Sunday, 26 October 2008

Familia haimtaki, kasaliti penzi letu-Jawabu

Asante M3 kwa kuleta mkasa huu hapa ili watu wachangie na vilevile kujifunza. Naomba ufikishe pole zangu kwa mhusika.

Huu bwana alipatwa na mshituko siku ya tukio na bado yuko kwenye mshituko ambao unaweza kuendelea kuwepo kwa muda mrefu zaidi kama ataendelea kunywa pombe kuzima/funika maumivu badala ya kukabiliana nayo ili kumaliza maumivu ya hisia zake.

Wanadamu tunatofautiana sana linapokuja suala la maamuzi hasa baada ya kushuhudia mtu “kakunja” mkeo , huyu bwana alimuamini mke wake kwa asilimia zote hasa ukizingatia milima na mabonde waliyopitia mpaka kufunga ndoa.
Kinachonisikitisha ni kuwa mke wake hajaomba msamaha, huenda na yeye bado haamini kuwa amebambwa “live” au hapati nafasi ya kufanya hivyo kwa vile wakati wote jamaa kalewa(mpatie anuani yangu ya barua pepe nijaribu kumuweka sawa).


Akumbuke tu kuwa mtu anapoamua kusaliti penzi mara. zote huwa anasaliti penzi na mmoja kati ya watu ambao wako karibu sana na yeye iwe ni rafiki wa mke/mume, jirani, mfanyakazi mwenzie, msaidizi wa kazi nyumbani n.k (kama umepitia moja ya makala zangu kuhusu kuteleza utanielewa). Hivyo suala la kusikitika kwa kusema “rafiki yangu mpenzi aliyenipa mtaji” aliondoe tena huyo ndio mbaya zaidi!


Ninachokiona hapa kutokana na maelezo yake ni kwamba, wewe(mume) huenda ulikuwa ukifanya kazi sana ili uweze kumtimizia mke wako mahitaji yake ili asije akashawishika na watu wenye mapesa(ukizingatia kuwa ametoka kwenye familia fulani).

Inawezekana kabisa kuwa ulikuwa umejisahau na kuweka nguvu zako zote na muda wako wote kwenye kutafuta pesa ukidhani kuwa kukidhi mahitaji ya mkeo kwa kuwa na Senti ndio kuonyesha mapenzi kusahau kuwa wanawake wengine mapenzi ya mwili ni muhimu zaidi kuliko pesa......ikiwa alikupenda na umasikini wako ni wazi kuwa pesa isingekuwa kishawishi kwa mkeo huyo.


Kitu muhimu unachopaswa kukifanya hivi sasa ni kutengana na mkeo kwa muda (kukaa mbali nae), kisha acha kunywa pombe (ulevi)hatua hii ya mwanzo itakusaidia kukabiliana na maumivu yako na wakati huohuo kujua hisia zako zimesimama wapi katika hali halisi.


Hatua ya pili ni kuzungumzia tukio hilo kwa uwazi kwa watu wa karibu na wewe ambao unajua kwa uhakika kuwa watakusikiliza, kukuelewa na kukusaidia kwa kukupa matumaini na ushauri mzuri utakaokufanya ajue hisia zako zilipo juu ya mke wako na nini unadhani kinaweza kuwa kumesababisha mkewe kutoka nje ya ndoa yenu.


Epuka watu wanaotoa ushauri wa haraka kama vile kumuita mkeo majina machafu, kukuambia umuache na ushauri mwingine ambao wewe unajua hautokusaidia.


Hatua ya tatu ni kukutana na wataalamu waliobobea kwenye masuala ya Ndoa na mahusiano ya kimapenzi ana kwa ana ili uweze kupata msaada mzuri zaidi utakaokusaidia kufanya maamuzi ya busara.

Mtaalamu yeyote wa masuala haya kitu cha kwanza kukuuliza kitakuwa je unampenda mkeo? Pili utaulizwa...kitu gani unadhani /hisi kinaweza kuwa ni sababu ya mkeo kutoka nje ya ndoa?


Ikiwa utahisi kuwa bado anampenda mkeo na kupata jibu nini hasa kinaweza kuwa sababu ya mkeo kuchomoka nje basi mtaalamu huyo atapaswa kuandaa siku ili wewe na mkeo mkutane na mpewe darasa kama “pea” na hapo kila moja wenu ataulizwa maswali kadhaa ili kuwasaidia nyote wawili kutambua hisia zenu kimapenzi. Baada ya hapo mtapewa muda ili muweze kuzungumza, yaani kuwasiliana sio kuzozana na kubishana.

Inawezekana kabisa baada ya hapo ukawa hayuko tayari kurudisha uhusiano kwa wakati huo, hiyo ni ruksa kabisa kwani itakuchukua muda kusamehe na kusahau . Lakini kuzungumzia hisia zenu mbele ya mtu ambae anaelewa masuala haya itawasaidia sana.


Hatua ya nne ni wewe na mkeo kuwasiliana, kuzungumza kwa uwazi kabisa kwa kutumia maswali yangu yafuatayo:-

1)-Uhusiano wenu tangu mmefunga ndoa mpaka ulipomfumania ulikuwaje? Kuna kitu chochote kipepungua/badilika?

2)-Kitu gani kiliwafanya mpendane na muamue kufunga ndoa? Je bado hicho kitu mnacho?

