DL kwenye Umuhimu/faida/hasara ya ndoa.


DL nafurahishwa na michango yako!


"Dear Dinah,
Naomba unipe nafasi nitoe maoni yangu machache kuhusu maudhui ya hapo juu.Siyo rahisi kutoa jibu moja kuhusu tendo la ngono kabla au bada ya Ndoa kama ni sahihi au afadhali au ni vyema au si sahihi au si vyema.


Tatizo kubwa linatokana na mambo mawili: Imani za kidini au miko ya kijamii, kwa upande mmoja, na lengo la wanaotaka kufanya kitendo hicho ni nini hasa, kwa upande wa pili.
Kwa upande wa imani za kidini –na hapa karibu dini zote, hasa Dini Samawiya (Dini za Vitabu Vitakatifu kutoka Mbinguni)- au hata miiko ya kijamii, ngono kabla ya ndoa inakatazwa –haramu- na ni mwiko kwa jamii, yaani marufuku.


Upigwaji marufuku huu unatokana na mtazamo wa kina wa dini na jamii mbali mbali kuhusu madhumuni hasa ya ndoa. Madhumuni ya ndoa, kidini na kijamii, ni kuendeleza na kutunza vizazi vya jamii (re-creation) kupitia ahadi (ndoa), mbele ya mashahidi kwamba ahadi hiyo itaheshimiwa na kutekelezwa chini ya taratibu zilizowekwa, kwa msingi wa upendo, uvumilivu na uungwana, mambo ambayo ndiyo mihimili ya Mapenzi (Love) .


Hivyo, madhumuni makubwa ni kuendeleza na kutunza kizazi; yaani matunda ya ndoa, ambayo ni watoto na familia. Raha na utanashati (recreation) na mapenzi (love), kwa maana hiyo, ni malengo ya pili, au ni matokeo ya lengo kuu la kwanza la ndoa: yaani kuendeleza vizazi.


Kwa mtazamo huo, basi, hapana mjadala kwamba ngono kabla ya ndoa, hata kama inatokana na pendo au mapenzi, haikubaliki; maana inakosa uhalali (leseni) wa jukumu la msingi la kuendeleza kizazi cha jamii (re-creation) mbele ya mashahidi. Raha na starehe (recreation) ni matokeo na natija ya madhumuni hayo halisi.


Ndoa, kwa maana hiyo, ni mapatano ya msingi ya utekelezaji wa ahadi. Kwa maana hiyo, ndoa lazima ije mwanzo kabla ya ngono na si venginevyo. Ukiacha maadili ya kidini na kijamii, na ukayaweka kando, na ukajiuliza je ni afadhali au si afadhali kufanya ngono kabla ya ndoa, basi bado hutaweza kupata jibu la haraka, hata wewe mwenyewe, kama hujajiuliza swali la msingi kabisa, kwanza.


Nalo ni hili: Nini hasa madhumuni ya ngono unayotaka kuifanya? Ni raha na starehe tu au ni raha na starehe pamoja na yanayoweza kutokana na raha hizo na starehe hizo? Ikiwa madhumuni makubwa ni raha na starehe (recreation) inayoweza kupelekea kupeyana ahadi (ndoa) kuhusu kuendeleza na kutunza kizazi basi unaweza kusema kwamba ngono kabla ya ndoa ni jambo la maana; maana inatoa mwanya mzuri wa kupima tabia, uelewano, uvumilivu na hata kiwango cha pendo au mapenzi, kwamba je upo uwezekano wa kufungamana kwa muda mrefu?


Ni pima maji; je unaweza kuyavulia maji nguo na kuyaoga au la? Lakini, na hapa napenda kusisitiza LAKINI laima nyote wawili muwe wakweli; wakweli kwenye nia yenu hiyo na si venginevyo.

Venginevyo mtakuwa, ama nyote wawili mnajidanganya, au mmoja wenu ambaye si mkweli anajidanganya na kumdanganya mwenziwe. Lakini ikiwa madhumuni halisi ni raha na starehe TU, basi ngono ndiyo tendo kuu la kutoa kiu hicho cha raha na starehe hiyo. Ila, kwa nanma ilivyo, ni jibu la muda tu. Suala la ndoa halipo wala halifikiriwi. Hapa wapo watu wa aina mbili.


Kuna wale ambao wanatafuta raha na starehe tu na si jambo jengine. Kila mmoja anatafua kukata kiu chake tu.Wengine ni wale ambao wanatafuta raha na starehe hata kwa kununua au kuuza miili: ambao jamii huwatambua kuwa ni malaya na wahuni. Miongoni mwa wahuni unaweza hata kukuta “wana ndoa”.


Makundi yote haya mawili yanayowinda raha na starehe tu yanachangia sana matatizo ya kusambaza maradhi mbali mbali, miongoni mwao wenyewe kwa wenyewe na miongoni mwa jamii zao na jamii za wengine. Wanaweza hata kuathiri familia zao wenyewe, kwa wale ambao wameshaoa au kuolewa.


