Sunday, 17 May 2009

Mume ni "control freak" nifanyaje aache?-Ushauri

"Hi dada dinah, pole na mizunguko kazi na maswali mengine magumu hata kuyatatua mwenyewe. Mimi ni mama mwenye mtoto mmja nimeolewa nina miaka minne katika ndoa yangu nilizaliwa miaka kadhaa iliyopita but not below 23.


Mimi na mume wangu tulikua tuna pendana sana na mpaka sasa mimi bado nampenda tena sana. Dada Dinah tatizo langu kubwa kwa mume wangu ni kwamba simuelewi kwani tangu tumeanza kuishi pamoja hataki mimi niende nyumbani kwetu wala niwasiliane na ndugu zangu ila kwao na kuwasiliana na ndugu zake hanizuii.


Nimejaribu kumtumia mama yangu amuombe niende lakini bado anatoa sababu, kwa mfano mama alimuomba niende kuwaona mume wangu akasema muda bado. Muda ulipo fika akatafuta safari akaniaacha mimi nikashidwa kuondoka.

Dinah anasema; Nadhani hii tabia yake ya kukukataza wewe kwenda kwenu ni uoga unaoweza kusababishwa na uzoefu mbaya kutoka kwa watu wengine wanaomhusu, huenda ikawa ex's au hata ndugu jamaa na marafiki ambao wapenzi/wake zao walikuwa wakitumia kisingizo cha kwenda "kuwaona nyumbani" na huko walikuwa wakifanya mambo machafu.


Natambua kwenda nyumbani ni muhimu na wazazi wako wangependa kukuona sio tu wewe bali hata wajukuu zao lakini kama inashindikana kutokana na kutojiamini kwa mume wako basi jaribu kumshawishi muende wote kuwaona nyumbani, ikishindikana basi waombe ndugu zake waje kukutembelea nyumbani kwako.

Umesema kuwa unampenda mumeo, kama kweli unampenda basi jaribu kumuelewa. Yeye kama mwanaume wa Kibongo hata siku moja hawezi kukueleza yaliyomkuta huko nyuma hasa kama yalihusu mpenzi wake wa zamani au yanahusisha yeye kuonekana muoga wa "kuchezewa denge" na wajanja.

********************************************************************************

Pili siku hizi kabadilika sana kiasi najuta hata kuolewa yaani kidogo kanitukana mara mshenzi mara mjinga mara ananitisha kunipiga kwa kusema mimi simjui vizuri ndio maana nashindwa kufanya atakavyo, ukweli ninachanganyikiwa mume wangu anakuwa kigeugeu anaweza akakwambia mimi sipendi uvaenguo ndefu ukivaa fupi kwa muda huo aliosema anafurahi sasa itokee siku nyingine akuambie tutoke ukivaa hiyo nguo fupi anaanza unaenda kumuonyesha nani? unatakautongozwe kwani mimi sikutoshi? ukivaa ndefu au suruali ananyamaza.

Dinah anasema; Mumeo anaamini ktk umilikishi, pamoja na kusema hivyo uhusiano wenu unakosa mawasiliano kitu ambacho ni muhimu sana ili yeye akuelewe wewe na wewe kumuelewa yeye na hiyo itaepusha hali ya kuchanganyikiwa kwako.

Mumeo anadhani kitendo cha kukuoa wewe basi anakumiliki na anataka ufanye yale atakayo yeye bila kujali hisia zako. Mumeo hajui kuwa wanawake huwa tunavaa kutoakana na tunavyojisikiwa au "mood", mavazi hutufanya tujisikie wazuri, warembo na tunavutia, mavazi hutufanya tufurahie siku, mavazi hutufanya tuwe na huzuni, mavazi hutufanya tutake kufanya mapenzi n.k.

Sasa, ili mumeo aelewe hilo ni kazi wajibu wako wewe kama mwanamke kumuelewesha kwa kutumia moja ya nguzo muhimu ya kuboresha uhusiano nayo ni Mawasiliano. Wakati unawakilisha hoja yako hakikisha unaiwakalisha kwa upendo, upole ili akuelewe vema pia kumbukakutumia uanamke wako ili kupata utakacho.

Wanaume wanajua nini hasa huwavutia kutoka kwa wanawake, wapo wanaovutiwa na vifua, wengine wanavutiwa na sura na baadhi ni makalio na wengi huvutiwa na sehemu ya mapaja. sasa kama mumeo anavutiwa zaidi na mapaja yako niwazi kuwa hatopenda ku-share sehemu hiyo na wanaume wengine hata kama ni kwa kuyaangalia tu.

