Wednesday, 24 September 2008

Ndoa ya mkataba....

Dada Dinah, unajua wakati mwingine najiuliza inakuwaje mambo kama haya yanafanyika na je yanauhalali gani kwa huyu na kwa mwingine isiwe hivyo!Wikiendi hii nikiwa nimejipumzisha kuvuta muda, unajua tena `funga’, ukiwa nyumbani inavyonoga.

Akaja binti jirani. Sikumuelewa awali, kwani alivyojistiri kinamna usingeweza kujua kuwa bado ni `mtoto wa watu'.`Nilikuja kumuona dada, nilikuwa na shida naye' alianza kujieleza kwa aibu, na niligundua kuna tatizo ambalo limemkwaza.

`Akija nitamuambia, kama ni lazima yeye' nilisema nikichelea nisije nikateleza na kuiathiri swaumu yangu.`Aaah, unajua ningemueleza mwanamke mwenzangu ni rahisi kunielewa, lakini hata wewe unaweza kunisaidia kwa ushauri, ingawaje najuwa wanaume mnalindana kinamna’.

Haya dada Dinah, kaa mkao wa kusikiliza kisa chenyewe. Binti huyu ni miongoni mwa wale mabinti wanaoolewa kwa kupitia mtu mwingine, anaweza akawa kaka mtu kamuolea mdogo wako, kwa hiari ya mdogo mtu.

Mwanaume muoaji ni wenzetu, wanaosoma na kubeba maboksi huko Ulaya, akaona asivunje taratibu na adabu za kwao. Aliomba wazazi wake wamtafutie `kimwana' huku bongo akirejea asisumbuke, kwani umri nao ulishaenda.

Na kweli wanandugu wakaifanya hiyo kazi barabara, na binti mrembo mwenye adabu na aliyekulia katika maadili akapatikana. Na akakubali kwa hiari yake mwenyewe kuolewa.Sasa ni mwaka wa tatu tangu ndoa ifanyike.

Bwana wanawasailiana na mkewe kwa barua na simu lakini hajafika, na `hawajaonana' na binti. Lakini mawasiliano, matumizi na mapenzi ya`telefoni' yalishamiri utafikiri walijuana kabla.Taarifa nyepesi nyepesi zikaja kuwa jamaa anaye mwanamama wa kizungu akipitisha naye muda kwa mkataba, kuwa akimaliza `masomo' yake wasijuane tena (nasikia hii ipo sana).

Na jamaa anawaambia rafiki zake kuwa ana mke home na huyu huku ni wa kupitisha muda tu, `rijali lazima uwe na kitu...'Binti kuipata hiyo akaona `anaonewa' kwanini iwe hivyo, kwanini kama ni hivyo naye asipate wa kupoteza naye muda kama mwenzake?


Yeye aliuliza na kuongeza, `sio kwamba nataka kufanya hivyo, sitaki kabisa machafu hayo, lakini nahisi sitendewei haki'Anaomba ushauri je upo uhalali wa namna hiyo? Zipo ndoa za mikataba? Je hata kama akija kutakuwa na mapenzi ya kweli, ili hali mwenzake keshaonja mapenzi ya kizungu?(akiwa na maana wenzetu `wadhungu’wanayajua mapenzi zaidi kuliko sisi, hivyo yeye ataonekana si kitu.Majibu niliyompa nayahifadhi kwanza, nisikie wenzangu mnasemaje na hili.

Na hasa hili jipya la `ndoa ya mkataba' je ipo ndoa ya namna hii.

Nawasilisha.emu-three

Jawabu: Hehehehe asante M3 ulivyoandika nimeburudika sana, nilifikiri nasoma liwaya. Uandishi wako unavutia kusoma. Shukurani kwa kuweka suala hilo hapa.

Nijuavyo mimi ni kweli kabisa kuwa kuna ndoa za "makaratasi" ambazo ndio tunaweza kuziita za mkataba japokuwa upande wa pili huwa hawajui kua ni ndoa ya "Muda", kwamba watu huamua kufunga ndoa na watu wengine ili baada ya muda fulani wapate haki ya kuishi nchi husika na muda huo unapokwisha basi talaka hutolewa kisheria na kila mtu anachukua ustaarabu wake.


Lakini ndoa hii inapokuwa imefunga ule upande wa pili (mara nyingi huwa wadhungu ) huwa hawajui kuwa wanaoa au kuolewa kutokana na Utaifa wao na sio mapenzi hivyo mapenzi hutolewa kama "ifuatavyo" na kila kitu kina kuwa kama uhusiano wowote ule wa ndoa mpaka hapo "mtaka makaratasi" anapopata Utaifa kama wa "mke/mume wake".


Huyu binti alihitaji kueleweshwa tangu awali kitu gani kinaendelea huko Ulaya na kwa uwazi kabisa kwanini kuna hiyo ndoa ya "mkataba" kisha angefanya uamuzi wa busara kabla hajafunga ndoa na "hewa" au Picha.

Huyu binti inaonyesha hamnazo kabisa au alibabaika kwa vile Jamaa yuko Ulaya, alikubali vipi kuolewa bila kujenga mapezi kwanza na "mume wake"? Anauhakika gani kuwa ataweza kuishi maisha yake yote na huyo "mume wake" na kuvumilia mapungufu yake? Tuyaache hayo.

Huyu binti kama mwanamke anaejiheshimu hapaswi kulipiza kisasi maana kuwa umbile la mwanamke linakuwa "ruined" kwa kungonolewa ovyo, pili matunda ya kungonoka ni magonjwa ya Zinaa na kumimbwa na hilo likitokea ni wazi kuwa atapoteza maisha yako kizembe na kijinga, pili akishika mimba na kuzaa ni wazi atakuwa amepoteza ndoa yake na wakati huohuo utakuwa na mtoto ambae huna uhakika kama baba yake atamuhitaji yeye kuwa mke wake.

Suala muhimu kwa huyu Binti ni kuzungumza na "mume" wake na kuomba kueleweshwa kwanini ndoa ya Mkataba ipo, faida yake ambayo bila shaka itamfaidia yeye pia na ukweli wa ndoa hiyo kuwepo kwa muda gani, kama mke basi ajaribu kumuwekea mipaka mume wake in terms of kutowa na familia ya "mkataba", ikiwa mume atakubali basi aendelee kuvumilia mpaka "mkataba" utakapokwisha.

Vinginevyo ni kutoa talaka ili awe huru kuendesha maisha yake nahatiame kukutana na mwanaume mwingine ambae atajenga mapenzi ya kweli na hatimae kukubaliana kufunga ndoa.

Suala la ujuzi wa kufanya mapenzi halina Uzungu ni mtu mwenyewe tu, uwezo kwa kufanya mapenzi, utundu wake, hali ya kutaka kujifunza na kujaribu mambo mapya, kuujua mwili wake, kuwa muwazi na mdadisi juu ya mwili wa mume wake......hey Dinah sio mzungu lakini niko juu zaidi ya wazungu wengi hehehehehehe.

Msalimie....

Tuesday, 23 September 2008

Hataki nikajitambulishe kwao-Ushauri!

