Sunday, 24 June 2007

Betty!

Mpendwa Betty pole kwa kutokujibu kwa wakati, hii ni kutokana na wingi wa shughuli. Kwanza kabisa napenda kukupongeza kwa uwazi ulionao wa kuzungumzia swala hili hapa, watu wengi huficha na kutoomba msaada wa kitibabu au hata ushauri tu wa kawaida kwa sababu ya uoga, kutokuelewa kama ni tatizo au aibu ya kujadili swala hili.

Kama nilivyosema kwenye maelezo yangu ya awali (wiki iliyopita) kuwa tatizo hilo huenda likawa limesababishwa na ulegevu wa misuli (pelvic floor) ambayo hufanya kibofu cha mkojo kufunga na kufunguka, ikiwa msiuli hii ikalegea basi tatito la kutokwa na mkojo ukicheka, hema kwa nguvu, kukohoa n.k. hujitokeza.

Tatizo hili linaweza kumpata mtu yeyote na sio wanawake pekee bali hata wanaume na watoto na husababishwa zaidi na unene kupita kiasi, uzee, Kuugua mara kwa mara, matatizo ya kupata choo, kuanza ngono mapema, matumizi ya madawa ya kuzuia mimba, na zaidi husababishwa na uzazi.

Ninachokushauri ni wewe kwenda kumuona Daktari wa magonjwa ya wanawake na atakusaidia ili kupunguza na kuondoa kabisa kero hiyo, huenda ikawa dawa, mazoezi vilevile anaweza kukushauri utumie bidhaa maalumu kwa ajili kuvuja mkojo bila kujitambua/kusudia.

Kila lakheri.

Wednesday, 6 June 2007

Kwenda nje ya Ndoa/Uhusiano/ukware/Umalaya

KWA maana ya haraka haraka ni mtu asiye na adabu/heshima, huruma, utu, muharibifu, mkatili, mlafi, mshamba na ni muuaji vilevile.

Tatizo hili limekithiri katika jamii yetu na sasa limekuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi ya watu au kwa maana nyingine wamefanya kuwa ni utamaduni wa kisasa (kwenda na wakati).

Tabia hii mbaya huathiri kwa kiasi kikubwa baadhi ya familia hasa ikiwa muhusika yuko ndani ya ndoa na amefanikiwa kupata Watoto.

Tabia hii haiko ndani ya ndoa pekee bali hata katika mahusiano ya kawaida ya kimapenzi tofauti ni kuwa ndani ya ndoa akina Baba ndio wako mstari wa mbele na walio nje ya ndoa baadhi hulipiziana visasi.

Wanawake walio katika ndoa hujitahidi kuwa wavumilivu wakiamini kuwa ndoa ni uvumilivu. Hapana! ndoa ni kuvumiliana (wote wawili) ikiwa mmoja wenu anamatatizo kiuchumi, kuugua, ajali n.k, lakini sio kwenye Uasherati jamani mwee!. Mimi wangu akitoka nje naua aisee!(hahahaha natania ila hatonipata tena)

Baadhi ya wanawake hushindwa kufanya uamuzi hasa ikiwa mwanaume ndiye “kitega uchumi” au wanafuata maadili mema ya mtanzani (utakufa kwa ngoma na maadili yako shaurilo). Wengine hung’ang’ania kubaki katika ndoa “for the sake of kids” na hii ni kutokana na kutokuwa na kipato kitakachomfanya amudu maisha yake na watoto ikiwa ataomba/kupewa Taraka.

Pamoja na mambo au sababu nyingine zinazopelekea tabia hii mbaya hizi zifuatazo hupelekea watu kutoka nje ya uhusiano wao wa kimapenzi/ndoa.

*Kutopata mapenzi ya kweli hasa ikiwa Kijana/Binti alilazimishwa kuoa/kuolewa na mtu ambaye hakumpenda “for the sake of Radhi ya Wazazi”, maadili, kuhofia umri n.k..

*Uchafu, kutojijali au kujipenda.-Wote mwanaumena mwanake.