Anashindwa kukuambia moja kwa moja kuhusiana na kutojiamini kwake na badala yake anatumia lugha ya ukali ili kufikisha ujumbe kuwa "sipendi wanaume wengine waone mali zangu"....sijui unanielewa dada mdogo?

Kumbuka kuwa huyo ni mumeo hivyo anatsahili kuheshimiwa na kama akikataa kata kata wewe kuvaa nguo fupi nje ya nyumba yenu basi jaribu kumuelewa na wewe tafuta mavazi mengine ambayo yataendelea kukufanya uvutie, ujisikie mrembo na mwenye furaha...sio lazima yawe mafupi sana (juu ya magoti) yanaweza kuwa chini kidogo ya magoti nakuachia sehemu kuwa ya miguu yako kuonekana na hiyo itakufanya ujisikie swaaaaaafi kabisa.

*****************************************************************************

Nimefikisha mara mbili nakuta msg zisizoeleweka kwenye simu yake ukimuuliza anakwambia hivi mara vile ilimladi tu usiendelee kumuuliza. Lakini hivi yeye akipiga simu ikatokea nimechelewa kupokea akirudi kutoka kazini nyumba inakosa amani kabisa.

Dinah anasema; Unatakiwa kupangilia maswali yako ili kupata majibu ya kuridhisha kama ujumbe wa simu ulioukuta unahashiria yeye kutokuwa muaminifu, kamwe hata siku moja usikubali maelezo yake ambayo unahisi kutoyaamini.

Hakikisha unafikiri huku unaongea/uliza pia sikiliza majibu yake huku unayatafakari ili akimaliza kujibu unamtundika swali lingine hii inakusaidia kupata ukweli na kama ukihisi unadanganywa basi ni wakati wa kuweka rules kwenye uhusiano wenu.

Huyo ni mume wako, mmeoana na sio amekuoa hivyo basi unahaki ya kusikilizwa, kuthaminiwa, kujua marafiki zake, wafanya kazi wenzake, ndugu na jamaa zake, kujua anawasiliana na akina nani na uhusiano wao gani, wapi hufanya matembezi na nyingine zote uzijuazo wewe ndani ya ndoa yanu. Kama unahisi unakosa haki zako kwenye ndoa yako ni wakati wa kuzidai na kuhakikisha zinaheshimiwa.

**************************************************************************

Juzi simu yangu ilijizima nikiwa salon iliyo nje ya uzio wa nyumba tanayo ishi akampigia rafiki yake akaja mpaka saloon nikaongea naye kupitia simu ya rafiki yake jamani hakukaa mpaka muda wa kazi uishe karudi hakuna salam ananiambia utanieleza uliko kuwa huku anatafuta mkanda aanze shunghuli mimi nikamwambia labda anasababu zake tu nyingine lakini mimi sijatoka hata gengeni sikwenda.


Siku hiyo ndipo alipo muita mtoto wake mwenye miaka minne nilimkuta naye akamuuliza, ndipo mtoto akamwambia "mama leo hajaenda mahali zaidi ya saloon anako sema" mume wangu akaona aibu akaondoka dada hata sasa nikimuuliza kwa nini ananifanyia hivyo ananiambia nisimkumbushe anakasirika mpaka nashindwa hata kuendelea kumuuliza dada ni mengi lakini naomba niasidae kwanza kama haya mama na nikisema nimalize yote leo nita kesha naandika. Ni mimi Mama T"


Dinah anasema: Samahani nilipitiwa na kudhani nimekwisha kujibu, pole sana kwa usumbufu niliokusababishia. naja kumalizia....Mama T, mume wako hajiamini hali inayomfanya ashindwe kukuamini wewe. Ukijiamini kuwa ni mpenzi mwema, unajua wajibu wako kwa mkeo huwezi kuhofia vitu vidogo kama kutopokea simu......wanaume wengi ambao sio waaminifu ndio huwa na tabia hiyo aliyonayo mumeo.


Huenda hajawahi kutoka nje ya ndoa yenu ila yuko njiani kufanya hivyo ndio maana anaonyesha wivu kupita kiasi, kutokana na ego zao (wanaume) huwa hawapendi au niseme hawawezi ku-hadle the idea ya "kutiliwa/tombewa" mkewe achilia mbali mpenzi wake, sasa kama yeye anafanya hivyo au anataka kufanya hivyo anataka kuhakikisha hakuna wa kulipiza kisasi kwa mkewe kwa kudhani kuwa atakaefanikiwa kukufanya wewe atafaidi kama yeye anavyo/atakavyofaidi mwanamke mwingine.