Hili Naomba Ushauri wako Dinah!!!Pole kwa majuku na juhudi zako za kutuhudumia sisi kama wana jamii. Nahitaji msaada wa usahauri na mawazo pia juu ya suala hili,

Mimi ninae mpenzi wangu kwa sasa tuna nae miaka mitatu tangu tuwe ndani ya uhususiano huko, pamoja na kuwa maisha yetu yako mbali kwa maana ya mikoa mimi huwa niko Dar kwa wazazi wangu naye Tanga ndio kwao kwa wazazi wake waliko jiwekeza.Lakini mimi nafanya kazi mkoa wa Kilimanjaro na yeye sasa kamaliza chuo yuko kwao Tanga. Suala kuu hapa ni mimi kushindwa kumuelewa huyu mwenzangu, mara kwa mara huwa nahitaji kufika kwao tukajitambulishe kuwa mimi na yeye tuko katika hayo mahusiano naye na ambayo mategemeo yetu ni ndoa na kumaliza maisha yetu tukiwa pamoja inshallah.Lakini kinachotokea hapo ni kwamba anakuwa kinyume na hilo na anasema ni vema tukienda kujifahamisha na tusikae mda mrefu then tufunge ndoa, muda ambao yeye aliokuwa anataka usizidi miezi 6, nikamwambia fine mimi niko tayari hata sasa, then hapo sasa akaingiza suala la kusoma.Kusoma huko ni kuwa mwaka huu kamaliza Advance Diploma ya Accounts na anahitaji kufanya CPA sasa kwa plani na mipangilio tukakuta kuwa kama mungu atajalia na kuenda vema basi mwaka 2009 mwezi wa tano atakuwa kamaliza, nami nikamwambia kuwa sasa tukajifahamishe then Mipango yetu ya ndoa iwe mwezi Decembar 2009 baada ya kumaliza pepazako.

Well, kilichoibuka hapo ni kwamba anasema yeye atakuwa tayari kufanya ndoa mwaka 2010 june, sasa kwa kweli mimi simuelewi mtu huyu kwani naona kama ananichanganya na mimi suala la kuwa niko tu hamapaka huko 2010 bila ya hata japo kufahamika kwa wazazi niko nae siwezi.


Bust still nampenda sana mpenzi wangu sasa sifahamu:- ni kwamba napenda mahala nisipo pendeka au nini hasa!!??Kwani hata wakati yuko chuo nikiwa niko Dar nilikuwa nikienda huko chuoni kwao Arusha na kaa nae kwa cku mbili na kuondoka zangu na baadae nilipokuja pata kazi hapa Kilimanjaro cha ajabu ni kuwa kwa almost mwaka mmoja alikuja mara tatu tu, na some time alikuwa akipata likizo chuo anathubutu kupita hapa moshi bila kushuka na kwenda kwao Tanga same applied akirudi chuo bila kushuka Moshi kuja kwangu.

Kwa hayo naomba msaada wenu wa mawazo ili nami niondokane na utata wa mapenzi.


Jawabu: Pole sana kwa kuwekwa njia panda, nafikiri kinachohitajika hapo kuzingatia na kuifanyia kazi kuu mbili kati ya zile tamo za kuboresha uhusaino wa kimapenzi ambazo kuelewana/kusikilizana, kuheshimiana na kuwasiliano.

Mnahitaji kuwasiliana kwa maana kuzungumza kwa uwazi kitu gani mhakihitaji kwenye maisha yetu kama "pea" au wapenzi mnaopendana na wenye nia moja ya kuishi maisha yenu tote pamoja kama mke na mume na wakati huohuo kuelewana nini kifanyike sasa na kitu gani kisubiri na bila kusahau heshima kwa maana ya kuheshimu uwepo na hisia za mwenzio kwa kumhusisha kwenye maamuzi yako balada ya kuamua kwanza kisha unaenda kumjulisha nini kinaenda kufanyika bila kujali kama ataafikia au la.....kwani pamojana kuwa umemwambia na anajua lakini hatokuwa na nguvu ya kuzia kile ulichoanza kukifanya.

Kutokana na Utamaduni wetu wa kibongo (kwa familia zinazoheshimu na kufuata maadili) mtu kuwa mpenzi (bf) anakuwa hana uzito sana kwenye maisha ya msichana husika isipokuwa tu kama mpenzi huyo atakuwa amechumbia na hapo ndio utakuwa unahusishwa zaidi kwenye maamuzi ya maisha yake ya baadae.

Hii inaweza kuwa moja ya sababu, kwamba yeye anaamua kufanya maamuzi kwanza kisha anakuja kukuambia kitu gani ameamua kufanya kwa vile anachokiona hapo ni yeye na sio ninyi kama pea/wenza.


Sababu nyingine inaweza kuwa jinsi anavyochukulia swala zima la kuchumbiwa na kufunga ndoa, unajua wanawake tunatofautiana, kuna wale ambao kuolewa au kuchumbiwa wanadhani ni "deal au bahati hivyo jamaa akionyesha nia ya kutekereza hilo huwa hawachelewi kukuruhusu uendelee na mipango ya kwenda kujitambulisha.


Wapo wanawake wengine ambao wao swala la kuchumbiwa na kuolewa kabla hawajafikisha maleongo yao ya kimaisha/masomo wanadhani ni kuharibiana maisha hivyo siku zote hukwepa na pengine kuua uhusiano mara tu utakapotangaza ndoa.


Vilevile wapo wachache ambao wanakuwa hawana uhakika (kama ilivyo kwa wanaume) kama wako tayari kuchumbiwa na hatimae kufunga ndoa japo kuwa wanamapenzi ya kweli na dhati kabisa, lakini mioyoni mwao wanahisi mwanaume husika sio "type" ya mume ambae wangependa kuishi nae milele hivyo hujizunguusha.


Bila kusahau sehemu ndogo sana ya jamii ambayo wazazi wanataka binti yao aolewe na kijana mwenye aina fulani ya maisha hali inayoweza kusababisha binti kuhofia kwenda kukutambulisha kwako kwa vile anajua kabisa akifanya hivyo ndio utakuwa mwisho wenu, lakini kwa vile anakupenda na angependa kuwa na wewe basi huamua kukwepa bila kukuambia ukweli ambao unaweza kukuumiza hisia zako na hatimae kuua uhusiano wenu.


Natambua kabisa vitendo vya huyu binti kubadili msimamo kila mara, kutokuja kukutembelea pale anapokuwa likizo na kugoma kwenda kujitambulisha kunakukatisha tamaa na kukufanya uhisi kuwa huyu binti huenda anauhusiano na mtu mwingine.

Unachopaswa kufanya hapa ni kutafuta muda na kuzungumza nae ana kwa ana na kumwambia hofu yako juu ya uhusiano wenu, mwambie kuwa huna tatizo kufunga ndoa mwaka 2010 (kutoka 2009-2010 sio mbali) ila kitu kitakacho kufanya uendelee kusubiri ukiwa na amani moyoni ni wewe kuchumbia (ku-book)kwa maana ya kwenda kwao kujitambulisha, kumvalisha pete na kulipa mahali (kama itahitajika).

Unaweza kumtambulisha hapa na akapata nafasi ya kuongea na mimi moja kwa moja ili niweze kumuweka sawa.
Kila la kheri.

Monday, 22 September 2008

Aliniambia ananipenda, sasa ananikwepa-Ushauri!

Habari dada Dinah, pole na majukumu yanayokuzonga kila siku, mimi ni msomaji na ni mpenzi wa blog yako kiasi ya kwamba siwezi kupitisha siku bila kufika hapo nikaangalie kipi kipya.

Tuyaache hayo leo nami kwa mara ya kwanza nimekuja na tatizo langu ambalo linanizonga na kunisumbua sana kichwa changu na jibu si lijui.

Mimi ni msichana mwenye miaka 24, kuna kijana mmoja niliwahi kukutana nae mwaka mmoja uliopita yaani 2007, kipindi hicho hakuwai kuniambia kitu chochote zaidi ya salamu kutokana na kukosa muda wa kuwa karibu, kwani hatujawi kukutana kwa ukaribu hata siku moja yaani mita 20.

