Friday, 28 November 2008

Niache Mpenzi kwa ajili ya Ndugu?-Ushauri.


"Dada Dinah,ningeomba ushauri wako.
Nimekua na mpenzi wangu kwa zaidi ya miaka miwili ingawa alikua anaishi kwao lakini alikua akija kwangu na hata kushinda au kulala siku zingine. Sasa hivi majuzi mdogo wangu wa kiume alihamia kwangu baada ya chuo chao kufungwa ghafla na hivyo tukawa tukiishi nae.


Tatizo likaanzia hapo, siku moja nikarudi nakumpa mdogo wangu hela akanunue vitu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, mpenzi wangu huyu akaanza kulalamika sana mpaka sasa bado hatujapata mwafaka.


Zaidi anadai kua kuwa atasitisha kuja kwangu kwani inaonekana amekua akikwaza ndugu zangu na pia anadai kua huyu mdogo wangu ham-respect na pia anaona kama yeye anamzibia uhuru wa kukaa nami kama ndugu yake.


Nilipokaa na mdogo wangu kumwuliza yeye alikana kabisa katu katu kwamba hana tatizo nae na pia anamheshimu sana kama shemeji yake. Niliporudi na kumueleza huyu mpenzi wangu akaruka akasema ni mnafiki na wala hamaanishi hivyo.


Cha ajabu nimemwambia niwakutanishe yeye na mdogo wangu amekataa akisema hawezi kukaa na kubisha na shemeji yake yeye atakachokifanya ni kutokuja kwangu. JE HAPO MIMI NIFANYEJE KWANI NIKO NJIA PANDA,nafikiria niachane nae au la kwani simwelewi anataka nini?

Jana nikawa nimempa hatima kua kama hawezi kuishi na ndugu zangu kwa upendo kama anaonipa mimi basi sioni sababu ya kuwa nae akanitumia msg kua NITAFUTE ATAKAE WEZA WAPENDA NDUGU ZANGU.Nimekua njia panda kwani kiukweli nilikua na malengo makubwa nae ila naona nashindwa. Je nifanyeje? Iteitei"

Jawabu: Pole kwa kuwekwa njia panda. Ningependa kufafanua kidogo tu hapa kabla sijaendelea. Hata siku moja Mpenzi wako hawezi kupenda ndugu zako kama anavyokupenda wewe! Husitegemee mpenzi wako kuwapenda ndugu zako, kwani halazimiki kufanya hivyo.


Yeye kukupenda wewe haina maana kuwa aipende familia yako nzima, ikitokea wanaelewana na wakampenda na yeye akawapenda kama ndugu zako (sio kama akupendavyo wewe) mshukuru Mungu, vinginevyo anapaswa kuwaheshimu (na wao wamheshimu pia) na sio kuwapenda. Kupenda ni hisia, hailazimishwi.


Ndugu wakati mwingine huwa wakorofi, baadhi huwa wanaamini kuwa unamaliza pesa kwa mwanamke na sio kwao kama ndugu zako. Wanasahau kuwa wewe sasa ni mtu mzima unastahili kuwa na maamuzi yako na kuendesha aina ya maisha utakayo au niseme kuwa na maisha yako.


Wewe umekuwa na mpenzi wako kwa muda wa miaka miwili na uhusiano wenu ni mzuri na wakaribu kiasi kwamba Binti huja kushinda na kulala kwako mara kwa mara. Katika hali halisi huyu binti alikwisha jiona yeye ndio mwanamke kwenye nyumba yako au hapo kwako, lazima alikuwa akijipa majukumu fulani kama "mwanamke" na jukumu moja wapo ni kufanya manunuzi kwa ajili ya matumizi hapo nyumbani.....huenda wewe ulikuwa hujui au hukutilia maanani kama mwanaume.


Sasa baada ya mdogo wako kuja hapo kwako, wewe ukahamisha jukumu moja la kufanya manunuzi kwa ajili ya matumizi hapo nyumbani ambalo labda kwake yeye mpenzi wako lilikuwa jukumu muhimu sana kama mwanamke wako au mwanamke ndani ya nyumba. Hakika hapo ndipo alipokwazika na kumempotezea kujiamini kwake.


