Nafasi ya Wife, Unapogundua mtoto si wako-Ushauri

"Mie nafurahia sana jinsi unavyosaidia watu sijui ni kipaji au ulisomea haya mambo ya kushauri watu. Leo na mie natoa uzoefu wangu wa maisha ya ndoa naamini kuwa utasaidia wanablogu hii na wasomaji wengine kuwa makini na wapenzi wao.

Mie nimeolewa miaka saba iliyopita na tumebarikiwa kupata watoto wawili. Wakati tunachumbiana na mume wangu aliwahi kuniambia kuwa alizaa na mwanamke mwingine na waliachana miaka michache kabla hajakutana na mimi.

Ukweli sikujisikia vizuri kuwa na mwanaume aliyezaa na mwanamke mwingine lakini alinihakikishia kuwa haikuwa wazo lake kuzaa na yule mwanamke ila mwanamke yule alijilengesha ili Mume wangu asimuache wakati ule wako pamoja. Nilijitahidi kumuamini lakini bado nyuma nilikuwa nasumbuliwa na maswali kibao.


Mume wangu hakuwa akijihusisha sana na mwanamke yule isipokuwa kama mtoto anahitaji mahitaji muhimu ambayo yule mwanamke hawezi kutimiza au kama mtoto anaumwa, basi mume wangu akiwa kwenye heka heka za kumshughulikia mtoto wake mimi nilikuwa naumia sana nikifikiria mambo mengi ya kimaisha na uhusiano kati ya watoto wetu na mtoto huyo wa nje ya ndoa wa mume wangu.


Siku moja nikamuomba mume wangu amlete mwanae hapa nyumbani ili ajenge uhusiano na wanangu, lakini mume wangu alikataa kwa madai kuwa ni mapema kwake kufanya hivyo. Nilimuelewa na nikaheshimu uamuzi wake. Siku zikapita na sasa inakaribia mwaka mume wangu hajagusia lolote kuhusiana na mtoto wake huyo wala mama wa mtoto huyo kama ilivyokuwa zamani.

Juzi juzi hapa basi tukapata wageni kutoka upande wa mume wangu, kwa bahati nzuri tunaelewana sana na tunaongea mambo mengi tu kuhusu maisha. Mmoja kati ya mawifi zangu akagusia kuhusiana na mtoto wa nje wa mume wangu akaniuliza kama najua kuwa mume wangu alizaa nje. Mie nikajifanya kuwa sijui ili nipate umbea zaidi manaa yake wao walikuwepo na kaka yao na huyo mwanamke kabla mimi sijatokea kwenye maisha ya kaka yao.

Wifi yangu alizungumza mambo mengi ya kutisha na kusikitisha kuhusiana na uhusiano wa kaka yake na mwanamke aliyezaa nae. Kilichonitisha ni mwanamke yule kwenda kwa mganga ili mume wangu wakati huo alikuwa bwanake wafunge ndoa.

Wifi alinisimulia harakati zote walizozifanya mpaka kumpeleka kaka yao kwenye maombi na kufanikiwa kumtoa kaka yao kwenye maisha ya mwanamke yule na mwaka jana wakaamua kufunga safari na mtoto yule mpaka Afrika ya Kusini na kufanya vipimo vya DNA na kugundulika kuwa mtoto yule kumbe hakuwa wa damu wa mume wangu.

Baada ya maelezo hayo nikakumbuka safari ya mume wangu kwenda Afrika kusini kwa wiki moja na aliporudi alikuwa kama mgonjwa mie nikadhani ni uchovu wa safari. Pia nikagundua kwanini mume wangu alikataa kumleta mtoto yule pale nyumbani na kwanini siku hizi hazungumzii kuhusu huyo mwanamke wala mtoto wake wa nje.

Nashukuru Mungu nimejua ukweli kuhusu lakini nasikitika na kushangazwa na kitendo cha mume wangu kukaakimya kipindi chote cha mwaka mzima bila kunieleza lolote juu ya DNA au kuniambia tu kwa kifupi kuwa yule mtoto sio wake. Kwanini ananichunia kuhusu suala hilo wakati mwanzo alinihusisha?

Je itakuwa sahihi kama nitamuuliza? Kama ndio je nitaanzaje kuuliza ili aseme mwenyewe badala ya yeye kuja kugundua kuwa dada yake ndio aliyetoboa siri kwangu?

Mwenzeni hapa nilipo sielewi nini cha kufanya pia namuonea huruma mume wangu kwani najua kabisa anaumia na kujuta ndani ya moyo wake kutokana na muda alioupoteza kwa mtoto yule.
Mrs Mwilima, Dar es Salaam."