Pale lengo la raha na starehe linapokumbana kiajali tu na uja-uzito, au kunogewa na fungamanisho la ngono, basi wana-ngono hao huanza kufikiria njia mojawapo ya ama kujipa majukumu ya matokeo hayo, au ya kuwatangazia wengine kwamba wawili hao ni wao-kwa-wao hawataki mshirika nao. Mojawapo wa njia za lengo hilo ni ndoa.


Nyengine ni Unyumba, au kuishi-kimada na kadhalika. Kwa vizazi vya siku hizi, u-BF-GF au wapendanao, ni mojawapo wa njia hizo. Hawa wa siku hizi, wanasaidiwa sana kufikisha malengo yao hayo na vidonge vya kuzuwiya uzazi. Ngono kwa hawa ni lengo la raha na starehe. Endapo watanogewa na kuelewana basi wanaweza kufunga ndoa.


Venginevyo, kila mmoja anafunga virago vyake na kuelekea kwengine, na kuanza upya. Hivyo, narudia kusema kwamba si rahisi kutoa jibu la mkato au jibu moja, kabla ya kujuwa madhumuni halisi ya tendo hilo la ngono. Ila naweza kusema kwamba ni afadhali sana na ni busara kubwa ndoa kuitangulia ngono na si kinyume chake.


Yaani ni bora kumtafuta wa kuishi naye kwa mapenzi kabla ya kufanya mapenzi yenyewe. Na hapo ndipo penye tofauti kati ya ngono na mapenzi. Ngono inaweza kukata kiu lakini haishibishi. Mapenzi yanakata kiu na yanashibisha. Ngono inatoa raha ya muda.


Mapenzi yanatoa raha ya muda mrefu. Ngono inapapatisha amani na utuilivu wako, na kupoteza vyako, na pengine hata vya wenziwako.Mapenzi yanadumisha amani na utulivu wako, pamoja na kutunza vyako na hata vya wenziwako.

Mwenye akili haambiwi chagua. Mwenye macho haambiwi tazama. Mwenye masikio haambiwi sikia. Kila kitu kiko wazi kama giza la usiku na anga la mchana.
Upo hapo?!!!" DL.

Comments

Anonymous said…
DL umeongea mpaka nahisi kukupenda. Asante dinah kwa kuiweka hii hapa hewani.
Anonymous said…
Nakupa heko DL, na nahisi wewe ni miongoni mwa watu wenye busara. Nasema hivi kwasababu, kama ingekuwa mada tofauti inayoongelea moja kwa moja `ngono' black and white wachangiaji wangekuwa wengi, lakini kwa vile mada hii ni ya kibusara zaidi kwa kawaida wachangiaji wanakuwa wachache. Sio kwamba nawalaumu, ila majibu ya vitu kama hivi yanahitaji umakini na busara zaidi. Au unasemaje dada Dinah?

Nakusifu DL kwa majibu yako mazuri ila mimi nasisitiza kwenye hoja ya kufanya ngono baada ya ndoa, na sivinginevyo, kwani kwa kuifanya kabla ya ndoa kwa nia ya `kupimana’ inatoa mianya ya madhara mengi. Nitadodosa machache kati ya mengi.

Kwanza inadhalilisha utu na heshima ya mwanadamu. Nasema hivyo kwasababu, mfano unapomuona mtu anatembea uchi ki kawaida mtamzomea na kumuita mwenda wazimu. Halikadhalika, watu mnapofanya mapenzi ni kawaida tunayafanya faragha, na ndio maana mkiwaona watu wanayafanya mapenzi hadharani mtawaita wendawazimu, hawana adabu na wanajidhalilisha.

Kwahiyo ndivyo ilivyo kwa mtu kumvulia mwenzake nguo kwa ajili ya starehe tu, mtu huyu anajidhalilisha, na kumdhalilisha mwenzake, kwani hataishia hapo, ataenda kwa huyu na yule, je anatofauti gani na kulifanya tendo hilo hadharani, je anatofauti gani na kutembea uchi?. Na ajabu mtu kama huyu akifanya tendo hili na watu wakamjua wanamuita `malaya’, ila yule anayefanya kwa siri lakini hajatulia kwa mtu mmoja haitwi hivyo. Hata kama huitwi hivyo inabidi/moyo unakusuta kuwa na wewe ni malaya. Lakini kama unglifanya tendo hili ndani ya ndoa ingekuwa vinginevyo, na ungetulia kwa mkeo/mumeo

Yupo bosi mmoja alitembea na wafanyakazi wake wote wa kike. Siku moja, binti mmoja akaropoka kwa kusema, `bosi, mimi ningeona raha kama kila ukiingia humu ofisini ungelivua nguo zako na utembee mbele yetu uchi. Bosi akashangaa na kusema `huna adabu wewe'
Yule binti akasema ‘kwani ina tofauti gani, kwani sisi wote hapa tumeshatembea na wewe, tunajua kila sehemu ya mwili wako, kama unavyotujua sisi. Ni vyema hata sisi ungeturuhusu tu tukatembea uchi kama wewe.’
Bosi akanyamaza kimya kwa aibu.
Ngono ikifanywa nje ya ndoa inakuwa haina heshima, inaleta magonjwa na huleta ufakiri. Hili liko wazi na mifano iko mingi, ila `ufakiri' tunajifanya hatuuoni. Je unapofanya ngono nje ya ndoa unaifanya bure? Lazima kuna gharama zitatumika, na gharama hizi hazina faida. Huenda gharama hizi zingekwepeka kama tendo hili lingefanywa ndani ya ndoa kwa ajili ya matunda ya badaye, kwani hapa wote mnakuwa na lengo moja na upend wa dhati.