Sasa mimi nikaondoka eneo lile tulilokuwa tunakutana kwa umbali nikaamia sehemu nyingine, ndio juzi tutakutana tena na tukapata muda hata wa kupeana mikono na kuongea mawili matatu, na tukapeana namba za simu.

Ikapita kama siku mbili akanipigia na kunikaribisha kwake,nami nikaenda tutakaa na akaniambia kuwa amevutiwa nami na anapenda awe nami, ki ukweli dada Dinah ni hata mimi nilivutiwa nae ingawa sikuweza kumjibu pale pale kwa kuona soo.

Baada ya kuachana siku hiyo yule kijana akawa amesafiri akakaa kama wiki moja, toka amesafiri ni mimi ndie niliyekuwa nampigia simu, mwishowe nikiwa nampigia akawa ananiambia nikate then anipigie.

Sasa kweli huyu jamaa ananipenda kweli au alikuwa ananibeep maana hata sijawahi kufanya nae kitu lakini ananikatisha tamaa kabisaa, maana hata alivyorudi hii ni wiki hatujaonana kwa kisingizio kuwa anakazi nyingi.

Wakati mwingine huwa namuona kabisa akipita kutoka kazini nikimpigia simu ananiambia kuwa bado hajatoka sasa je huyu kijana anamapenzi ya kweli au alikuwa anataka kuonja na kuondoka, please naomba unisaidie dada yangu maana ki ukweli huyu kijana nampenda but nahisi kama nitaingia kusikofaa.

Sara"

Jawabu: Asante sana Sara kwa ku-share suala hili mahali hapa. Mwanaume anapokuambia kuwa anakazi nyingi (busy) harudishi simu zako au anakiongea basi inakuwa kwa kifupi/haraka fahamu kuwa hilo ni buti la kistaarabu.

Unapaswa kumshukuru Mungu kuwa huyo jamaa anakukwepa hasa kama unaamini kuwa kila kitu hutokea kwa sababu zake. Huyo bwana lazima kuna kitu kinamsumbua ambacho mimi na wewe hatukijui. Inawezekana kabisa jamaa anamatatizo ya kiafya na anahofia kukuumiza ikiwa atakuambukiza, huenda alikuwa anajaribu zali ili apate nafasi ya kukungonoa lakini baada ya kutopata "kidude" akahisi humfai kwa vile umembania, labda alidhani anataka kuwa na wewe kama mpenzi lakini baada ya kusafiri akagundua kuwa hisia alizokuwa nazo juu yako zimekwisha kwa maana hazikuwa za kweli.


Ni heri mwanuame anae epuka kukupotezea muda kwa kuepuka kuwa karibu au kuonana na wewe kuliko yule anaeijifanya anakupenda na unakuwa nae kila siku lakini anajua wazi uhusiano wenu hauna maisha marefu yaani anakuchukulia wewe wa "kupita tu".

Mimi nakushauri uache kupoteza muda wako kuwaza na kuumia kihisia na badala yake mdharau na uendelee na maisha yako, Mungu atajaalia siku moja utakutana na kijana atakaekupenda kwa dhati na kuwa pale kwa ajili yako.

Kila lililojema.

Mimi ni mzuri, nifanye nini kuwa nae?-Ushauri

"Dada dinah naomba msaada wako kuna Kaka fulani nampenda sana na najua mimi ni mzuri hawezi kunikataa ila sitaki kumuambia kwamba nampenda sijui nifanye nini ili niweze kuwa naye naomba msaada wako dada"

Jawabu: Asante kwa barua pepe,kutokana na maelezo yako mafupi ni kuwa "umefika bei" lakini unahofia kukataliwa ndio maana hutaki kumwamabia kuwa unavyojisikia juu yake. Suala la uoga wa kukataliwa (kutokuwa na uhakika kama utakubaliwa) pia huwakumba wanaume lakini kwa vile wanaume wameumbwa na ujasili wanayo namana ya ku-deal na "rejection" kitu ambacho sisi wanawake hatuna.

Mwanaume ukimkatalia atajitahidi kukushawishi na mwishoni unajikuta unaanza kudondokea kidogo kidogo, mwanamke ukikatataliwa inakupunguzia ile hali ya kujiamini, aibu mbele ya mwanaume huyo na ukimfuatilia ili kujaribu kumshawishi utaonekana unawalakini kwa vile mwanamke sio muwinaji bali anawindwa.

Kitu muhimu unachopaswa kutambua ni kuwa hakuna uhusiano kati ya uzuri wa mtu na mapenzi kwa vile uzuri wa mtu uko machoni mwa mtu(mtazamaji) huenda wewe ukajiona umzuri sana na pengine rafiki na jamaa wa karibu wanakuona na kukusifia kama vile Mungu alitumia muda wake vizuri sana alipokuwa akikuumba wewe. Hiyo sio tiketi ya yeye kukupenda au kutaka kuwa na wewe kwa vile mimi na wewe hatujui kama anakuona mzuri kama unavyojifikirua/jijua.


Kwa vile huna uhakika kama na yeye anahisia juu yako(hujagusia kwenye maelezo yako kana na yeye anaonyesha "interest") kumwambia moja kwa moja haitokuwa sahihi hivyo unahitaji kuwa karibu nae kwa kurafikiana kwanza, kama mwanaume atajua wazi kuwa "unamzimia" na hakika atakutokea lakini kama hana hisia za kimapenzi juu yako basi hatofanya hivyo namtabaki marafiki tu.

Njia rahisi ni kutafuta mawasiliano yake kama anuani ya barua pepe au nambari yake ya simu kisha anzisha mazungumzo nae lakini hakikisha unabaki na ahiba yako kama mwanamke. Kama jamaa hana mpango na wewe utatambua na ikiwa jamaa anampango na wewe pia utafahamu.

Akionyesha kuwa na mpango na wewe basi unaweza kumualikwa kwa ajili ya kinywaji pale dukani kwa Mangi (popote patulivu) au kwenda kwenye tamasha/mkutano/kanisani n.k. vilevile kama kuna sherehe basi jaribu kumpa taarifa mapema ili aweze kuhudhulia hali itakayokufanya uwe karibu nae zaidi kwani kati ya wageni/watu wote watakao kuwepo mahali hapo ni wewe tu ndio atake kuwa anakujua hali itakayo mfanya asicheze mbali.

Wanaume ni wepesi kutambua ikiwa wanapendwa bla hata kuambiwa hivyo baada ya muda fulani atajua tu kuwa unamtaka na atakutokea/tongoza au vyovyote itakavyokuwa ilimradi tu lengo lifikiwe ambalo ni kuwa nae kama mpenzi wako.

Kama huna namna ya kupata nambari yake ya simu njoo nikupe mbinu moja rahisi sana ya kufanikisha hilo.

Kila la kheri.

Wednesday, 17 September 2008

Uzoefu wa tamaduni 2 tofauti kwenye mapenzi.....

Sup yo!

Baadhi yetu tumekuwa na mahusiano ya kimapenzi na watu tofauti ktk safari yetu ya kimaisha, kwa kawiada kama ilitokea ulitoka na wanaume/wanawake 2 kwa nyakati tofauti na hatimae kuwa kwenyeuhusiano lakini wote wana Tamaduni moja kama yako, inakuwa rahisi kuendelea na uhusiano mpya bila kuona tofauti ya mapenzi unayopokea kwani utakuwa umeisha zoea kutoka kwa yule wa awali(ulieachana nae).


