Monday, 25 August 2008

M3 kwenye faida/hasara/umuhimu wa Ndoa!

Nilibahatika kupitia mitandao mbalimbali ili kuona maelezo mbalimbali yahusuyo mada hii. Mengi niliyoyakuta ni yaleyale ninayoyafahamu ambayo hata hivyo yameniacha nikiwa na maswali mengi badala ya majibu.

Najua dada Dinah, hata wewe umeliona hilo na kwa uzoefu wako wa kusaidia watu katika nyanja nzima ya maisha na kuridhishana kimaumbile unaweza ukatoa jibu lenye kutosheleza.

Labda nikokotoe maelezo kidogo kwanini nimeuliza hili ili kila mchangiaji aone nini umuhimu wa kufundishana na kuelezana dhana nzima ya neno ndoa, na kwanini kabla ya ndoa kuna vipengele anuai kama `uchumba’ na baada ya ndoa kuna vitu kama `fungate’ na baada ya fungate kuna nini tena?

Wengine hukimbilia `talaka’ au `misukosuko ya ndoa’ ambayo huenda imesababishwa na kutokuelewa zana nzima ya ndoa, na kwanini hii ndoa ikawepo! Wengine wamediriki kusema haina haja ya ndoa, eti kila mtu akijisikia amtafute amtakaye amalize shida zake, lakini hatimaye uzee unapotinga anajuta na anakiri kweli kuna umuhimu wa kumtafuta mwenza, ni kwanini?


Kutokana na hili nikaona kuna haja ya kutafiti kwa undani kwanini kukawa na ndoa. Hii ndoa kwanini iwe na vipengele fulani, vinasaidia nini. Na kawanini ndoa ambayo kiujuujuu tunaiona kuwa ni `raha’ ni `uhalalisho’ wa kutenda yale yaliyokatazwa, ni `kusaidiana’ kwani unaunganisha `jamii’ mbili.


Lakini kwa wengine imekuwa ni kinyume na matarajio, na wengine huishia kusema kuwa `ndoa ni ndoana’ kwani ikikunasa hunasuki. Na wachache waliofanikiwa wamekaa kimya hawataki kuwanasua walinasa kwenye ndoana hii.Tumepata maelezo mengi ya `ngono na kungonoana’ lakini hapa bado tunahitaji maelezo yanaisaidia `ngono!’


Kwani tuelewe kuwa sisi ni binadamu na tuna taratibu zilizokubalika na kututofautisha na viumbe wengine, kuwa tendo hili ni la baraka, na baraka hii haiji kama wanavyofanya wanyama.


Baraka hizi huja kwa taratibu maalumu, nayo ndiyo mchakato mzima wa kuiendea ndoa. Na hata wale waliochepuka na kuishi bila `ndoa’ hujiona hawana baraka hizi, hatimaye huamua na kusema `tunaibariki ndoa’ na ajabu kabisa, wakiamua kuibariki ndoa yao wanaumua kwenda `fungate’!.


Sasa ni kwanini ndoa, na kwanini hawa waliamua kuibariki ndoa yao bado wanakimbilia kufanya fungate na ili hali walishapimana vya kutosha?Hili linahitaji uwanja mpana wa maelezo.

Ninaomba dada Dinah, ulikuze na uliwekee vipengele ili tujifunze, sio sisi tu tulio ndani ya ndoa lakini hasa vijana wetu wanajiandaa kuingia katika uwanja huu mpana wa `mke na mume’, ili wasije wakataabika, na kuishia kuchukiana badala ya `kupendana’ na baya zaidi tunaweza tukapunguza tatizo kubwa la gonjwa la `ukimwi’ kama kweli tutakuwa tumefuatilia kwa namna yake utaratibu huo mzima wa ndoa na kabla na baada.

Kama nimekosea tusahihishane.

Mimi emu-three

2 comments:

rosemary said...

wow !!nimefurahia blog hii

Ignorant said...

M3 nimependa sana maswali yako. Kutokana na upana wa mada yenyewe, kunaweza kujitokeza mada zingine nyingi tu. Kwa haraka haraka, naona kuna mada ya hasara na faida za ndoa, kuna suala la kujadili nini kihusike katika harusi, umuhimu au sababu za fungate, maandalizi kabla ya kuoa au kuolewa, umuhimu wa ndoa, nafasi ya utamaduni katika ndoa n.k (ni maoni yangu tu).

Kwa ninavyofahamu mimi, ndoa ni makubaliano ya watu wawili kuishi pamoja kama mume na mke. Makubaliano haya pia uhusisha ushirikiano wa kingono (sexual). Ndoa ni taasisi ambayo huhalalishwa au kusimamiwa na viongozi wa dini, serikali au hata kwa tamaduni zingine wazazi au rafiki. Madhumuni ya ndoa ni mengi na hutofautiana baina ya mtu na mtu. Baadhi ya sababu za kufunga ndoa hujumuisha matakwa ya kidini, kuzaa watoto, pesa/kujikwamua kiuchumi, kuimarisha familia, kuhalalisha mahusiano ya kingono, kutafuta uraia n.k.

Kwa upande mwingine, ndoa pia ni taasisi ya jamii, ndiyo maana tunaona vijana wanapata maswali mengi kama sio shinikizo la kuoa au kuolewa kutoka kwa ndugu, marafiki, jamaa na wazazi. Mie mwenyewe niliwahi kuelezwa kua kwa kua nimemaliza shule, kilichokua kinasubiriwa na familia ni kuona naoa. Kwa utaratibu huu, naweza sema kua unaweza jikuta unatamani au unaoa kabisa ili kuwaridhisha wazazi na marafiki, kwani bila hivyo kwao unaonekana si kamili.

Kwa mtazamo wangu, kupima faida na hasara za ndoa ni suala gumu kidogo kwani linahitaji kuangalia mafanikio katika kutimiza matarajio aliyokua nayo muhusika pindi alipokua anafanya maamuzi ya kufunga ndoa. Kuna uwezekano mkubwa kwa wahusika wa ndoa moja kua na madhumuni tofauti ingawa kila mmoja atajihahidi kuficha madhumuni yake yasijulikane kwa mwenzie. Katika ndoa kama hizi, kila mmoja atajifanya anaoa au kuolewa kwa ajili ya mapenzi. Pindi mmoja wapo anapogundua kudanganywa, ndoa hugeuka chungu na pengine kuvunjika kabisa. Katika hali kama hii, yule anaehisi kudanganywa atakua rahisi kutokuona faida za ndoa.

Kutokana na uwepo wa sababu nyingi zinazopelekea wanadamu kuamua kuoa au kuolewa, wale ambao watafanikiwa kuishi maisha ya ndoa kama walivyotarajia wana nafasi kubwa ya kuonyesha faida za ndoa. Kwa wale wataokumbana na machungu katika ndoa ni rahisi sana kuyatafsiri hayo machungu kua hasara za ndoa ingawa hii inaweza isiwe sahihi kwani si kila ndoa inaweza kua na hayo masahibu.

Suala la kufanya au kutokufanya fungate linategemea sana tamaduni za wahusika. Wengi wa wahusika huwa wanashiriki fungate kama taratibu tu na pengine kwa sababu watu wengine wanafanya hivyo. Pia ieleweke kua kuna tofauti kati ya ndoa na harusi. Leo hii tunashuhudia baadhi ya waumini wa madhehebu au dini fulani ambazo harusi zao haziruhusu pombe wakiandaa sherehe ya ziada ambazo hujumuisha pombe ili kuwaridhisha wachangiaji wanaokunywa pombe.

Dinah tupe vitu