwezo wako kwa wote siyo mama mkwe pekee yake.

Muhimu, mkwe wako ndio awe wa kwanza kuziona hizo zawadi na mruhusu yeye achague anachotaka na zinazobaki muulize umpe nani na nani, fanya atakavyotaka hata kama ni tofauti na ulivyopanga wewe mwanzoni maadamu wengine hujawaeleza kwamba umewapelekea zawadi(usiwaeleze kabla).

Ukifika jishushe sana kwa mkwe wako, kubali kuonekana kama mjinga (ni kwa muda tu),usifanye chochote bila kumuuliza (hata kama majibu unayo), usipike chochote bila kumuuliza, usiende popote bila ruhusa yake (hata kama mumeo kakuruhusu), kuwa mvumilivu sana baada ya muda si mrefu atajiona mshindi, ataona haki yake kama mama kapewa, ataanza kubadilika pole pole nakukupenda, japokuwa mwanzoni anaweza kuwa anakusimanga/kukunyanyasa wewe vumilia tu (hakuna lisilo na mwisho) baadae utakuwa kipenzi kuliko hata watoto wake wa kuzaa na hapo atakuwa kama mtumwa wako!!!

Yeye ndio ataanza kuhakikisha hakuna anayekuudhi wala kukusema vibaya na utashangaa mwenyewe!!!

Angalizo: NI LAZIMA WEWE UWE MVUMILIVU SANA MWANZONI KAMA NILIVYOELEZA.
Anonymous said…
WEWE MCHUKULIE KM JINSI ALIVYO MUHESHIMU COZ NDIO MZAA CHEMA,USIMNUNIE MSALIMIE KM KAWAIDA UWE UNAMPIGIA SIMU YA KUMSALIMIA.ILIMRADI WEWE NA MUMEO MNAELEWANA BASI ASIKUPE SHIDA IGNORE MATATIZO YAKE KWAKO ISITOSHE HAMKAI PAMOJA.KWA NINI UJIPE WAHKA WA NAFSI?
Anonymous said…
Kitu kikubwa ukiwa kama Mama wa mtoto, pamoja na mumeo mna haki ya kimsingi ya kumbatizia mtoto wenu sehemu mnayoishi nyie wawili, yaani baba na mama wa mtoto. Mama mkwe wakati wake wa kuongoza familia yake ulishakwisha kama hawezi kuheshimu familia za wenzake,yaani pamoja na za watoto wake, huyo ni kuwa hana heshima na wala haheshimu utu wa watu wengine, hata afanyiwe nini. Cha muhimu, kaeni kwenu alikeni watu wote mnaowataka kwenye ubatizo, na mamamkwe akiwa mmojawapo, waje kusheherekea na nyinyi kwa pamoja. Tena huyo mamamkwe ikiwezekana hata nauli na pocket money ya njiani mumtumie kabisa na nguo ya ubatizo asije akapata kisingizio. Nguo mtoto wake wa kike amuulize anataka ya aina gani hata ikibidi mumpe huyo mtoto wa kike hela amnunulie mamayake kwa msaada wa mama kuchagua alioipenda, halafu baadae ataambiwa hela zimetoka wapi. Aache watu waishi kwa raha kwenye ndoa zao, kama yeye alivyoishi kwenye ndoa yake. Kama aliharibu ya kwake hana haki ya kuharibia wengine. Mtazamo wangu tu. FULL STOP
CALCA said…
Inaonyesha na Bwana ako yupo side ya mama ke.kwasababu kama hangekuwa hafurahiswi natabia ya Mama ke.Angefanya Mbinu zozote za kuclear huko kuto elewena kati yako na huyo Mama mkwe.Mfano angeenda huko kijijini nakumkalisha kitako Mama ke na kuclear hilo tatizo.
Anonymous said…
Mdogo wangu, mimi nimeolewa mwaka wa nane nina watoto 3, mama mkwe Mungu ampumshishe Roho yake, lakini ni kama wako, niliolewa nchi nyingine lakini ni africa na kaka ya mume wangu alikuwa anacheat sana na mke wake ambayo ni Mke mwenzangu alivyoanza kulalamika, yaani familia ya mume wangu ilivyomvaamia na kumwambia heee huyu mume wako ni mwanaume unadhani wewe ni mwanamke mwenyewe, wanawake wako wengi na nilazima akihitaji mabadiliko ya 'mboga' apate - yaani niliona hivi hivi yule shemeji yangu kafa ukimwi, na mke akafwata, hardly 2yrs sasa niambie basi watoto wangu walikuwa wadogo sana wakwanza ndio alikuwa 1yr, nikaletewa group la watoto walioachwa na shemeji na mke wake watatu, wakumbwa na wakawa wanawapiga watoto wangu si unajua tena watoto wadogo wakiona mwenzao anacheza na kitu wanataka, hawa watoto wakawa wakatili hiyo iliniuma, na muda si mrefu na mume wangu mwenyewe akaanza shughuli hizo za kucheat, yaani nilimtelekeza, nikachukua watoto wangu, sasa nimemaliza degree yangu ya kwanza naendelea na masters na niku mbali sana naye, yaani sitaki ushamba katika maisha, kama mtu ameona au kuolewa na bado ana haha haha nje, si aende nje tu basi kiishe
Anonymous said…
Pole sana mama M.