Wewe kama mwanaume ulitakiwa kugundua hilo (alipokasirika) na kumrudishia jukumu hilo yeye, kwamba endelea kumpa pesa za manunuzi ya vitu yeye na sio Mgeni (mdogo wako). Huyu mpenzi wako aliposema kuwa anasitisha kuja hapo kwako kwa vile Mdogo wako hamheshimu na vilevile kuwapa uhuru ninyi kama ndugu, alitegemea wewe kuwa upande wake kama mpenzi wake.


Sio kwa kumuunga mkono na kwenda kumsakama mdogo wako bali kwa kumhakikishia kuwa unampenda na hakuna mtu atakaeingilia na kuharibu penzi lenu. Avumilie kwa sasa kwani mdogo wako yuko hapo kwa muda tu.


Kwasababu hukumuelewa (wanawake wengine husema hivi kumbe wanamaanisha vile), ndio maana amekataa kukutana na kupatanishwa, alichotaka huyu ni kuhakikishiwa nafasi yake kwako kama mpenzi na kurudishiwa jukumu ambalo labda alikuwa kalizoea kama mwanamke wako.

Uwepo wa mdogo wako hapo nyumbani inakuwa ni tishio kwake hasa kama hawakuwahi kukutana kabla, kwani baadhi ya wanawake hudhani kuwa ndugu wanaweza kuwa-feed wapenzi wao maneno ili watimuliwe.......sasa kwa vile Dogo ni mwanaume huenda hata muda mwingi unatumia nae kuliko kufanya hivyo na mpenzi wako hali inayoweza kumfanya ajishitukie....(asijiamini).


Nilichokiona hapa ni kuwa ninyi wawili mnapendana na wote hamjui mnataka nini kutoka kwenye uhusiano wenu na hivyo mnabaki kupigana mikwara, yeye hataki kuja kwako tena ili kukupa uhuru na ndugu yako.


Wewe unataka aishi na ndugu zako kwa upendo kama anaokupa wewe na akishindwa huoni sababu ya kuwa nae(sasa uko nae kwa ajili ya ndugu zako au kwa vile unampenda?)......kumbuka yeye hajatamka kuachana na wewe.....lakini kutokana na mkwara wako kakupa jibu zuri kabisa kuwa ukatafute mtu atakaependa ndugu zako kitu ambacho hakiwezekani!


Kuishi na ndugu na kuwapa upendo kama anaokupa wewe ni kitu ambacho hakiwezekani (rejea maelezo yangu ya awali), lakini kuishi nao kwa heshima ili kuboresha amani inawezekana.


Kosa-Ulishindwa kung'amua kuwa umemnyang'anya mpenzi wako jukumu ambalo lilikuwa muhimu, pia ulishindwa ku-handle the issue kama mwanaume na badala yake ukatoa lawama huku na kuzipeleka kwa Mdogo wako alafu tena kwa mpenzi wako na mbaya zaidi ukaegemea upande wa mdogo wako badala ya mpenzi wako ambae pengine angekuwa mkeo (una mipango mingi nae).


Nini cha kufanya-Mtafute Mpenzi wako, Omba msamaha kutokana na uamuzi wako(kama mwelevu na yeye pia atakuomba msamaha kwani alikosa pia kwa kusema vitu indirect) na kaeni chini mzungumzie hili suala kwa uwazi zaidi.


Kama kutakuwa na tatizo lolote au mpenzi wako anahisi kutojiamini mbele ya ndugu zako basi mhakikishie mapenzi yako juu yake, ni kiasi gani umeji-commite kwake na ungependa penzi lenu liende wapi kama ni uchumba alafu ndoa.....kama hivyo ndivyo basi ungependa yeye na ndugu zako kuheshimiana (sio kupendana).


Siku nyingine maneno maneno yakitokea usiende kuuliza upande wapili kabla hujapata ushahidi, "handle" kiutu uzima kwa kufanya uchunguzi, pata ushahidi kisha zungumza nao kwa nyakati tofauti na kuwapa onyo.


Hakuna sababu ya kumuacha Mpenzi wako kwani inaonyesha kuwa anakupenda, ila hajiamini. Kama na wewe unampenda na unamtaka basi mtafute, muelezane, msameheane, muonyeshane mapenzi na mrudiane.


Kila la kheri.

14 comments:

Anonymous said...

dada dinah natumaini wewe ni mzima, NAOMBA KUULIZA SWALI hivi wanawake wanao kwenda kwa WAGANGA WA KIENYEJI ili wanaume wao wasiwaache huwa wanafanikiwa kweli? Naomba unijibu dada dinah najua shoga yangu ambaye anataka kwenda kwa muganga kwasababu bwana yake anataka kumuacha,je hii kitu inafanya kazi?