Ukianza uhusiano na mtu mwenye utamaduni wa Kiafrika alafu labda uhusiano hakuenda vema mkaamua kuachana na ukaja kuwa na mtu mwenye Utamaduni wa Kimagharibi ni wazi kuwa utahisi huyu wa Kimagharibi anakupenda kuliko yule wa kiafrika na hapo ndio ile sentensi maarufu ya “wanaume wa kiafrika hawajui mapenzi” inapojitokeza.


Hali kadhalika ukianza uhusiano na mtu mwenye utamaduni wa Kimagharibi kisha ukaachana nae na kwenda kuungana na mwenye utamaduni wa Kiafrika utahisi kutopata “vikorobwezo” vyote vya kimapenzi kama ulivyozoea na hivyo utahisi/tamani kutaka kumbadilisha kwa vile kile ulichokizoea kutoka kwa “mmagharibi” hukipati kwa “mwafrika”.


Vilevile uki-date mtu kutoka nchi za Kiarabu na kule Mashariki bila kusahau Asia khabari inakuwa tofauti kabisa ikiwa utakutana na mtu mwenye Utamaduni wa Kiafrika au Kimagharibi.......


Kwa kifupi Wanaume wa Kiafrika wanasifika kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuridhisha mwanamke kwa nje-ndani kwenye sekta ya chumbani na Mwanamke wa Kiafrika anasifa ya kuwa wa “moto “na kuongeza hamu kwa mwanaume ya kuendelea kufanya mambo fulani bila kusahau sifa kubwa kabisa kuwa hawachoki(pretending kuwa una-enjoy kumbe umejichokea ka’ punda mtoto).....


Wanaume wa Kimagharibi wanasifa ya kujua kucheza na mwili wa mwanamke na kumridhisha ki-romance kabla hajamalizia na mambo fulani, wakati wanawake zao wanasifa kuu ya kutokuendeleza ugomvi (pretending things are ok) wakati sisi wanawake wa kiafrika hatuna hiyo.....ukiniudhi u’ll c it on my face and everything else.....


Lakini hayo yote niliyoelezea hapo juu sio mapenzi niliokusudia kuyaelezea, hayo huja mwisho wa siku. Mapenzi ninayozngumzia hapa ambayo sote tungependa kuonyeshwa, yale mapenzi yanayotufanya tuhisi kwamba hakuna matatizo hapa duniani, ni mapenzi ya vitendo a.k.a kuwa affectionate(nilizungumzia jinsi ya kuwa affectionate kwenye makala za nyuma) ambayo mimi binafsi nadhani kuwa sote wake kwa waume tunahitaji kuwaonyesha wapenzi wetu bila kujali the rest of the world.


Sasa ikiwa wewe umekutana na mpenzi ambae hafanyi vile vitu ambavyo wewe unahisi kuwa ndio mapenzi yenyewe (kutokana na ulivyozoea......ki-Univesal) basi usisite kuliweka wazi hilo kwa mpenzi wako mpya amabe yeye anaamini kuwa “affecionate” ni mpaka mjifungie chumbani.


Kufanya hivyo hakutokufanya uonekane umeiga bali ndio hali halisi ya kwenye uhusiano wa kimapenzi uliowahi kuwa nao hivyo ukikutana na mtu ambae hakupi yale uyajuayo ni wazi kuwa utahisi kuwa "hakufai"....si ndio?


Imagine wewe mwanaume umezoea (kutoka kwa mpenzi wako wa kwanza) kupigwa busu-mate mara tu unapofika nyumbani, sasa umekutana na Dinah binti wa kiswahili wala sina habari......si utahisi sivyo-ndivyo?


Au wewe Mwanamke umezoea (kutoka kwa mpenzi wako wa mwanzo) kuvuliwa na kupigwa nje-ndani akaimaliza kalala, sasa uko na Noel mkaka mwenye Utamaduni wa kimagharibi anaanza kukushika, kukulamba na kukubusu kwa takribani dk 45 kabla hajakufanyia mapenzi.....jamani si utahisi Peponi kumekushukia siku hiyo?


Inapendeza sana na hakuna ubaya ikiwa wapenzi mtachanganya tamaduni (kutokana na uzoefu wenu) ili kuwa na mahusiano ya kimapenzi mazuri, yenye afya na thabiti......kufurahia maisha ndio sababu ya kuishi.

Mida-mida basi....

Monday, 15 September 2008

Mume wangu kaoa M'ke mwingine,kumtaliki ni sahihi?-Ushauri.

"Hi Dinah habari za leo?
Nashukuru kwa maelekezo yako , ni mimi nilieuliza jinsi ja kupost mada. Jina langu kapuni.

Dinah nimekua mpenzi na msomaji wa blog yako, kwa kweli inamambo mengi kwa upande wangu nahisi inatoa elimu, na mara nyengine kuburudisha. Hua nasoma blog nyingi ila ni chache zimekua zikinivutia mada zake. Udumu mdogo wangu katika hili.

Mimi nijiite ni mama mzee tu nina umri wa miaka 40,nilianza mahusiano ya kimapenzi nikiwa na umri wa miaka 22,nikiwa katika mazingira ya kishule nikimaanisha chuo kikuu nje ya nchi, kabla ya hapo sikua nataka kusikia hayo mambo kwa kutegemea tutakae anza ngono ndio awe Mume wangu.

Nili bahatika kukutana na huyo kijana kwa bahati sijui niite mbaya , tulikua ni dini tofauti (mie muislamu yeye mkristo)kabla ya kuanza ngono, nilimueleza kuwa mie niko serious, sasa ikifikia hatua tukaona ni bora tuoane utakua tayari kubadili dini alikubali.

Hapo sikusita tukaendeleza kungonoka kwa miaka kadhaa tukiwa masomoni. Baadae tulirudi TZ , tukabahatika kupata mtoto, binti nzuri kabisa na tulifunga ndoa ya kiisilamu, kwa maana kua aligeresha wazee ili tupate ridhaa yao tuwe pamoja.

Baada ya muda mfupi tu wa hiyo ndoa , alinitaka nami niende kanisani tukafunge tena, nimi nilimshauri kama ni hivyo tuende bomani itakua ndio neutral, lakini aligoma kwa wakati huo, tulikua tunaishi kwenye nyumba ambayo ilikua chini ya mamlaka yangu, alihama na kuniambia huko aendako, nitaenda pale nitakapokubali kufunga ndoa ya kanisani.

Niliacha aende kwa wakati huo. Siku moja nilienda kumtembelea huko alikohamia, wakati nagonga nikasikia redio inalia mara redio ikawa kimya, baadae nilipofungua nikakuta mwanamke ametoka humo ndani. Mie niliamua kuondoka nikarudi kwangu.

Baadae jioni mume wangu alikuja kwangu na nikamuomba msamaha kwa kua sikumwambia kua naenda na kwa kuwa ameamua kuwa na yule labda nae atakua ameondoka, baadae yeye aliomba msamaha na kuniambia anataka kuwa nami ili tumlee mtoto.

Na aliniahidi anamuacha huyo msichana, na akaniruhusu kuhamia kwake, mie bila kusita nilihamia. Baada ya miezi mitatu akaenda shule ya miaka minne nje ya mkoa wa DSM. Alikua anakuja kila mwisho wa mwezi lakini kadiri miaka ilikua ikienda nikawa nahisi upendo wake kwangu ulikua unapungua, kwa maana kua alikua akija ingawa ni siku mbili lakini hashindi nyumbani kwa kutumia visingizio niko na huyu na yule (marafiki).