3)-Mnataka nini kutoka kwenye uhusiano wenu na je wewe unataka nini kutoka kwa mpenzi wako?

4)-Unahisi nini kila unapomfikiria au kumuona mpenzi wako hivi sasa?

5)-Unamchango gani au unanafasi gani kwenye uhusiano wenu?

6)-Vitu gani huwa mnafanya pamoja kama wapenzi?

7)-Mara ngapi mnafanya mapenzi kwa wiki na je mnatosheka?

8)-Je unadhani mpenzi wako anahitaji ku-improve? Nini hasa kiwe “improved”?

9)-Ikiwa unapewa nasafi ya kumuwekea mwenza wako mipaka ni mipaka gani utamuwekea?

10)-Ni wazi kuwa hamuaminiani kwa asilimia zote kutokana na tukio, je unadhani utaweza kumuamini tena mwenza wako ?

Haya maswali huwa nayatumia ninapofanya 1-2-1 na pea yenye matatizo ili kurudisha uhusiano wao ulipokuwa na kuwapa mbinu nyingine(kutokana na majibu yao) ili kuboresha uhusiano wao na kuzuia makosa kutokea tena......D'hicious inaamini ktk kuboresha mahusiano na sio kuvunja.

Kila la kheri.

2 comments:

Anonymous said...

Nawashukuru sana wachangiaji na hasa huyu mchangiaji ambaye dada Dinah,ameonelea amweke wazi. Nitakuwa tayari kumtambulisha kwake,kama wenyewe watakubali,kwani shauri zima bado ni la siri.
Lakini itakuwa sio jambo jema kama nitakaa kimya bila kuwajulisha ni nini kimeendelea baada ya tukio hilo zima.
Yule mwanamke kashindwa kuvumilia na aliamua kutafuta ushauri, na cha ajabu alikuja kumuona mke wangu. Mke wangu wangu alimshauri wakutanishwe na mumuwe na kifanyike kikao cha `usuluhishi' lakini kikwazo ikawa jinsi gani atakavyomuingia mume wake. Pia ukumbuke shemeji yangu huyu hana mahusiano mema na kwao kutokana na historia nzima ya mahusiano yao.
Yeye(shemeji) anadai hakutenda tendo hilo kwa hiari yake mwenyewe,anahisi kuna nguvu za giza,kwaani anampendasaanamume wake, na ikitokea vinginevyo anahisi ni bora `afa tu'.
Anadai siku ya tukio, jamaa alikuja nyumbani kama kusalimia tu na kwa vile anamjua kama rafiki mkubwa wa mume wake hakuwa na shaka. Alipompa mkono tu, akajisikia mwili mzima ukilegea,na akajikuta akifanya kila alichoambiwa na huyo jamaa,na matokeo yake alijikuta yupo chumbani mwake na kutokea yaliyotokea.
Mimi niliiona kama ni hadithi ya kujitetea tu, ingawaje mke wangu anasema wapo watu wanaotumia njia za giza kuwapumbaza watu hata kuwaibia na haitakuwa ajabu watu kufanya mambo kama hayo.
Swali langu ni hili, je kuna ukweli wa mazingaumbwe ya namana hii? Na kama ni kweli tufanyeje kuwasaidia hawa jamaa,na kama ni uongo tutahakikishaje ili kugundua udhaifu wa uongo huu.
emu-three

Anonymous said...

M3 na wengineo! Kulogwa ama kutologwa ukweli umebaki hapo hapo; PENZI LIMESALITIWA!

Mimi ni mwanaume na nitakachokisemahapa najua kitawashangaza wengi lakini ni ukweli!

Hii mimi imenitokea yaani nimewahi kusaliti penzi na nimewahi kusalitiwa! napenda kuwaambia kuwa nimejifunza kitu kikubwa baada ya kusalitiwa! naam ! Samtaimz tunahitaji sindano ili tupone! Sasa cha muhimu hapo ilikuwa kama alivyosema Dinna ni kujiangalia sote wawili! Na beleieve me kusalitiana ni moja ya milima na mbonde yaliyomo katika uhusiano! Sisi wote tulitafakari kwa kina na ni baada ya mwenzangu kuniomba msamaha kwa kunisaliti; lakini chanzo ni mimi kumsaliti yeye; mimi kujisahau na kuweka pembeni na kisha baada ya kulijua hilo nilitoa msamaha kwa moyo mmoja! Tulichukua hatua ya kujifunza upya na kukumbusha juu ya mapenzi yetu na kikubwa zaidi sote tuling'amua kuwa tulikuwa wajinga kwa kudhani tukijiiba tutakuwa tunapata suluhisho! Tuling'mua kuwa tulicho nacho ni kikubwa zaidi ya vitu vingine vyote na zaidi ya yote tulijua kuwa katu watu wa nje hawaezi kutusaidia kutauta mataizo yetu wenyewe; hivyo tulichukua jukumu la kuanza kujenga upya palipobomoka; kukumbusha juu ya ahadi zetu na zaidi ya yote kuthaminiana kwa ahali ya juu! Namshukuru mungu nisemapo haya tumeoana na tuna mtoto mmoja! Na bado tunapendana! Ubarikiwe Dada Dina; safari ijayo nitachangia kutokana namafundisho ya imani yangu ya kikristo