Dinah anasema:Mama Mwilima shukrani zikufikie kwa ushirikiano wako. Mimi binafsi sidhani kama ni sahihi kwa wewe kumuuliza mumeo kitu ambacho hakipo tena kwenye maisha yake. Hata mimi nahisi kuwa Dada mtu ambae ni wifi yako alitumwa na familia ya mumeo kukueleza wewe ukweli huo ktk mtindo wa siri, hii inawezekana ni ktk harakati za kuzuia mumeo kuumia zaidi kwa kujibu maswali mengi zaidi kutoka kwako kama mkewe (una haki zote za kujua kila kitu kuhusu mumeo).

Nini cha kufanya:Sahau kuwa mumeo alikuwa na mtoto kwani imejulikana sio wake, hivyo hakuna sababu ya kushupalia kitu ambacho hakipo tena na badala yake zingatia hali ya sasa ya mumeo. Natambua mumeo anahitaji muda ili kupona maumivu hayo (mwaka mmoja hautoshi kuponya maumivu yaliyowekwa kila siku ndani ya miaka yote aliyoishia kidhani mtoto ni wake), na wewe mkewe ndio mtu pekee utakaefanikisha uponaji wake wa haraka ili wote kwa pamoja muanze kuishi maisha yenye furaha na amani kama zamani.

Mpe ushirikiano mumeo, muonyeshe mapenzi ya kihisia zaidi na kumjali ktk kipindi hiki kigumu cha kukabiliana na masumbufu ya Kiakili na Kisaikolojia usikute hata Kiuchumi kwani Miaka yote hiyo alikuwa akipenda, kujivunia, kujali na akihudumia mtoto wa mwanaume mwingine akidhani ni wake.

Wewe pia unatakiwa kuwa mvumilivu kwani kipindi hiki mumeo anaweza akawa na hofu juu ya watoto wenu hao, inawezekana kabisa akawa anajiuliza mara nne-nne kama kweli ni wake au analelea mtu mwingine?

Ukiona hali yake inaendelea kuwa hivyo basi nakushauri wewe na wanafamilia kushirikiana na kumtafutia msaada wa Therapy ili kukubali ukweli, kusahau yaliyopita ili aweze kuendelea na maisha yake.

*****Haya mambo yapo sana na yanasikitisha lakini ukweli unabaki pale pale kuwa mama ni mtu pekee anaejua baba wa mtoto, Mtu unapoambiwa "huyu mwanao/mwanangu" Kisaikolojia watu wanaweza kuona mtoto kafanana sana na wao au babu, bibi, baba, shangazi yake n.k. lakini ukweli ni kufanya hiyo DNA Test kama unawasiwasi.

Kila la kheri Mrs Mwilima.

Comments

Anonymous said…
Kwanza nakupa pole, pili huyo mzee mwenzangu inabidi uwe nae karibu sana maana shock aliyoipata haina mfano. Kwanza kuendewa kwa waganga na pili kuambiwa mtoto sio wake. Kuna uwezekano kabisa asiamini mwanmke tena!! Kwa mtazamo wangu kama mwanaume nahisi dada mtu alipewa huo ujumbe aufikishe kiaina, ukijifanya hujui ukute yeye alishaambiwa kwamba umeshapewa kila kitu, unawezaleta balaa lingine. Inawezekana kabisa alishindwa hata kuongelea hilo swala na wewe. Ningekushauri umuulize wifi yako kwanza kama kaka yake anajua kwamba unajua kila kitu. Utakuwa umepunguza matatizo mengi kwa kumjulisha kwamba unajua yote yaliyomsibu na unampa pole na kwamba upo tayari kumsaidia ku-heal (sahau) hayo matatizo. uzuri ni kwamba wewe ulishaonyeshe dalili nzuri ya kumkubali mtoto, so mambo ni rahisi kwa upande wako. tumia hii nafasi kumuonyesha kwamba unamjali, na, kwa mtazamo wangu hii itaongeza pendo kwenu na kumsaidia yeye kusahau yaliyomsibu.

Mdau Mti Mkavu a.k.a M2
Anonymous said…
Pole na hongera kwa sababu umefahamu ukweli kila kitu. Kwa kuwa alishakueleza kuwa ana mtoto kabla ya kuwa na wewe na kwa kuwa watoto wenu wawili bado ni wadogo kwa sasa; nadhani ndio maana mumeo aliona asimlete huyo mtoto kwanza ili asikuongezee kazi. Ingawa ni rahisi wewe kuhisi kuwa labda alikuwa anatafuta mbinu ya kuweza kuonana na huyo mzazi mwezake, lakini siyo kweli kwani asingekuwa na wewe. Mara nyingi ni vigumu wanawake kuamini kuwa kweli uhusiano wao ni kwa sababu ya mtoto tu. Ushauri: Onyesha uko naye katika wakati huu mgumu kwake (mmeo) kwani anakaibiliwa na mambo makuu wawili: mosi kupoteza mtoto uliyemtunza na kudhani ni damu yako; pili kupoteza imani kwa mwanamke. Kama mtu anaweza kukuambia kuwa huyu mtoto ni wako kumbe siyo, je atashindwa kutoka nje ya ndo? Mwambie ukweli kwamba kuna jambo uliambiwa na wifi yako, na unaungane naye kumpa pole! Onyesha kuwa uko naye kwenye tatizo hilo na mpe matumaini kuwa Mungu hakupenda iwe hivyo kwani kila kitu tulichonacho hapa duniani hupewa na Mungu na kuna kusudi lake.