Suala muhimu ni kuzungumzia matatizo yenu kwa wazi na bila kuhusisha hasira. Unapozungumza na mumeo kamwe usianze kwa kuuliza maswali kama "kwanini unanifanyia hivi au vile" na badala yake unamuweka katka mazingira mazuri na tulivu kiakili na kimwili (usihusishe ngono, kwani atakupa majibu ili kupata mambo na sio kumaanisha) kisha unazungumza nae sio kutaka majibu kwa kuuliza bali akusikilize na kukuelewa.


Unaweza kuanza..MF-"Ayoub nakupenda sana mume wangu, najua kuna vitu vingi sana nafanya ambavyo huwa havikufurahishi lakini kati ya hivyo hakuna hata kimoja kinahusisha mimi mkeo kusaliti ndoa yetu. Naomba mpenzi wangu ujenge uaminifu kwangu kamavile ninavyokuamini".....wakati unasema hayo na mengine unayodhani ni muhimu ili kusaidia kubadilisha tabia yake mbaya basi unapaswa kutumia uanamke wako kumfanya aendelee kuwa interested kukusikiliza.

Wanaume wakati mwingine wanahitaji muongozo kutoka kwa wake zao as if ni mama zao, sio ktk kuwa-control,lisha, ogesha,beba n.k bali kuwaelekeza namna ya kuishi kama pea/wapenzi/wenza......sisi wanawake tunabahati kuwa tunafundishwa kabla hatujaishi na wanaume au hata kuolewa. Wanaume wengi wanajifunza wenyewe tu hapa Duniani hivyo basi kuna mengi hawayajui hasa namna ya kuishi na mwanamke lakini wewe kama mwanamke unatakiwa kuongoza (sio kwa kumuambia hujui kitu la hasha! tumia busara na mapenzi).


Sasa, ikiwa hamtoelewana ninyi kama wapenzi basi ni vema kupeleka matatizo yenu juu zaidi. Kwa kawaida wanandoa huwa tunakimbilia kwa wazazi, lakini kumbuka wazazi wanatupenda sisi watoto wao hivyo kwa vyovyote vile kutakuwa na "kaupendeleo" upande mmoja tofauti kabisa kama mkikutana na mtu baki lakini anauzoefu au niseme mtaalam wa mambo ya ndoa na mahusiano itakuwa vema zaidi.


Labda nikuulize au unaweza kujiuliza mwenyewe....je unampenda mumeo? Uko tayari kujaribu kuifanya ndoa yenu iwe bora au unahisi kuchoka na mapenzi yanapungua kutokana na visa vingi, ila unakaa ndoani ili "usidhalilishe" wazazi wako na jamii kw aujumla?

Kumbuka kwamba, tunafunga ndoa kwa vile tunapendana na tunataka kuishi pamoja kila siku za maisha yetu kwa furaha, amani na upendo mpaka kifo kitutenganishe. Lakini kama ndoa inakosa au haina vile vigezo muhimu kwanini hasa ilifunga ndoa kwanini uendelee kuwepo ndani ya ndoa hiyo?

Majibu utakayopata kuhusua hisia zako juu ya ndoa yako, uhusiano wako na mumeo na hisia zako za kimapenzi kwa mumeo zitakusaidia kufanya moja ya maamuzi makuu mawili yafuatayo:-

1-Kwa kushirikiana nyote wawili mjitahidi na kufanya ndoa yenu iwe bora.
Au
2-Kuvunja ndoa hiyo na kila mmoja wenu kuendelea na maisha kivyake.

Kila lakheri.

8 comments:

Anonymous said...