Anonymous said...

Ndugu huyo bibiye hakufai kabisaaaaa! waswahili husema dalili ya mvua ni mawingu, au panapofuka moshi jua pana moto!!Pengine usipoziba ufa utajenga ukuta.

Unapooa ujue kuwa unaongeza ndugu katika ndugu ulionao wa mama na baba mmoja.Pia vilevile kwake anayeolewa pia anaongeza mtoto wa kiume kwa wazazi wake.Sasa wewe Bwana kama huyo mwanana wako kaanza makeke ya kutupiana madongo na mdogo wako,ya nini kukawia kumwambia hatakufaa kuwa mke.Haiwezekani kabisa useme utaoa mke ambaye mtaheshimiana ninyi tu.Hapo utakuwa umeoa kwa ajili ya kutombana tu na wala hakuna jingine.

Tafadhali usijaribu hata kuwakusanya uwapatanishe kwani utapoteza muda wako bure kwani huyo mpenziwe hajakorofishwa lolote na huyo mdogo wako.Inaelekea huyo mwanana wako ana kawivu ndani ya moyo wake, au huyo mdogo wako kamkatili kurushana nawe hapo kama alivyozoea.
haya basi the ball is in your court,keep your heart open to make a good decision on that issue.Bye

Anonymous said...

POle sana dadangu,mimi ninachodhani ni kuwa huyo mpenzi wako hakupendi mana kama anakupenda inakuwaje anawachukia ndungu zako, "shuti akipenda boga apende na maua yake pia.

Kaa ongea naye ukiona vipi tafuta ustaarabu mwingine kwa sababu inavyoonesha mdogo wako ni kweli anamuheshimu shemeji yake iweje yeye actaki eti anashindwa kuwa huru kwani ni mahari amekulipia mpaka akupangie masharti. huyo ni mtu wa kuja tu also is ur B/f and not husaband acje kukugombanisha na nduguzo then akaja kuacha njia panda.Unatakiwa kuwa mwangalifu sana na kutulia mungu atakupa mtu mwingine mtakaye ishi pamoja na kwa mapenzi zaidi.

Nancy said...

Duh! Pole sana, hicho kimeo achana nacho. Ndugu hasa wa familia yako ni muhimu sana katika maisha yako. Ukipata kilema leo mumeo anaweza kukukimbia lakini familia yako hawatakuacha. Usikubali kuwa na mtu asiyethamini ndugu zako. Huyo hana mapenzi ya kweli may be anapenda kile ulichonacho. Usihofu muombe Mungu maana mume mwema atoka kwa Mungu.

Dinah said...

Annony @1:18:00 AM, Kuwafanya wapenzi wao mazuzu ndio huwa wanafanikiwa(hakuna tofauti na muuaji eti?).

Nilikwisha jibu swali kama hilo na nilitoa maelezo ya kutosha.

Jaribu kutafuta/google "dinahicous Limbwata" tafadhali.

Asante kwa suhirikiano.

Anonymous said...

ndugu yangu yani bila kuchelewa mwache haraka huyo mwanamke hakufai hatakidogo yani mwanamke kama huyo haoni hatari hata kukuua au kukutenganisha na na ndugu zako dizaini hizo za wanawake ndio wanaowekea limbwata waume zao au sumu

Anonymous said...

Ndugu zako wana umuhimu mkubwa sana katika maisha yako, na unatakiwa usivunje udugu labda kuwe na sababu za wao kukutia katika majanga.
Unapooa mke, (sizungumzii `mpenzi tu kama huyo) kama anajua nini maana ya ndoa, atawaheshimu ndugu zako, kwani wao na wewe mumetokea katika shina moja.
Mtihani mkubwa kama utamleta mke awe anawachukia ndugu zako, bila sababu ya msingi. Ukimchunguza sana mke wa namna hiyo, utagundua kuwa hata wewe anakupendea kwa kitu fulani, sio kwa mapenzi ya kweli. Kwahiyo kuwepo kwa wanandugu ni kikwazo katika kutimiza malengo yako.
Wewe umegundua hilo mapema, na pia amekupa hitimisho kuwa umtafute ambaye atawapenda ndugu zako, na baya zaidi hataki kusuluhishwa. Hii inaonyesha ana udhaifu fulani, kama kweli ndugu yako sio mtomvu wa adabu.
Fanya utafiti wa kina kwanza, kuhusu huko kutokuelewana na ndugu yako, isije ikawa ndugu yako ni mkorofi.
Pili jaribu kumuelimisha mpenzio tena na tena, akikataa,basi mshukuru Mungu, huenda ikawa heri kwako.
Hayo ndiyo yangu
emu-three

Anonymous said...