Hatimae alimaliza akarudi nyumbani,nikaanza kubaini simu za usiku hata saa tano,sita anapigiwa , MSG, baada ya uchunguzi niligungua ni yule mwanamke wa miaka ile na kwa MSg tayari wakawa wanaitana mke/mme. Kwa wakati huo yule mwamamke hakua nchini.

Nilipomuuliza mume wangu hii ni heshima gani ya ndoa, yeye alisema eti yule mwanamke hayupo nchini ninaogopa nini, na baadae nikabaini kadi ya benki ya yule mwanamke anayo huyu baba (mume wangu). nikamwambia hongera kwa kuaminiwa.

Kwa kweli nyumba nilizidi kuiona mbaya, nikimlaumu kwa hilo, mara nyengine aliniambia nikamshitaki kwa wakubwa. Siku moja nilichukua hatua ya kushitaki kwa kaka yake, lakini kaka yake alichonijibu sikuamini,ila nikahisi,hawanifurahii kwenye ukoo wao kwa sababu ya dini.

Shemeji aliniambia eti mimi nitafute watu wengine, ukweli sikutafuta mtu na hapo nilimwambia huyu baba (mume wangu) kama mie ninatafuta nyumba nikipata nitahama kwake kwani inaonekana ameshanichoka nahata heshima hana na ametegesha ili nijifukuze mwenyewe ili yeye asipate lawama.

Nilikua namuambia kua wanaume waliowengi wenye heshima hua wanamahusiano nje lakini wanaficha kwa wake zao, alinyamaza. Baadae akanitangazia kuanzia mwezi fulani nitaanza kulala mitara, na kweli ulipofika huo mwezi akaanza kulala huko siku nyengine.

Nilikata tamaa na hiyo ndoa Niliamua kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja , kutafuta shule, na kutafuta nyumba, kwa bahati mungu alijibu sala zangu zote, nilibahatika kupata shule nje ya nchi na nikapata nyumba.

Nilipomuambia nimepata nyumba , nitaondoka kwako hakuleta hata ile lugha ya kusema usiondoke mke wangu, nilihama mwaka juzi mwishoni na baada ya muda mfupi nikaenda shule nje ya nchi ambapo niko hadi sasa. Mwaka jana wakati nikiwa likizo nimekuta ndio anafunga ndoa ya kanisani, na hakuniambia kama ameamua kuoa ilihali tunandoa ya kiisilamu.

Nilichoamua dada ni kua nikiaenda likizo hii nimtake tuende mahakamani ili tuvunje hio ndoa na nibadilishe document, Naomba ushauri kwa hilo, niko right????

Pamoja na hayo, jambo jengine ni kua , mtoto nilienae ni mmoja, ningetamani nipate mwengine, umri ni 40kuna jibaba moja lilionesha interest ya kuzaa nami, ila hofu yangu ni mume wa mtu ana watoto wawili anasema ananipenda ila ndio hinyo, kusubiri hadi nipate asie na mke pia kwa umri wangu sio rahisi sana (inachukua muda) naogopa kuingia kwenye menopolse kabla sijajaribu tena kuzaa.

Naomba mnishauri mwenzenu, niamuaje hapo? ili nikija huo mwezi wa 12 niwe na maamuzi kama nijaribu na huyo mume wa mtu au nifanyeje?

Nawakilisha

Pole kwa maelezo mengi unajua hua ninatension ya maisha yangu ndio maana nikianza kuyaeleza hua naeka mdorongo huo, sikutegemea kua na ndoa ya aina hio

Kila la kheri".

Jawabu: Asante kwa ku-share sehemu ya maisha yako ya kimapenzi na ndoa mahai hapa. Shukurani za dhati kabisa kwa wote waliotoa michango juu ya hili.

Nisingependa kuegemea sana kwenye kitu amabacho kimepita lakini hata hivyo nitagusia kidogo tu kuwa kosa kubwa lililofanyika ni kufunga ndoa kwa "kuzuga" ndugu na jamaa wako kitu ambacho Mumeo pia alikitaka kwa kufunga ndoa ya "kuzuga" kanisani.

Unajua kila mtu huwa anazingatia vitu fulani muhimu ktk maisha yake ya kimapenzi na hatimae ndoa, na hujitahidi kwa kila wawezalo ili kuhakikisha vile vitu muhimu vinakuwepo kabla hawajaamua kuendelea mbele na masuala mengine kwenye uhusiano husika.

Kwako wewe na mume wako (kutokana na maelezo yako) pamoja na mambo mengine Dini na kuridhisha familia zenu vilikuwa ni vitu muhimu zaidi hivyo basi hilo lingezingatia yote yaliyotokea yasingetokea ( hatuwezi kubadilisha kilichokwisha fanyika)......


Uamuzi wako wa kumtaliki mumeo ni sahihi kabisa ila fanya hivyo kisheria ili kutopoteza haki zako kama mke. Jaribu kutembelea Mahaka yako ya Wilaya ya mahali ulipo na omba kuonana na Hakimu, mara nyingi inachukua wiki moja mpaka miezi 3 inategemea na uzito wa Kesi yenu.


Mahakama kupitia Hakimu ndio itatoa "samansi" ili mume wako aende mahakamani, usimfuate wewe kama wewe (nje ya sheria) kwani inaweza ikakusumbua na vilevile kufanya kesi kuwa ndefu, zingatia kuwa utakuwa nyumbani kwa likizo tu sio kwamba unaishi huko hivyo muda ni muhimu.


Hilo la wewe kutamani/taka kuzaa tena kabla hujafikia "kikomo cha hedhi" limetulia lakini usijifikirie wewe zaidi bali yule mtoto atakae zaliwa na yule ulienae hivi sasa. Fikiria maisha yao ya baadae na mahusiano yao na baba zao.


Hilo baba lenye kuonyesha "interest" kuzaa na wewe wakati tayari anamke na watoto halija kaa vema kwani atakuwa anacheza nje ya ndoa yake kitu ambacho wewe machungu yake unayajua, sasa kwa kujali hisia za mwanamke mwenzio na kuepuka huyo mwanamke mwenzio kutopata maumivu uliyopitia wewe (mume wako alipoibiwa na mwanamke mwingine na hatimae kufunga ndoa) jiepushe na huyo jamaa.


Miaka 40 sio uzee (uzee ni muonekano wa ngozi yako na unavyojiweka wewe sio namba), nina hakika kabisa kuna vijana wengi tu ambao hawajaoa au wale "Wajane" (wanaume wanaitwaje vile?...)na wako huru kabisa kuanzisha uhusiano mzuri na wewe na hatimae kujizalia mtoto au watoto zaidi.

Kila la kheri dada....

Saturday, 13 September 2008

Tunaposingiziwa kila kitu.....

Ni matumaini yangu Mfungo unakwenda vema kabisa na senti ya "kurekebisha" Futari ipo kwani sote tunajua kuwa kipindi hiki ni ghali miongoni mwetu, mbaya zaida unaishi nyumba ya kupanga ambapo nijuavo mimi (kule bara) ni sharti kufuturu pamoja sio familia bali majirani pia, na kila aliyefunga hupenda kuchangia kile alichopika na wenzake, lakini M'Mungu anaangalia kilicho moyoni na matendo yako hivyo hata kama ukifuturu supu ya dagaa poua tu......tuachane na hayo.