Pole.

Elewe kuwa uhusiano wake na huyo aliyekuwa mzaze mwenyezake ulikuwa zamani; na amini hinvyo!
Anonymous said…
Ushauri wa Mchangiaji wa kwanza ni mzuri sana, ameeleza karibu yote niliyotaka kukushauri - fanyia kazi ushauri wake utaona matokeo yake.

Maisha ni rahisi sana kama tutaboresha mawasiliano yetu itanaondoa dhana au hisia mbaya zisizo na msingi juu ya wengine.
Anonymous said…
Hiyo ni hali ya kawaida kama vile kukataliwa baada ya kuwa marafiki kwa muda. Inauma sana,lakini wakati mwingine unatakiwa kushukuru Mungu, kwani amekupa mwanga mapema na kugundua kuwa huyu sio damu yako.
Lakini hata hivyo anatakiwa ashukuru kuwa amesaidia kulea, kwani kihali halisi watoto wote ni wetu na kama ukipata nafasi ya kusaidia kulea kusomesha, usiogope kufanya hivyoo kwa kisingizio kuwa yeye sio damu yangu.
Mimi nakupa heko wewe kwa kutokukata tamaa,na inabdi umweke karibu sana mume wako, kwani majanga yaliyomkuta yamemuathiri kifikira, hasa ukizingatia hujui ni madawa gani aliyopewa, pili hali ya kubambikiwa inamfanya asiwe na imani kwa wanawake(hii ni hali ya kawaida kwa kila mwanadamu). Kwahiyo wewe unatakiwa umuonyeshe kuwa hiyo sio kweli.
Unaweza ukamtumia huyo wifi yako kufikisha ujumbe, lakini ni vyema ukatafuta muda muafaka ukamueleza kinagaubaga kuwa angalau unayajua yaliyomkuta na mweleze kuwa yeye ni wewe na wewe ni yeye, kinachomsibu yeye kinakuathiri wewe pia halikadhalika kwa upande wako. Kwahiyo mwambie ayasahau yaliyopita na agange yajayo, na kama atakuwa na uwezo asiache kumsaidia huyo mtoto aliyebambikiwa, kwasababu sio kosa la mtoto, na pia huenda hata huyo mke alikuwa hana uhakika kama alikuwa na tabia ya `kihuni'. Mwambie wema hauozi na alilolifanya ni wema na huyo mtoto ataukumbuka, huwezi jua mbeleni.
emu-three
Anonymous said…
Napenda nikushauri dadangu kwamba hilo lisikuumize kichwa kwavile anayeumia kichwa ni yule aliyegundua kwamba mtoto siye wake kwa vile ameingia gharama kubwa kutunza mtoto huyo.kama mumeo alikuambia ana mtoto nje alikuambia hivyo kwa upendo wake tu na alipenda ulitambue hilo ili kesho na keshokutwa usijeonana na huyo mtoto ukaanza kung'aka,hivyo basi kwavile wewe umepata udaku kupitia huyo wifi yako hunasababu ya kuwaza au kuhofu juu ya hilo badala yake wewe ungeshukuru maana hutakuwa na mawazo ya huyo mtoto kuja kulelewa na wewe tena maana mumeo hatamchukua na kumleta kwako kwavile amejua mtoto siyo wake,kuendelea kuchokonoa juu ya jambo hilo kwa mumeo wakati umeshapata ukweli ni kumwongezea maudhi mumeo na hata kuhatarisha mahusiano ya mumeo na dadake ambaye amekueleza taarifa hizo maana siku ukimuuliza juu ya jambo hilo lazima atataka ajue habari hizo umezipata wapi.Nakushauri utulie tuliii bila kuchokonoa,badala yake subiri siku uambiwe na yeye mumeo kama atajisikia kufanya hivyo na kama hatakuambia wewe hunahaja ya kuhoji maana haikughalimu chochote kuambiwa ama kutoambiwa kwavile mtoto huyo hawa husu tena.
Anonymous said…
Maamuzi hayajutiwi,mambo yale yalikuwa ya wkt ule,yuko sawa.wala hapaswi kulaumiwa.huu ni wkt wako ss kwa kua umelijua tatizo waweza kuzungumza nae. Yeye hawezi kukuambia chochote kwa kukurupuka,pengine kwa kuogopa kukuudhi. Lianzishe ili umuweke sawa,matatizo yake,yako.ni sehemu ya maisha yenu.kama mambo yanaharibika muhimu kukaa chini na kuyazungumza.kama wanawake mna nafac kubwa sana kuhakikisha maisha yanakua ya amani na upendo cku zote. Ni hayo tu kwa mtizamo wangu.