Kuna kitu kinaitwa `wivu’ na hiki kila mtu anacho, tatizo ni jinsi gani kila mmoja anavyoweza kuishi nacho. Wivu ni ile hali ya uwoga na kutokujiamini kuwa `huenda’ nika-, au kwanini yule isiwe mimi, na vitu kama hivyo. Neno hili linaweza likawa na maana pana kutegemeana na nini unachokiangalia.
Kwa upande wetu tunaangalia wivu katika mapenzi, `huenda, nikakosa,huenda…’ ndio hisia inayojijenga moyoni.
Ukiangalia kwa undani, huu ni uwoga wa hisia, kwasababu unachokiogopa huna ushahidi nacho, ndio maana tunajaribu kuweka vizuizi, kwa wapenzi wetu, tunataka uvae hivi, au usionekane vile kwasababu wengine watakutamani,na matokeo ni kukosa.
Wivu unaweza ukawa mzuri,kama wivu huo ni wamaendeleao, kwa mfano,unataka mkeo au mumeo aonekane kama au zaidi ya yule. Ndio maana wengine wakasema kama huna wivu kwa mwenzako humpendi.
Mwenzangu wewe mumeo ana wivu, na wivu wake ni wa kutokujiamini. Na hii inachangiwa, na udhaifu wake na pia wewe mwenyewe muuliza swali. Udhaifu wake kwasababu inahisi huenda akatokea mtu akakupa kile ambacho hana au hawezi kukupa. Sasa kinachotakiwa ni wewe kumuonyesha kuwa hicho kitu anacho na kuwa hakuna mwingine anayeweza kukuchukua, ndio maana nasema na wewe unahusika. Mara nyingi , mwizi huogopa sana kuibiwa,kwahiyo anajihami mara kwa mara. Inabidi wewe uhakikishe unaiondoa hiyoi hali kwa kumpa kile ambacho kitamuondoa hofu.
Je utawezeaji kumuonyesha mwenzako kuwa yeye ni yeye tu na kumuondoa hofu? Hili ni swali muhimu; kwanza kabisa nikumjengea mwenzako imani kwa maneno matamu na vitendo vya mvuto, kiasi kwamba anakuwa anajiamini kuwa wewe unampenda peke yake(nyama ya ulimi). Kauli zinaweza kuashiria vinginevyo. Tujaribu kuchunguza kauli zetu, pia muonekano wetu. Kwanini ujirembe na kuvaa nguo nzuri au nguo za mvuto tu wakati wa kutoka? Hali kama hiyo unaweza ukaifanya wakati wowote.
Wanaume wengine wana hofu kuwa wanawake wakienda kwao hubandikwa mambo kinyume na mume anavyotaka (Kuna baadhi ya matukio,mke akienda kwao hupewa madawa,limbwata nk. Mume akishamuoa mke anamjenga kwa tabia yake aitakayo na hapendi ije ivurugwe, wengi wanaamini nyumbani kwao mke ni rahisi kuivunja hiyo tabia kama atakwenda kwao mara kwa mara(Hizi ni hisia za wivu wa kutojiamini)
Jambo jema ni kukaa na kuongea, na maongezi kama haya yana muda wake, sio kulazimishana. Muda muafaka ni baadhi ya starehe, kila mmoja akiwa anaraha na mwenzake. Cha ajabu ni kuwa maongezi kama haya yanaanzishwa kipindi mmoja akiwa hayupo tayari kuyapokea, inabidi tusomane tabia.Kuna mambo tunayadharau kwa kusema kwanini nimfanyie yeye tu, kwanini mimi.... Ni vyema wewe kama unaelewa nini kinasababisha hili au lile fanya vile mwenzako anataka ili umpe mwanya wa kujiamini, na muda ukifika elezea hoja yako!
emu-three

Anonymous said...

Dinah,do not post hiyo habari ndeeeeefu niliyokwandikia kuhusu Shule za msondo na niniiiii.Hausiani na mada zilizomo kwenye blog yako,ni katika kutaka kufahamiana tu dadayangu.

Ndimi,
seketab@yahoo.co.uk

Anonymous said...

Habari gani? Pole sana dada yangu mpendwa kwa yanayokusibu, kwa hakika hilo ni chozi lishikalo moyo! Kwa uchache kabisa ni kuwa kuna dalili kubwa ya usaliti ktk ndoa yako. Madhila yote anayokufanyia ni kwamba anajaribu kujihami kwa yale anayokufanyia na kwahiyo hayo yote anafanya kama protective mechanism. Nakushauri fanya uchunguzi kmyakmya huku ukijichunguza nawewe mapungufu yako!. Ikiwezekana tafuta siku jiandae vema na umuombe mumeo kwa upole kwamba una mazungumzo naye. Kumbuka kuwa hekima bora zaidi, namaanisha kuwa usikimbilie kumlaumu, baadala yake muambie kuwa unaona siku hiz amebadilika, na umuulize kwa upole kuwa umemkosea nini au unakosea wapi ili uweze kujirekebisha. Jaribu pia kumuuliza kuwa anataka umfanyia mambo yapi ili afurahi nawe ufurahi. Mwishowe mweleze pia yanayokukera na yanayokuvutia kwake. Kumbuka ktk yote hayo usikimbilie kulaumu baadala yake uwe na lengo la kuyajenga. By ma cster & enjoy ur luv.
By Mwatima.

Anonymous said...

huyo mumeo keshajua udhaifu wako ndio maana anakufanyia mkusudi anajua huna la kufanya

Anonymous said...