Unajua kwenye mahusiano yetu ya kimapenzi iwe ni ndoa au wale "bado wapo wapo" lakini wanawapenzi huwa hakukosi mikwaruzano na mtu akikuambia kuwa kwenye uhusiano wao hawajawahi kutofautia na kusababisha mabishano, mzozo ambao unaweza kusababisha kununiana (mara nyingi sisi wanawake)basi ujue mmoja wao ni muoga kuachwa yaani anakuwa mtumwa wa uhusiano a.k.a "ndio bwana" au uhusiano wao bado mchanga.


Kuzozana kwenye uhusiano ni afya kwani inadhihirisha kuwa ninyi wapenzi na mnapendana sana tu lakini hamko sawa kiakili, kimwili,kimtazamo, kifikra, kidamu(ndugu)na bila kusahau kijinsia. Natambua kuwa kuna wakati mnaelewana vema kabisa na kujihisi kama vile mungu alikushushia yule uliyemtaka, mwanamke habishi wala kuuliza maswali au mwanaume hakutumikishi wala kukutawala (si mwajua wanaume wa kibongo kwa ku-control??? hehehehe).


Ninachojaribu kusema hapa ni hivi, wanaume ni walalamishi pia kwenye mahusiano mengi ya kimapenzi lakini sisi wanawake ama huwa hatuoni au hatujali kwa kufikiria kuwa mwanaume kila wakati yeye yuko sahihi(well most of the time huwa wanakuwa sahihi kuliko sisi wanawake lakini hiyo haifanyi kila wasemalo/kufanya ni sahihi).


Kinachosikitisha au kunisikitisha ni kuwa sisi wanawake tumekuwa tukisingiziwa na hatimae kujulikana kuwa ni walalamishi au tunapenda kulalama kila wakati. Lakini ukweli ni kuwa wanaume ndio wanaongoza kama sio wako mstari wa mbele kulalama kwenye mahusiano kuliko sisi wanawake, kwa vile mfumo dume bado uko miongoni mwetu basi huwa tunadhani kuwa mwanaume anahaki ya kulalama au kujaribu kukumiliki kimtindo.


Mume/mpenzi akichelewa kurudi nyumbani au asipokujulisha/julia hali katikati ya siku (kutokana na maendeleo ya Tekinolojia)ni wajibu wake kujieleza kwanini kachelewa na asipofanya hivyo basi wewe kama mkewe/mwenza wake una haki zote za kuuliza aliko kuwa na alikuwa akifanya nini na yeye ni wajibu wake kutoa majibu mpaka utakaporidhika.......lakini tunachokosea hapo ni namna ya kuuliza, wengi wetu huwa tunauliza kwa hasira kwa vile huwa tunafikiria mabaya zaidi(yuko na nani) kuliko mapenzi yetu na ile hali ya kujali juu ya mpenzi.


Hali kadhalika wewe mwanamke ni wajibu wako kum-alifu mume/mpenzi wako mahali uliko au hata mipango yako ya siku nzima na kuwa "intouch" na ikitokea umechelewa basi unapaswa kutoa maelezo ya kutosha na kuridhisha......lakini kwa bahati mbaya hili likitokea mwanaume huwa mkali na kutoa shutuma ambazo hujawahi hata kuzifikiria. Kwanini anafanya hivyo basi? kwasababu bado anaile "nakumiliki" anakuwa "controling".....unakuwa binti mbele yake na sio mpenzi tena.

Kuuliza kwake mwanume kwa ukali na konyesha umiliki dhidi yako ni kwasababu (kama nilivyosema hapo awali) anakuwa na mawazo mabaya/machafu zaidi kuliko kujali na mapenzi juu yako.

Katika hali halisi sote kwenye uhusiano (wake kwa waume) tunapaswa kujifunza namna ya kuzungumza na wapenzi wetu, badala ya kuuliza maswali katika mtindo wa "talking to you" iwe "talking with you", onyesha uaminifu wako kwa kumuamini mwenza wako, hata kama meudhika au kwazika na kuchelewa kwake basi jitahidi kuuliza maswali kwa mapenzi, kwa upendo katika hali ya kujali na mambo yatakuwa bomba.

Mida mida basi mpendwa.....

Thursday, 11 September 2008

Mume wangu amebadilika sana,nifanye nini?

"Dada Dinah nakupa hongera sana kwa kazi unayoifanya kwa ajili yetu. Baada ya kuwa mpitiaji wa blog yako na kujifunza mambo mbali mbali kuhusu ngono na kukusoma jinsi unavyowaelezea watu kwa upeo wa hali ya juu nimeamua kuchangia tatizo langu ili nipate malezo kutoka kwako.

Nimekuwa kwenye ndoa na mume wangu kwa muda wa miaka 15 na tumejaaliwa kuzaa watoto watatu. Nilivyofunga nae ndoa mimi nilikuwa sio mtu wa kujishughulisha sana kutokana na kutokuwa na Elimu ya awali kama wewe na matokeo yake nimejifunza mambo mengi hapa na kwenda kuyafanyia kazi kla ninapofanya mapenzi na mume wangu.

Tumekuwa tukifurahia zaidi maisha yetu kitandani kuliko ilivyokuwa hapo zamani na cha kushangaza mume wangu hajawahi kuniuliza kuhusiana na kubadilika kwangu kitandani lakini amekuwa akiwahi kurudi nyumbani lakini kinachonikera ni tabia yake ya kunichunga kwa kunipigia simu kila wakati na kuuliza nilipo, sio kawaida yake.

Je ananichunga kwa vile yeye ndo mtokaji au imekuwaje? Naombeni ushauri wenu ili nisije kuwa nachezwa shere. Ashura"

Jawabu: Shukurani Ashura nafikiri mpenzi wako anajitahidi kukuonyesha kuwa anakujali na kukupenda. Huenda kabla ya hapo (haikuwa kawaida yake) hakuwa na hofu ya "kuibiwa" kwa vile ulikuwa hujamuonyesha uwezo wako wa kufanya "mambo fulani", katika hali halisi alijua kabisa kuwa "kingono" hujiamini kama ulivyosema wewe kuwa hukuwa mtu wa kujituma mlipofunga ndoa.

Lakini baada ya kujifunza na kufanyia kazi yale uliyojifunza kupitia hapa amegundua kuwa mambo yako ni makubwa na akishangaa-shangaa iwe kutokukuridhisha kingono au kutokukuonyesha anakujali na kukupenda basi mtu mwingine anaweza "kupata mambo" anayopata hivi sasa.

Mume wako anastahili pongezi kwa kutokukushutumu au kukuhoji umejifunza/julia wapi na badala yake anafurahia na wewe na kujitahidi kukuonyesha yuko pale kwa ajili yako(najua ni tabia mpya na hakika inakera kwa vile hukuzoea) lakini hana jinsi zaidi ya kuhakikisha Mke wake yuko salama popote alipo na hakuna mtu atakaethubutu "kutaifisha mali zake".

Kwa kawaida wanaume wengi huishiwa hali ya kujiamini ikiwa wapenzi wao ni wakali/watundu na hapo utaona "ulinzi" unaongezeka.

Hongera sana na kila lililojema kwenye maisha yano ya ndoa na familia.

Friday, 5 September 2008

Tumekutana mtandaoni,nahisi penzi la dhati-Ushauri

"Nimetokea kumpenda msichana ambaye yupo mbali nami, namaanisha yeye yupo Dar nami nipo Tanga. Nilikutana naye kwenye "chatting sites" na alinipatia nambari yake ya Simu pamoja na picha nami nikampa zangu.

Najua mapenzi ya mbali wakati mwingine hayana uaminifu, sasa nitafanyaje ili anianimi zaidi kuwa nampenda kwa dhati, ingawaje huwa namuambia sana avute subira tutakutana."