Ndugu yangu Pole sana! huyo mwanamke hakufai kabisa, inakuwaje huu ni uhusiano tu wa kawaida ameshaanza mambo kama hayo? halafu anakwambia tafuta mwingine wa kukupendea ndugu zako, hiyo ni straight forward, she is just care about you, nobody else! Kazi kwako kufanya maamuzi na kuona uzito uko wapi kwa ndugu zako au mpenzio

Anonymous said...

wewe dina me nadhani ni miongoni mwa wanawake wenye roho mbaya na choyo utamshauri vipi ushauri kama ulioutoa eti mpenzi hana wajibu wa kuwapenda ndugu zako kumbe mpuuzi hivyo!!hujui ukishakua na mpenzi naye nipart ya familia?coz hata watoto wako watakuja kujengeka na misingi utakayokua nayo wewe!!ujue ukiwachukia ndugu wa mpenzi wako hata watoto nao watajengeka chuki!!kwa damu zao halisi ambao ni baba zao wadogo n.k
utajenga vipi familia yenye umoja na mapenzi usipopendana na ndugu?

Dinah said...

Anony @3:04:00 PM, Kupenda sio wajibu na upendo ni hisia hailazimishwi.

Mimi ninapojibu mtu swali najibu kwa kuangalia pande zote mbili na sio kuegemea upande mmoja.

Kama umesoma vema utagundua kuna mahali nimesema....ikitokea ndugu wanampenda na yeye akawapenda basi inakuwa bonus, vinginevyo halazimiki kuwapenda wala wao kumpenda bali kumheshimu kwa maana ya kuheshimiana.

Ile kasumba ambao na wewe unaifuata ya "ukipenda mume/mke penda na familia yake" ni potofu na huenda ikakufanya uteseke kama itatokea hiyo familia ya mkeo/mumeo haikupenda uolewe na mtoto wao.

Utaishia kujipendekeza and all that crap wakati wenzako hawana habari au mpango na wewe.

Unachokiona miongoni mwa famili mbili tofauti zilizokutanishwa na watu wawili wanaopendana sio mapenzi bali ni maelewano kwa vile hakuna jinsi kwani tayari ni jamaa moja baada ya kuunganishwa na watu wawili ambao wanapendana kwa dhati.

Jamii hizi mbili zinajengeana heshima na maelewano ili kuepusha matatizo na mifarakano.

Kumbuka kwenye jamii kubwa watu wanatofautiana, kuna wanaopenda na kupendwa na famili za ukweli wengine haiwi hivyo.

Sasa mimi siwezi kujibu kwa kuegemea upande mmoja tu.

Nimekuwa nikifanya hii kazi kwa miaka 5 sasa, ninauzoefu na uhakika na ninachokifanya au kusema.

Next time, b4 u put ur Comment ya kunikosoa unapaswa kuelewa nilichokisema, kufikiria suala husika kwa mapana na marefu....fikiri jambo nje ya jamii yako na remeber not to put urself in it.

Asante kwa ushirikiano.

Anonymous said...