*Kutoridhika au kutosheka na wakati mwingine uroho tu- Wanaume zaidi.

*Mmoja wenu kuwa na shughuli nyingi za kikazi/Biashara, kusafiri – Wote mwanamke na mwanaume..

*Tamaa ya kumiliki vitu Fulani –Wanawake zaidi.

*Kujaribu na kujifunza mambo mapya/mitindo lakini kutokana kufuata maadili unaogopa kuwa wazi kwa mpenzi wako-Wake kwa waume..

*Kukosa tendo la ndoa kwa muda mrefu ikiwa mwanamke ana Mimba kubwa /amejifungua n.k-Wanaume.

Kamanilivyowahi kusema kwenye makala moja iliyopita kwamba pamoja na mambo mengine mapenzi ni kuambizana ukweli, ikiwa mwenzi wako hakuridhishi, mchafu n.k ni vyema ukatafuta muda na ukamweleza taratibu tena kwa upendo, kumbuka hakuna Mwanadamu aliyekamilika hapa Duniani kila mmoja anakasoro zake.

Mpenzi wako (haijalishi mwanaume/mwanamke) ni kama mtoto anatakiwa kubembelezwa, kuelekezwa na ikiwezekana kufundishwa baadhi ya mambo ambayo hayajui.

Kama wewe ni mtu mzima na umepitia/unajua haya acha wenzako wanaoinukia maisha ya mapenzi wajifunze.

Asante na karibu tena.

Saturday, 2 June 2007

Utatambua vipi kama ni yeye au sio?

UHUSIANO wa kimapenzi unaimarishwa na mambo mengi kutegemeana na wahusika wenyewe lakini haya matano (5) ambayo ni kusikilizana, kuaminiana, kuheshimiana, kusaidiana, kushirikiana ni muhimu na yakifuatwa vyema na pande zote mbili basi uhusiano wenu utakuwa mzuri na wenye afya.

Mara zote tunapoanzisha uhusiano huwa hatuko wazi kwa asilimia mia moja kusema tunataka nini kutoka katika uhusiano huo mpya. Mara zote sisi wanawke ndio huwa tunakuwa na kimbelembele kujua uhusiano tulionao unakwenda wapi katika kipindi kifupi, kwamba tunataka kufahamu kama ni “ring au fling” lakini kwa vile wanaume tunaokuwa nao kwenye uhusiano huwa hawataki kutukatisha tamaa au hanawana uhakika na hisia zao juu yetu wanawake hulazimika kutudanganya na baadhi hulipa na mahali kwa wazazi ili kutupa matumaini na at the end huwa hakuna ndoa.

Kwa wanawake inakuwa ngumu (baadhi hatujakuzwa hivyo) kuwaeleza wanaume kuwa tunachotaka ni uhusiano usio makini (casual) ili kukidhi mahitaji ya kifedha au kimwili na matokeo yake huwa tunatafuta njia za mkato ili kuwaudhi wenza wetu hali itakayo wafanya wamalize uhusiano na sisi.

Wanaume hujikakamua na kusema wazi ikiwa hawako tayari kuwa nauhusiano wa muda mrefu au hawako tayari kufunga ndoa kwa wakati huo na hivyo huturahisishia wanawake(ambao sio ving’ang’anizi) kuelewa uhusiano wenu utakwenda ama unakwenda wapi?.

Natambua kuwa kuna baadhi yetu huwa na uhakika kuwa uhusiano wao ni “ndoa” baada ya miezi mitatu ya kuwa pamoja na wengine huwachukua hadi miaka mitano kuwa tayari ama kuwa na uhakika na wanachokitaka kutoka kwenye uhusiano, hii ni kutokana na jinsi walivyokuzwa ama kushuhudia maisha mazuri au mabaya ya ndoa za wazazi wao au ndugu wakaribu.