******Ufafanuzi***Unahisi kumpenda kwa dhati, huwezi kupenda mtu kwa dhati kabla hujajua mambo mengu juu yake ikiwa ni pamoja kasoro zake na kujifunza kuishi nazo/vumilia.

Jawabu: Asante kwa kuleta swali lako mahali hapa, Ni kweli kabisa mapenzi ya mbali huwa hayana uhaminifu hasa kama hamjuani, kwamba hamjawahi kuonana/kutana. Kumuamini mtu amabe unajua kwa picha na sauti sio rahisi.

Mtu anajifunza kukuamini baada ya kukujua/fahamu kwa karibu zaidi au niseme kwa ktk hali halisi unamuamini mtu kutokana na matendo yake na sio maelezo/maneno sasa ili mpenzi wako mtarajiwa aweze kukuamini ni vema ukaanza kuonyesha mapenzi yako kwa kumtembelea au kumualika Tanga na kuwa-spend sometime pamoja ili kufahamiana vema.

Wapo watu wengi wamefanikisha mapenzi na hatimae ndoa baada ya kukutana kwenye mtandao kama ilivyotokea kwenu ninyi, na mara nyingi umbali huwa ni mkubwa zaidi na unagharimu pesa nyingi (Mambo ya nauli).

Lakini kwa bahati nzuri ninyi mnaishi karibu na pia gharama za usafiri sio kubwa sana, kama kweli uko makini na maneno yako basi mfungie safari hali itakayomfanya ajifunza kukuamini kuwa unampenda kweli.

Kila lakheri!

Thursday, 4 September 2008

Umbali wetu memfanya atoke, je niendeleze?-Ushauri

Habari ya leo dada dinah, pole na kazi za kutuhabarisha mambo kadhaa wa kadhaa yanayokua yanajadiliwa hapa. wengi wetu tunafaidika sana na masomo yanayokua yanajadiliwa.

Mimi naomba ushauri wa swala hili linalonitatiza kwa mda mrefu sasa. nimekua na relation na bf wangu kwa mda usiopungua miaka 4 sasa. mwanzoni mapenzi yetu yalikua mazuri sana naeza sema kama romeo n juliet but baada ya mda nikaanza kuhisi mwenzangu alikua anacheat.

Nilipomuuliza alikana akasema hawezi fanya hiyo kitu, ukapita mda tena same thing ikatokea hadi hao aliokua anacheat nao wakaanza kunipigia simu na kunitukana na maneno kibao ya kunikashfu lakini mwenzangu still alikana kua na uhusiano naye nakusema anamfahamu huyo mtu lakini hawana relation yoyote.

Miezi michache iliiopita niligundua kitu tena kwamba they have relationship na nilipomuuliza tena akaomba msamaha na kujutia yote aliyoyafanya kwenye relationship yetu na kusema wameachana na huyo dada na kwamba yeye ananipenda mimi na anasema anataka kunioa mimi.

Kuna wakati nilisema labda anafanya hivyo(cheating) kwa sababu muda mwingi tumekua tukiishi miji tofauti kutokana na majukumu tulionayo na kazi tunazofanya.

Sasa naomba ushauri kweli niendelee kumuamini kama kweli hii relationship itafikia kwenye hiyo hatua ya kua mume na mke au itaishia huku tu na kupotezeana mda?

Kweli nampenda sana na najua kama nampenda na sikatai once tukiwa pamoja i feel his love na hata nikiwa sipo nae communication za hapa na pale zinakuwepo sana.

Dada dinah na wadau wengine naomben ushauri wenu kwenye hili suala."

Jawabu: Habari ni njema kabisa, karibu sana mahali hapa. Pole sana, na pia napenda kukupa hongera kwa kuwa mvumilivu, hapo ni Gf tu......wengine wala tusingefika hapo ulipo!

Nimepata matumaini baada ya kuona kuwa umefanyia uchunguzi na kugundua kuwa ni umbali ndio unaweza kusababisha mpenzi wako atoke nje ya uhusiano wako.

Lakini nimekereka na tabia ya mpenzi wako kutokuwa muaminifu, kutojiheshimu yeye na mwili wake, Kutokuwa mvumilivu mbaya zaidi ni kukosa adabu na heshima kwako na kuigawa nambari ya simu yako kwa mtu anae-cheat nae na kuruhusu mtu huyo kukudhihaki na kukutukana ili akukatishe tamaa umuachie mpenzi wako awe wake moja kwa moja.....wanawake wengine wanastahili kuuwawa taratibu kwa mateso makuu akyanani!

Nilichokigundua kutokana na maelezo yako ni kuwa Mpenzi wako anajua na anauhakika kabisa kuwa unampenda, tena sio unampenda tu bali unampenda kwa dhati.

Penzi lako la kweli na dhati kwake linamfanya aamini kuwa hata akifanya kosa gani hutom-buti kwa vile unampenda sana na kwa dhati, anajua na anauhakika kabisa lolote atakalofanya na kisha kuja jieleza utamsamehe na kuendelea na maisha kama kawaida.

Sasa mpendwa baada ya kudhani kuwa umbali ndio sababu ulipaswa kupunguza umbali huo ili kuangalia kama kweli ndio sababu ya yeye kuchoropoka/kutokuwa muaminifu, kwa vile kisheria hamjafnga ndoa ilikuwa rahisi kwa mpenzi wako kukufuata wewe huko uliko (Kuomba uhamisho) au wewe kuhamia huko aliko nakuishi pamoja au karibu zaidi.

Kwa vile hilo halijafanyika mapaka tunavyoongea hivi sasa basi hujachelewa linaweza kufanyika wakati wowote kuanzia leo(kama unapenda na yeye anakupenda) ili kuona kama kweli uhusiano wenu unamaisha marefu au la!

Kitu muhimu cha kuzingatia kabla hujachukua uamiuzi wa kuhama kumfuata au yeye kukufuata jaribu kuwakilisha hoja hiyo kwake uone atalichukuliaje, akija juu au kukupa jibu lisiloridhisha ujue hakufai huyo tena toka "nduki" usiangalie nyuma.

Akikubaliana na wewe basi endelea kuangalia mwenendo wake, akiendelea na tabia yake chafu wakati mko karibu kama sio kuishi pamoja kwa
mara nyingine nakwambia toka "baruti" na uangalie maisha yako na hakika utakutana na mpenzi atakae kuthamini, heshimu na kukupenda kwa dhati.

Natambua itakuuma sana tena sana, itachukua muda mrefu kuanza maisha yako ya kimapenzi au hata kuoenda tena lakini siku moja yataisha na utakuwa "fresh", mwenye kujiamini, mwenye kupendeza, mwenye kuvutia.....kama hili litatokea na unahitaji ushauri basi njoo tena mahali hapa tutakuwa na wewe kila hatua ya maisha yako ya kimapenzi.......au sio wadau?

Kila la kheri!

Wednesday, 3 September 2008

Nifuate Moyo wangu au Imani ya Dini?-Ushauri

"Dear Dinah Naomba ushauri wako na wadau wenzangu wa blog yetu hii Mimi ni binti mwenye umri wa miaka 25 sasa niko Australia, ila ninatokea Mombasa na nimekulia Arusha.

Katika kipindi cha nyuma nilikuwa na mahusiano ya kimapenzi na watu tofauti kila nikipata mpenzi hanifai either hatuko sawa kidini au kifikra .Kwa kuwa nilikuwa disappointed na mimi mwenyewe na mahusiano yangu nikaamua kutafuta mvulana mwenyewe bila kutafutwa .