KWELI HAPA DINA UMECHEMSHA!HATA MIMI NAUNGANA NA MCHANGIA MADA HAPO JUU
LAZIMA DINAH UJUE MAPENZI YA KUTOMBANA TU NA KUACHANA HAYA HAYACOUNT MAPENZI YA NDUGU KWENU BUT KAMA MNAITAJI KUWA WANANDOA NDUGU WANACOUNT SANA KUJENGA FAMILIA ILIYOBORA AMANI UPENDO NA HATA KUKUZA PENZI LENU
INGAWA KAMA NDUGU NI WAKOROFI HAINA HAJA YA KUWASIKILIZA BUT KWA NILIVYOSOMA HUYO MWANAMKE ANAMATATIZO EITHER ANMZUGA HUYO JAMAA AU ANAROHO DHAIFU,NANDIOMAANA HATAKI KUPATA SURUHISHO NA HUYO NDUGU WA JAMAA,PIA KWANINI HATAKI KESI ISIKILIZWE?WKT NDUGU WA HUYO JAMAA YUPO TAYARI WAKUTANISHWE
KWA JINSI NILIVYOELEWA MADA HII DINAH HAPO UMECHEMSHA,MWANAMKE AMBAYE HATAKI NDUGU HUYO SIO MWANAMKE NA NDIO MAANA MAKABILA YA PWANI MWANAMKE ANATAKIWA KITU CHA KWANZA APENDE NDUGU NDIO NGUZO YA YEYE KUPENDANA NA JAMII,NDOA AMBAYO HAINA UPENDO NA NDUGU NAMAANISHA KAMA SIO WAKOOFI HUTAKI WAJE KWAKO ETI KISA WATAPATA MATUMIZI KWANGU NI AIBU KUBWA PIA UTAWAFUNDISHA NINI WATOTO WAKO KAMA MCHANGIA WA MADA HAPO JUU ALIVYOCHANGIA

Anonymous said...

Huwezi kuwapenda ndugu kama hawakupendi alafu jamaa anataka ndugu zake wapendwe kama yeye anavyopendwa inamaana awape na ngono pia.Kuna mindugu mingine ikijua unatoka na kaka yao basi inakuwa tabu visa na vituko kila kukicha.Familia bora haijengwi na ndugu inajengwa na wazazi wawili wanaopendana kwisha habari yake hao ndugu wanamaisha yao wayaangalie kivyao na wapendwe hukohuko na wake zao.

JayJay said...

Wachangiaji wa hapa mnaniacha hoi kumbe ndio maana wanaume na wanawake wengi hutoka nje ya ndoa zao kwa vile watu mnapoteza muda kufurahisha ndugu na kusahau wake au waume zenu.

Unapokutana na mtu na kumpenda unawaona ndugu zake? Of course ndugu wanakuja kutambulishwa hapo baade ili kupata baraka zao na sio ili waingilie uhusiano wenu. Kama hamja-click na ndugu zake au yeye haja-click na ndugu zangu haina maana penzi letu jali-click pia.
Ndugu bwana wanaheshimiwa tu lakini sio wakati wote unajikuta unawapenda au wao kukupenda wewe.

Ndio ni ndugu zako wa damu wao na wewe pendaneni na mimi na ndugu zangu tutapendana lakini wote kama familia moja tunaheshimiana na kuelewana, hatupendani, msichanganye mambo hapa.Nimependa mtoto wao na sio ukoo mzima na yeye kanipenda mimi na sio ukoo wangu mzima.
Tanzania fumbueni macho, acheni mila na desturi za kijinga ambazo zinaweza kusababisha kuoa na kuolewa tusipopendwa.
Dinah big up kwa majibu yako mazuri.

Anonymous said...

Wanaume tunatabia ya ajabu sana, yaani kumlazimisha mtu kupenda ndugu zako ndio sababu ya kumuoa? Ingekuwa mwanamke ndio ndugu yake kafanya hivyo wala kusingekuwa na mkutano na asingethubutu kukuambia kama hupendi ndugu yangu basi siwezi kuwa na wewe, atajitahidi kuwaweka ndugu zake mbali na kuhakikisha penzi lenu linakuwa vizuri.

Mimi nilipokuwa na mpenzi wangu (sasa ni mke wangu) wazazi na ndugu zake hawakunipenda infact hawanipendi mpaka kesho lakini binti yule ambae ni mkeo wangu sasa alisimama upande wangu na hatimae tukafunga ndoa, siku yakufunga ndoa nduguzake wengi walisusa na hawakuonekana japokuwa walialikwa lakini haikumfanya mke wangu kuniacha kwa ajili ya ndugu zake.

Kuna watu ambao wakikutana wanajikuta kupendana lakini wengine wakikutana inakuw angumu kupendana sasa kwa vile hawalazimishwi kukupenda basikubali tu lakini waheshimu na muache mwenyenye ndugu aendeleze upendo kwani ni ndugu zake na wewe ambae hupendwi heshimu hilo.

Kama alivyosema mchangiaji hapo juu kuwa kila mtu anamaisha yake kivyake hivyo maisha ya watu wengine tuyaheshimu.

Wanaume tuache ujinga wa kunipenda penda na nduguzangu, ndugu wengine hawapendeki na mtu huwezi kupoteza muda kujipendekeza.
Asanteni.