Dada Dina kulikoni?
Ulituaga vizuri kwamba utanatoka ukirudi mambo yatakuwa waaa. Sasa inakuwaje tunarusha comment na shida zetu hatuzioni kwa siku 2 au zaidi? Usituvunje moyo. Tunakujaga na usongo san ahapa kuona nani kasema nini na watu wamenishauri nini leo. Ukikuta patupu unafunga ukurasa umenyong'onye kweli. Okoa tafadhali.Sijui na huu utabaki kwako!?

Anonymous said...

Sikiliza Dada yangu, mimi nakwambia kabisa jinsi nimeshaona na kusoma'maana kustudy' tabia ya walioowana. Mara nyingi mambo yanakuwa shwari mwanzoni jinsi ulivyoelezea. Sasa ni miaka mnne na mumeo anakuchukua'treat' kama wewe ni wewe upo jela jela hivi -- yaani hata hakuamini, mpaka amuulize mtoto wa miaka minne. Mimi mwoono wangu ni kwamba your husband can pass to be a saddist na sababu zifuatazo, anafurahi kukuona unayong'onyea kwa uoga na labda hata machozi, anarudi kazini na nyumba inavurugika. Umeelezea kuwa 'akaanza kutafuta mkanda' inamaana pia anakupigaga??? Jamani kina dada, mama na wote Ndoa sio kupelekwa toharani wakati bado tupo duniani, ndoa ni za kuonyesha upendo, uelewano, na ni za kukuza familia ambazo kesho zitakuwa mfano bora. Yaani sasa ni mara ngapi mtoto wako atayaona hayo, na kama ni wa kiume basi subiri ... ataanza kukutreat exactly the same way kakianza tu kukua, jinsi tangu utoto anaona baba anavyokutreat. Huyo uliomwoa si Mungu ambaye unatakuwa kumwogope, ni mzazi mwenzako, sasa kama hata hauko free na yeye then when are you supposed to feel free?? or with whom???. Mimi naona wanaume wanatakiwa wabadilike, wajue kuwa ndoa sio sawa na kununua ng'ombe kwenye mnada ambaye utaweza kumfanyia chochote unachotaka. Ndoa hujengwa na wote wawili, inahitaji willpower na mapendo... wakati wa raha au uchungu. Mimi kweli kweli nakwambia, miaka itapita na huyo mume usipoonyesha uko strong and kuclaim/wants to be recognised a his wife with respect and all that goes with it, then hata miaka 10 ikipita hizo treatment zitaendelea na za zaidi, and the worst part will be that you would have taken in so so much and your confidence will be none existance na uzee umeshaingia. Ndio unasikia kina mama wengine wanasema, mmmhhh wacha nijikalie tu kwa ajili ya wanangu .. in a loveleeessss marriage. Gud luck

Anonymous said...

DALILI KUBWA YA WANAUME ABUSIVE NI KUMTENGA MKE WAKE(ISOLATION), KUMTENGA NA NDUGU, MARAFIKI, MAJIRANI NA WATU WENGINE WANANAOMZUNGUKA! HII NI DALILI MOJA KUBWA SANA WANAWAKE WOTE LAZIMA MUIJUE. HATUA YA PILI INAFUATIA VERBAL ABUSE(ANAANZA KAULI ZA KUKUUMIZA, MATUSI NA KUKUPONDA, HATUA YA TATU NI KUKUPIGA NA HII YA TATU INAPOTOKEA MARA NYINGI ATAKULAUMU KUWA WEWE NDIO UMEJITAKIA. WAKATI HUO AMESHAKUMALIZA SELF CONFIDENSE YAKO, UNAKUWA NA LOW SELF ESTEEM NA INSECURITIES KWASABABU MWANZONI ALISHAKUABUSE EMOTIONALLY. NASIKITIKA KUKUAMBIA KUWA BAHATI MBAYA SANA MUMEO NI MMOJA WA HAO WANAUME, NI VYEMA UKAGUNDUA DALILI HIZI ILI UJUE UTACHUKUA UAMUZI GANI! NAKUTAKIA KILA LA HERI!

Anonymous said...

Dada

Mumeo huyo pengine akawa na mpenzi mwingine, na pengine huyo mpenzi wake ni girlfriend, mchumba au mke wa mtu mwingine. So pengine anaona kama mwanamke wa mtu anaweza kuwa na mahusiano na mwanaume mwengine, basi hisia hizo anazipandikiza kwako. Nina maanisha kwamba anaweza kuwa anafikiri na wewe unacheat kinamna.