katika kitabu cha biblia kuna maneno mwanaume na mwanamke watawaacha wazazi wao wataungana nao watakuwa kitu kimoja. kwa nini ukubali kuingiliwa kataka ndoa yako??? hata kama ni mzaa chema anatakiwa awe na adabu na hofu katka familia ya watu.

kaa na mume wako ongea nae kwa upendo mweleze hauko comfotable kwenda kwa mkwe wako kubatiza, mwombe mbatizie hapo mlipo kama kualika watu ndio mualike na mkwe wako akiwa mmja wapo.

simama ndugu yangu usikubali kuendeshwa katika ndoa yako ila heshima iwepo kwa ndugu wote.

la mwisho simama katika maombi, mfunike mume wako, mtoto wako kwa damu ya Yesu iliyotukomboa.

from opugsl
Anonymous said…
Ann wa 7:15, hata kama utamaliza hiyo masters usidhani utaondoa ushamba wa maisha kwani ulishambika zamani ulipoolewa naye huyo ulidhani ulipata mume wa ng,ambo ya nchi yako ukaishia kudanganywa sasa unatuambia umemkimbia, hahahahaaaaaaaaa unakumbuka wakati ndebele ameishapita. Ila nakupongeza sana kwa kukata elimu, hayo mambo ya kuolewa achaneni nayo tafuteni misingi iliyo bora maishani mwenu wadada.Nimeona kina dada wengi ndo mumechangia kwenye suala la huyu mwenzenu.

Wewe mdada nenda kambatize mtoto kule ndiyo kwenu, acha kuendelea kushindana na mama mkwe wako.Wewe ndiye wa kutafuta suluhisho hasa ukijua kuwa yule ndiyo mama mkwe wako jinyenyekeze chini.Nakushangaa unajiweka kichwa kigumu nawe ni mtoto.Unaweza kushindana na mzazi wako.Kama mtu mwingine alivyokushauri wewe jifanye mjinga siku ipite.Na kumshinda mwelevu wewe fumba kichwa kwani mwisho wa siku atajiona mwenye ndiye mjinga.Fanya wema uende zako yeye mwenyewe ataona kosa.
Anonymous said…
Dada, kwanza nakupa pole kwa yote yaliyokukuta. Ndo maisha hayo. Nakushauri uufuate ushauri aliotoa kaka Hamis. Kwa kweli huna budi kujifanya mjinga. Watu watakushauri kwa kila style lakini kumbuka nawe ni mtoto mbele ya ule mama. Jiulize ingekuwa ni mama yako uko hivyo je ungefanyaje? Nakutakia kila la heri, na Mungu akusaidie ufanye uamuzi ulio muafaka. Pole sana kwa misuko suko ya ndoa.
Anonymous said…
Wewe anny wa 12:48:00pm usitumie maandiko matakatifu kiholela bila uangalifu :mtu atamwacha babaye na mamaye naye ataambatana na mkewe/mumewe nao watakuwa mwili mmoja" baada ya kunukuu hayo umeendelea kusema huyu mdada achukue zake wala hakuna haja ya kuingiliwa na mama mkwe wake.Ni kweli hao wawili waliambatana na wakawa mwili mmoja.

Sasa maandiko hayohayo yanasema" waheshimu baba yako na mama yako ili siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Mungu wako"

Kama hao vijana hawatawaheshimu wazazi wao ujue kuwa watenda kosa kubwa mbele za Mungu huyohuyo na mbele za jamii inayowazunguka.Nadhani muhimili mwema wa ushauri kwa huyo mdada ni kutoendelea na chuki.Bibilia ulionukuu maneno yako pia inatumabia kuwa "Mpende adui yako" maana huko ndiko kushinda majaribu na kujenga utu mwema miongoni mwa watu wengi tunaooweza kupishana nao. Suala la huyu dada ni jepesi sana na haliko na ushindani wowote kwa sababu mama mkwe wake hakai naye.Jambo muhimu tu wewe dada achana na mawazo na chuki dhidi ya mkwe wako wewe ndiye wa kuchukua jukumu kusamehe na kusahau.Kumbuka kama angekuwa mumeo anachukizana na mama yako wewe ingekuwaje kwako?wazee wetu mara nyingine huwa wamepitwa na wakati wanayo ya zamani hivyo elimu mpya wao hawana ni muhimu kuwasamehe tu.
Anonymous said…
wewe nenda then mtie adabuhuyo mama hajatulia mambo gani yakizamani hayo.
abbey said…
Pole sana mdada! Nakuomba sana fuata ushauri wa HAMIS M, Huo ndo utakaokusaidia pekee
Anonymous said…
Wapendwa asanteni sana kwa michango yenu nimefarijika mno na nimepanuka mawazo zaidi jinsi ya kudeal na huyu mama mkwe yaani nafarijika sana asanteni mno mungu awazidishie.