Swala muhumi ni kuchukulia mambo taratibu na kutolazimisha (hasa kwa wanawake), ikiwa Mungu anataka kuwa huyo uliye nae ndio awe mume/mke wako basi ndivyo itakavyokuwa hivyo hali kadhalika ikiwa sio yeye hamtofika mbali hata kama utalazimisha atafunga ndoa na wewe kukuridhisha tu au kuhofia umri au hata kuhofia kudhaniwa Shoga na jamii inayomzunguuka.

Lakini ikumbukwe kuwa sote wake kwa waume hatuna mioyo ya ujasili wa kufanya hivyo na baadhi yetu huwa tunaonyesha kwa vitendo kuwa hatuko tayari kuuchukua uhusiano tulionao kwenywe hatua ya juu zaidi na badala yake huwa tunafanya vitendo bila kujitambua lakini vinaashiria wazi kabisa kuwa mtazamo wako na wa mwenza wako kwenye uhusiano wenu ni tofauti japo kuwa mnapendana kupita kiasi.

Vilevile kuna wakati unahisi ama unajua kabisa kutoka moyoni mwako kuwa humpendi sana mpenzi wako kama ambavyo ungependa kumpenda lakini unaendeleza uhusiano na yeye kwa kuhofia kumuumiza au kumuonea huruma ingawaje mwishoni mmoja kati yenu ni lazima atakumbana na ukweli na kuukubali ukweli huo kuwa hautakiwi.

Sasa, kuna vijimambo hujitokeza ndani yauhusiano ambavyo vitakufanya utatambue kuwa mpenzi wako hayuko makini sana na wewe au kakuchoka ila hajui jinsi yakutoka.

Uchelewaji: Mmeagana kukutana na wewe umesubiri kwa takriban saa nzima, lakini anapofika ana-act kuchelewa dakika tano tu na bila aibu wala huruma haombi msamaha kwa kukugandisha vilevile hatokupa sababu ya msingi/maana (mwanamke kuchelewa kwenye “date” ni muhimu na ni sehemu ya urembo ukiachilia mbali kujiandaa kuku-impress wewe bali pia umuone wakati anaingia na kukufanya wewe ujivunie kuwa na mrembo kama yeye).

Utani:Ni kitu kizuri na husaidia kuwaweka karibu kimapenzi, lakini ikiwa mwenza wakoa nakutania kuhusu mambo ambayo mnayafanya mkiwa wawili tu, au kasoro zako mbele ya rafiki zake, ndugu zake nakukucheka huo hautakuwa utani bali kukudhalilisha.

Kutotilia maanani: Mfano kuna swala muhimu unataka mzungumze lakini yeye anapiga tarehe kila unapoomba muda na yeye na siku akikubali kukaa chini ili mzungumze basi majibu yake yatakuwa ndio au hapana, hatoi maelezo ya kutosha kuhusiana na issue unayomueleza hasa ikiwa inahitaji maamuzi yenu kama wenza.

Kutojali: Wakati wote wewe ni mtu wa kupiga simu kujua yuko wapi, ikiwa anaumwa au anamatatizo kifedha wewe unakuwa pale kwa ajili yake lakini kibao kikikugeukia humuoni na wala haonyeshi kujali kuwa unamatatizo na kwamba anapaswa kuwa hapo kukupa moyo wa kukabiliana na yanayokukabili.

Sehemu ya mwisho ktk maisha yake: Kukatisha miadi na wewe kwa ajili ya kuonana na rafiki zake, wakati wote wote wewe ni mkosaji mbele ya wazazi wake na ndugu zake.

Kutengwa: Akitoka hatoki na wewe kwenda matembezini, kila akichelewa kurudi basi alikuwa na rafiki ambae hupaswi kumjua, hukutambulisha kwa jina lako badala ya “mpenzi wangu” ikifuatiwa na jina lako.

Kutoheshimu ndugu familia yako: Sote hatujakamilika, lakini ukikosea kidogo tu basi ukoo mzima utaunganishwa kwenye kosa hilo Mf ndio maana mama’ko yuko hivi, umerithi kutoka kwa baba yako, kwenu wote mko hivi au vile n.k.

Kwa leo naishia hapa tukutane tena baadae,

Upendo na amani ndio nguzo bora ya maisha marefu.