Kuna mfano mmoja, kijana alishitakiwa kwa kutembea na binti wa shule. Katika kuonyeshwa kuwa tendo hilo sio zuri, yule mjumbe akamchukua dada wa yule kijana mzinzi na kuanza kumfokea mbele ya kaka yake.
`Wewe binti kwanini umefanya uzinzi na mwanangu?' Hili lilipangwa na kwahiyo yule binti alitakiwa ajibu vipi. Yule binti akasema `Yeye alinitaka/alinitongoza.
Nia kubwa ni kumuonyesha kaka mtu kuwa uzinzi kabla ya ndoa sio jambo jema.
Yule kijana aliyekuwa amewekwa pembeni kusubiri kesi yake kusikia vile alikurupuka kwa hasira na alipoulizwa unakwenda wapi akasema anataka kumfundisha adabu mtoto wa yule mjumbe kwanini ametembea na dada yake ilihali bado anasoma. Kwahiyo ngono kabla ya ndoa ni fadhaha, na chuki ndani ya familia.
Swala kubwa kwa kila mtu nikujiuliza, je upo radhi kwa dada yako aziniwe kabla ya ndoa?. Je utafurahi ukiona dada yako ana mimba kabla ya ndoa? Je unaona raha ukimuona dada yako anatembea na huyu na yule kwa ajili ya ngono tu kabla ya ndoa? Na Je wewe kama mzazi/ndugu ni furaha gani unayoipata ukishuhudia mwanao/ndugu yako anaoa, au anaolewa?
Majibu yapo wazi!
Ngoja niishie hapa ili tupate michango mingine
emu-three
BRAYAN said…
Nataka kuweka msisitizo kwamba ngono ni starehe yenye majuto kwani ukishamaliza hamu zako basi mawazo kibao,ila ndoa ni starehe ya milele na hasa ukiwa umependa na kupendwa kwa dhati.Cha msingi ni uvumilivu tuu kwani hakuna binadamu aliye mkamilifu kwa kila jambo bali wote tunamapungufu yetu.
KKMie said…
Sana tuu M3, yaani mapa nasikia furaha. Pamoja nakuwa hawachangii(wengi hawako kwenye ndoa) lakini wanasoma nakupata ujumbe sawia kabisa.

Yako (view) na yangu pia nitaiweka, najaribu kuweka kama topic za kujitegemea ili wasomaji wapate kitu cheupe.

Shukurani sana.
Anonymous said…
Dinah,
Sijui mimi utanisaidiaje dadangu. Nimekaa kimya kuhusu mada hii lakini leo nimeona niseme kitu kinachoujaza moyo wangu.
Mimi niliishi bila kungonoka na malengo yangu yalikuwa kwamba hadi niolewe. Na atakayenioa ndiye nitamvulia nguo zangu. Kwa kweli nilifanikiwa kwani niliishi miaka hadi 26 ndio nikaolewa na kuanza kuonja tendo la ndoa kwa mara ya kwanza. Cha ajabu hata mwanamme tuliyeoana naye aliniambia hajawahi kufanya ngono tangu akue. Sote tulikuwa walokole wa kweli.Tulianza tendo la ndoa kwa kujifunza na baadae tulifikia/tumefikia hatua ya kufurahia kweli ngono.
Tumeishi miaka kumi na Mungu akatujali kupata watoto watatu. Mwaka wa kumi na moja na kwa mara ya kwanza nikamfumania mme wangu akifanya mawasiliano na mwanamke mwingine. Kwa kweli iliniumiza sana kwani sikuwa na mawazo kama huyu wangu atafanya hivyo. Baada ya mvutano hadi akakiri na akaomba msamaha sana. Akaniahidi hatarudia tena maishani mwake. Lakini mimi hadi leo hivi ninapoandika nimekata tamaa kabisa. Naona kama ananidanganya tu anaendelea na kuvua vua nguo, japo yeye aliniambia alikuwa hajafikia huko ndio alikuwa anaanza kutokana na sasabu aliyojieleza (Alikuwa analalamika mimi nisisafiri kikazi, simjali). Naumia jinsi nilivyojitunza ili nipate wangu tu kumbe akawa wetu wengi.
Imefikia hatua hata nikiona mijadala hii inayohusu kujitunza mimi nimekata tamaa kabisa. Nahisi siwezi tena kumwambia mtu ajitunze hadi ndoa. Sioni tena maana. Sijui najaribiwa!?
Dina unasemaje na wengine mtakaopitia ujumbe huu? Kula raha kifo chaja!!
Nitaikosa mbingu, duh!