Nikafanikiwa kumpata kijana ambaye tumekua pamoja tunajuana vizuri tu (tumuite JP) .Mahusiano yetu yalikuwa ya kirafiki , baada ya muda akaniambia anahisi ananipenda tukawa na mahusiano ya mapenzi kwa mwaka mmoja. LAKINI mahusiano yetu kipindi chote yalikuwa kwa simu.

Kwa sababu mimi niko huku nje na yeye yuko Arusha. Tumewasiliana kwa kipindi kirefu tukafikia hatua ya kukubaliana kama Mungu akipenda tunaweza tufunge ndoa. Hivi karibuni mwezi mmoja umepita alikuja kunitembelea rafiki yangu wa kiume (rafiki wa kawaida tu) kutoka nchi jirani(tumuite LUCKY).


Tumekaa pamoja kwa muda wa siku kumi kipindi chote tulichokaa tulizoeana sana kupita mazoea ya mwanzo hisia za mapenzi zikajitengeneza ndani yetu na tukagundua tunapendana sana tu .


Tatizo linakuja nimempenda huyu rafiki yangu LUCKY sana ila yeye tunatofautiana kimila kitamaduni na kidini japokuwa kifikra tuko sawa sana na tunaendana kwa mambo mengi. Wakati JP tuna Dini moja japokuwa tamaduni tofauti na yeye hajachacha sana kielimu na kifikra yuko sawa vya kutosha japo kuna tofauti kidogo ambazo hazistui sana .

Ukweli ni kwamba JP naye nilihisi kumpenda, ila kwa sababu siajonana naye kwa muda mrefu mapenzi si strong sana na pia mapenzi yetu yalianza kufifia haswa kipindi LUCKY alipokuja huku kwangu.

Hivi karibuni nikaamua kuchukua uamuzi wa kumuacha JP kwasababu nilihisi ntampotezea muda. Kwasasa nahisi kama nilifanya uamuzi usio wa busara. Kwa sababu Wazazi wangu hawata kubali nioane na mtu wa dini tofauti na mimi mwenyewe roho inanisuta nahisi kama nitaikosea Imani yangu.

Ninashindwa kuelewa je nampenda LUCKY kweli au ilikuwa mapenzi ya muda. Je ni kweli simpendi JP au ni kwa sababu yalikwa mapenzi ya mbali na pia sababu hatujaonana kwa muda mrefu??

Au nimuache pia LUCKY nisubirie nyota yangu inimulikie mtu mpya? Yaani sina raha wala amani kwa sasa. Nakaribia kurudi nyumbani Rafiki zangu wote wanaolewa na najua swali litakalo fuata kwangu ni nitaolewa lini.

Kujieleza nampenda mtu Dini tofauti sitaweza. Sijui nifanye nini? Naomba ushauri je nibaki na LUCKY kwasababu nampenda niachane na Imani za kidini nifuate moyo.

Au nikapendane na JP kwa sababu ninamjua vizuri na ni Dini moja kuhusu mapenzi tutazoeana huko huko baaada ya ndoa? Au nisubiri labda nitapata bahati nyingine??

Ni mimi R"

Jawabu:Asante R kwa ushirikiano, kutokana na maelezo yako inaonyesha wazi kuwa kuna vitu 3 muhimu sana kwenye uhusiano wako wa kimapenzi, Mosi ni Imani yako ya Dini, Pili Uwezo wa kiakili wa mhusika na Tatu ni Tamaduni.

Nasikitika kusema kuwa yote hayo hayahusiani kabisa na mapenzi, unapompenda mtu huangalii wala kujali ananini? aina ya maisha yake, Dini, Umri,muonekano n.k.

Penzi linajitokeza popote, kwa yeyote na wakati wowote, huwezi kupanga kumpenda mtu hata siku moja jampokuwa kama wanadamu huwa tunapenda kujiwekea viwango fulani vya aina ya wanaume/wanawake tunaotaka kuwa nao kama wapenzi lakini ukweli ni kuwa sio lazima utakuja mpenda mwenye "viwango" vyote utakavyo ama atakuwa na tatu kati ya kumi au ukiwa na bahati basi itakuwa tano kati ya kumi.

Kutokana na umri wako bado unakua kiakili hivyo ni mapema sana kusema kuwa umekuwa "disappointed", katika kipindi ulichonancho wanawake wengi ndio wanaanza kuijua miili yao na pia kuharakisha maisha wakitaka kuwa wamefunga ndoa by the time wanaumri wa miaka 30 hali inayosababisha wengi kuhisi hawana "bahati" kwa kuacha au kuachwa kwa vile wanaharakisha mambo ambayo wapenzi hawako tayari kuyafanya (wanataka ku-enjoy life kwanza) hali inayosababisha kutokuwa na amani ndani ya uhusiano.

Nilichokigundua hapa ni kuwa upweke ulichangia kwako kutokuwa na msimamo juu ya penzi la PJ na wewe na ni sababu kuu ya wewe kujihusisha kimapenzi na rafiki yako Lucky.

Kwa kawaida mwanamke anapofanya mapenzi huwa anahisi kujiamini "sexually" na kupendwa, hapo ndio tatizo lilipojitokeza na kukufanya um-buti PJ lakini ukweli unaujua moyoni mwako unajua wazi kabisa kuwa unampenda PJ(maelezo yako yananieleza hivyo).

Ili kufupisha hadithi (usije hisi "nakudongoa" bure hehehehe), Kwa vile PJ ana vitu muhimu unavyovitaka mwanaume awe navyo Imani, Tamaduni na Uwezo wa kiakili ukiachilia mbali kuwa anakupenda (kajtolea kaka wa watu kukupa moyo wake japo ukombali na kukusubiri ni wazi kuwa mabegi kayashusha juu yako).

Mimi nakushauri urudi kwa PJ na kumuomba msamaha na kueleza kitu gani kilikufanya umtose (usiseme ulikuwa na Lucky kwani utamuumiza), Sio rahisi kumpata mtu ambae ana "viwango" 3 muhimu kati ya vitano utakavyo kutoka kwa mwanaume......PJ anavyo.

Unaweza kutumia sehemu ya maelezo yangu haya "Akili yangu ilikuwa haijatulia na nilikuwa sijui nataka nini, nilipagawa na nidhani kuwa nahitaji muda kidogo kujua nataka nini na ili kufanikisha hilo sikutaka kukupotezea muda kwa sababu sikujua nitaamua nini na ndio maana nikampa nafasi (kibuti) ili uwe huru incase ungeamua kupenda mwanadada mwingine badala yangu."

Tuombe Mungu PJ hajaamua kuendelea na maisha yake na alikuwa anakusubiri urudi (wanaume wakipenda kweli huwa wanasubiri urudi).

Nenda taratibu na maisha, hata siku moja usiharakishe na pia unapoamua kufunga ndoa fanya hivyo kwa kujua kuwa uko tayari na pia una mapenzi ya kweli kwa mwenza wako kwani ndoa ni milele.

Ndoa ni Muhimu na ni sehemu ya pili ya maisha yetu baada ya kuzaliwa lakini usilazimishe ndoa kwa vile tu rafiki zako wamefunga ndoa au kulazimishwa/songwa na familia ufunge ndoa haraka kabla hawajaondoka Duniani n.k.

Furahia kila siku kama inavyokujia na umshukuru Mungu kwa kukuwezesha angalau kuiona siku mpya kuliko kujaribu kufanya mambo haraka kuridhisha jamii na marafiki.

Kila la kheri!